Navigation Menu



image

Historia ya Mtume Ibrahimu

Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Ibrahim katika quran

HISTORIA YA NABII IBRAHIIM(A.S) NA KUANDALIWA KWAKE:

Nabii Ibrahiim(a.s) ni Mtume wa Allah(s.w) aliyemfuatia Salih(a.s) katika wale waliotajwa katika Qur-an. Alizaliwa na kulelewa katika mji wa Ur huko Iraq. Baba yake,Azara,alikuwa akichonga masanamu na kuyauza kwa washirikina waliokuwa wakiyaabudu badala ya Allah(s.w). Hivyo ni wazi kuwa NabiiIbrahiim(a.s) aliletwa kwa jamii iliyozama katika giza la ushirikina.


 

Kuandaliwa kwa Nabii Ibrahiim(a.s)
Tangu angali mdogo, NabiiIbrahiim(a.s) aliyakinisha kuwepo kwa Allah(s.w) kwa kuchunguza dalili zilizomzunguka katika maumbile ya mbingu na ardhi. Baada ya kuyakinisha kuwepo kwa Allah(s.w), alichukua azma ya kumtii kwa unyenyekevu katika maisha yake yote kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:


 

“(Kumbukeni habari hii) Mola wake (Ibrahim) alipomwambia “Silimu” (Jisalimishe) akanena: Nimejisalimisha kwa Mola wa walimwengu wote”. (2:131)


 

Imani yake ya kweli juu ya Allah(s.w), ilimpelekea kuwa na tabia njema isiyo na mfano wake katika jamii kama tunavyojifunza katika Qur-an:

Hakika Ibrahim alikuwa Imamu (mfano mzuri wa wema wa kuigwa), mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, mtii kamili, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.(16:120)


 

(Alikuwa) mwenye kuzishukuru neema Zake (Mwenyezi Mungu zilizo juu yake), akamchagua na kumuongoza katika njia iliyonyooka. Na tukampa wema katika dunia; na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema (pia). (16:121-122)

“...........Kwa yakini Ibrahim alikuwa mwingi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu na mvumilivu”. (9:114)


 

“Na mtaje Ibrahim katika kitabu (hiki) bila shaka yeye alikuwa mkweli sana, Nabii.” (19:41)


 

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa NabiiIbrahiim(a.s) alikuwa Hanifa, yaani aliyejiepusha na Dini za upotevu na hakuwa mshirikina. Alikuwa mnyenyekevu kwa Allah(s.w) na mtii kamili. Alikuwa mwenye kushukuru neema za Allah(s.w), alikuwa mkweli, mwingi wa kurejea kwa Allah(s.w) na alikuwa mvumilivu. Pia alikuwa mwepesi katika kukirimu wageni kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:


 

“Na wajumbe wetu walimwendea Ibrahim kwa bishara, (njema) wakasema: “Salaam – amani”, akasema (Ibrahim). “Juu yenu pia iwe amani”. Na hakukaa (Ibrahim) ila mara alileta ndama (aliyechomwa vizuri).” (11:69)

 

Nabii Ibrahiim(a.s) Kumlingania Uislamu Baba Yake

 

Baada ya NabiiIbrahiim(a.s) kutoa shahada ya kweli alipomuahidi Mola wake: “Nimejisalimisha kwa Bwana Mlezi wa Walimwengu Wote” alianza kulingania Tawhiid kwa watu wa jamii yake. Kwa hekima aliona aanze kumlingania baba yake, aliyekuwa mchonga masanamu na kiongozi wa Ibada ya masanamu. Alianza kumlingania kwa kutumia hoja zenye mashiko katika akili ya mwanaadamu kama ifuatavyo:


 

(Wakumbushe) alipomwambia baba yake: “Ewe baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyosikia na visivyoona na visivyofaa chochote?” (19:42)


 

“Ewe baba yangu! Kwa yakini imenijia ilimu isiyokujia. Basi nifuate nitakuongoza njia iliyo sawa.(19:43)


 

Ewe baba yangu! Usimuabudu Shetani, hakika Shetani ni mwenye kumuasi (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa rehema.(19:44)


 

“Ewe baba yangu! Hakika naogopa kukupata adhabu inayotoka kwa Mwingi wa rehema (Mwenyezi Mungu), (ukifanya hivyo) utakuwa mwenziwe shetani.” (19:45)


 

Babu yake, badala ya kuyatia akilini aliyofikishiwa na mwanawe, alimkemea, kumtisha na badaye kumfukuzilia mbali nyumbani kwake.


