image

Hstoria ya Nabi Daud

Katika somo hili utawenda ujifunza uhusu historia ya Mtume Daud

HISTORIA YA MTUME DAUD(A.S).

 

Nabii Daudi(a.s) aliishi Bait-Ul-Lahm karibu na mji wa Jerusalem zaidi ya miaka 200 baada ya Mtume Musa(a.s). Nasaba yake inatokea kwa Mtume Ya‘aquub(a.s). Pamoja na kuwa Mtume wa Allah(s.w), Daudi alikuwa pia mfalme wa Mayahudi (Bani Israil).


 

Kupewa Daudi(a.s)Utume na Ufalme


Kiasi cha miaka mia mbili hivi baada ya Mtume Musa (a.s), Mayahudi walipigwa sana na kuonewa na Wafalastin. Waliteka Sanduku takatifu la Waisrail ambamo ndani yake walihifadhi mbao ambazo zimeandikwa amri kumi alizoteremshiwa Nabii Musa (a.s). Aidha yalikuwamo ndani yake masazo mengine ya vitu vitukufu alivyoacha Nabii Musa na Nabii Harun. Sanduku hili Mayahudi walilitukuza sana kiasi kwamba hata wakienda vitani huenda nalo na likiwa mbele ya macho yao huamini kabisa kuwa watashinda vita. Kwa hiyo kunyang'anywa sanduku lao hilo na Wafalastin kuliwavunja nguvu kabisa (Mayahudi).


 

Ilikuwa ni katika kipindi hicho cha kuzidiwa nguvu na Wafalastin, Mayahudi walitamani wapate mfalme atakaye watawala na awaongoze kaitka vita. Biblia inataja kuwa Mtume wao katika kipindi hicho alikuwa Samuel. Kwa hiyo walimwomba Samuel awateulie mfalme.


 

Qur'an inataja kuwa Twaluti alichaguliwa kuwa mfalme. Lakini Mayahudi walimkataa. Hata hivyo Twaluti alibakia kuwa kiongozi wao na akawaongoza Mayahudi waliomtii hata wakamshinda adui yao. Qur'an inarejea habari hii katika aya zifuatazo:


 


"Hukusikia habari ya wakubwa wa Kibanii Israil baada ya Musa walipomwambia Nabii wao: "Tuwekee mfalme ili tupigane katika njia ya Mwenyezi Mungu". Yeye (Mtume wao) akasema:

"Haielekei ya kuwa hamtapigana ikiwa mtaandikiwa kupigana?" Wakasema: "Itakuwaje tusipigane katika njia ya Mwenyezi Mungu na hali tumetolewa katika majumba yetu na watoto wetu?" Lakini walipoandikiwa kupigana waligeuka, isipokuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua sana madhalimu". (2:246).


 

Na huyo Mtume wao akawaambia: "Mwenyezi Mungu amekuchagulieni Twaluti kuwa mfalme". Wakasema: "Vipi atakuwa na ufalme juu yetu; na hali sisi tumestahiki zaidi kupata ufalme kuliko yeye; naye hakupewa wasaa wa mali?" Akasema: "Mwenyezi Mungu amemchagua juu yenu na amemzidishia wasaa wa ilmu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa (na) Mwenye kujua". (2:247).


"Na Nabii wao akawaambia: "Alama ya ufalme wake ni kukujieni lile sanduku ambalo mna ndani yake kituliza nyoyo zenu, kitokacho kwa Mola wenu, na mna masazo ya yale waliyoyaacha watu wa Musa na watu wa Harun, walilichukua malaika. Bila shaka katika hayo mna dalili kwenu ikiwa nyinyi mnaamini" (2:248).


