Menu



Namna ya kumvalisha sanda maiti, na kushona sanda ya maiti

Namna ya kumvalisha sanda maiti, na kushona sanda ya maiti

Namna ya Kumkafini Maiti



Kumkafini maiti au kumvalisha sanda ni Faradhi Kifaya. Nguo nzuri ya kutumia kwa ajili ya sanda ni nguo nyeupe ya pamba kama tunavyofahamishwa katika Hadithi ifuatayo:
Ibn Abbas amesimulia kuwa Mtume wa Allah (s.a.w) amesema: Vaeni nguo nyeupe, kwa sababu hilo ni vazi lenu lililo bora kuliko yote, na wakafinini maiti wenu nguo (nyeupe). (Abu Daud, Tirmidh na Ibn Majah).



Pia ni vyema nguo hiyo isiwe ya gharama kubwa na nguo iliyotumika ni bora zaidi kama tunavyofahamishwa katika Hadith ifu atayo:



Ali (r.a) amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: “Msigharamie sana nguo ya sanda, kwani inakwenda kuozeana (kaburini)”. (Abu Daud).


Hajj (mwenye kuhiji) akifa wakati wa Hija, akiwa bado kwenye “Ihram” (vazi rasmi la kuhijia - shuka mbili nyeupe zisizo shonwa), Ihram yake huwa ndio sanda na kichwa chake kubakia wazi bila ya kufunikwa kama tunavyofahamishwa katika Hadithi:



Abdullah bin Abbas(r.a) amesimulia kuwa mtu mmoja alikuwa pamoja na Mtume (s.a.w) ngamia wake alimkanyaga, wakati akiwa anahiji mpaka akafa, Mtume wa Allah akasema:“Muosheni na maji na majani ya mkunazi na mumkafini kwa hayo mashuka yake mawili, msimpake manukato na msimfunike kichwa chake, na hakika siku ya Kiyama atafufuliwa akiitikia Labbaika. (Bukhari na Muslim).



Ukubwa wa kitambaa cha sanda utategemea ukubwa wa maiti. Sanda ya mwanamume ina vipande vitatu vilivyo sawa sawa na sanda ya mwanamke ina vipande vitano.



Sanda ya Mwanamume na Namna ya Kuivika



Sanda ya mwanamume ina vipande (majamvi) vitatu. Utaratibu wa kutayarisha sanda na kukafini ni kama ifuatavyo:
1. Weka kipande cha kwanza juu ya mkeka au jamvi, kisha cha pili na cha tatu na kila kipande kifukizwe ubani na kupakwa marashi. Vipande vyote hivi vitatu vishikizwe na uzi katikati.



2. Pasua kamba katika pembe mbili za jamvi la kwanza, kamba moja kwa ajili ya kufungia kichwani na nyingine ya kufungia miguuni. Kamba nyingine ya kumfungia maiti katikati itatolewa kwenye jamvi la pili. Kamba nyingine tatu za kufungia juu ya mkeka zitatoka kwenye jamvi la pili na la tatu.



3. Maiti italazwa juu ya vipande vyote vitatu. Ichukuliwe pamba iwekwe manukato kisha iwekwe juu ya viungo vyote vya sijda - kipaji cha uso, viganja vya mikono, magotini na kwenye vidole vya miguu; pia pamba hiyo itumike kuzibia matundu yote mwilini - mdomo, pua, masikio na makalio.


4. Maiti itatatizwa na kipande cha kwanza mpaka kimuenee - kwa kuanza kutatiza kunjo la kushoto, kisha kunjo la kulia lije juu. Vipande viwili vilivyobaki vitatizwe kama hicho cha kwanza. Kisha zile kamba zitumike kufunga vitanzi kichwani, miguuni na tumboni ili sanda isije vuka na kumuacha maiti uchi. Katika hali hii maiti itakuwa tayari kwa kuswaliwa. Inaweza kuwekwa kwenye jeneza hivyo hivyo au inaweza kuzungushiwa mkeka kwanza ndio iwekwe kwenye jeneza.



Sanda ya Mwanamke na Namna ya Kumvika



Sanda ya mwanamke kawaida inavipande vitano. Vipande vikubwa viwili sawa na vile vya sanda ya mwanamume. Kipande cha tatu ni shuka au gagulo (under skirt), kipande cha nne ni kanzu na kipande cha tano ni ukaya au kipande cha nguo cha kufunikia kichwa na uso. Utaratibu wa kutayarisha sanda na kukafini ni kama ifuatavyo:
1. Vipande vikubwa viwili vitatandikwa kimoja hadi kingine kama inavyofanywa kwa sanda ya mwanamume.



