Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu Historia ya Nabii Isa
Nabii Isa(a.s) huitwa “Yesu”, na “Jesus” katika Biblia ya Kiswahili na Kiingereza. Majina yote hayo matatu yanamkusudia mwana wa Maryamu aliyezaliwa bila baba, ambaye ni Mtume wa mwisho kwa Bani Israil.
Nabii Isa(a.s) ni mtoto wa Maryamu aliyekuwa mwana wa Imraani. Kizazi cha Imraani kilichaguliwa na Allah(s.w) kupewa Utume kama tunavyofahamishwa:
Hakika Mwenyezi Mungu alimchagua Adamu na Nuhu na kizazi cha
Ibrahiimu na kizazi cha Imraani juu ya walimwengu wote(3:33)
Mke wa Imraani aliweka nadhiri kwa Allah(s.w) kuwa mtoto atakayemzaa atamuweka wakfu. Alitarajia kuwa atazaa mtoto wa kiume.
Aliposema mke wa Imraani: “Mola wangu! Nimeweka nadhiri kwako aliye tumboni mwangu kuwa wakfu, basi nikubalie, bila shaka Wewe ndiye usikiaye na ujuaye.(3:35)
Basi alipomzaa alisema: “Mola wangu! Nimezaa mwanamke”- Na Mwenyezi Mungu anajua sana aliyemzaa -”Na mwanaume si sawa na mwanamke. Na nimempa jina Maryam. nami namkinga kwako, yeye na kizazi chake, uwalinde na shetani aliyewekwa mbali na rehema zako (3:36)
Baada ya kupigwa kura juu ya nani awe mlezi wa Maryam, Nabii Zakaria akachaguliwa kuwa mlezi wa Maryam. Allah(s.w) akaikubali ile nadhiri na dua ya mama yake Maryam.
Basi Mola wake akampokea (mtoto) kwa mapokezi mema na akamkuza kwa makuzi mema, na akamfanya Zakaria awe mlezi wake. Kila mara Zakaria alipoingia chumbani(kwa Maryam) alikuta vyakula pamoja naye. Akauliza: “Ewe Maryam! Unapatawapi hivi? Akajibu: “Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila kutarajia(3:37)
Aya hizi zinatuonesha kuwa Maryam alikuwa katika malezi mema na uangalizi wa karibu toka kwa Nabii Zakaria(a.s) kiasi cha kuepusha mazingira ya ufuska yasimfikie.Allah(s.w) aliweka maandalizi haya mapema ili atakapoleta muujiza wake kwa Maryam kuzaa mtoto bila ya kuwa na mume isionekane kuwa alikuwa mzinifu, bali iwe ni dalili ya kuwepo Allah(s.w) mwenye nguvu na uwezo wa kila kitu.
Kutokana na mazingira hayo na hifadhi ya Allah(s.w) Maryam akakua vyema na kupata hadhi ya kuwa mwanamke bora kuliko wanawake wote:
“Na (kumbuka) Malaika waliposema: “Ewe Maryamu! Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuchagua na kukutakasa na kukutukuza kuliko wanawake wa ulimwengu (wote).(3:42)
Baada ya maandalizi hayo ya kimalezi pamoja na hifadhi ya Allah(s.w) aliyopewa Maryam, Allah(s.w) akamtuma Malaika kumueleza Bi Maryam habari za kumzaa masihi, Isa(a.s) bila ya baba ila kwa amri ya Allah(s.w) ya “Kuwa ikawa”. Malaika akamwambia:
Ewe Maryam! Mwenyezi Mungu anakupa habari njema (za kumzaa mtoto kwa) neno litokalo kwake. Jina lake Masihi Isa bin Maryam, mwenye heshima katika dunia na akhera, na ni miongoni mwa waliotukuzwa.(3:45) Naye atazungumza na watu katika utoto na katika utu uzima wake, na ni katika watu wema (3:46)
Maryam Akasema:Mola wangu! Nitapataje Mtoto hali mtu yoyote hakunigusa? Akajibu: Ndivyo, vivyo hivyo; Mwenyezi Mungu huumba anavyopenda: anapohukumu jambo, huliambia ‘Kuwa’, likawa(3:47) Na Mwenyezi Mungu atamfunza kitabu na hekima, na kujua Taurati na
Injili. Na ni Mtume kwa wana wa Israili...................(3:48-49)
Allah(s.w) anatueleza kuwa Nabii Isa(a.s) alizaliwa chini ya mtende, na wala hakuzaliwa kwenye zizi la ng’ombe lenye najisi kama wanavyodai katika Biblia.
