20. Kuepukana na Kulaani Ovyo



Kulaani ovyo kumekatazwa katika Uislamu. Mtu anapolaani wengine anakuwa amejisahau kuwa naye ni mkosaji. Mtume (s.a.w) ametukataza kulaani ovyo katika Hadithi zifuatazo:



Ibn ‘Umar (r.a) amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: “Si sawa kwa Muumini kuwa mkubwa wa kulaani”. Na katika upokezi mwingine, Mtume amesema, “Si stahiki ya Muumini kuwa mkubwa wa kulaani”. (Tirm idh).



Abu Dard (r.a) amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allah akisema: “Watu wenye mazoea ya kulaani hawatakuwa mashahidi wala wenye kushufaia katika siku ya Kiyama ”. (Muslim).



Ibn Abbas (ra) ameeleza kuwa upepo ulipeperusha nguo ya mtu. Kwa hiyo aliulaani (upepo). Mtume wa Allah (saw) alisema ; “Usiulaani kwa sababu umeamrishwa ufanye hivyo na kwa sababu laana inakurudia mwenye kulaani kitu kisichostahiki kulaaniwa (kisicho na hatia). (Tirmidh na Abu-Daud).



Muislamu anatakiwa ajiepushe na tabia ya kulaani na badala yake awe mwingi wa kuwasamehe wenye kumkosea na kuwatakia msamaha kwa Allah (s.w) ili naye asamehewe dhambi zake.