image

Historia ya Nabii Ayyuub

Katika somo hiliutakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii ayyuub

HISTORIA YA NABII AYYUUB(A.S)


Ayyuub(a.s) ni katika Mitume wa Allah(s.w) waliotajwa katika Qur-an kwa umadhubuti wake katika imani juu ya Allah(s.w) na Subira.

Ayyuub(a.s) aliishi Kaskazini Mashariki ya Bara Arabu. Alikuwa tajiri sana mwenye mali nyingi, watoto wengi na watumishi wengi. Lakini hakutakabari bali alimuabudu Mola wake na kumshukuru ipasavyo

 

Mitihani Iliyomfika Ayyuub(a.s)


Nabii Ayyuub(a.s) alitahiniwa na Mola wake kama ifuatavyo:

(1) Mali yake, watoto wake na watumishi wake wote walipatwa na majanga wakatoweka. Akabakia yeye na mkewe ambaye naye alikuwa mcha-Mungu.

 

(2) Pamoja na kupotelewa na mali yake na watu wake wote, alishikwa na maradhi mabaya ya kuota vidonda mwili mzima kuanzia kichwani hadi miguuni. Alijaribu kutumia dawa zote alizoweza, lakini hakupata nafuu yoyote

 

Nabii Ayyuub(a.s) hakutetereka katika imani yake kutokana na majanga yaliyomfika bali alisubiri na kuwa karibu zaidi na Mola wake kuliko hata wakati alipokuwa katika hali yake ya mwanzo ya utajiri na afya nzuri. Na Allah(s.w) anamsifu mjawake, Ayyuub kama ifuatavyo:

“…. Bila shaka tulimkuta ni mwenye subira mja mwema; kwa hakika alikuwa mnyenyekevu sana.” (38:44)

 

Nabii Ayyuub(a.s) aliona kuwa aliyempa mali, watoto na wale watumishi aliokuwa nao ni Allah(s.w) kama amana. Hivyo, aliona hapakuwa na kosa lolote kwa Allah(s.w) kuchukua amana yake. Pia aliridhika na hali ya ugonjwa aliyokuwa nayo. Kwa ujumla Nabii Ayyuub (a.s) aliridhika na kusubiri juu ya matatizo yote yaliyomfika na kupata matunda ya subira kama Allah(s.w) anavyotubashiria:

 

Na tutakutieni katika msukosuko wa (baadhi ya mambo haya); hofu na njaa na upungufu wa mali na wa watu na wa matunda. Na wapashe habari njema wanaosubiri.(2:155) Ambao uwapatapo msiba husema: “Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye tutarejea (atatupa jaza yake).(2:156)

 

Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao na rehema; na ndio wenye kuongoka. (2:157)

 

Dua ya Ayyuub(a.s)


Nabii Ayyuub(a.s) aliendelea na maradhi yale mazito kwa kipindi kirefu (ina semekana miaka saba). Mwishowe akaona amuelekee Mola wake na kumuomba amuondolee maradhi yale kama tunavyojifunza katika ya zifuatazo:


 


Na (Mtaje) Ayyubu, alipomwita Mola wake (akasema) “Mimi imenipata dhara, nawe ndiwe Unayerehemu kuliko wote wanaorehemu.” (21:83)

Dua ya Ayyuub(a.s) ilikuwa makubuli kwa Mola wake kumuelekeza dawa ya matibabu yale:


 

(Mwenyezi Mungu akamwambia):- “Uharikishe mguu wako (patachimbuka chemchem chini yake, maji yake yatakuwa dawa yako). Basi haya maji baridi ya kuogea (koga), na (haya maji baridi) ya kunywa, (yanywe).” (38:42)


 

Baada ya kutumia dawa hii Nabii Ayyuub(a.s) alikuwa mzima wa afya kama alivyokuwa hapo awali kabla ya ugonjwa. Furaha zaidi kwake, pamoja kurudishiwa afya yake, pia alirudishiwa mali na watu wake kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:


 

Basi tukamkubalia (wito wake) na tukamuondolea dhara aliyokuwa nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao. Ni rehema inayotoka kwetu, na ukumbusho (mzuri kwa wafanyao Ibada. (21:84)


 

Na tukampa watu wake na wengine kama wao pamoja nao, kwa rehema itokayo kwetu, na (ipate kuwa) mauidha kwa watu wenye akili. (38:43)

 

Nabii Ayyuub(a.s) Kutekeleza Kiapo Chake


Mkewe Ayyuub(a.s) alikuwa naye ni mama mcha-Mungu mwenye subira. Alimuuguza mumewe kwa kipindi kirefu kiasi hicho katika hali ngumu bila ya kuchoka. Lakini inasemekana siku moja aliteleza na kutamka maneno ambayo yalimchukiza Nabii Ayyuub(a.s) kwa kuwa yalikuwa yanamtoa katika imani ya Allah(s.w). Inasemekana mkewe aliteleza na kusema, “Hivi huu ugonjwa utaendelea mpaka lini?” Nabii Ayyuub(a.s) alimkemea mkewe juu ya kauli yake hiyo na kumuahidi kuwa akipona atamuadhibu kwa kumcharaza bakora mia.