Basi (Maryam)akachukua mimba yake, na akaondoka nayo mahali pa mbali. Kisha uchungu ukampeleka katika shina la mtende, akasema: “Laiti ningekufa kabla ya haya, na ningekuwa niliyesahaulika kabisa. (19:22-23)
Mara ikamfika sauti kutoka chini yake inamwambia: “Usihuzunike”. Hakika Mola wako amejaalia kijito cha maji chini yako”. Na litikise kwako shina la mtende, litakuangushia tende nzuri, zilizo mbivu. (19:24-25) Basi ule na unywe litue jicho lako.(19:26)
Maryam akamtwaa mwanawe, akaenda naye kwa jamaa zake amembeba. Watu wakastaajabu na kuwaza, imewezekanaje Maryam asiye mzinzi kumpata mtoto bila kuolewa. Na wengine wakauliza:
...............“Ewe Maryam! Hakika umeleta jambo la ajabu: Ewe dada yake Haruni! Baba yako hakuwa mtu mbaya wala mama yako hakuwa hasharati (19:27-28)
Kwa maswali hayo, ikawepo haja ya kumtakasa Maryam kuwa japo hakuolewa, hakumpata mtoto huyo kwa zinaa. Ndipo ikatimia kauli ya Allah(s.w) kuwa Nabii Isa(a.s) atazungumza akiwa kichanga.
Maryam akaashiria kwake (yule mtoto wamuulize yeye). Wakasema:“Tutazungumzaje na aliye bado mtoto kitandani? (19:29)
(Yule mtoto) akasema: “Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, Amenipa kitabu na Amenifanya Nabii. Amenifanya mbarikiwa popote nilipo. Na ameniusia swala na zaka maadamu ni hai. (19:30-31)
Na ameniusia kumfanyia wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, muovu. Na amani iko juu yangu siku niloyozaliwa, siku nitakayokufa na siku nitakapofufuliwa kuwa hai(19:32-33)
Mtume Isa(a.s.)alipewa Utume na kuamrishwa kufikisha ujumbe wa Allah(s.w) kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israil. Akibainisha juu ya jambo hili, Nabii Isa(a.s) alisema: “............Enyi wana wa Israili; Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati na kutoa habari njema ya Mtume atakayekuja nyuma yangu ambaye jina lake litakuwa Ahmad. (61:6).
Na katika Biblia tunafahamishwa kuwa Nabii Isa(a.s)alisema kauli hiyo kwamba yeye ni Mtume kwa wana wa Israili tu. Ukweli huu unajitokeza pale Yesu alipojibu, akisema: Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israili(Mathayo 15:21-24)
(i) Mungu ni mmoja,wapekee,si watatu,na yeye si Mungu
Kwanza kabisa, Nabii Isa(a.s) aliwataka watu wamjue na kumuamini Mwenyezi Mungu mmoja aliye wa pekee, na kuwataka wakubali kuwa yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akawaambia:
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu na ni Mola wenu. Basi mwabuduni. Hii ndiyo njia iliyonyooka (3:51)
Ujumbe huu wa Nabii Isa, unapatikana pia katika Biblia. Nabii Isa amenukuliwa katika Bibilia akifundisha Wana wa Israili kuwa yeye si Mungu, ila ni Mtume, na kwamba Mwenyezi Mungu ni mmoja, wapekee na ndiye Mungu wa kweli.
Na uzima wa milele ndiyo huu, wakujue wewe Mungu wa pekee wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma. (Yohana 17:3)
Maneno haya ya Nabii Isa(a.s) yanatuonesha ukweli kuwa yeye si mungu, na wale wanaong’ang’ania kumwita, Yesu ni mungu, hawayafuati mafundisho yake, bali wanafuata uzushi wa mafundisho na maagizo ya wanadamu. Hili analithibitisha Yesu katika Biblia:
Enyi wanafiki, ni vyema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema,Watu hawa wananiheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami. Nao wananiabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu.(Mathayo 15:7-9)
(ii) Hakuna dhambi ya asili
Yesu amefundisha kuwa kila mwanadamu huzaliwa akiwa huru pasina tone lolote la dhambi, na kwamba watoto ndio wakuu katika Ufalme wa mbinguni na Ufalme wa mbinguni ni wao.Na hakuna yeyote atakayeingia katika Ufalme wa mbinguni(peponi) ila atakayejitahidi kutotenda maovu, na kujitahidi kufanya mema akawa safi kama mtoto.
Saa ile wanafunzi wake wakamwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika Ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amini, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika Ufalme wa mbinguni. Basi yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika Ufalme wa mbinguni(Mathayo 18:1-4)
Na katika maandiko mengine ya Biblia, tunasoma: Yesu akasema: Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, Ufalme wa mbinguni ni wao(Mathayo19:14)
Kutokana na mafundisho haya ya Yesu, hakuna mtu yeyote muovu atakayeingia katika Ufalme wa mbinguni (Peponi), kwa kuamini kwamba Yesu kafa msalabani kwa ajili ya dhambi zake.
