Lengo la Zakat na jinsi Linavyofikiwa
Lengo la Zakat linawiana na neno “Zakat” lenye maana ya kutakasa au utakaso. Mali itolewayo Zakat inakusudiwa iwe kitakaso kama inavyobainishwa katika Qur-an:
“Chukua sadaqat katika mali zao uwatakase kwa ajili ya hizo na kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu. Na Mwenyezi Mungu ndiye asikiaye na ajuaye.” (9 :103)
Pia imepokelewa kwa Ibn Abbas (r.a) kuwa Mtume (s.a.w) amesema:
“Mwenyezi Mungu (s.w) hakuamrisha Zakat kwa sababu nyingine ila ni kuitakasa mali iliyotolewa ”.
Zakat huitakasa:
(i) Mali ya mtoaji.
(ii)Nafsi ya mtoaji.
(iii)Nafsi ya mpokeaji.
(iv)Jamii ya Kiislamu kwa ujumla.
(i)Zakat inavyotakasa mali ya mtoaji
Zakat ni sehemu ndogo ya mali (1 / 40 au 2.5%) inayotolewa kutokana na mali anayomiliki Muislamu na kuwapa wanaohitajia miongoni mwa fukara, maskini, wasafiri walioharibikiwa na wengineo kama ilivyobainishwa katika Suratul-Tawba aya ya 60. Sehemu hii ya mali inayaotolewa Zakat ni haki ya wale wanaostahiki kupewa Zakat iliyopitishiwa mikononi mwa huyu mwenye mali kama amana tu kama inavyobainika katika Qur-an:
“Na katika mali zao ilikuwepo haki ya kupewa maskini aombaye na ajizuiaye kuomba ”. (51:19).
Mali iliyotolewa Zakat inatakasika kwa sababu:
Kwanza, huepukana na haki za watu wanaostahiki kupewa zaka, hivyo mali yote huwa halali na safi. Ambapo kama mali haitatolewa Zakat itachanganyika na haki za watu.
Pili, Mu is lamu mwenye kutoa Zakat na sadaqat anafahamu vyema kuwa kutoa huko hakutasihi mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w) iwapo chumo lake limepatikana katika njia za haramu. Hivyo Muislamu mwenye tabia ya kutoa Zakat na sadaqat atajitahidi kufuata njia za halali katika kuchuma kwake na kujipatia mali iliyo halali.
(ii)Zakat na Sadaqat Inavyotakasa Nafsi ya Mtoaji
“Kutoa ni moyo si utajiri”. Msemo huu ni wa msingi sana. Maana hasa ya msemo huu ni kwamba si utajiri utakaomfanya mtu atoe mali yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu bali ni moyo wake utakaomlazimisha kutoa. Utowaji wa mali na kuwapa wengine kwa ajili ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu si jambo la dharura bali ni jambo la kudhamiria na kutenda kutokana na msukumo wa nafsi yenye yakini juu ya maisha ya Akhera.
Muislamu anapotoa mali yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kuwapa wanaostahiki kwa upande mmoja, Mwenyezi Mungu huitakasa nafsi yake na uchoyo, ubakhili, upupiaji mali, kuabudu mali, majivuno, kiburi, dhulma na maovu mengineyo yatokanayo na umilikaji mali. Kwa upande mwingine, mwenye kutoa mali yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu huivika nafsi yake pambo la huruma, ukarimu, upendo na uchungaji haki za wengine.
Pia utoaji wa zakat na sadaqat huwa ni sababu ya mja kufutiwa dhambi zake na kustahiki Pepo ya Mwenyezi Mungu kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:
“Enyi mlioamini! Je! Nikujulisheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iumizayo?(Basi biashara yenyewe ni hii): Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganieni dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu, haya ni bora kwenu; ikiwa mnajua (kuwa ni bora, basi fanyeni).(Mkifanya hayo, atakusameheni dhambi zenu na atakuingizeni katika Mabustani yapitayo mito mbele yake na (atakupeni) maskani mazuri mazuri katika Bustani za milele: huku ndiko kufuzu kukubw a.(61 :10-12)
Katika Surat-Tawba, tunafahamishwa kuwa wale Waislamu waliozembea kuandamana na Mtume wa Mwenyezi Mungu katika msafara wa Tabuku kwa ajili ya kushughulishwa na mali, baada ya kutubia kwa Mola wao walitoa sadaqat ili kutakasa nafsi zao kama tunavyojifunza katika aya ya (9:102-103):
Na (wako) wengine wamekiri dhambi zao (w am etubia kw a Mw enyezi Mungu w akapokelew a). Wamechanganya vitendo vizuri na vingine vibaya, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa
kusamehe na mwingi wa kurehemu. Chukua sadaqat katika mali zao (Ee Muhammad) uwatakase kwazo na kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua...” (9:102-103).