 

Katika jamii za jahiliyah nasaba ya mtu na uwezo wake wa kiuchumi ilikuwa ni vigezo muhimu katika kuteua kiongozi. Mayahudi kwa kuyatupa mafundisho ya Mitume wao na kwa ukaidi wao walivitilia mkazo vigezo hivi vile vile. Kwa hiyo alipoteuliwa Twaluti kuwa kiongozi wao, wakaona hafai kwa kuleta hoja ya mali. Hata hivyo, hoja hiyo inavunjwa na elimu na siha nzuri. Uislamu unasisitiza umuhimu wa kuiboresha akili kwa elimu na kiwiliwili kwa siha nzuri. Katika Uislamu mtu hapewi uongozi kwa sababu ya nasaba au uwezo wake wa kiuchumi bali kwa elimu na Ucha- Mungu wake.


 

Twaluti baada ya kupewa uongozi aliyaongoza majeshi ya Mayahudi kupambana na Jaluti na majeshi yake. Kundi kubwa katika Mayahudi liliasi. Lakini wachache waliobaki wenye imani thabiti walifanya subira na kwa kumtegemea Allah(s.w) wakamshinda Jaluti. Nabii Daud(a.s) katika mapambano haya alikuwa katika jeshi la Twaluti na ndiye aliyemuua Jaluti. Baada ya ushindi huo Mayahudi walimchagua Nabii Daudi kuwa mfalme wao. Ni katika kipindi hicho hicho cha historia Daudi alipewa Utume kama inavyobainika katika aya zifuatazo:


 

Basi Taluti alipoondoka na majeshi alisema: "Mwenyezi Mungu atakufanyieni mtihani kwa mto. Basi atakayekunywa humo si pamoja nami, na asiyekunywa atakuwa pamoja nami; ila


 

atakayeteka kwa kiasi cha kujaza kitanga cha mkono wake (akanywa hayo tu, huyo hana makosa)". Lakini walikunywa humo isipokuwa wachache tu miongoni mwao. Basi alipovuka yeye na wale walioamini pamoja naye, walisema: "Leo hatumwezi Jaluti na majeshi yake". Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mola wao: "Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wafanyao subira" (2:249).


 

Na walipotoka kupambana na Jaluti na majeshi yake, walisema hao watu wa Twaluti: "Mola wetu! Tumiminie subira na uithibitishe miguu yetu, na utusaidie juu ya watu hawa makafiri" (2:250).


 


Basi (hao watu wa Twaluti) wakawaendesha mbio (hao maadui zao) kwa idhini ya Mwenyezi Mungu; na Daudi akamwua Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa (huyu Daudi) ufalme na hikima (Utume). Na akamfundisha aliyoyapenda" (2:251).


 

Yapo mambo kadhaa muhimu ya kuzingatia kutokana na mafundisho ya aya hizi. Kwanza, ni suala la utii. Kuwa na uongozi madhubuti na utii wa wale wanaoongozwa kwa kiongozi wao ni jambo kubwa sana katika kutengemaa kwa mambo ya watu. Kama hakuna utii kwa uongozi, basi jamii ni yenye kuharibikiwa tu. Twaluti anaondoka na jeshi kubwa kupambana na adui wa kutisha. Twaluti hana hakika na utii wa jeshi lake. Basi Allah(s.w) akamwelekeza awafanyie mtihani wa kutokunywa maji hadi kukata kiu. Wasiotii asiwachukue kwenda nao huko kwenye uwanja wa vita wasije wakakhalifu amri vitani.

Ni dhahiri kuwa kama mtu hawezi kufanya subira na kuvumilia kiu yake kwa muda mdogo tu; basi hawezi kuhimili kishindo cha kutoa roho kwa ajili ya Allah kwenye medani ya vita.


 

Pili, fundisho lingine kubwa linalopatikana ni kuwa katika kuipigania Dini ya Allah(s.w) wingi sio hoja, bali imani thabiti, subira na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Watu wachache wa Twaluti walihisi isingekuwa rahisi kulishinda jeshi kubwa la Jaluti. Lakini wale wenye yakini hasa ya kukutana na Mola wao hawakusita. Bali walimkabili Mola wao kumwomba awamiminie subira na ujasiri wa kupambana na adui. Basi kwa idhini ya Mola wao walishinda vita.


