image

Hstora ya Nab Sulaman

Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Sulaman

HISTORIA YA MTUME SULAIMAN(A.S)

 

Sulaiman(a.s)alikuwa mtoto wa Nabii Daudi(a.s) na pamoja na kuwa Mtume alirithi pia kiti cha ufalme wa baba yake. Ufalme wake ulidumu kati ya mwaka 965 B.C. hadi 926 B.C. Ufalme wake ulienea Palestina ya leo, Transjordan na baadhi ya eneo la Syria. Qur'an inamtaja Sulaiman kuwa mrithi wa Nabii Daudi(a.s) katika aya zifuatazo:

 

"Na Sulaiman alimrithi Daudi na akasema: Enyi watu! Tumefundishwa (hata kutambua) usemi wa ndege na tumepewa kila kitu, hakika hii ni fadhila iliyo dhahiri" (27:16).

"Na tukampa Daudi (mtoto anayeitwa) Sulaiman, aliyekuwa mtu mwema, na alikuwa mnyenyekevu mno" (38:30).


 

Nabii Sulaiman(a.s) anatajwa katika historia kama mfalme ambaye haujapata kutokea uflame mkubwa kama wake. Mwenyezi Mungu alimpa uwezo hata wa kumiliki majini. Walimtumikia katika

kazi zake mbali mbali. Ufalme huu unatajwa kuwa Nabii Sulaiman(a.s)aliupata baada ya kumuomba Mola wake ampe ufalme ambao hataupata mwingine yoyote baada yake.


 

"Akasema: Mola wangu! Nisamehe na unipe ufalme, asiupate yoyote baada yangu. Bila shaka wewe ndiwe Mpaji" (38:35).

Dua hii Nabii Sulaiman(a.s) anaiomba akiwa tayari ni mfalme. Lakini baada ya hapo ndio ufalme wake ukapanuka, kama aya zinazofuatia aya zinavyobainisha:


 

"Basi tukamtiishia upepo unaokwenda pole pole kwa amri yake, anakotaka kufika. Pia na (Tukamtiishia) mashetani, kila ajengaye na azamiaye (lulu). Na wengine wafungwao minyororoni (wanapokhalifu amri zake)" (38:36-38).


 

Pamoja na ufalme na mamlaka makubwa kiasi hiki aliyopewa Sulaiman,lakini pia alipewa elimu ya kumtambua Allah(s.w) na kupewa utume. Kwa hiyo alikuwa ni mja mwenye shukrani kwa neema hizo alizofadhilishwa:


 


Na bila shaka tuliwapa Daudi na Sulaiman ilimu (kubwa kabisa na wakamshukuru Mwenyezi Mungu) wakasema: "Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Aliyetufadhilisha kuliko wengi katika waja wake waliomuamini" (27:15).

 

Uchambuzi wa Neema Alizopewa Nabii Sulaiman(a.s).

(i) Kutiishiwa Upepo
Qur'an inatufahamisha kuwa Nabii Sulaiman alitiishiwa upepo akaweza kuutumia apendavyo kwa amri yake.

 

"Na kwa Sulaiman (Tukautiisha) upepo wa nguvu uendao kwa amri yake katika ardhi ambayo tumeibarikia. Nasi ndio tunaokijua kila kitu. Na kwa Sulaiman (Tukautiisha) upepo (uliokwenda) safari yake ya subuhi (mwendo wa) mwezi mmoja, na safari yake ya jioni (mwendo wa) mwezi mmoja" (34:12).


 

Aya hizi zinaweka wazi kuwa, Nabii Sulaiman aliweza kufanya safari ndefu sana baharini kwa wepesi kabisa kwa vile Allah(s.w) aliutiisha upepo kiasi kwamba ulivuma katika mwelekeo wa vyombo vyake. Kwa hiyo safari ya mwezi mzima aliweza kuifanya kwa masaa machache. Na tukiwa leo katika karne ya sayansi na teknolojia ambapo madege husafiri kwa kasi ya maelfu ya kilometa kwa saa, haiwi viguvmu kwa fahamu zetu kuielewa neema hii aliyopewa Nabii Sulaiman.


(ii) Kutiishiwa Majini.
Nabii Sulaiman(a.s) alitiishiwa majini ambayo aliyatumikisha kumfanyia kazi mbalimbali.

"Na (Tukamtiishia) mashetani wenye kumpigia mbizi (ili wamletee lulu) na wakimfanyia vitendo vingine visivyokuwa hivyo. Nasi tulikuwa walinzi wao" (21:82) Tazama pia (34:12-13) na (27:17).