 

“Akasema (yule baba yake) “Je! Unaichukia miungu yangu, ewe Ibrahim? Kama huachi (haya unayosema) lazima nitakupiga mawe. Na niondokelee mbali kwa muda mchache (huu).” (19:46)


 

Nabii Ibrahim(a.s)hakutetereka na kurudi nyuma alipofukuzwa nyumbani mwa baba yake. Alibakia na msimamo wake wa kulingania Dini ya Allah(s.w) kwa moyo mkunjufu huku akitarajia msaada kutoka kwake Allah(s.w) pekee.


 

“Na mimi nakuondokeeni (na kujiepusha) na mnayoyaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu. Hakika sitakuwa mwenye kukhibu (kukosa ninalotaka) kwa kumuomba Mola wangu.” (19:48).

 

Nabii Ibrahiim(a.s) Kuulingania Uislamu kwa Jamii Yake

 

Nabii Ibrahim(a.s), baada ya kupingwa mawe na kufukuzwa na baba yake mzazi, hakukata tamaa bali aliamua kuikabili jamii na kuifikishia ujumbe wa Uislamu kwa hekima kwa kutumia hoja madhubuti.


 


(Na kumbukeni) Ibrahimu alipomwambia baba yake Azara “Unawafanya masanamu kuwa waungu? Hakika ninakuona wewe na watu wako mumo katika upotofu (upotevu) ulio dhahiri.(6:74)


 


Na namna hivi tulimwonyesha Ibrahimu Ufalme wa mbingu na ardhi (kuwa ni wa Mwenyezi Mungu), na ili awe miongoni mwa wenye yakini.(6:75)


 

Na usiku ulipomwingilia (Ibrahimu na hali kakaa na makafiri) akaona nyota, alinena “(Nyota) hii ni Mola wangu.” Ilipotua (ikapotea), alisema (kuwaambia wale makafiri kama kwamba yu pamoja nao katika Ibada ile): “Sipendi waola wanaopotea (hawawepo ila wakati makhsusi tu).(6:76)


 

Na (usiku wa pili) alipouona mwezi unachomoza alisema: “Huu (mwezi) ndio Mola wangu.” Ulipotua alisema: “Asiponiongoza Mola wangu, bila shaka nitakuwa miongoni mwa watu wapotofu(Na Mola huyu hawezi kuniongoza kwani anakuwa hayupo wakati mwingine).” (6:77).


 


Na (siku ya tatu) alipoliona jua linachomoza alisema (kuwaambia): “Hili (jua) ndilo Mola wangu. Huyu Mola mkubwa kabisa.” Lilipotua alisema “Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayoyashirikisha (na Mungu).(6:78)


 

(Mimi) nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeziumba mbingu na ardhi. Hali ya kuwa nimewacha dini za upotevu. Mimi (ni Mwislamu) si miongoni mwa washirikina.” (6:79)

Watu wa jamii yake walimshangaa kwa msimamo wake wa kumpwekesha Allah(s.w) na kujadiliana naye kama ifuatavyo:


 


Na watu wake wakajadiliana naye (kwa kumwambia Unaacha Ibada ya wazee! Utadhurika)! Akasema: “Je, Mnanihoji juu ya Mwenyezi Mungu, mnaowashirikisha naye. Isipokuwa Mola wangu akipenda jambo (kuwa, basi litakuwa). Mola wangu anakijua vyema kila kitu. Basi je, hamshiki mauidha (6:80)


 

“Na nitawaogopaje hao mnaowashirikisha, hali nyinyi hamwogopi kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kile ambacho

hakukiteremshia dalili kwenu (yoyote ya kuonyesha kuwa ni mungu)? Basi kundi gani katika mawili haya (langu au lenu) linastahiki zaidi kupata amani? Kama nyinyi mnajua jambo (lijibuni hili).(6:81)


 

“(Hapana shaka kuwa) wale walioamini na hawakuchanganya imani yao na ushirikina kuwa hao ndio watakaopata amani, nao ndio walioongoka.(6:82)


 