(iii)Zakat inavyotakasa Nafsi ya Mpokeaji
Kama mali ilivyo mtihani kwa tajiri ndivyo ilivyo mtihani kwa maskini au mwenye dhiki. Kwa tajiri mali ni mtihani kwa sababu anao uhuru wa kuitumia mali yake apendavyo ambapo ni amana tu kwake kutoka kwa Mola wake. Kwa maskini kukosa mali ni mtihani kwake kwa sababu anaweza kumdhania Mwenyezi Mungu (s.w) vibaya kuwa ni muonevu na mwenye kupendelea kati ya waja wake; wengine akawafanya matajiri na wengine akawafanya mskini. Pamoja na dhana hii mbaya juu ya Mwenyezi Mungu (s.w) maskini na mwenye dhiki huweza kujenga moyoni mwake tabia ya unyonge, udhalili, husuda, uadui, uhasama na tabia nyingine mbaya zinazosababishwa na ukosefu wa mali.
Utoaji wa Zakat na Sadaqat kwa wanaostahiki umewajibishwa kwa Waislamu wenye kumiliki mali ili pamoja na kuwatakasa wao wenyewe, iwatakase pia wapokeaji kutokana na husuda, chuki, uhasama, unyonge, na kadhalika, na badala yake kuwavisha nyoyoni mwao upendo, udugu, shukrani, uchangamfu, ushirikiano na maadili mengineyo yanayotokana na kukirimiwa mali kwa jina la Mwenyezi Mungu (s.w).
Pia mwenye kupokea Zakat au sadaqat daima atakumbuka kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwaruzuku waja wake bila hesabu.
(iv)Zakat na Sadaqat Inavyotakasa Jamii ya Waislamu
Tumeshaona jinsi Zakat na Sadaqat zinavyotakasa nafsi za watoaji na wapokeaji ambao wote wako katika jamii moja. Fikiria jamii ambayo kwa upande mmoja matajiri wake hutoa haki za maskini na wale wote wanaostahiki kupewa Zakat na Sadaqat huku wakiwahurumia na kuwakumbatia ndugu zao hao na kwa upande mwingine hao wanaoipokea zakat na Sadaqa, wanaipokea kwa moyo wa uchangamfu na upendo wakijua kuwa wamepokea tunu hiyo kutoka kwa Mola wao kupitia kwa ndugu zao waadilifu. Unafikiri jamii hii itakuwa na watu wenye mahusiano ya namna gani? Bila shaka jamii hii itakuwa ni jamii yenye kuishi kwa upendo na udugu na yenye kudumisha amani. Kila mmoja katika jamii atakuwa anapata mahitajio yake muhimu ya maisha. Jamii ya namna hii ni lazima iwe na maendeleo ya vitu na utu kwa sababu zifuatazo:
Kwanza, kila mmoja atakuwa na uwezo wa kimwili na wakisaikolojia wa kufanya kazi kwa juhudi zake zote. Inafahamika kuwa katika Uislamu uvivu na uzembe ni haramu. Hivyo kila aliyekuwa na dhiki ya muda mfupi baada ya kupewa Zakat na Sadaqat, atapata nguvu na uwezo wa kujikwamua katika dhiki yake hiyo, na baada ya muda mfupi naye atazalisha mali ya kutosha kutoa Zakat na Sadaqat. Hali hii huiwezesha jamii kufikia wakati ambao watu wasiojiweza watakuja kuwa wachache sana na sehemu kubwa ya zakat kupelekewa kwenye miradi ya maendeleo ya jamii kama vile ujenzi na uendeshaji wa shule na vyuo, hospitali, barabara, n.k.
Pili, uhusiano mzuri kati ya matajiri na wenye dhiki katika jamii unaojengwa kwa njia ya kusaidiana kwa Zakat na Sadaqat, huwafanya waislamu washikamane na kushirikiana ipasavyo katika kuusimamisha na kuuhami Uislamu jambo ambalo huwapelekea kupata radhi za Mwenyezi Mungu, baraka zake na upendo wake kama tunavyojifunza katika Qur-an:
“Kwa yakini Mwenyezi Mungu anawapenda wale wanaopigana katika njia yake, safusafu, (mkono mmoja); kama kwamba wao ni jengo lililokamatana barabara”. (61:4).