 

Ni ahadi yake Allah(s.w) kwamba wakipatikana waumini wakweli wenye kusubiri, basi watawashinda maadui zao pamoja na wingi wao:


"Ewe Mtume (wa Mwenyezi Mungu)! Wahimizewalioamini wende vitani. Wakipatikana kwenu watu ishirini wanaosubiri watashinda mia mbili (katika hao makafiri. Basi nyinyi mkiwa ishirini lazima msimame mupigane na watu miteni). Na kama wakiwa watu mia moja kwenu watawashinda elfu moja ya wale waliokufuru, maana hao ni watu wasiofahamu (uhai wa Akhera, basi wanaogopa kupigana kwa ushujaa sana wasije wakafa. Basi watu mia katika nyinyi wasiwakimbie watu elfu katika wao)." (8:65).


 

Pamoja na ukweli huu, waumini wanatakiwa wafanye juhudi kubwa kukusanya nguvu zao na kusoma mbinu mbali mbali.


Basi waandalieni(wawekeeni tayari)nguvu mziwezazo (silaha) na mafarasi yaliyofungwa(kufuga)tayari tayari(mipakani),ili kwazo nguvu hizi muogopeshe maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu,(mnawajua) na pia (maadui zenu)wengineo wasiokuwa wao, msiowajua nyinyi(lakini) Mwenyezi Mungu anawajua. Na chochote mtakachokitoa katika njia ya Mwenyezi Mungu(kama hii misaada ya vita vya Jihadi)mtarudishiwa (kamili) sawasawa wala hamtadhulumiwa." (8:60).


 

Hata hivyo, silaha kubwa zaidi ni kuziunganisha nyoyo za waumini chini ya lengo moja tu la kuihami Dini ya Allah(s.w). Maadui wa Dini ya Mwenyezi Mungu pamoja na wingi wao wanashindwa kuikabili nguvu ya waumini, kwa sababu nyoyo na malengo yao ni mbali mbali.


 

"Hakika nyinyi (Waislamu) mnaogopwa zaidi katika nyoyo zao kuliko wanavyomuogopa Mwenyezi Mungu, maana wao ni watu wasiofahamu (lolote"). "Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipokuwa katika vijiji vyoa vilivyohifadhiwa, au nyuma ya kuta. Vita vyao baina yao vikubwa. Utawadhani kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio na akili" (59:13-14).

Kwa hiyo suala zima la kuwaelemisha Waislamu na kisha kuwaunganisha chini ya lengo moja tu la kuisimamisha na kuilinda Dini ya Allah, ni jambo la msingi sana.


 

Tatu, jambo lingine la msingi ambalo tunapaswa tulizingatie, ni mazingira yaliyopelekea Nabii Daudi (a.s) kupewa ufalme na utume. Qur'an inatufahamisha kuwa Daudi alipewa Ufalme na Utume baada ya kumwua Jaluti. Hii inatudhihirishia kuwa heshima na jaza njema haipatikani ila kwa juhudi ya mtu binafsi katika kutekeleza majukumu. Hapana heshima pasi na kuwajibika. Aidha katika malipo ya kesho Akhera yatategemea pia juhudi ya mtu na kuwajibika kwake mbele ya Allah(s.w).

 

Neema Alizotunukiwa Nabii Daudi(a.s)


 

(i) Kupewa Utume na Elimu.

Nabii Daudi pamoja na kupewa utume na ufalme, alifunuliwa elimu kubwa:

"Ewe Daudi! Hakika tumekujaalia kuwa khalifa katika ardhi; basi wahukumu watu kwa haki wala usifuate matamanio ya nafsi yasije yakakupoteza na njia ya Mwenyezi Mungu" (38:26).


 

"Na bila shaka tuliwapa Daudi na Suleiman ilimu (kubwa kabisa) wakasema: "Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu. Aliyetufadhilisha kuliko wengi katika waja wake waliomuamini". (27:15).


 

(ii)Kupewa Zaburi.