 

Ilivyokuwa kawaida mwanaadamu huishi na kushirikiana na wanaadamu wenzake. Aidha viumbe wa jinsi nyingine huishi na kuhusiana wao kwa wao. Asili ya umbile la awali la mwanaadamu ni udongo. Majini wao wameumbwa kwa moto.


 

Katika hali ya kawaida mwanaadamu hakupewa uwezo wa kumwona jinni. Lakini pamoja na tofuati hiyo ya kimaumbile Allah(s.w) Muweza wa yote alimpa Nabii Sulaiman uwezo wa kuyamiliki majini.


 

(iii) Utawala Juu ya Ndege
Pamoja na kuwa mfalme, mwenye kutiiwa na watu, na mwenye uwezo wa kuyatumia majini kufanyia kazi, Nabii Sulaiman alipewa uwezo pia wa kuwatawala na kuwatuma kazi ndege. Hili linawekwa wazi na aya zifuatazo:

"Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake katika majini na watu na ndege, nayo yakapangwa makundi makundi" (27:17).

"Na akawakagua ndege (na asimuone Hud-Hud) akasema: "Imekuwaje mbona simuoni Hud-Hud, au amekuwa miongoni mwa wasiokuwapo (hapa leo)"? (27:20).


 

(iv) Uwezo wa kusikilizana na viumbe wengine.

Kama alivyokuwa ameneemeshwa baba yake (Nabii Daudi): Nabii Sulaiman alipewa uwezo wa kusikia lugha za viumbe wengine mbali na binaadamu. Katika Qur'an wanatajwa ndege na wadudu.


"Na Suleiman alimrithi Daudi na akasema: "Enyi watu! Tumefundishwa (hata kutambua) usemi wa ndege na tumepewa kila kitu; hakika hii ni fadhila iliyo dhahiri" (27:16).


 

Habari ya kutambua lugha ya wadudu; inabainishwa katika tukio ambapo Nabii Sulaiman alikuwa akipita mahali na jeshi lake. Wadudu chungu wakapeana taafira wachukue hadhari Nabii Sulaiman asije akawaponda hali ya kuwa hana habari. Nabii Sulaiman alifahamu walichokuwa wanaambizana wadudu chungu. Kwa hiyo akalisimamisha jeshi lake mpaka walipoingia mashimoni mwao. Kisha akamshukuru Mola wake kwa neema hii.


 


Hata walipofika katika bonde la wadudu chungu; alisema mdudu chungu (kuwaambia wenziwe); "Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu; asikupondeni Sulaiman na majeshi yake, hali ya kuwa hawakuhisini (hawana habari)" (27:18).


 

Basi akatabasamu akilichekea neno lake, na akasema: "Ee Mola wangu! Nipe nguvu nishukuru neema yako uliyonineemesha mimi na wazazi wangu, na nipate kufanya vitendo vizuri uvipendavyo, na uniingize kwa rehma yako katika waja wako wema" (27:19).


 

Historia inaonesha kuwa mara nyingi utajiri, wingi wa watoto, uflame na mamlaka makubwa huwa ndio chanzo cha watu kutakabari na kufanya udhalimu na ufisadi katika ardhi. Tunayo historia ya Firauni, Karun, Hamana na wengineo ambao walitakabari na kufanya ufisadi kwa ajili ya utajiri na mamlaka waliyokuwa nayo. Aidha tunao kina Musolin, Stalin, Hitler, Ngueso n.k. Wapo pia Maraisi wengine ambao hawapo katika rekodi za madikteta, lakini huwanyonya, huwatesa na kuwafanyia udhalimu wa kila namna raia zao.


 

Nabii Sulaiman(a.s) aliwatawala binaadamu wenziwe, majini hadi ndege. Lakini kwa kutambua kuwa yote aliyokuwa nayo ni neema kutoka kwa Allah(s.w) na kwamba ipo siku atasimamishwa katika mahakama tukufu ya Allah(s.w) kujibu jinsi alivyoitumia neema ile; anakuwa mnyenyekevu na mwenye kuchunga mipaka ya Allah(s.w). Anafahamu kuwa kila kiumbe kina lengo la kuumbwa kwake na kina haki ya kuishi. Kwa hiyo anajali hata maisha ya mdugu chungu.