(iii)Waumini wanatakiwa kufuata sheria za Mwenyezi Mungu kwa kuweka Ufalme wake hapa duniani
Nabii Isa(a.s) aliwafundisha watu wamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake katika kila kipengele cha maisha yao. Na kwamba njia ya maisha yenye kuleta amani ya kweli na maisha ya furaha ni kufuata sheria za Mwenyezi Mungu na kuacha mafundisho ambayo ni maagizo ya wanadamu. Katika Qur,an tunafahamishwa kuwa aliwaambia Waisraili. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu na ni Mola wenu. Basi mwabuduni. Hii ndiyo njia iliyonyooka. (3:51)
Na katika Biblia, amenukuliwa akiwataka watu wamuombe Mwenyezi Mungu awezeshe Ufalme wake ustawi duniani kama ulivyo stawi mbinguni ili dunia isitawaliwe na kuongozwa kwa sheria zistawishazo ufuska na ufisadi katika jamii. Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni; Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, hapa duniani kama mbinguni (Mathayo 6:9-10)
Mwenyezi Mungu pekee ndiye aliyewawezesha Mitume na Manabii kufanya miujiza. Allah(s.w) aliwapa mitume miujiza ili kuwa dalili ya kuwathibitishia watu kuwa yeye ndiye aliyewatuma. Hakuna Mtume au Nabii aliyedai kufanya miujiza kwa uwezo wake mwenyewe. Na hivi ndivyo Nabii Isa alivyowaambia wana wa Israili.
.........Nimekujieni na hoja kutoka kwa Mola wenu, ya kwamba nakuumbieni, katika udongo, kama sura ya ndege, kisha nampuliza, mara anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu na wenye mabalanga, na ninawafufua waliokufa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na nitakuambieni mtakavyo vila na mtakavyo weka akiba katika nyumba zenu. Bila shaka katika haya imo hoja (ya kuonesha kuwepo Mwenyezi Mungu) kwenu ikiwa ni watu wa kuamini(3:49)
Ni dhahiri kuwa miujiza yote aliyoifanya Nabii Isa(a.s), aliifanya kwa lengo la kuwathibitishia watu kuwa yeye ametumwa na Mwenyezi Mungu. Katika Biblia, Yesu alibainisha hili wazi kabla hajafanya muujiza wa kumfufua Lazaro:
Yesu akainua macho yake juu, akasema: Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia siku zote; lakini ni kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kuwa ndiwe uliyenituma. Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake umefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake (Yohana 11:41-44)
Kwa kuzingatia maandiko haya, utabaini kuwa hawasemi kweli wale wanaodai kuwa Yesu ni Mungu eti kwasababu alifanya miujiza ya kufufua wafu.
Nabii Isa(a.s) alipoona ukaidi wao umeshitadi, akatoa wito maalum kwa wanafunzi wake ili wajitokeze wale watakaokuwa tayari kuwa naye bega kwa bega kupambana na madhalimu na kuufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa wengine. Hivyo, akawauliza:
Lakini Isa alipoona ukaidi wao, alisema: Nani watakuwa wasaidizi wangu katika kumtangaza Mwenyezi Mungu (mmoja)? Wanafunzi wakasema: “Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemwamini Mwenyezi Mungu na ushuhudie kwamba sisi tumejisalimisha. Mola wetu! Tumeyaamini uliyoyateremsha na tumemfuata Mtume, basi tuandike pamoja na washuhudiao (3:52-53)
Baada ya hapo, wanafunzi wa Nabii Isa (a.s) wakamtaka awaombee chakula maalumu kutoka kwa Allah(s.w), wakasema:
Ewe Isa Mwana wa Maryam! Je Mola wako anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni? Akasema(Nabii Isa), “Mcheni Mwenyezi Mungu kama kweli ninyi ni wenye kuamini kweli(5:112) Wakasema: “Tunataka kula katika hicho, na ili nyoyo zetu zitulie na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia(muujiza huo)(5:113) Akasema Isa bin Maryamu: “Ewe Mwenyezi Mungu, Mola wetu! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu, na wa mwisho wetu, na kiwe Ishara itokayo kwako, basi turuzuku, kwani wewe ndiye mmbora wa wanaoruzuku(5:114)
Mwenyezi Mungu akasema: “Bila shaka Mimi nitakiteremsha juu yenu, lakini miongoni mwenu atakayekataa baada ya haya, basi Mimi nitamuadhibu adhabu ambayo sijamwadhibu yoyote katika walimwengu(5:115)
Njama za kutaka kumuua Nabii Isa(a.s) zilianza kwa kumuuliza maswali ya kumtega na kumfitinisha kwa Serikali ili imuone kuwa anachochea watu wasilipe kodi na kuhatarisha maslahi ya wakubwa Serikalini. Fitina hizi zilifanywa na Mafarisayo na Makuhani, wakamwendea Yesu wakisema:
Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yeyote, kwa maana hutazami sura za watu. basi utuambie waonaje? Ni halali kumpa kaisari kodi, ama sivyo? (Mathayo 22:16-17)
Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema:
Mbona mnanijaribu enyi wanafiki? Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu (Mathayo 22:18-21)
Baada ya hila hizi kushindwa, zikapangwa njama za kutaka kumuua.
Basi wakuu wa Makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu anafanya ishara nyingi.Tunamwachia hivi, watu wamwamini. Yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie Taifa zima(Mathayo11:47-48,50)
Nabii Isa(a.s) alimuomba Allah(s.w) amlinde na shari za watu wabaya waliopanga njama dhidi yake. Yesu alikwenda bustani ya Gestmane kuomba. Alipofika, akawaambia wanafunzi wake:
Roho yangu ina huzuni kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.(Mathayo 26:38 39)
Mwenyezi Mungu alikubali dua ya Nabii Isa (a.s) kwa kumuhakikishia kuwa atamlinda dhidi ya njama za watu madhalimu.