Katika Qur'an vinatajwa vitabu vikuu 4 vya Allah(s.w). Vitabu hivyo ni Zaburi, Taurati, Injili na Qur'an. Zaburi alipewa Mtume Daudi (a.s).

“…Na Daud tukampa Zaburi" (4:163).


 

(iii)Kipawa cha Mawasiliano na Viumbe Wengine Zaidi ya Wanaadamu.

Ilivyo kawaida wanaadamu huwasiliana wao kwa wao hasa kwa njia ya lugha. Na wanyama na viumbe wengine nao

wana namna ya kuwasiliana wenyewe kwa wenyewe. Lakini Allah(s.w), Muweza wa yote alimjaalia Nabii Daudi kuwa na mawasiliano na viumbe wengine. Aidha alitiishiwa baadhi ya viumbe akawa anashirikiana navyo katika kumdhukuru Allah(s.w).


 


"Subiri juu ya hayo wanayosema, na umkumbuke mja wetu Daudi Mwenye nguvu (ya kuendesha Utume na Ufalme); kwa yakini yeye alikuwa mwelekevu sana".Hakika sisi tuliitiisha milima (iwe) pamoja naye, ikimtukuza (Mwenyezi Mungu pamoja naye) jioni na asubuhi. Na pia Ndege waliokusanywa (makundi kwa makundi), wote walikuwa wanyenyekevu kwake" (38:17-19).


 

(iv)Ustadi Katika Matumizi ya Chuma.

Umuhimu wa matumizi ya chuma hasa katika kuihami Dini ya Allah ni jambo kongwe katika historia ya mwanaadamu. Moja ya neema aliyopewa Nabii Daudi ni ujuzi wa kukifua chuma na
kutengeneza zana mbali mbali ikiwa ni pamoja na zana za vita.


 


"Na kwa hakika Tulimpa Daudi fadhila kubwa kutoka kwetu. (Tuliyaamrisha majabali yawe yanaitikia Dua pamoja naye. Tukayaambia): Enyi milima! Rejezeni sauti pamoja naye. Na (nyie) ndege (pia )". Na tukamlainishia chuma" (34:10).


 

"(Tukamwambia): Tengeneza (nguo za chuma) pana, na upime vizuri katika kuunganisha; na fanyeni vitendo vizuri, bila shaka Nayaona (yote) msiyoyatenda" (34:11).


 

"Na tukamfundisha (Daudi) matengenezo ya mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika mapigano yenu. Je! Mtakuwa wanaoshukuru?" (21:80).

 

(v)Hakimu Muadilifu

Nabii Daudi alipewa ilimu na akili ya kukata hukumu:

"Na Tukautia nguvu ufalme wake na Tukampa ilimu na (akili ya)
kukata hukumu" (38:20).


 

Yapo matukio mawili katika historia ya maisha ya Nabii Daudi yanayotoa kielelezo cha unyenyekevu wake katika kuifuata haki. Tukio la kwanza ni lile linalobainishwa katika Qur'an Surat Sad aya ya 21 mpaka 25. Katika aya hizi zinatajwa habari za watu wawili waliokuwa wanagombana na kumwendea Nabii Daudi ili awahukumu. Nabii Daudi aliathiriwa mno na maelezo ya upande mmoja kiasi kwamba akatoa hukumu bila ya kusikiliza upande wa pili. Lakini punde akatanabahi na kugundua kosa alilolifanya akarejea kwa Mola wake na kuomba maghfira. Tukio hili linabainishwa katika Qur'an kama ifuatavyo:


 

"Na je imekuwasilia habari ya wagomvi walipopindukia (ukutani kuingia) chumbani kwake (Nabii Daudi?)" (38:21).


Walipomuingilia Daudi na akawaogopa. Wakasema: "Usiogope; (sisi ni) wagombanao wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe; basi tuhukumu, kwa haki wala usipendelee, na utuongoe katika njia iliyo sawa" (38:22).