Na hizi ndizo (baadhi ya) hoja zetu tulizompa Ibrahimu juu ya watu wake. Tunamyanyua katika vyeo yule tumtakaye (kwa kuwa anakwenda mwendo tunaoutaka). Hakika Mola wako ndiye Mwenye hikima (na) ndiye ajuaye. (6:83)

 

Allah(s.w) Amnusuru Ibrahim (a.s) na Hila za Makafiri

 

Pamoja na kudhihirikiwa na ukweli wa udhaifu wa miungu wa kisanamu, watu wa NabiiIbrahiim(a.s) hawakusilimu,badala yake wakapitisha hukumu ya kumteketeza kwa moto wakasema:

“Mteketezeni kwa moto na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo.” (21:68)

Allah(s.w) alimnusuru Mtume wake kwa kuuamrisha moto uwe “baridi na salama” kwa Ibrahim:

Tukasema:“Ewe moto! Kuwa baridi na salama juu ya Ibrahimu.” (21:69)

“Basi walitaka kumfanyia vitimbi (vya kumchoma moto) lakini tukawafanya wao kuwa wadhalilifu. Na Tulimuokoa yeye na Lut....... (21:70-71)


 

Nabii Ibrahiim(a.s) Kuhama Iraq

 

Nabii Ibrahiim(a.s) pamoja na jitihada zote alizozifanya za kuulingania Uislamu kwa hekima na kwa hoja madhubuti kwa baba yake, Mfalme na jamii kwa ujumla hakupata watu walioamini ila mkewe Sarah na mpwawe Lut(a.s). Kwa hali hiyo, Nabii Ibrahiim(a.s) baada ya kupata idhini ya Mola wake, alihama nchini mwake, Iraq, na kwenda katika nchi nyingine za Mashariki ya kati ili kulingania Uislamu humo. Alianza kuhamia Shamu (Syria).


 


“Basi Lut akamuamini na akasema (Ibrahiim). Hakika mimi nahamia katika (nchi aliyoniamrisha) Mola wangu, bila shaka yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.” (29:26) Na (Ibrahiim) akasema:Nakwenda. Mola wangu ndiye atakayeniongoza.” (37:99)


 

Nabii Ibrahiim(a.s) baada ya kuhama Iraq alizizungukia nchi nyingi za Mashiriki ya kati ikiwa ni pamoja na Misri, Palestina, Trans-jordan na Hijaz. Sehemu zote hizi aliweka vituo vya harakati alivyokuwa akivitembelea. Alimuweka mpwa wake, Lut(a.s),katika kituo cha T rans-jordan.Aliporuzukiwa watoto wema aliowaomba,Ismail(a.s) na Is-haq(a.s) aliwaingiza kwenye harakati,na akamfanya Ismail(a.s) mkuu wa kituo Hijaz na Is-haq(a.s) mkuu wa kituo cha Palestina. Allah(s.w) aliwateua viongozi hawa wa vituo vya harakati kuwa Manabii wa sehemu hizo na Mzee Ibrahiim(a.s) akiwa kiongozi wao.


 

Mji wa Makka katika nchi ya Hijaz alipokuwa akiishi Ismail (a.s), ulifanywa kuwa makao makuu ya harakati za kuhuisha Uislamu. Makka ilianza kutumika rasmi kama kituo kikuu cha harakati pale Mzee Ibrahiim (a.s) walipokamilisha kujenga upya Ka’abah na Allah(s.w) kumuamrisha awatangazie watu kuja kuhiji pale kila mwaka.


 


“Na Ibrahiim alipoinua kuta za nyumba (hii ya Al-Ka’abah) na Ismail (pia) (wakaomba wakasema:) “Ee Mola wetu! Tutakabalie (amali yetu hii ya kujenga huu msikiti). Hakika wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.” (2:127)


 


Na (kumbuka) tulipomkalisha Ibrahimu mahali penye ile Nyumba (takatifu na tukamwambia): “Usinishirikishe na chochote na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya waizungukao na wanaokaa hapo (kufanya ibada yao) na wanaorukuu na kusujudu, (wanaosali).” Na (tukamwambia) “Utangaze kwa watu habari za Hija, watakujia, (wengine) kwa miguu na (wengine) juu ya kila mnyama aliyekonda (kwa machofu ya njiani) wakija kutoka katika kila njia ya mbali. (22:26-27)

 

Ujumbe wa Nabii Ibrahiim(a.s) kwa Mfalme Namrudh

 

 