“Mwenyezi Mungu aliposema: “Ewe Isa! Mimi nitakukamilishia muda wako wa kuishi na nitakuleta kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru, na nitawaweka wale waliokufuata, juu ya wale waliokufuru mpaka siku ya kiama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu,Nitakuhukumuni katika yale mliyokuwa mkihitilafiana”(3:55)
Katika mahubiri yake huko nyuma, Nabii Isa (a.s) aliwasisitiza sana watu kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa kumuomba msaada. Aliwaambia:
Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona, naye abishaye hufunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, Je! si zaidi Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? (Mathayo 7:7-11)
Kwa mujibu wa Yesu mwenyewe, Mwenyezi Mungu humsikiliza maombi yake na kumkubalia daima. Hebu na tuyarejee maneno yake aliyoyasema pale alipoomba jambo kubwa la kumfufua Lazaro:
Yesu akainua macho yake juu, akasema: Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia siku zote; lakini ni kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kuwa ndiwe uliyenituma. Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake umefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.
(Yohana 11:41-44)
Ndiyo kusema kuwa ikiwa Yesu ametangaza kuwa,”Ombeni, nanyi mtapewa”, Na kwakuwa Mungu, huwapa “mema wao wamwombao”, na Yesu mwenyewe anakiri kuwa Mungu anamsikia siku zote, haiwezekani kabisa asulubiwe hali ya kuwa Mungu yupo na alishamuomba!
Katika Qur,an tukufu, Mwenyezi Mungu aliye muweza na mjuzi wa mambo anathibitisha kuwa aliyesulubiwa si Nabii Isa(a.s):
Na kwa kusema kwao: “Sisi tumemuua Masihi Isa, mwana wa Maryam Mtume wa Mungu”, hawakumuua wala hawakumsulubu ila walibabaishiwa (mtu mwingine aliyefananishwa na Nabii Isa). Na hakika wale waliokhitilafiana katika hayo wamo katika shaka nalo. Wao hawana yakini juu ya hili, isipokuwa wanafuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumuua(4:157).
Bali Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwake, Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima (4:158)
Hukumu ilipitishwa Nabii Issa auawe kwa kusulubiwa. Lakini Allah(s.w)alimnusuru na badala yake akasulubiwa Yuda msaliti aliyefananishwa naye kwa sura na sauti. Kwa hiyo aliyesulubiwa si Yesu bali ni Yuda aliyemsaliti Yesu kama inavyotueleza kwa uwazi Injili ya barnabas katika sura ya 214, 215, 216 na 217.
“Yesu akatoka nje ya nyumba, akaenda bustanini kusali, kama ilivyokuwa ada yake kusali, kwa kurukuu mara mia na kusujudu kwa paji lake la uso. Yuda, ambaye alipajua mahali alipokuwa Yesu na wanafunzi wake, akaenda kwa kuhani mkuu, na akanena: “Ukinipa kilichoahidiwa, nitakupa mkononi mwako Yesu mnayemtafuta: Kwani yu pekee na wanafunzi kumi na moja’.
Kuhani mkuu akajibu: “Wataka kiasi gani?’ Akasema Yuda, “Vipande thalathini vya dhahabu.”
Kisha papo hapo kuhani mkuu akamuhesabia pesa hizo, na akamtuma Mfarisayo kwa gavana kuchukua askari na kwa Herodi, na Wakatoa kikosi chao, kwani waliwahofia watu; wakachukua silaha zao na huku wakiwa na kurunzi na taa ya bakora zao, wakatoka nje ya Yerusalemu.
Askari waliokuwa pamoja na Yuda walipokaribia mahali alipokuwa Yesu, Yesu alisikia kishindo cha watu wengi wakija, naye kwa hofu akaingia ndani ya nyumba. Na wale wanafunzi kumi na moja walikuwa wamelala.
Kisha Mwenyezi Mungu kwa kuiona hatari iliyomkabili mja wake, akamwamuru Jibrili, Mikaili, Rafaili na Urieli, watumishi wake wamuondoshe Yesu ulimwenguni.
Malaika watakatifu wakaja na wakamtoa Yesu nje kupitia katika dirisha la upande wa Kusini. Wakambeba na kumweka katika mbingu ya tatu akiwa katika kundi la Malaika wanaomsabihi Mwenyezi Mungu daima.
Yuda akatangulia kuingia kwa ufidhuli, kabla ya wote katika kile chumba ambacho Yesu alikuwamo. Wanafunzi walikuwa wamelala. Hapo Mwenyezi Mungu Mwingi wa miujiza akafanya muujiza, kwani akambadilisha Yuda kwa sauti na sura akawa kama Yesu hadi tukaamini kuwa alikuwa ni Yesu. Naye baada ya kutuamsha akatuuliza Bwana Yesu aliko. Ndipo tukastaajabu na kumjibu: ‘Wewe, bwana ndiye bwana wetu; je, sasa umetusahau?’
