18. Kuepukana na Kibri na Majivuno


Kibri, majivuno na majigambo ni katika tabia mbaya iliyokemewa vikali katika Qur-an kama ifuatavyo:

“Wala usitembee (usiende) katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuzipasua ardhi wala huwezi kufikia urefu wa mlima. Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza mbele ya Mola wako”. (17:37-38)

“Wala usiwatazame (watu) kwa upande mmoja wa uso, wala usiende katika ardhi kwa maringo, hakika Allah hampendi kila ajivunae ajifaharishaye”. (31:18).
Mtu mwenye kiburi hujiona kuwa ni bora, wa juu na wa maana zaidi kuliko wengine. Kibri na kujiona husababishwa na neema mja alizotunukiwa na Mola wake kama vile utajiri, madaraka, umaarufu, elimu, nguvu nyingi, uzuri wa sura, n.k. Mwenye kibri na kujiona anasahau kuwa kama alivyozipata neema hizi bila ya kupeleka barua yoyote ya maombi kwa Allah (s.w) ndivyo anavyoweza kukatikiwa na neema hizi na asiweze kufanya chochote. Katika Qur-an tunapigiwa mfano wa Qaaruni aliyetakabari kutokana na hiyo neema ya mali aliyokuwa nayo.Lakini Allah(s .w) alipomuondolea neema hiyo hakuweza ku fanya lolote. Rejea Qur-an: (28 :76-8 3).


Kibri na majivuno huzaa maovu yafuatayo: dharau, ukatili, uonevu, udhalimu na kutoshaurika. Waislamu tunaaswa tujiepushe mbali na tabia hii mbaya ambayo malipo yake ni moto wa Jahannam kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:

“Itasemwa: “Ingieni milango ya Jahannam mkae humo” Basi ni ubaya ulioje wa makazi ya wanaotakabari! (39:72).
Pia Hadithi zifuatazo zinatubainishia kina cha uovu wa kibri:
Abu Hurairah (r.a) Amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Allah (s.w) amesema, “Utukufu ni nguo yangu na kibri ni kilemba changu. Yeyote atakayeshindania kimojawapo katika hivi ataangamia. (Muslim).


Abu Hurairah (r.a) amesimulia kuwa, Mtume wa Allah amesema: “Yule ambaye moyoni mwake mna chembe (punje) ya kibri hataingia peponi” Sahaba mmoja akauliza: “Je, kama mtu anapenda nguo nzuri na viatu?” Mtume (s.a.w) akasema, “Allah (s.w) ni mzuri na anapenda vizuri. Kibri ni kukataa ukweli na kupuuza watu”. (Muslim)
Abu Hurairah (r.a) amesema kuwa Mtume wa Allah amesema: “Siku ya Kiyama, Allah (s.w) hatamwangalia yule anayevaa vazi lake kw a kibri” (Bukahri na Muslim).
Msingi mkuu wa kibri ni ukafiri - kumkadhibisha Allah (s.w) na ujumbe wake:

“Nitawaepusha na (kuzingatia) aya zangu wale wanaotakabari katika nchi pasipo haki; na ambao kila hoja wanayoiona hawaiamini; na kama w akiiona njia ya uw ongofu haw aishiki kuwa ndiyo njia, lakini w akiiona njia ya upotofu (upotevu) wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu ya kuzikadhibisha Aya zetu na kuzipuuza ”. (7:146)

“Na wale watakaokadhibisha aya zetu na kuzifanyia kiburi hao watakuwa watu wa Motoni, watakaa humo daima. (7:36).