2. Kikatwe kitambaa cha ukubwa wa shuka ya kawaida ya kufunga kiunoni. Kisha kipande hiki kiwekwe juu ya vipande viwili vikubwa katika sehemu ya chini atakapolazwa maiti ili shuka hii itatizwe kiunoni kama mtu anayefunga shuka ya kawaida.



3. Kisha ikatwe kanzu ambayo haishonwi vizuri, kwa kukunja kitambaa na kutoboa katikati ili iwe sehemu ya kuingiza kichwa wakati wa kuvalisha na kushikiza pembeni kwa uzi kufanya mfano wa kanzu kata mikono. Kanzu itatandikwa juu ya kipande kikubwa cha pili katika sehemu ya juu na sehemu ya chini itakuwa juu ya ile shuka (gagulo) baada ya kuwekwa manukato na kufukizwa ubani.



4. Kitambaa cha ukaya cha kutosha kufunika kichwa na uso kitaingizwa ndani ya shingo ya kanzu na kunyooshwa kwa juu. Baada ya hapo matayarisho ya sanda ya mwanamke yatakuwa yamekamilika.


5. Maiti ataanza kuvalishwa kanzu, kisha juu yake atafungwa shuka. Kisha atawekwa pamba yenye manukato viungo vyote vya sijda pamoja na sehemu zote za matundu kama inavyofanywa kwa maiti ya mwanamume. Baada ya hapo, maiti itatatizwa na vipande vikubwa viwili kimoja baada ya kingine, kila mara kunjo la kulia likiwa juu na itafungwa vile vile kwa kamba tatu - miguuni, tumboni na kichwani na kuwa tayari kuingizwa kwenye jeneza na kuswaliwa.



Sanda ya Watoto
Sanda ya watoto wadogo, wa kike au wa kiume ni vipande vitatu tu kama ile ya wanaume wakubwa.
Namna ya kumswalia Maiti
Swala ya maiti au swala ya jeneza ni faradhi kifaya. Ni faradhi kifaya kwa sababu ikifanywa na wachache au na mtu mmoja tu katika jamii inatosheleza na Waislamu wote wanasalimika na ghadhabu za Allah (s.w).




                   


Download App Yetu

Jifunze zaidi, na wasiliana nasi ukiwa na App yetu. Bofya link hapo chini kuweza kuipakua.

Download Now Bongoclass

Nyuma Endelea

Ndio     Hapana     Save post
Author: Rajabu image Tarehe: 2024-05-10 14:53:23 Topic: Fiqh Main: Post File: Download PDF Views 1342

Share On:

Facebook WhatsApp

Post zinazofanana:

Mafungu ya urithi katika uislamu

Hspa utajifunza viwango maalumu vya kutithi mirathi ys kiislamu.

Soma Zaidi...
Mgawanyiko katika kuitumia mali unayomiliki

Unajuwa namna ambavyo matumizi ya mali yako, yanavyogawanywa? Jifunze hapa mgawanyiko wa mali yako.

Soma Zaidi...
Mambo ambayo hayafunguzi funga

Hii ni orodha ya mambo ambayo hayawezi kuharimu funga yako endapo utayafanya.

Soma Zaidi...
NI ZIPI NGUZO NA SHARTI KUU ZA SWALA ILI IKUBALIWE

Sharti za SwalaSharti za Swala Sharti za swala ni yale mambo ya lazima anayotakiwa Muislamu ayachunge na kuyatekeleza kabla hajaanza kuswali.

Soma Zaidi...
Mambo yaliyo haramu kwa mwenye hedhi na nifasi

Katika post hii utakwenda kujifunza mambo ambayo ni haramu kwa mwanamke aliye na hedhi na nifasi

Soma Zaidi...
kuletewa ujumbe

(c)Kuletewa Ujumbe na Malaika kutoka kwa Allah (s.

Soma Zaidi...
Usitamani kifo hata ukiwa mchamungu mno ama muovu mno

Katika uislamu imekatazwa kutamani kufa hata kama utakuwa ni mtu muovu sana ama mchamungu sana.

Soma Zaidi...