Hisia za wanafunzi wa Yesu kama zilivyoelezwa katika Injili ya Barmabas zinafanana na zilizoelezwa katika Injili nyingine. Injili ya Barnabas yasema kama ifuatavyo na hatua za mwisho za kusulubiwa kwa Yuda Iskariot badala ya Yesu:
“Makuhani Wakuu pamoja na waandishi wa Wafarisayo, walipoona kuwa Yuda hakufa kwa mateso waliyomfanyia na kwa kuhofia kuwa Pilato aweza kumwacha kutundikwa Msalabani. Hivyo wakamhukumu Yuda pamoja na maharamia wawili wafe pamoja naye kifo cha msalabani. Hivyo wakampeleka kwenye Mlima wa Kalvari ambako walikuwa wakinyongwa watu waovu. Wakamsulubisha uchi, ili kumdhalilisha zaidi. Yuda hakufanya chochote isipokuwa kulalamika, “Mwenyezi Mungu kwanini umenitupa, mwovu ametoroka nami nafa, waandishi wa wafarisayo wamchukue Yuda kama mhalifu anayestahili kifo cha msalabani pasi na haki?
Amini nasema kwamba sauti sura na umbo la Yuda vilifanana mno na Yesu kiasi ambacho wanafunzi wake na waumini wengine waliamini kuwa ni Yesu. Hivyo baadhi yao wakayawacha mafundisho ya Yesu kwa kuamini kuwa Yesu alikuwa yu Nabii wa uwongo, na kwamba alifanya miujiza kwa hila za uchawi kwani Yesu aliesema kuwa hatakufa hadi karibu na mwisho wa ulimwengu. Lakini wale waliosimama imara katika mafundisho ya Yesu walisononeshwa sana nyoyo zao kumwona yule aliyefanana kabisa na Yesu (katika hali ile) na wakasahau aliyosema Yesu. Mungu atamfisha karibu na mwisho wa ulimwengu. Ukiwaondoa wafuasi ishirini na watano waliokimbilia Damascus, wengine wote kati ya wale wafuasi 72 walimwona na walikula pamoja na Yesu. Hata hivyo Yesu aliitumia fursa hiyo pia kuwakemea wale ambao waliamini kuwa yeye alikuwa amekufa na kufufuka. “Na aliwakemea wengi ambao waliamini kuwa yeye alikuwa amekufa na kufufuka kwa kusema: ‘Je, mnadhani kuwa mimi na Mwenyezi Mungu tu waongo? Kwani Mwenyezi Mungu amenijaalia mimi kuishi hadi karibu na mwisho wa ulimwengu, kama nilivyokwishakuwaambia. Amin, Amin nawaambia, sikufa bali (alikufa) Yuda, Msaliti. Jihadharini, kwani shetani atafanya kila jitihada kukudanganyeni. Basi kuweni mashahidi wangu kwa Israeli yote na kwa ulimwengu wote kwa yote mliyoyasikia na
kuyaona.” Baada ya kusema hayo alimwomba Mwenyezi Mungu awajaalie waumini uokovu, na awajaalie waasi toba. Na alipomaliza dua yake akamkumbatia mama yake, na kusema:
‘Amani iwe juu yako, wewe mama yangu, tulizana kwa Mwenyezi Mungu aliyekuumba wewe na mimi! Baada ya kusema hivyo aliwageukia wanafunzi wake na kusema: ‘Rehema za Mwenyezi Mungu na amani ziwe juu yenu! “Nao wakashuhudia kwa macho yao Malaika wane wakimchukua Yesu hadi mbinguni.” (Injili ya Barnabas, sura ya 221)
Maelezo haya ya Barnabas, aliyekuwa miongoni mwa wale wanafunzi kumi na moja waliokuwa pamoja na Yesu yanathibitishwa na Qur-an pale Allah(s.w) anapotufahamisha:
Na kwa kusema kwao: “Sisi tumemuua Masihi Isa, mwana wa Maryamu Mtume wa Mungu”, hawakumuua wala hawakumsulubu ila walibabaishiwa (mtu mwingine waliyemdhani Nabii Isa). Na hakika wale waliokhitilafiana katika hayo wamo katika shaka nalo. Wao hawana yakini juu ya hili, isipokuwa wanafuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumuua Bali Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwake; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na mwenye hekima.” (4:157-158)
Hapa pana fundisho kubwa kwa kila mwenye kupigania na kusimamisha haki. Mateso na magumu yanayompata mtu katika kazi hii isiwe ni sababu ya kukata tamaa. Bali imzidishie imani na kumtegemea zaidi Allah(s.w). Na hatima ya mambo yote ni ushindi kwa waliosimama katika haki.