Nabii Ibrahim anavunja masanamu

NabiiIbrahiim(a.s) hakuishia kulingania Uislamu kwa baba yake na watu wa kawaida tu bali alisonga mbele na kumkabili Mfalme Namrudh kwa mjadala juu ya upweke wa Allah(s.w). Mfalme Namrudh alikuwa akiwanyonya na kuwadhulumu watu kama ilivyo kawaida ya watawala wa kitwaghuti kupitia kanuni na sharia za dini za kishirikina. Namrudh alijipa uungu kama inavyodhihiri katika majadiliano yake na Ibrahiim(a.s):


 

Hukumsikia yule aliyehojiana na Ibrahimu juu ya Mola wake kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa Ufalme? Ibrahimu aliposema: “Mola wangu ni yule ambaye huhuisha na hufisha,” yeye akasema: “Mimi pia nahuisha na kufisha.” Ibrahimu akasema: “Mwenyezi Mungu hulichomozesha jua mashariki, basi wewe lichomozeshe magharibi.” Akafedheheka yule aliyekufuru; na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu. (2:258)


 

Nabii Ibrahimu avunja masanamu

Ibrahim(a.s) Avunja Masanamu Kuwatanabahisha Washirikina. NabiiIbrahiim(a.s) alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake, kuwaonesha watu wake kwa hoja madhubuti udhaifu wa masanamu wanayoyaabudu badala ya Allah(s.w),


 

Na hakika tulimpa Ibrahimu uwongofu wake zamani na tulikuwa tukimjua (vizuri). (Wakumbushe alipowaambia watu wake): “Ni nini masanamu haya mnayakalia wakati wote (kuyaabudu)?” (21:51-52)


 

Wakasema, “Tuliwakuta babu zetu wakiyaabudu, (basi na sisi tunayaabudu).Akasema: “Bila shaka nyinyi na baba zenu mulikuwa katika upotofu (upotevu) ulio dhahiri.” Wakasema: “Je! Umetujia kwa (maneno ya) haki au umo miongoni mwa wachezaji?” (21:53-55)


 

Akasema:“(Siyo! Mimi si mchezaji) Bali Mola wenu ni yule Mola wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliyeziumba. Nami ni miongoni mwa wenye kuyashuhudia haya.” (21:56)


 

Na wasomee habari za (Nabii) Ibrahimu. Alipomwambia baba yake na kaumu yake: “Mnaabudu nini?” Wakasema: “Tunaabudu masanamu, daima tunawaabudu.” Akasema: “Je, yanakusikieni mnapoyaita?” (26:69-72)


 

Au yanakufaeni (mkiyaabudu) au yanakudhuruni (mkiacha kuyaabudu)?” Wakasema: “(Hayafanyi haya) lakini tumewakuta baba zetu wakifanya hivi.” Akasema: “Je, mumewaona hawa mnaowaabudu” “Nyinyi na wazee wenu waliotangulia?(26:73-76)


 


Bila shaka hao ni adui zangu (basi nitawadhuru. Mimi simuabudu) ila Mola wa walimwengu wote. Ambaye ameniumba na Yeye ananiongoza. Na ambaye ndiye anayenilisha na kuninywesha, (anayenipa chakula na kinywaji). Na ninapougua; Yeye ndiye anayeniponesha. Na ambaye atanifisha kisha atanihuisha. Na ndiye ninayemtumaini kwamba atanisamehe makosa yangu siku ya malipo.(26:77-82)


 

Alipoona watu wake hawamuelewi, Nabii Ibrahim (a.s) aliazimia kuvunja masanamu yao atakapopata mwanya ili kuwaonesha kwa vitendo udhaifu wa miungu wanayoiabudu. Alipopata fursa ya kuingia Hekaluni, bila ya kuonekana, aliyavunja masanamu yote yaliyokuwemo na kuacha lile kubwa lao.