 

Baada ya Nabii Ayyuub(a.s) kupona, Allah(s.w) alimuelekeza namna yakutekeleza kiapo cha kumuadhibu mkewe aliyemfanyia ihsani na kuvumilia shida kiasi kile, kwa maelekezo ya Allah(s.w) hakupaswa kumcharaza bakora mia, bali aliagizwa achukue vijiti mia avifunge pamoja kisha ampige navyo mara moja kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:


 


“Na shika kicha cha vijiti tu mkononi mwako, (si fimbo); kisha mpige kwacho (mkeo kwa kiapo ulichoapa kuwa utampiga kwa mabaya aliyoyafanya), wala usivunje kiapo.” Bila shaka tulimkuta ni mwenye subira, mja mwema; kwa hakika alikuwa mnyenyekevu sana. (38:44)

 

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Ayyuub(a.s)


Kutokana na kisha hiki cha Nabii Ayyuub(a.s) tunajifunza
yafuatayo:

(i) Binaadamu hapa ulimwenguni yuko mtihanini kama Qur-an inavyobainisha:


 

Ametukuka yule ambaye Mkononi mwake umo ufalme (wote); Naye ni mwenye uweza juu ya kila kitu. Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni (kukufanyieni mtihani); ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Naye ni Mwenye nguvu na Mwenye Msamaha. (67:1-2)


 

Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika; (ya mwanamume na mwanamke), ili tumfanyie mtihani (kwa amri zetu na makatazo yetu); kwa hiyo tukamfanya ni Mwenye kusikia (na) Mwenye kuona. (76:2)


 

Mwanaadamu anachoweza kufanya si kuepa mitihani bali kutekeleza wajibu wake kwa kadiri ya uwezo wake na kufanya subira juu ya mazito mbali mbali yatakayomfika huku akimtegemea Allah(s.w) ipasavyo


 

(ii) Muumini baada ya kumcha-Allah(s.w) ipasavyo alipokee kwa moyo mkunjufu lolote litakalomfika likiwa la kheri au lenye sura ya shari, kwani Allah yuko pamoja na waja wake.


 

(iii) Kwa elimu ndogo ya mwanaadamu kuna matukio mengine yanamtokea mwanaadamu kwa sura ya shari, kumbe ni ya kheri kwake na kinyume chake kama Allah(s.w) anavyotutanabahisha katika aya ifuatayo:


 

Mmelazimishwa kupigana vita (kwa ajili ya dini). Nalo ni jambo zito kwenu. Lakini huenda mkachukia kitu, nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayejua, (lakini) nyinyi hamjui. (2:216)


(iv) Muumini wa kweli anatakiwa awe anamkumbuka Allah(s.w) nyakati zote katika hali zote, akiwa na dhiki au wasaa. Na mtu anapokuwa katika dhiki ndio anazijua na kuzithamini vizuri neema mbali mbali alizoneemeshwa na Mola wake na ndio anakuwa na nafasi nzuri ya kushukuru. Kwa mfano ni kweli kuwa mtu hawezi kujua thamani ya shibe kama hajafikiwa na dhiki ya njaa.


 

(v) Waumini wanalazimika kutekeleza ahadi au viapo wanavyotoa katika kufanya mambo ya kheri.


 

(vi) Hapana kizuizi chochote kiwezacho kuwazuia waumini kumcha-Mola wao na kusimamisha Uislamu katika jamii.


 

(vii) Matatizo yanayowafika waumini pasina yale ya kujitakia (ya uzembe), ni nyenzo muhimu za kunoa imaniyao juu ya Allah na kuwapa hamasa na msukumo wa kusimamisha Uislamu katika jamii.

           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-06-27 12:36:51 Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 58


Sponsored links
👉1 kitabu cha Simulizi     👉2 Kitau cha Fiqh     👉3 Kitabu cha Afya     👉4 Madrasa kiganjani    

Post zifazofanana:-

Hstora ya Nabii Ilyasa
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Ilyasa Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Ibrahimu
Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Ibrahim katika quran Soma Zaidi...

Hstora ya Nab Sulaman
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Sulaman Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Adam
ata post h utawenda ujfunza hstora ya Nabii Adam ulngana na Quran navyoeleza Soma Zaidi...

Hstoria ya Nabii Yusuf
Katika makala hii utakwenda ujfunzakuhusu historiaya Nabii Yufuf katika Quran Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ya'qub
Katika somo hili utawenda ujfunz ahstoraya Nabii Ya'qub na familia yake Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Musa
atika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Musa Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Shu'aib
atika makala hii utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Shu'aib katika Quran Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Nuhu katika Quran
Katika somo hili utakwenda kujifunza historia ya Mtume Nuhu kulingana na melezo yaliyo kwenye Quran Soma Zaidi...

Histora ya Nabi Zakariya
Katika somo hili utakwenda ujfunza kuhusu hslistoria ya Nabi Zakariya Soma Zaidi...

Hstora ya Nab Ishaqa katika quran
Katika post hii tutakwenda kujifunza historia ya Mtume Ishaqa Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Idrisa
Katika somohili utakwenda kujifunza historia ya Nabii Idrisa (amani iwe juu yake) Soma Zaidi...