(iv)Dai kuwa Qur-an ni zao la Mwenye Kifafa na Aliyepagawa na Shetani:Waandishi kadhaa wa kikafiri katika maandishi yao wamedai bila kutoa ushahidi wowote unaotokana na historia kuwa Mtume Muhammad (s.a.w) alikuwa mwenye kifafa na mwenye kupagawa na Shetani na maneno yake alipokuwa katika hali ya ugonjwa ndiyo yaliyonukuliwa na kuunda Kitabu cha Qur-an!Udhaifu:
Udhaifu wa dai hili tunaweza kuuona kwa kujiuliza maswali yafuatayo: Je, kifafa, ugonjwa mbaya kama tunavyoufahamu, umewahi kumtokea mtu katika historia ya mwanaadamu na bado akawa mtu mwenye kutoa sheria za kufuatwa na umati wa watu wengi zaidi ya robo ya dunia? Je, historia ya mwanaadamu imewahi kumshuhudia mgonjwa wa kifafa au mwenye kupagawa na shetani kuwa na hadhi na uwezo mkubwa kuliko mtu yeyote ulimwenguni kama ilivyokuwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w)? Kama mgonjwa wa kifafa ndiye aliyeandika Qur-an, inakuwaje waandishi hodari wenye akili timamu na wanafalsafa wakubwa washindwe kuandika kitabu mithili ya angalau sura moja ya Qur-an na kukabili changa moto iliyotolewa na Qur-an karne nyingi zilizopita:"Je! Ndiyo wanasema ameitunga? Sema: "Hebu (tungeni na nyie) mlete sura moja mfano wake na waiteni muwezao (kuwapata waje).- isipokuwa Mwenyezi Mungu - (wa kuwasaidieni) kama nyinyi mnasema kweli (kuwa haya ameyazua Muhammad)." (10:38)Kitaalam inafahamika kuwa ugonjwa wa kifafa baada ya muda humfanya mgonjwa kuwa taahira (punguani). Pia ugonjwa wa kifafa humdhoofisha mgonjwa na hutisha wauguzaji na wenye kumuangalia mgonjwa wakati ameshikwa na kifafa. Hapana ushahidi wowote katika historia ya Mtume (s.a.w) ambayo iko bayana mno kuliko historia ya mtu yeyote, kuwa alikuwa mwenye kifafa au mwenye kupagawa na shetani.