 


“Oh! Kwa uzushi tu, miungu badala ya Mwenyezi Mungu – ndiyo mnayoitaka?” “Basi nini fikira yenu juu ya Mola wa walimwengu wote? (Mnamuona hatoshelezi ndio mnatafuta waungu wengine?)” Kisha akatazama mtazamo (mkubwa) katika nyota (akasema “Nitachukua fursa ya kuwajulisha uwongo wa Dini yao kwa kuwaonyesha kuchomoza kwake hizo nyota wanazoziabudu na kuchwa kwake).” Akasema: “Hakika mimi ni mgonjwa.” Nao wakamuacha, wakampa kisogo (wakenda zao viungani katika mandari zao). Basi alikwenda kwa siri kwa miungu yao akaiambia (kwa stihzai): “Muna nini? Mbona hamli? (Vyakula hivi vya mihanga mlivyowekewa?)” “Mumekuwaje! Hamsemi?” Kisha akawageukia kuwapiga kwa mkono wa kulia, (kwa mwisho wa nguvu zake). (37:86-93)


 

“Basi akayavunja vipande vipande isipokuwa lile kubwa lao (aliliacha) ili wao walirudie.” (21:58)


 


Watu wa Nabii Ibrahiim(a.s) walipokuta miungu yao imefanywa vile walihamaki.
Wakasema: “Nani aliyeifanya hivi miungu yetu? Hakika huyo yu miongoni mwa madhalimu (wakubwa)”. Wakasema: “Tulimsikia kijana mmoja akiwataja anayeitwa Ibrahimu.” Wakasema:“Basi mleteni mbele ya macho ya watu, wamshuhudie (kwa ubaya wake huo).”(21:59-61)


 

Makemeo yaIbrahiim(a.s) dhidi ya masanamu hayo, hayakuwa siri. Hivyo walimtuhumu kuwa ndiye aliyefanya kitendo hicho, wakamkamata na kumshitaki hadharani:


 

“Wakasema: Je! Wewe umeifanya hivi miungu yetu, ee Ibrahim? (21:62) Kwa kuulizwa swali hili Nabii Ibrahim (a.s) alipata fursa adhimu aliyokuwa akiitafuta:


 

Akasema: “Siyo, bali amefanya (hayo) huyu mkubwa wao, basi (muulizeni na) waulizeni (pia hao waliovunjwa) kama wanaweza kunena!” Basi wakajirudi nafsi zao, (wakafikiri udhalilifu wa waungu hao walio nao, wasioweza kujipigania) na wakasema: “Hakika nyinyi mlikuwa madhalimu (wa nafsi zenu kwenda kuwaabudu wasiokuwa na maana). Kisha wakainamisha vichwa nyao, (wakasema) “Hakika umekwishajua ya kwamba hawasemi (kwanini unatucheza shere?(21:63-65)


 

Akasema:“Je! Mnaabudu badala ya Mwenyezi Mungu (miungu) isiokufaeni chochote(mnapowaabudu)wala kukudhuruni (chochote mnapoacha kuwaabudu)?” Kefule (udhalilifu) yenu na ya hivyo mnavyoviabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu. Je! Hamfikiri? (21:66-67)

 

Ibrahiim(a.s) Aomba Kupata Kizazi Chema

 

Nabii Ibrahiim na mkewe Sarah walikaa mpaka wakawa wazee bila ya kupata mtoto. Ibrahim(a.s) alinyoosha mikono ya maombi kwa Mola wake, kuomba watoto wema watakao msaidia katika harakati zake za kusimamisha Uislamu katika jamii. Aliomba:


 


“Ee Mola wangu! Nipe (mtoto awe) miongoni mwa watenda mema.” Ndipo tukampa habari njema ya (kuwa atapata) mtoto mpole. (Basi akapata. Naye ndiye Nabii Ismaili). (37:100-101)


 

Aliamua kuoa mke wa pili, Hajirah, aliyekuwa mjakazi wa mkewe Sarah. Dua yake ilipokelewa na Hajirah akajifungua mtoto Ismail (a.s) akiwa mtoto wa kwanza wa Ibrahim (a.s). Baadaye pia Allah(s.w) alimruzuku mtoto wa pili, Is-haqa, kutoka kwa Sarah, wote wawili wakiwa wazee vikongwe:

“Tena tukambashiria (kumzaa) Is-haqa. Nabii, miongoni mwa watu wema (kabisa)” (37:112)


 


(Mkewe Ibrahiim akastaajabu) akasema: Ee mimi We! Nitazaa na hali mimi ni mkongwe, na huyu mume wangu ni mzee sana? Hakika hili ni jambo la ajabu.” Wakasema (wale wajumbe- Malaika): Je! Unastaajabu amri ya Allah? Rehema ya Allah na Baraka zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika (Allah) ndiye anayestahiki kusifiwa na kutukuzwa.” (11:72-73).