Tatu, uchumi wa halali ni miongoni mwa sharti za utoaji Zakat na Sadaqat. Hivyo katika jamii ambayo utoaji wa Zakat na Sadaqat umedumishwa, lazima pawe na uadilifu katika uchumi ambapo kila mtu hupata haki yake na kufaidika ipasavyo. Njia zote za uchumi haramu zikiepukwa katika jamii ni wazi kuwa udhalimu, wizi, ujambazi, kamari, riba, hongo na rushwa hutoweka na humuhamasisha kila mtu kuchuma kwa juhudi zake zote. Matokeo yake ni jamii kuendelea kiuchumi na kudumisha amani.
Ukusanyaji na Ugawaji wa Zakat ni Suala la Jamii
Mafanikio ya Zakat katika kuinua hadhi na uchumi wa jamii hayatapatikana iwapo utoaji na ugawaji wa Zakat utaendelea kubakia kuwa shughuli ya mtu binafsi.Tunafahamu vyema kuwa uchumi wa jamii haujengwi na mtu binafsi bali unajengwa kwa ushirikiano na kila mwana jamii. Hivyo, Zakat ikiwa sehemu kubwa na muhimu ya uchumi wa jamii ya Kiislamu, haina budi kukusanywa na kugawanywa na jamii. Kama Mtume (s.a.w) anavyosisitiza:
“Nimeamrishwa nichukuwe zakat kutoka kwa matajiri miongoni mwenu na niigawanye kwa maskini (wanyonge) miongoni mwenu ”.
Katika utekelezaji wa amri hii Mtume Muhammad (s.a.w) pia kama Rais au Mkuu wa dola ya Kiislamu aliwateua watu (Maamil) wa kwenda katika kila nyumba ya tajiri na kukusanya Zakat na kuziweka kwenye Hazina (Baitul-maali). Maamil waliwajibika pia kuigawa Zakat kwa wanaostahiki kutoka kwenye Baitul-maali.
Kwa ujumla ukusanyaji na ugawaji wa Zakat wakati wa Mtume (s.a.w) ulikuwa ni kazi ya Serikali na wenye kuishughulikia Zakat katika ukusanyaji na ugawanyaji wake walikuwa wakilipwa kutokana na Zakat hiyo. Rejea tena Qur-an:
“Sadaqat (zaka) hupewa watu hawa:Mafakiri, na maskini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao juu ya Uislamu na katika kuwapa uungwana watumwa na katika kuwasaidia wenye deni na katika (kutengeneza) m am bo aliyoamrisha Mw enyezi Mungu na katika (kupew a) w asafiri (w alioharibikiw a). Ni faradhi inayotoka kw a Mw enyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mj uzi (na) Mwenye hikima ”. (9:60)
Kutokana na aya hii tunaona kuwa fungu la tatu la Zakat hutumika kama mshahara kwa Maamil wanaozitumikia katika kuzikusanya na kuzigawanya. Hii yote inathibitisha kuwa amri ya zakat ni lazima itekelezwe kijamii chini ya usimamizi wa dola au jumuiya ya Kiislamu. Hivi ndivyo Mtume (s.a.w) alivyoitekeleza pamoja na Makhalifa wake waongofu. Mafanikio yote yaliyopatikana katika kusimamisha na kuimarisha Dola ya Kiislamu yalipatikana kutokana na utaratibu mzuri alioufuata Mtume (s.a.w) na Makhalifa wake waongofu katika kuinua uchumi wa jamii kwa Zakat na sadaqat na njia nyinginezo.
Jifunze zaidi, na wasiliana nasi ukiwa na App yetu. Bofya link hapo chini kuweza kuipakua.
Download NowMambo ya faradh kwa maiti ya muislamu (EDK form 2: dhana ya elimu ya uislamu)
Soma Zaidi...Katika somo hili utakwenda kujifunza maana ya twahara katika uislamu. Pia utakwenda kujifunza hukumu za twahara, aina za twahara na mambo mengineyo
Soma Zaidi...Katika post hii utakwenda kujifunza mambo ambayo ni haramu kwa mwanamke aliye na hedhi na nifasi
Soma Zaidi...Mambo haya yanaweza kuharibu funga ya mtu ama kupunguza malipo ya funga.
Soma Zaidi...Ugumba ni “ugonjwa wa mfumo wa uzazi unaofafanuliwa kwa kushindwa kupata ujauzito baada ya miezi 12 au zaidi ya kujamiiana bila kinga mara kwa mara. Utasa kutoweza kwa kiumbe hai kufanya uzazi wa ngono au kutoweza kupata mimba au kuchangia mimba.
Soma Zaidi...Aina za Swala za Sunnah.
Soma Zaidi...