Navigation Menu



image

Maudhui ya Qur-an na Mvuto wa Ujumbe Wake

Maudhui ya Qur-an na Mvuto wa Ujumbe Wake

(viii)Maudhui ya Qur-an na Mvuto wa Ujumbe Wake



Ukiisoma Qur-an na kuizingatia kwa makini na ukawa unaijua lugha yake vizuri utakiri kuwa Qur-an ni Kitabu cha Allah (s.w) kwani ujumbe wake hupenya katika moyo hata wa yule anayeipinga.



Tunafahamishwa katika historia kuwa Waarabu waliopinga Qur-an walikuwa wakipiga kelele na kuziba masikio ili wasipate ujumbe wake wakati ilipokuwa ikisomwa. Kwani kila mwenye kuielewa vizuri lugha ya Qur-an aliathiriwa na ujumbe wake.



Mfano wa athari ya kupenyeza kwa Qur-an katika nyoyo za wanaadamu ni ule wa Labiid ibn Rabiah aliyesilimu kutokana na changa moto ya aya za Qur-an dhidi ya shairi lake. Kwa kuwa yeye alikuwa mwanafasihi mashuhuri na aliyejiamini mno katika fani ya mashairi, baada ya kusoma aya chache za sura ya Qur-an alikiri kuwa Qur-an si mashairi na wala haiwezi kuwa zao la mwanaadamu. Ilibidi akiri kuwa Qur-an ni Kitabu cha Allah (s.w) na akasilimu mbele ya Mtume (s.a.w)



Mfano mwingine ni ule wa 'Umar bin al-Khattab. Akiwa bado mmoja wa viongozi wa Washirikina waliokuwa katika harakati za kumpiga vita Mtume Muhammad (s.a.w) na dini aliyokuwa akiitangaza. 'Umar alichukia sana aliposikia kuwa dada yake amesilimu. Baada tu ya kupata habari ya kusilimu kwa dada yake aliharakisha kwenda nyumbani kwa dada yake kwa hasira na upanga mkononi.Alikuta nyumbani kwa dada yake ikisomwa Qur-an iliyoandikwa katika kipande cha karatasi ambacho alidai apewe. Dada yake alikataa kumpa mpaka alipokubaliana na masharti yake. Baada ya kusoma na kurudia aya chache za Suratu-Twaha (sura ya 20) alipoa na kuondoka moja kwa moja kwenda kwa Mtume Muhammad (s.a.w) na kusilimu.



Baada ya kusilimu, 'Umar ibn al-Khattab alikuwa ngao ya kuutetea Uislamu kwa hali na mali kwa muda wote wa maisha yake na alikuwa Khalifa wa pili wa Mtume (s.a.w) na kiongozi wa Kiislamu aliye mashuhuri katika historia ya ulimwengu. Hebu turejee aya chache za sura hii zilizokuwa ndio sababu ya kusilimu 'Umar kutokana na mvuto wake:



Twaaha! Hatukukuteremshia Qur-an ili upate mashaka. Bali iwe mawaidha kwa wenye kunyenyekea. Kiteremsho kinacho toka kwa Yule aliyeumba ardhi na mbingu zilizoinuka juu. Ndiye Mungu mwenye rehema. Aliyetawala juu ya kiti cha Enzi. Ni vyake (tu peke yake) vyote vilivyomo Mbinguni na vilivyomo ardhini na vilivyo baina yao na vilivyomo chini ya ardhi. Na ukinena kwa sauti kubwa (au ndogo ni sawa sawa) kwani hakika Yeye anajua yaliyosiri na yaliyofichikana zaidi. Mwenyezi Mungu hakuna aabudiwaye kwa haki isipokuwa Yeye. (20:1-7)



Je, unaonaje ujumbe wa aya hizi za mwanzo ambazo hasa ni utangulizi wa sura hii? Utaona kuwa namna Qur-an inavyowasilisha ujumbe wake kwa watu ni tofauti kabisa na uwasilishaji wa ujumbe katika uandishi wa mwanaadamu. Si tu kuwa ujumbe wa Qur-an unanasa kwa kila mwenye kuijua lugha yake, bali hukuti udhaifu wowote katika uandishi wake kama vile kuwa na maneno yanayopingana pamoja na kwamba uandishi wake mpaka kufikia kwenye msahafu huu tulionao ulichukua miaka 23 na mpangilio wa aya na sura ni tofauti kabisa na utaratibu wa kushuka kwake. Qur-an yenyewe inathibitisha hili katika aya zifuatazo:



Hawaizingatii nini hii Qur-an? Na kama ingelitoka kwa asiyekuwa Allah bila shaka wangalikuta ndani yake hitilafu nyingi. (4:82).


Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa; Kitabu chenye maneno yanayowafikiana na yanayokaririwa; (bila kuchosha) husisimka kwayo ngozi za wale wanaomuogopa Mola wao; kisha ngozi zao na nyoyo zao huwa laini kwa kumkumbuka Mola wao. Huo ndio uongofu wa Allah; kwa huo humuongoza Amtakaye, na anayeachiwa na Allah kupotea basi hakuna wa kumuongoa. (39:23)



Pamoja na kuona kuwa Qur-an ni Kitabu cha Allah(s.w) kutokana na mvuto wake na ukamilifu wake, hebu tuangalie maudhui ya aya mbali mbali za Qur-an ambazo zinaonekana wazi kuwa haziwezekani zikawa zimetungwa na Mtume Muhammad (s.a.w) na wala hapana yeyote miongoni mwa wanaadamu aliyemfundisha:


"Ameziumba mbingu pasipo nguzo, mzionazo na ameiweka milima katika ardhi ili (ardhi) isikusukesukeni (isikutetemesheni)…" (31:10)
Aya hii inatufahamisha kuwa maumbile mbali mbali katika anga ikiwa pamoja na dunia yameshikiliwa na nguvu ya uvutano (gravitational force) ambayo hatuioni kwa macho yetu. Kama aya hii ilitungwa na Muhammad (s.a.w) miaka mingi kabla ya ugunduzi wa kuwepo kwa nguvu ya uvutano kati ya dunia, jua na sayari nyingine na kabla ya maendeleo ya sayansi yaliyopo hivi leo juu ya ulimwengu (universe) kwa ujumla kwa nini akaongeza neno "mzionazo" badala ya kusema tu "ameziumba mbingu pasipo nguzo?" Yeye alijuaje kwamba kuna nguvu ya uvutano na haionekani? Zaidi ya hivyo Mtume (s.a.w) angelijuaje kabla ya ugunduzi wa sayansi wa karne ya 19/20 A.D kuwa kuwepo kwa milima katika sehemu zake ni muhimu sana katika kuithubutisha dunia na kuifanya isiyumbe yumbe wakati ikizunguka kwa kasi sana katika muhimili wake, na kuzuia tetemeko? Imegundulika hivi karibuni kuwa milima ina mizizi.



Ujumbe wa aya hii wenye maelezo ya kisayansi yaliyotolewa na wanasayansi wa karne hizi za usoni hauwezi kuwa umetolewa na Mtume (s.a.w) katika karne ya Saba wakati uvumbuzi huu haujafahamika kwa mtu yeyote. Kwa hiyo ujumbe wa aya hii ni hoja tosha kuwa Qur-an ni neno linalotoka kwa Mjuzi wa yote.


"Na bila shaka katika wanyama muna mazingatio makubwa kwa ajili yenu. Tunakunywesheni katika vile vilivyomo matumboni mwao baina ya choo na damu, (Tumekunywesheni) maziwa safi (na) mazuri kwa wanywao." (16:66)



Ukweli kwamba maziwa katika wanyama hutengenezwa katika "mammary glands" kutokana na chakula kilichochunjwa kutoka tumboni na kikasafirishwa katika mikondo ya damu ni ugunduzi wa kisayansi wa hivi karibuni katika karne ya ishirini (20). Sasa Muhammad (s.a.w) angelipata wapi utaalamu huu kama kweli yeye ndiye mwandishi wa Qur-an?



"Na kwa yakini tulimuumba mwanaadamu kwa udongo uliosafi,kisha tukamuumba kwa tone la manii lililowekwa katika makao yaliyohifadhika. Kisha tukalifanya tone hilo kuwa pande lenye kuning'inia, kisha Tukalifanya kuwa pande la nyama kisha tukalifanya kuwa mifupa na mifupa tukaivisha nyama, kisha tukamfanya kiumbe mwingine. Basi Ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa Waumbaji." (23:12-14)


"Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai (uzazi) iliyochanganyika (ya mwanamume na mwanamke) ili Tumfanyie mtihani, kwa hiyo Tukamfanya ni mwenye kusikia (na) mwenye kuona." (76:2)



Kama Mtume Muhammad (s.a.w) ndiye mwandishi wa aya hizi, angelijuaje au ni nani angelimfundisha wakati ule uhakika huu wa kisayansi juu ya hatua za kukua mtoto katika mfuko wa uzazi tokea kwenye mbegu za uzazi hadi kuwa mwanaadamu kamili?Hebu tumalizie mifano kwa kuzingatia tena aya zifuatazo:


"Naye (Mwenyezi Mungu) Ndiye anayeziunganisha bahari mbili hii ni tamu inayoondosha kiu, na hii ni yenye chumvi kali; na akaweka kinga kati yao na kizuizi kizuiacho." (25:53)



"Amezikutanisha bahari mbili. Baina yao kuna kizuizi, haziingiliani (hazichanganyiki)." (55:19-20)
Aya hizi na aya nyinginezo za Qur-an zinatufanya tuzidi kuwashangaa wale wanaodai kuwa mtunzi wa Qur-an ni Muhammad (s.a.w). Ni hivi karibuni tu, 1983, mtaalamu mmoja wa Ufaransa, Capitain Jecques Constean, amegundua kuwa maji ya bahari mbili hayachanganyiki jambo lililoelezwa katika Qur-an karne 14 zilizopita. Mtaalamu huyu aliposoma aya hizi za Qur-an ilibidi akiri:



“Nimeshuhudia kuwa Qur-an ni maneno ya Allah (s.w). Sayansi yetu ya leo inathibitisha tu yale yale yaliyoelezwa na Qur-an karne 14 zilizopita." Aya hizi tulitozinukuu kama mifano na nyingine nyingi kama hizi zinatufahamisha juu ya utalaamu wa hali ya juu, juu ya maumbile ambao ndio tu umegunduliwa katika karne hizi za 19/20 kutokana na utafiti wa kisayansi. Yapo mambo mengi yaliyoelezwa katika Qur-an juu ya maumbile ambayo mpaka hivi sasa mwanaadamu hajaweza kuyatolea maelezo ya kisayansi.



Kwa hiyo ukiichunguza Qur-an kwa makini na kuifanyia utafiti kwa kiwango cha utalaamu kilichofikiwa hivi sasa utaona kuwa Qur-an ni
Kitabu kinachoweka bayana na kuelezea kila kitu kinachohitajika katika kuleta ufanisi wa maisha ya mwanaadamu hapa ulimwenguni na huko Akhera. Qur-an yenyewe inadhihirisha hili katika aya zifuatazo:


“Alif Lam Raa, Hizi ni aya za Kitabu kilichokusanya kila yanayohitajiwa na kikayadhihirisha kwa vizuri." (15:1)


"Hizi ni aya za kitabu kielezacho (kila linalohitajiwa)." (26:2)


"Twa Sin. Hizi ni aya za Qur-an, (Kitabu kilichojaa kila yenye faida) na kitabu kielezacho (kila linalohitajika)." (27:1)


"Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala haiwi kwake (kuwa mtunga mashairi). Haikuwa (Qur-an) ila ni ukumbusho na Kitabu kibainishacho (kila yanayohitajiwa).Ili amwonye aliye hai na ihakikike kauli (ya kuadhibiwa) juu ya makafiri." (36:69-70)


Haa Miim. "Naapa kwa Kitabu (hiki) kinachobainisha (kila linalohitajika)." (44:2)



Aya zote hizi zinatufahamisha kuwa Qur-an imetubainishia kwa uwazi na kwa lugha nyepesi kila linalohitajika katika kuendesha maisha yetu ya kila siku kwa ufanisi. Anashuhudia ukweli huu kila mwenye kuisoma Qur-an kwa mazingatio. Kwa hiyo, ni muhali kabisa Qur-an kuwa kitabu kilichotungwa na mwanaadamu bali ni lazima mwandishi wake awe ni yule aliye mjuzi wa mambo yote yaliyo nyuma na mbele ya maisha ya mwanadamu na mwenye ujuzi huo si mwingine ila Allah (s.w).




                   







           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Topic: Quran Main: Post File: Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 577


Sponsored links
👉1 Kitabu cha Afya     👉2 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)     👉3 Madrasa kiganjani     👉4 Simulizi za Hadithi Audio     👉5 kitabu cha Simulizi     👉6 Kitau cha Fiqh    

Post zifazofanana:-

WAQFU WAL-IBTIDAAI
Jifunze namna ya kusoma quran, pata mafunzo ya tajwid hapa Soma Zaidi...

Sifa za waumini katika quran
Soma Zaidi...

Quran si maneno ya mwenye kifafa
Soma Zaidi...

surat al mauun
SURATUL-MAM’UUN Imeteremshwa Maka, anasimulia Ibn Jurayj kuwa Abuu Sufyan ibn Harb alikuwa na kawaida ya kuchinja ngamia wawili kila wiki, hivyo siku moja yatima mmoja alikuja kwake na kumlilia shida, na hakumsaidia kwa chochote na hatimaye akampiga yat.. Soma Zaidi...

Sura za makkah na madinah
Quran (EDK form 3: Dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

quran na sayansi
Soma Zaidi...

Uthibitisho kuwa Qur-an ni neno la Allah (s.w)
Uthibitisho kuwa Qur-an ni neno la Allah (s. Soma Zaidi...

quran na sayansi
2:UUMBWAJI KWA MAJI YA UZAZIUumbwaji wa mwanadamu umepitia hatua mbalimbali na haya yote yamefanywa kwa sababumaalumu ili tipate mazingatio. Soma Zaidi...

Sifa za wanafiki katika quran
Soma Zaidi...

Sababu za kushuka surat al-Fiyl
Al fiyl ni neno la Kiarabu lenye maana ya tembo. Sura hii inazungumziakisa cha jeshi lenye tembo. Jeshi hili lilikuwa na nia ya kuvunja al qaaba Soma Zaidi...

HUKUMU ZA MADD YAANI KUVUTA HERUFI KWENYE USOMAJI WA QURAN
Jifunze namna ya kusoma quran, pata mafunzo ya tajwid hapa Soma Zaidi...

Ni nini maana ya Idh-har katika usomaji wa Quran
Hapa utajifunza kuhusu hukumu ya Idh-har katika usomaji wa Quran. Soma Zaidi...