 

Nabii Ibrahiim(a.s) aliwalea watoto wake kiharakati na aliwausia kumcha-Allah na kuendeleza harakati mpaka mwisho wa maisha yao.


 


(Kumbukeni habari hii) Mola wake alipomwambia: “Nyenyekea;” akanena “Nimenyenyekea kwa Mola wa walimwengu (wote)”. Na Ibrahimu akawausia haya wanawe; na Yaakubu (pia akawausia wanawe): “Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuchagulieni Dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa wanyenyekevu.” (2:131-132)

 

Mitihani aliyopewa Nabii Ibrahimu kutoka kwa Allah

 

Tumeona katika historia yake kuwa Nabii Ibrahiim(a.s) alipata majaribu mengi katika harakati za kuhuisha Uislamu alipokuwa nchini mwake Iraq. Baba yake alimfukuza nyumbani na jamii nzima ikamtenga na kumuhukumu kuchomwa moto hadharani. Bila shaka alipata madhila ya aina hiyo hiyo alipokuwa amewalingania Uislamu washirikina wa nchi nyingine alimohamia. Kama hiyo haitoshi Allah(s.w) alimuongezea mingine miwili mizito.


 

Mtihani wa kwanza, ni pale alipoamrishwa na Mola wake, kujitenga na mkewe Hajira na mtoto wake mchanga, Ismail, na kuwaacha peke yao jangwani karibu na Ka’abah. Nabii Ibrahiim(a.s) alitii amri hii ya Mola wake na kutegemea msaada wake kwa familia yake huku akiomba dua ifuatayo:


 


“Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka (nimewakalisha baadhi kizazi changu (mwanangu Ismaili na mama yake, Hajrah) katika bonde (hili la Makka) lisilokuwa na mimea yoyote; katika nyumba yako takatifu (Al- Kaaba )Mola wetu! Wajaalie wasimamishe Sala. Na ujaalie nyoyo za watu zielekee kwao (wapende kuja kukaa hapa ili pawe mji) na uwaruzuku matunda ili wapate kushukuru.” “Mola wetu! Hakika wewe unajua tunayoyaficha na tunayoyadhihirisha. Na hakuna chochote kinachofichikana kwa Mwenyezi Mungu katika ardhi wala katika mbingu.” (14:37-38)


 

Mtihani wa pili na mzito zaidi ni pale Nabii Ibrahiim(a.s) alipoamrishwa na Allah(s.w) kuwa amchinje Ismail, mtoto wake mmoja pekee, aliyekuwa anamtarajia, amsaidie katika harakati za kusimamisha Uislamu. Vile vile katika hili Nabii Ibrahiim hakusita, bali alitii amri ya Mola wake na kulitekeleza kwa moyo mkunjufu. Pia mtoto wake Ismail, alikuwa radhi kwa hili kwa ajili ya kutafuta radhi za Mola wao.


 

“Basi (Ismail) alipofikia (makamu ya) kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ee Mwanangu! Hakika nimeona katika ndoto ya kwamba ninakuchinja. (Na ndoto za Mitume ni wahay). Basi fikiri, waonaje?” Akasema: Ee baba yangu! Fanya unavyoamrishwa utanikuta Insha-Allah miongoni mwa wanaosubiri.” (37:102)


 

Basi wote wawili walipojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu), na akamlaza kifudifudi (amchinje). Pale pale tulimwita: “Ewe Ibrahimu:” “Umekwishasadikisha ndoto. (Usimchinje mwanao).” Kwa yakini hivi ndivyo tunavyowalipa watendao mema. (37:103-105)


 

Bila shaka (jambo) hii ni jaribio lililo dhahiri, (mtihani ulio dhahiri). Basi tukamkomboa kwa mnyama wa kuchinjwa mtukufu. (37:106-107)

 

Nabii Ibrahiim(a.s) Afanywa Kiongozi wa Harakati za Uislamu Ulimwenguni

 

“Na (kumbukeni habari hii) Mola wake alipomfanyia mtihani (Nabii) Ibrahiim kwa amri nyingi; naye akazitimiza. Akamwambia: ‘Hakika mimi nitakufanya kiongozi wa watu (wote) (Ibrahim akasema): ‘Je, na katika kizazi changu pia?” Akasema: “(Ndio lakini) ahadi yangu haitawafikia madhalimu.” (2:124)


 

Katika aya hii tunajifunza kuwa NabiiIbrahiim(a.s) alipewa uongozi na kuwa mfano wa kuigwa na walimwengu wote baada ya kufaulu mitihani mingi na mizito iliyomthibitisha kwa ulimwengu kuwa alikuwa mnyenyekevu na mtii kamili kwa Allah(s.w).