Hakika huyu ni ndugu yangu, yeye ana kondoo majike tisini na tisa, na mimi nina kondoo mmoja tu jike, lakini amesema: "Nipe huyu wako nikufugie, (na mimi mwenyewe sitaki) na amenishinda katika maneno" (38:23).


 

Akasema: "Kweli amekudhulmu kwa kukuomba kondoo wako kuongeza katika kondoo wake, na bila shaka washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipokuwa wale walioamini na kutenda mema, na hao ni wachache". Na mara Daudi akaona ya kwamba tumemtia mtihanini. Akaomba maghufira kwa Mola wake, na akaanguka kunyenyekea na akaelekea (kwa Mola wake) (38:24).


 

"Basi tukamghufiria (tukamsamehe) hayo. Na kwa hakika ana yeye kwetu cheo kikubwa na mahali pazuri (marejeo mazuri)" (38:25).


 

Katika tukio hili kosa alilolifanya Nabii Daud ni kule kukata hukumu kabla ya kusikiliza upande wa pili. Kama inavyobainishwa na aya hizi msemaji wa awali alikuwa hodari wa kuyapanga maneno kiasi kwamba alimfanya Nabii Daud amwone ana haki kabla hata hajasikiliza upande wa pili. Lakini hata hivyo kwa ule Ucha-Mungu wake alizindukana na kuomba maghufira.


 

Hili ni fundisho kubwa sana kwetu kuwa katika hali yoyote itakayokuwa, mtu asipitishe hukumu kwa kutegemea maelezo ya upande mmoja tu.

Katika tukio la pili Nabii Daud(a.s) na mwanawe Sulaiman(a.s) waliletewa shauri. Mbuzi wa mtu mmoja waliingia shambani na kuharibu kabisa mimea ya mtu mwingine. Uharibifu huo ulikuwa ni mkubwa kiasi cha kumkosesha kabisa mavuno muhusika kwa mwaka mzima.


 

Nabii Daud(a.s) alitoa hukumu kuwa mbuzi waliohusika na uharibifu ule, apewe mwenye shamba kama fidia. Lakini mtoto wake Sulaiman aliona hukumu iliyo ya haki zaidi si kumpa mwenye shamba mbuzi wale moja kwa moja. Bali awachukue akae nao anufaike na maziwa, sufi na watoto watakaozaliwa kiasi cha kufidia hasara ya mazao yake kisha mbuzi warejeshwe kwa mwenyewe. Nabii Daud kwa vile alikuwa ni mtu wa haki mwenye kusimamia uadilifu hakusita kuchukua rai hii japo imetoka kwa mtoto wake. Tunakumbushwa katika Qur'an:


 

"Na (wakukbushe) Daudi na Suleiman walipokata hukumu juu ya konde, walipolisha humo mbuzi wa watu usiku. Nasi kwa hukumu yao hiyo tulikuwa mashahidi, (tunaona, tunasikia") (21:78). Tukamfahamisha Suleiman (kuliko Mzee wake, Daudi). Na kila mmoja tulimpa hukumu na ilimu" (21:79).


 

Ikumbukwe Daud(a.s) alikuwa ni Mtume kisha Mfalme wa Wayahudi, lakini hakuwa na takaburi za kifalme. Alikuwa laini katika kusimamia uadilifu. Alikuwa mtu rahisi mbele za watu kiasi kwamba alifanya kazi za mikono ili kujitafutia riziki yake na familia yake


 

(vi) Mtoto Mwema, Sulaiman (a.s)

"Na tukampa Daud (Mtoto aliyeitwa) Suleiman aliyekuwa Mtu Mwema na aliyekuwa mnyanyekevu.(38:30)

 

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Daud(a.s)


Kutokana historia ya Nabii Daud (a.s) tunajifunza yafuatayo


 

(i) Katika kuchagua kiongozi wa kuendeleza harakati za kusimimisha Uislamu katika jamii hatunabudi kuzingatia sifa nne za msingi zifuatazo:

(a) Elimu ya mwongozo na mazingira – (58:11)

(b) Ucha-Mungu-mwenye kujitahidi kufuata kwa unyenyekevu maamrisho ya Allah(s.w) na Mtume wake na kujitahidi hivyo hivyo kujiepusha na makatazo yao – Qur’an (49:13)

(c) Siha au Afya nzuri na ushupavu. Mtume(s.a.w)
amesema:

“Muumini mwenye afya nzuri (kawiyyu) ni bora zaidi kuliko muumini nyoronyoro (legelege).”