Pamoja na Isa(a.s) kufundisha tawhiid kwa kauli na vitendo; baada ya kuondoka kwake, mafundisho yake yalipotoshwa. Sura ya 222 ambayo ni ya mwisho katika Injili ya Barnabas inaeleza kama ifuatavyo juu ya kilichotokea baada ya Yesu kuondoka:
“Baada ya kuondoka kwa Yesu, wanafunzi wakatawanyika katika sehemu mbali mbali za Israeli na za ulimwengu. Na haki inayochukiwa na shetani, ilibughudhiwa, kama ambavyo daima inabughudhiwa na batili. Watu kadhaa waovu kwa kusingizia kuwa walikuwa wanafunzi (wa Yesu), wakahubiri kuwa Yesu alikufa na kufufuka. Na wengine wakahubiri,kwamba Yesu ni mwana wa Mungu, miogoni mwao Paulo. Lakina sisi kama nilivyoandika, tunaohubiri kwa wale wamchao Mwenyezi Mungu, tunahubiri ili waokoke siku ya mwisho na Hukumu ya Mwenyezi Mungu, Amin.”
Mafundisho ya Nabii Isa(a.s) yalipotoshwa katika maeneo yafuatayo:
(i) Imani ya Utatu
Imani ya Mungu mmoja aliyofundisha Nabii Isa (a.s) iligeuzwa na kufanywa imani ya Utatu. Mungu mmoja akagawanywa katika sehemu tatu; Mungu Baba, Mungu Mwana na Roho Mtakatifu. Hata mafundisho ya Biblia yenyewe yapo kinyume na imani hii. Rejea vifungu vifuatavyo:
“Yesu akamwambia, kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliyemwema ila mmoja ndiye Mungu.” (Marko 10:18)
“Yesu akamwambia, Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie. Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, Mungu wangu naye ni Mungu wenu.” (Yohana 20:17)
“Kwa Sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena nitakayosema.” (Yohana 10:49)
“Mungu akanena maneno haya yote akasema: Mimi Bwana Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi (Kutoka 20:1-3)
‘Sikiliza Ee Israeli, BWANA, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.” (Kumbukumbu la Taurat) (6:4)
Ama katika Qur-an imani hiyo inakanushwa kabisa na aya zifuatazo:
Kwa hakika wamekufuru wale waliosema: “Mwenyezi Mungu ni mmoja katika (wale waungu) watatu; (yeye ndiye wa tatu wao).” Na kama hawataacha hayo wayasemayo, kwa yakini itawakamata – wale wanaoendelea na ukafiri miongoni mwao – adhabu iumizayo.(5:73)
(ii) Imani ya Uungu wa Yesu
Kuhusu imani juu ya Uungu wa Isa(a.s) na mama yake Qur’an inasema:
Kwa yakini wamekwisha kufuru wale waliosema: “Mwenyezi Mungu ni Masihi bin Maryamu.” Sema: “Ni nani atakayemiliki (kuzuilia) chochote mbele ya Mwenyezi Mungu kama yeye angetaka kumwangamiza Masihi mtoto wa Maryam, na mama yake na vyote vilivyomo katika ardhi na Ufalme wa mbinguni na ardhi na vilivyomo kati yake ni vya Mwenyezi Mungu (tu peke yake). Muumba apendavyo, na Mwenyezi Mungu ni muweza juu ya kila kitu. (5:17).
Masihi bin Maryamu si chochote ila ni Mtume . (Na) bila shaka Mitume wengi wamepita kabla yake. Na mamake ni mwanamke mkweli, (na) wote wawili walikuwa wakila chakula Tazama jinsi tunavyowabainishia Aya, kisha tazama jinsi wanavyogeuzwa (kuacha haki). (5:75)
(iii) Imani ya Uwana wa Mungu wa Nabii Isa(a.s)
Kuhusu itikadi ya Wakristo ya Yesu kuwa mwana wa Mungu, Qur’an inatufahamisha:
Na Mayahudi wanasema: “Uzeri ni mwana wa Mwenyezi Mungu;” na Wakristo wanasema: “Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu..” haya ndiyo wasemayo kwa vinywa vyao. Wanayaiga maneno ya wale walio kufuru kabla yao, Mwenyezi Mungu awaangamize. Wanageuzwa namna gani hawa! (9:30).
Hakuwa (Nabii Issa) ila ni mja tuliyemneeemesha na tukamfanya mithali (nzuri) kwa wana wa Israili. (43:59).
(iv) Imani ya kusulubiwa Yesu Msalabani
Imani ya kufa na kufufuka Nabii Isa(a.s) ni imani ya msingi katika dini ya Ukristo. Imani hii imesimama juu ya dhana zifuatazo:
- Dhambi ya asili.
- Haja ya kuwa na Mpatanishi.
- Kafara ya damu (kifo), kwa ajili ya dhambi.