 

“Hakika Ibrahiim alikuwa Imamu (mfano mzuri wa wema wa kuigwa), mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, mtii kamili, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.” (16:120)


 

Kutokana na dua yake, Mitume wote waliomfuatia wametokana na kizazi chake. Kupitia kwa Is-haqa(a.s) kuna Mitume wote wa bani Israil, kuanzia kwa Israil (Yaquub(a.s)) mwenyewe hadi kwa Nabii Issa(a.s) na kupitia kwa Ismail(a.s) tunaye Mtume Muhammad(s.a.w), ambaye ni Mtume wa mwisho na Mtume wa walimwengu wote kama alivyokuwa babu yake, Ibrahiim(a.s).Katika Qur-an tunahimizwa kufuata mila ya Nabii Ibrahiim:


 


Na nani atajitenga na mila ya Ibrahimu (akaichukia Dini hii ya Kiislamu) isipokuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Na kwa yakini sisi tulimchagua (Ibrahimu) katika dunia; na kwa hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema (kabisa). (Kumbukeni habari hii) Mola wake alipomwambia: “Nyenyekea:” Akanena “Nimenyenyekea kwa Mola wa walimwengu (wote)”. (2:130-131)


 

Na nani aliye bora kwa Dini kuliko yule ambaye ameuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye ni mwema, na anafuata mila ya Ibrahimu (kuwa Muislamu kweli kweli). Na Mwenyezi Mungu amemfanya Ibrahimu kuwa ni kipenzi chake. (4:125)


 

Mila yaIbrahiim(a.s) inayosisitizwa hapa si nyingine ila ni kuwa “Mnyenyekevu na mtii kamili” kwa Allah(s.w), kiasi cha mtu kuwa tayari na kwa moyo mkunjufu kumchinja mwanawe aliye mwema na anayempenda na kumtarajia sana. Pia kufuata mila ya Ibrahim ni kuwa tayari kufanya juhudi za kusimamisha Uislamu katika jamii na kutokomeza ushirikina bila ya kujali lolote litakalotokea hata kama ikibidi kugombana na kutengana na jamii nzima.


 

Hakika nyinyi muna mfano mzuri (wa kuiga) kwa Ibrahimu na wale waliokuwa pamoja naye, walipowambia jamaa zao (makafiri). “kwa yakini sisi tu mbali nanyi, na mbali na hayo mnayoyaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu; tunakukataaeni, umekwisha dhihiri uadui na bughudha ya daima baina yetu na nyinyi mpaka mtakapomuamini Mwenyezi Mungu peke yake....…” (60:4)

Ili kujikurubisha na mila ya Ibrahimu, Allah(s.w) ametuamrisha na kutufundisha kupitia kwa Mtume(s.a.w) kuwa tumuombee (tumswalie) Mtume na kujiombea sisi wenyewe kwa kusema:


 

“Ee Allah! Mrehemu Muhammad na wafuasi wa Muhammad kama ulivyomrehemu Ibrahim na wafuasi wa Ibrahim. Hakika wewe u mtukufu na msifiwa wa haki. Ee Allah! Mbariki Muhammad na wafuasi wa Muhammad kama ulivyombariki Ibrahim na wafuasi wa Ibrahiim. Hakika wewe u mtukufu na msifiwa wa Haki”.

 

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Ibrahiim(a.s)

Tukimchukua Nabii Ibrahimu kama kiongozi wa kuigwa katika harakati za kuhuisha na kusimamisha Uislamu katika jamii tunajifunza yafuatayo:


 

(i) Mwanaharakati hanabudi kujitakasa yenye binafsi na kuwa mnyenyekevu na mtii kamili kwa Allah(s.w) kabla ya kuiendea jamii.


 

(ii) Hatunabudi kuanza kulingania familia zetu kabla ya kuiendea jamii-Nabii Ibrahim alianza kumlingania baba yake Azara.


 

(iii) Tulinganie Uislamu kwa kutumia hoja madhubuti na mbinu mbali – Qur-an (16:125).