 

Nabii Sulaiman kwa kutambua kuwa neema zote hizo alizotunukiwa ni mtihani kwake,tunamuona akimuomba Mola wake ampe nguvu ya kuweza kushukuru neema alizompa.(Qur’an 27:19).


 

Kwa maana amjaaliye asitakabari na kuzitumia neema hizo kwa namna ambayo itawadhuru wengine iwe ni kwa kukusudia au kutokufahamu.


 

Ardhi yetu hii haitokuwa na amani, uhuru na salama ya kweli mpaka tuwe na viongozi wanaojali haki, uhuru na usalama wa binaadamu wenzao kama Sulaiman alivyo wajali hata wadudu chungu. Na hawa hawawezi kuwa wengine ila wale wanaomtambua Mungu mmoja na kumcha kweli kweli. Viongozi watakaoongoza si kwa kufuata miongozo na katiba zilizobuniwa na watu bali kwa kufuata Kitabu cha Allah na Sunna ya Mtume wake (s.a.w).

 

Kusingiziwa Nabii Sulaiman Uchawi

 

Pamoja na Ucha-Mungu aliokuwa nao Nabii Sulaiman watu hawakuacha kumsingizia mambo machafu. Na hii imekuwa ni tabia ya watu wabaya kuwasingizia Mitume uovu ili wapate kuwapoteza watu na njia ya Allah. Nabii Suleiman katika jumla ya mambo aliyosingiziwa ni kuwa alikufuru akafundisha watu elimu ya uchawi. Qur'an inajibu shutuma hizo katika aya ifuatayo:


 


Wakafuata yale waliyoyafuata mashetani (wakadai kuwa yalikuwa) katika uflame wa Sulaiman; na Sulaiman hakukufuru, bali mashetani ndio waliokufuru, waliwafundisha watu uchawi (waliokuwa wakiujua wenyewe tangu zamani) na (uchawi) ulioteremshwa kwa malaika wawili; Haruta na Maruta; katika (mji wa) Babil. Wala (Malaika hao) hawakumfundisha yeyote mpaka wambwambie: "Hakika sisi ni mtihani (wa kutazamwa kutii kwenu); basi usikufuru;" Wakajifunza kwao ambayo kwa mambo hayo waliweza kumfarikisha mtu na mkewe (na mengineyo). Wala hawakuwa wenye kumdhuru yeyoyte kwa hayo ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza ambayo yatawadhuru wala hayatawafaa. Na kwa yakini wanajua kwamba aliyekhiari haya hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera. Na bila shaka ni kibaya kabisa walichouzia nafsi zao. Laiti wangalijua (hakika wasingefanya hivi). (2:102)


 

Pamoja na aya hii kumtakasa Nabii Sulaiman na yale aliyokuwa akisingiziwa, mafundisho yafuatayo hapana budi tuyazingatie. Kwanza, tunafahamishwa kuwa elimu ya uchawi ipo; lakini ni mtihani kwa wanaadamu. Kujifundisha na kuufanyia kazi uchawi ni kufru na atakayehiari kuufuata hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera.


 

Jambo la pili tunalotakiwa tulizingatie ni kuwa Muislamu hana haja ya kubabaika anapopatwa na janga lolote. Mwenyezi Mungu anatufahamisha kuwa huo uchawi hauwezi kumdhuru mtu ila kwa idhini yake Allah(s.w).".............Wala hawakuwa wenye kumdhuru yeyote kwa hayo ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu….........." (2:102).


 

Kwa hiyo Muislamu amtegemee Allah(s.w) na alikabili tatizo lolote litakalomtokea kwa kuchunga mipaka ya Allah(s.w) na kuomba msaada wake.

 

Kisa cha Malkia wa Sabaa.

 

Sabaa ulikuwa mji katika nchi inayojulikana leo kama Yemen. Watafiti wa mambo ya historia na geografia wanasema Sabaa ilikuwa kiasi cha umbali wa maili hamsini kutoka mji wa Sanaa. Watu wa Sabaa walikuwa wakiabudu Jua na walimfanya mtawala wao kuwa ni mwanamke - malikia.