Wakristo wanaamini kuwa baada ya Adam(a.s) kumkosea Mola wake; kizazi chake chote kilirithi dhambi. Kwa hiyo kila anayezaliwa anazaliwa na dhambi. Ili salama ipatikane kwa mwanaadamu ni lazima apatikane asiye na dhambi awe mpatanishi kati ya Mungu na mwanaadamu. Mtume Isa (Yesu) anadhaniwa ndiye asiye na dhambi na mpatanishi. Lakini ili dhambi za wanadamu zioshwe imekuwa lazima damu ya Yesu imwagike. Kwa hiyo kufa Yesu msalabani ilikuwa hitajio la lazima ili wanaadamu waokolewe na dhambi. Imani hii inasonga mbele na kudai kuwa Mkristo wa leo amepunguziwa kazi. Hana haja ya kufuata sheria. Lililo wajibu juu yake ni kuamini tu kuwa yesu ni Mtoto wa Mungu na alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi zake.
Lakini kuhusu dhana ya dhambi ya asili Qur-an inatufunza kuwa Nabii Adam alitubu na Mola wake akapokea toba yake.
Kisha Adam akapokea maneno (ya maombi) kwa Mola wake, (akaomba), na Mola wake Akapokea toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kupokea toba (kwa wenye kutubia) na mwingi wa kurehemu (2:37)
Ama kuhusu mtu kutolewa kafara kwa ajili ya dhambi za mtu mwingine, Biblia ina haya ya kusema:
“Lakini watoto wao hakuwaua, ila alifanya sawa sawa na alivyo amuru, akisema, mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa dhambi yake mwenyewe. (2 mambo ya nyakati 25:4)
Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.” (Kumb, … 4:16).
“Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi, Bali kila mtu atakufa kwa Sababu ya uovu wake mwenye; kila mtu alaye zabibu kali meno yake yatakuwa ganzi.” (Yeremia: 31:29-30).
Siku ya kiyama itakuwa nzito sana kwa wale waliokuwa wakiamini na kutangaza kuwa Nabii Isa(a.s) ni Mungu, na kumuabudia kinyume cha alivyofundisha. Allah(s.w) atamuuliza Nabii Isa(a.s)
Na(Kumbukeni)Mwenyezi Mungu atakaposema:“Ewe Isa bin Maryam! Je wewe uliwaambia watu ‘Nifanyeni mimi na mama yangu miungu badala ya Mwenyezi Mungu?’. Aseme: “Wewe umetakasika na kuwa na mshirika. Hainistahiki mimi kusema ambayo si haki yangu. Kama ningelisema bila shaka ungelijua; unayajua yaliyomo nafsini mwangu, lakini mimi siyajui yaliyo nafsini mwako; hakika wewe ndiwe ujuaye mambo ya ghaibu. (5:116)
Sikuwaambia lolote ila yale uliyoniamrisha; ya kwamba
‘Mwabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu na Mola wenu’. Na nilikuwa shahidi juu yao nilipokuwa nao; na uliponikamilishia muda wangu, Wewe ukawa mchungaji juu yao, na Wewe shahidi juu ya kila kitu. Ikiwa utawaadhibu, basi bila shaka hao ni waja wako; na ukiwasamehe basi kwa hakika wewe ndiwe mwenye nguvu na Mwenye hikima.(5:117-118)
Mwenyezi Mungu atasema: “Hii ndiyo siku ambayo wakweli utawafaa ukweli wao”. Wao watapata Bustani zipitazo mito mbele yake. humo watakaa milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi; nao wawe radhi naye. Huko ndiko kufaulu kukubwa(5:119)
Mwenyezi Mungu si kiumbe. Yeye ndiye Muumba wa kila kitu kilicho na kisicho na uhai. Kuzaa ni sifa za viumbe vya Mwenyezi Mungu, hivyo Mungu si baba mzazi wa Yesu wala si baba wa mwanadamu yeyote. Qur,an tukufu inatuamrisha:
Sema: Yeye Mwenyezi Mungu aliye mmoja (tu). Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuhitajiwa na viumbe. Hakuzaa wala hakuzaliwa. Na wala hafanani na yeyote(112:1-4)
Ama katika Biblia, neno Baba limetumika kuonesha sifa ya ulezi wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake, hivyo, Mwenyezi Mungu kuitwa Baba haimaanishi kuwa kamzaa Yesu au binadamu yeyote miongoni mwetu. Na ndiyo maana akasema:
Wala msimwite mtu baba duniani, Maana Baba yenu ni mmoja aliye wa mbinguni, wala msiitwe viongozi;maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo(Mathayo 23:9-10)Na katika maandiko mengine ya Biblia, Yesu amenukuliwa akisema: Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni; Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, hapa duniani kama mbinguni (Mathayo 6:9-10)
Kwa maana hii, Mwenyezi Mungu ni Baba wa watu wote, si baba wa Yesu tu. Ni Baba yetu, ila si kwamba katuzaa, bali ulezi wake wa kutujaalia riziki za kila aina na kutupatia elimu na teknolojia ya kuweza kuzitumia neema na riziki hizo. Hivyo Isa(a.s) si mwana wa Mungu wa kuzaa, bali ni kiumbe wake aliyemuumba kwa neno la ‘Kuwa’, likawa kama alivyo muumba Adamu.
Bila shaka mfano wa Isa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama Adamu; alimuumba kwa udongo, kisha akamwambia “Kuwa”, akawa.(3:59)
Kutokana na Historia ya Nabii Isa(a.s) tunajifunza yafuatayo:
(i) Mtoto aliyezaliwa ndani ya ndoa ataitwa kwa ubini wa Baba yake na si vinginevyo na mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa ataitwa kwa ubini wa Mama yake.