(d) Mwenye tabia njema – Pia Mtume (s..a.w) kasema;

“Aliye kipenzi changu kuliko wote katika nyinyi (Waislamu) ni yule aliyewazidi kwa tabia njema” (Al-Bukhari).


 

(ii) Utii kwa kiongozi muumini (mcha-mungu) ni msingi wa mafanikio kwa waislamu


 

(iii) Waumini wachache wenye msimamo na wenye kumtegemea Allah(s.w) wana uwezo wa kusimamisha haki (Uislamu) katika jamii.(2:249)


 

(iv)Tusitoe hukumu juu ya shutuma kabla hatujapata maelezo na kuyapima kutoka kwa yule anayeshutumu na anayeshutumiwa.


 

(v) Tushukuru neema na vipaji vya ziada alivyotutunukia Allah(s.w) na kuwa mstari wa mbele katika kusimamisha uadilifu katika jamii – Nabii Daud (a.s) alikuwa mfalme juu ya watu, milima, upepo na ndege, lakini hakutakabari.


 

(vi) Hatunabudi kuwaandalia maadui wa Uislamu silaha zinazolingana na wakati huu wa sayansi na teknologia – Nabii Daud(a.s)alitumia chuma kuandaa silaha na mavazi ya kivita – Pia rejea agizo la Allah(s.w) (8:60)


 

(vii) Hatunabudi kuwa na mazoezi ya kivita yatakayo tuwezesha kuwa jasiri na wavumilivu katika vita dhidi ya maadui wa Haki (Uislamu)

- Mfalme Twalut alilipa jeshi lake zoezi la kutokunywa maji ya mto ule ili kupima utii wao na uvumilivu wao.

 





           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-06-27 16:17:11 Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 28


Sponsored links
👉1 Kitabu cha Afya     👉2 Madrasa kiganjani     👉3 kitabu cha Simulizi     👉4 Kitau cha Fiqh    

Post zifazofanana:-

Chanzo cha Mapato katika serekali ya Kiislamu wakati wa Makhalifa
Soma Zaidi...

Historia ya maimam Wanne wa fiqh
Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Nuhu katika Quran
Katika somo hili utakwenda kujifunza historia ya Mtume Nuhu kulingana na melezo yaliyo kwenye Quran Soma Zaidi...

Uasi katika dola ya kiislamu na matokeo yake
Uasi katika dola ya kiislamu na matokeo yake. Soma Zaidi...

Upinzani Dhidi ya Ujumbe wa Mtume(s.a.w)
Mtume(s. Soma Zaidi...

Hadhi na Haki za mwanamke katika jamii za kiafrika hapo zamani
3. Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Yahya
Katika somo hili uatkwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yahya Soma Zaidi...

HISTORIA YA KUJENGWA UPYA KWA AL-KA'BAH (NYUMBA TUKUFU YA ALLAH)
KUJENGWA UPYA KWA AL-KA’ABAHItambulike kuwa Al-ka’abah ndio mjengo wa kwanza kujengwa duniani. Soma Zaidi...

Darsa za Sira historia ya Mtume (s.a.w) Jaribio la 04
Soma Zaidi...

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Ayyuub(a.s)
Kutokana na kisha hiki cha Nabii Ayyuub(a. Soma Zaidi...

Imam Tirmidh na Jami'u At-Tirmidh
Soma Zaidi...

Bara la Arabu Zama za Jahiliyyah
Wakati Mtume(s. Soma Zaidi...