 

Pamoja na ushirikina wao, Allah(s.w) aliwaneemesha watu wa Sabaa kwa kila kitu walichohitajia katika maisha yao. Nabii Sulaiman aliwafahamu watu wa Sabaa kupitia kwa ndege Hud-Hudi kama aya zifuatazo zinavyobainisha:


 

"Na akawakagua ndege (na usimuone kidege Hud-Hud) akasema: "Imekuwaje mbona simuoni Hud-Hudi, au amekuwa miongoni mwa wasiokuwepo (hapa leo)". "Kwa yakini nitamuadhibu adhabu kali au nitamchinja au ataniletea hoja iliyo wazi (ya kumzuilia kuja hapa leo)." "Basi hakukaa sana mara (Hud-Hudi akafika) akasema (kumwambia Nabii Suleiman) Nemegundua usilogundua, na ninakujia hivi kutoka (nchi inayoitwa) Sabaa na (nakuletea) habari yenye yakini"."Hakika nimekuta mwanake anawatawalia; naye amepewa kila kitu na anacho kiti cha enzi kubwa"."Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia njia (ya kheri), kwa hivyo hawakuongoka" (27:20-24).


 

Baada ya taarifa hizo Nabii Sulaiman alituma ujumbe kumnasihi malkia aingie katika Uislamu. Awali malkia baada ya kushauriana na mawaziri wake aliona apoteze lengo la Sulaiman kwa kumpa zawadi. Lakini lengo la Mitume ni kufikisha ujumbe wa Allah si kuchuma. Kwa hiyo Nabii Sulaiman alimrejeshea zawadi zake na akaendeleza harakati za kumvuta malkia katika haki mpaka akasilimu. Habari hizi zimebainishwa kwa urefu katika aya Qur’an(
27:27-44).


 

Jambo tunalotakiwa tulizingatie hapa ni ule msimamo thabiti wa Nabii Sulaiman katika kazi ya kuwalingania watu. Mara nyingi watawala hulewa tamaa ya kujilimbikizia madaraka na mali wakasahau wajibu wao mbele ya Muumba wao. Malkia wa Sabaa alidhani kwa kutumia mali angemtoa Nabii Sulaiman kwenye lengo lake. Lakini haikuwa hivyo.


 

Hali hiyo si kwa viongozi tu na wakuu wa nchi, bali hata sisi tulio katika harakati za Da'awah tuwe makini tusitolewe kwenye lengo kwa hongo ya mali au wadhifa.

 

Kifo cha Nabii Sulaiman


Pamoja na utukufu na umadhubuti wa ufalme wake Nabii Sulaiman muda wake wa kuishi ulipokwisha aliondoka kama walivyoondoka Mitume,wafalme na wanaadamu wengine. Aidha, historia inatuonyesha kuwa kifo chake kilikuwa ndio mwanzo pia wa kuanguka kwa himaya kubwa aliyokuwa ameijenga. Tunasoma katika Qur'an:

 

"Na Tulipomkidhia mauti (alipokufa) hakuna aliyewajulisha mauti yake ila mnyama wa ardhi, (mchwa) aliyekula fimbo yake. Basi ilipoanguka, majini walitambua kama wangalijua siri wasingalikaa katika adhabu hiyo idhalilishayo" (34:14).


 

Waliomfuatia Nabii Sulaiman waliendesha maisha ya anasa na ufisadi matokeo yake yakawa ni kuporomoka kwa ufalme kuliko pelekea kuwafanya majini yawe huru.

 

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Sulaiman(a.s)

Kutokana na histoira ya Nabii Sulaiman (a.s) tunajifunza yafuatayo

 

(i) Kila muumini anapotunukiwa neema na vipaji vikubwa
zaidi kuliko wengine anatakiwa amshukuru Allah(s.w) zaidi kwa kujitahidi kufanya wema zaidi na ibada maalumu za ziada kuliko watu wengine kwani hiyo ni amana na mtihani kwake. Hili aliliona Nabii Sulaiman(a.s) pale aliposema.

“………….Haya ni kwa fadhila za Mola wangu, ili anijaribu nitashukuru au nitakuwa mwizi wa fadhila, na anayeshukuru anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anayekufuru kwa hakika Mola wangu ni mkwasi, karimu (27:40)


 

- Mtume(s.a.w) katika kumshukuru Mola wake, alikuwa akisimama usiku mpaka miguuu yake ikawa inavimba. Maswahaba walipomrai kuwa asijitaabishe hivyo, kwani kashasamehewa madhambi yake yaliyopita naya baadaye, aliwajibu: “Ni siwe mja mwenye kushukuru? ”


 

(ii) Waumini wana dhima ya kuulingania Uislamu mijini na vijijini,ufike katika kila kona ya nchi na ulimwnegu kwa ujumla tukianzia kwenye familia zetu.