(ii) Waumini wanaharakati hawanabudi kumuomba Allah(s.w) awape watoto wema watakaofanya jitihada za makusudi za kuutawalisha Uislamu katika jamii.
(iii) Tuwalee na kuwaelimisha watoto elimu ya mwongozo na mazingira (elimu juu ya fani mbali mbali) si kwa kutaraji maslahi ya dunia bali kwa ajili ya kusimamisha ukhalifa katika ardhi.
(iv) Wanaharakati wanaposingiziwa au kupakaziwa maovu wasitengeneze majukwaa ya kujitetea na kujisafisha bali washitakie kwa Allah(s.w) na kumuomba awasafishe na kuwatakasa hapa hapa duniani.
- Allah(s.w) anawaasa waumini wasijali matusi na fitina za wanafiki na makafiri, bali waendelee kutenda inavyostahiki.
Na sema (uwaambie): “Tendeni mambo (mazuri) Mwenyezi Mungu atayaona mambo yenu hayo na Mtume wake na Waislamu. Na mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahiri; naye atakwambieni (yote) mliyokuwa mkiyatenda.” (9:105)
(v) Msingi wa mafundisho ya Uislamu ni Tawhiid. Yaani tunatakiwa tuufundishe Uislamu kwa mujibu wa Qur-an na Sunnah na kwa lengo la kumuabudu Allah(s.w) katika kila kipengele cha maisha ya binafsi na jamii na kusimamisha Ukhalifa katika jamii – Hii ndio njia sahihi ya kufundisha Uislamu.
(vi) Ukitafakari vizuri utagundua kuwa maumbile yote ya Allah (s.w)yaliyotuzunguka pamoja na nafsi zetu ni miujiza.
Hivyo kuletewa muujiza maalumu, haitakuwa ni sababu ya kumfanya mtu amuamini Allah(s.w) ipasavyo kama atashindwa kutafakari maumbile mbali mbali yaliyomzunguka.
(vii) Kama mbinu ya kulingania Uislamu katika jamii hatunabudi kuunda kundi la harakati litakalokuwa tayari kuufundisha Uislamu kwa usahihi wake, kuamrisha mema na kukataza maovu – Qur’an (3:104).
(viii) Nyakati zote wapinzani wakuu wa kusimama kwa Uislamu katika jamii ni washika dau (Al-Malaau) wa Dola za kitwaaghuut.
(ix) Tunapoamua kujiingiza kwenye harakati za kuhuisha na kusimamamisha Uislamu katika jamii hatunabudi kujiegemeza (kutawakali) kwa Allah(s.w) na kuomba msaada wake na kutegemea ulinzi wake.
(x) Mwanaharakati muda wote anatakiwa awe tayari kukabili au kukabiliwa na misukosuko au kufa kwa ajili ya Allah(s.w),Mtume wake na kusimamisha Dini yake.
Je! umeipenda hii post?
Ndio Hapana Save post
Rajabu Tarehe 2024-06-27 18:59:26 Topic: visa vya Mitume Main: Masomo File: Download PDF Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 522
Sponsored links
👉1 Simulizi za Hadithi Audio
👉2 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)
👉3 Kitau cha Fiqh
👉4 kitabu cha Simulizi
👉5 Madrasa kiganjani
👉6 Kitabu cha Afya
Historia ya Mtume Hud katika Quran
Katika makala hii utakwenda kujifunzahistoria ya Mtume Hud katika Quran Soma Zaidi...
Hstora ya Nab Sulaman
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Sulaman Soma Zaidi...
hHistoria ya Nabii Dhul-kifl
Katika makala hii tutakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Dhul-kifl Soma Zaidi...
Historiaya Nabii Isa
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu Historia ya Nabii Isa Soma Zaidi...
Historia ya Nabii Ayyuub
Katika somo hiliutakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii ayyuub Soma Zaidi...
Historia ya Nabii Musa
atika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Musa Soma Zaidi...
Historia ya Nabii Idrisa
Katika somohili utakwenda kujifunza historia ya Nabii Idrisa (amani iwe juu yake) Soma Zaidi...
Hstoria ya Nabi Daud
Katika somo hili utawenda ujifunza uhusu historia ya Mtume Daud Soma Zaidi...
Historia ya Nabii Nuhu katika Quran
Katika somo hili utakwenda kujifunza historia ya Mtume Nuhu kulingana na melezo yaliyo kwenye Quran Soma Zaidi...
Historia ya Mtume Muhammad (s.a.w) wa ufup
Huu n ufupisho wa Historia ya Mtume Muhammad s.a.w. Tumekuandalia histori hii kwa urefu zaidi kwenye Makala zetu zinazofuata Soma Zaidi...
Historia ya Mtume Swaleh (Salih)
Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Swalehe katikaQuran Soma Zaidi...
Hstora ya Nabii Yunus
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yunus Soma Zaidi...