 

(iv) Tulinganie Uislamu kwa watu wa kada zote – kwa raia wa kawaida wa mijini na vijijini, wasomi na maofisa katika sekta mbalimbali na viongozi wa jamii katika ngazi mbalimbali kwa kupanga na kutumia fursa zinazojitokeza – Nabii Ibrahim (a.s) alihojiana na mfalme Namrudh.


 

(v) Tusimchelee yeyote katika kulingania Uislamu.


 

(vi) Tuwe tayari kukabiliana na machungu ya kutengwa na familia na jamii kwa ujumla kwa ajili ya kusimamisha Uislamu.


 

(vii) (a)Tuwe – tayari kutoa nafsi zetu, nafsi za wapenzi na wandani wetu kwa ajili ya Allah(s.w) – Qur-an (9:111).


 

(b) Tumpende Allah(s.w) na Mtume wake na kupigania dini yake kuliko tunavyopenda nafsi zetu na jamaa zetu wa karibu. Qur-an (9:23:24), (58:22).


 

(viii) Tuwe na vituo vya harakati vya kistratejia na tuwe na viongozi madhubuti katika vituo hivyo.


 

(ix) Tufanye harakati za kuhuisha na kusimamisha Uislamu katika jamii kistratejia.


 

(x) Tuwe tayari kuhama makazi yetu tuliyoyazoea, kuhamia maeneo ya kistratejia kwa ajili ya kuhuisha na kusimamisha Uislamu katika jamii.


 

(xi) Tuandae vizazi vitakavyoturithi katika harakati – Nabii Ibrahim(a.s)aliomba watoto wema watakaomrithi katika harakati.


 

(xii) Tuzihusishe familia zetu katika harakati – Bi Hajarah aliridhia kubaki mwenyewe Makka na kitoto chake kichanga kwa ajili ya kutii amri ya Allah(s.w).


 

(xiiii)Tuwahusishe jamaa zetu wa karibu katika harakati – Nabii Ibrahim(a.s) alihama kutoka Iraq na mpwa wake Lut (a.s) na kumfanya kuwa kiongozi wa kituo cha harakati cha Transjordan.


 

(xiv) Tuwe wepesi wa kumuelekea Allah(s.w) kwa maombi mbalimbali ya kuomba msaada wa Allah(s.w) na kumshukuru kama alivyokuwa akifanya NabiiIbrahiim(a.s) Qur-an.(37:100-101) (14:39)


 

(xv) Tumuombe Allah(s.w) aturehemu na kutubariki kama alivyomrehemu na kumbariki Nabii Ibrahim (a.s) kwa kumswalia Mtume(s.a.w) mara kwa mara kama tukavyo mswalia katika swala.






           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-06-26 09:37:37 Topic: visa vya Mitume Main: Masomo File: Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 389


Sponsored links
👉1 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)     👉2 Kitau cha Fiqh     👉3 Kitabu cha Afya     👉4 Simulizi za Hadithi Audio     👉5 Madrasa kiganjani     👉6 kitabu cha Simulizi    

Post zifazofanana:-

Historia ya Mtume Ibrahimu
Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Ibrahim katika quran Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Hud katika Quran
Katika makala hii utakwenda kujifunzahistoria ya Mtume Hud katika Quran Soma Zaidi...

Hstoria ya Nabi Daud
Katika somo hili utawenda ujifunza uhusu historia ya Mtume Daud Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Al-yasa’a
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Mtume Al-yasa'a Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Muhammad (s.a.w) wa ufup
Huu n ufupisho wa Historia ya Mtume Muhammad s.a.w. Tumekuandalia histori hii kwa urefu zaidi kwenye Makala zetu zinazofuata Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ismail katika quran
KKatika somohili utakwenda kujifunzahistoriaya Mtume Ismail Mtoto wa Nabii Ibrahim Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Nuhu katika Quran
Katika somo hili utakwenda kujifunza historia ya Mtume Nuhu kulingana na melezo yaliyo kwenye Quran Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Musa
atika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Musa Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Yunus
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yunus Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ayyuub
Katika somo hiliutakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii ayyuub Soma Zaidi...

Hstoria ya Nabii Yusuf
Katika makala hii utakwenda ujfunzakuhusu historiaya Nabii Yufuf katika Quran Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Swaleh (Salih)
Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Swalehe katikaQuran Soma Zaidi...