 

(iii) Kiongozi wa Harakati za Kiislamu katika jamii hanabudi kuwanamtandao wa waumini na wanaharakati watakao muwezesha kupata taarifa za hakika juu ya hali halisi ya Uislamu kutoka kila kona ya jamii husika.


 

(iv) Nguvu za elimu, Imani thabit,uchumi na nguvu za kujeshi ni nyenzo muhimu sana katika kusimamisha uislamu katika jamii.


 

(v) Hatunabudi kuzichunguza habari tunazozipata juu ya watu kabla ya kuzifanyia kazi- Nabii Suleiman hakumuamini Hud Hud moja kwa moja:-


“Akasema (Suleiman) Tutatazama kama unasema kweli au umo katika waongo. Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha uwaache, na utawatazama wanashauriana vipi” (27:27-28)


 

(vi) Baada ya kupa uhakika juu ya jambo ovu,mara moja tuweke mikakati ya kuliondoa kwa kutumia mbinu zinazostahiki.


 

(vii)Kutafuta ushauri kabla ya kufikia maamuzi ni katika sifa muhimu za kiongozi wa kiislamu.


 

(viii)Pamoja na kutafuta ushauri kwa wadau wa jamii yake, kiongozi mweledi ni yule anayeangalia mbali. Malkia wa Sabaa pamoja na kushauriwa na mawaziri wake kuingia vitani, hakupendelea kwa kuzingatia matokeo. Aliona saluhu ni bora zaidi kuliko vita (27:34 - 35).


 

(ix) Nikawaida ya viongozi wa kitwaghuut kuwahonga au kuwarubuni viongozi wa kiislamu kwa kuwakaribisha Ikulu, kuwapa mirunda ya pesa, magari,majumba, vyeo vya bandia n.k.


 

(x) Kiongozi au mwanaharakati wa kiislamu anayefanya biashara na Allah(s.w) kwa kutarajia pepo hahongeki au hawezi kurubuniwa kwa namna yoyote ile. Wanaohongeka ni wanafiki wanaopenda maisha ya dunia zaidi kuliko ya akhera.


 

(xi) Imekuwa ni tabia ya maadui wa kiislamu, wakiwemo wanafiki,kuwapakazia watu wema makosa mbalimbali na kuwaita majina mabaya ya kuwadhalilisha na kuwafadhehesha ili watu wasiwasikilize na kuwafuata. Hufanya hivyo ili kujenga mazingira ya kuwapoteza watu na Dini ya Allah(s.w)


 

(xii)Uchawi ni njia ya Shetani na ni haramu kwa muislamu kujifunza na kuifanyia kazi elimu ya uchawi.

- Waislamu wanaelekezwa na Mola wao kuwa mara kwa mara wajikinge na shari za wachawi, mahasidi na shari za viumbe wake wengine wanaoonekana na wasio onekana, kwa kusoma kwa mazinagiatio Suratul-Ikhlas na Al- muwadhatain(Al-Falaq na An-Nas).

           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-06-27 16:23:29 Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 80


Sponsored links
👉1 Kitabu cha Afya     👉2 kitabu cha Simulizi     👉3 Kitau cha Fiqh     👉4 Madrasa kiganjani    

Post zifazofanana:-

Histora ya Nabi Zakariya
Katika somo hili utakwenda ujfunza kuhusu hslistoria ya Nabi Zakariya Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Idrisa
Katika somohili utakwenda kujifunza historia ya Nabii Idrisa (amani iwe juu yake) Soma Zaidi...

Hstora ya Nab Ishaqa katika quran
Katika post hii tutakwenda kujifunza historia ya Mtume Ishaqa Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Adam
ata post h utawenda ujfunza hstora ya Nabii Adam ulngana na Quran navyoeleza Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Lut
Katika somo hili utakwenda kujifunza historia yaMtume Lut kutoka katika Quran Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Shu'aib
atika makala hii utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Shu'aib katika Quran Soma Zaidi...

Hstoria ya Nabi Daud
Katika somo hili utawenda ujifunza uhusu historia ya Mtume Daud Soma Zaidi...

hHistoria ya Nabii Dhul-kifl
Katika makala hii tutakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Dhul-kifl Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Yahya
Katika somo hili uatkwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yahya Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ayyuub
Katika somo hiliutakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii ayyuub Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Ilyasa
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Ilyasa Soma Zaidi...

Hstora ya Nab Sulaman
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Sulaman Soma Zaidi...