Kufunguliwa Yusufu(a.s) Kutoka Gerezani


Yusufu(a.s) alisahauliwa gerezani kwa muda mrefu. Kilichopelekea akumbukwe ni ndoto aliyoota Mfalme. Alipoamka aliwaita makuhani na kuwahadithia:

.............Hakika mimi nimeona ng’ombe Saba wanene wanaliwa na ng’ombe Saba ving’onda. Na nimeona mashuke Saba mabichi na mengine yaliyokauka. Enyi wakubwa nitafsirieni ndoto yangu ikiwa ninyi mnaweza kutafsiri ndoto(12:43)

Wakasema: ni ndoto iliyovurugika wala sisi hatujui tafsiri ya ndoto hizi(12:44)

Yule mfungwa aliyefasiriwa ndoto na Yusufu(a.s) kuwa atatolewa gerezani alimkumbuka Yusufu na akawaambia:

........Mimi nitakwambieni tafsiri yake. basi nitumeni (12:45)Alipofika gerezani, akamwita:

Yusufu! Ewe mkweli! Tueleze hakika ya ng’ombe Saba wanene kuliwa na ng’ombe Saba dhaifu. Na mashuke Sabaa mabichi na mashuke makavu, ili nirejee kwa watu wapate kujua. (12:46)

Akasema: Mtalima miaka Saba mfululizo kwa juhudi. Na mtakavyovivuna viacheni katika mashuke yake isipokuwa kidogo mnavyokula.(12:47)

Kisha itakuja baadaye miaka Saba ya shida itakayokula vile mlivyolima, isipokuwa kidogo mtakachohifadhi (12:48)

Walipopata taawili ya ndoto hii, Mfalme kwa furaha kubwa kabisa alisema


Mleteni kwangu nimchague awe mtu wangu mwenyewe. Basi alipozungumza naye (Mfalme) alisema, Hakika wewe leo kwetu umekwishakuwa ni mwenye hishima na muaminiwa.(12:54)Yusufu alimuagiza mjumbe wa mfalme kuwa kabla hajotoka gerezani lijulikane lile shauri la wanawake waliomtaka kwa nguvu na kumchochea aingie katika maasi - Qur’an (12:50). Yusufu(a.s) alitaka hilo lifanyike ili apate kusafika kwa Al-Aziz na kwa jamii nzima kuwa hakumfanyia dhuluma ile aliyosingiziwa.


Mfalme aliwakusanya wanawake na kuwauliza

“...............Nini jambo lenu lilikuwa mlipomtamani Yusufu kinyume cha matamanio yake? wakasema ‘Hasha lillahi! Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mkewe Al-Aziz naye akasema: Sasa haki imedhihirika, mimi ndiye niliyemtamani kinyume cha nafsi yake, na bila shaka yeye yu miongoni mwa wa kweli (kabisa)” (12:51)Baada ya hapo ndipo Yusufu(a.s) alipokubali heshima ile aliyopewa na kupendekeza awe msimamizi wa hazina ya nchi.

Akasema nifanye niwe mtazamaji wa hazina ya nchi; hakika mimi ni mlinzi mzuri na mjuzi hodari (12:55)Tendo hili la Yusufu(a.s) kudai kesi yake na wanawake iangaliwe na Mfalme na haki itolewe, lilinyanyua sana hadhi yake. Kwanza aliifasiri ndoto ngumu ya Mfalme ambayo iliwashinda wachawi, wanganga na watabiri wote wa kutegemewa katika nchi. Pili alipotakiwa na Mfalme atoke gerezani, alikataa mpaka kesi ifikishwe mahakamani, mkosaji abainishwe. Matokeo ya kesi yakawa wanawake kukiri mbele ya hadhara ya Mfalme kuwa Yusufu(a.s) hakuwa na hatia bali wao ndio waliokuwa waovu.Ilidhihiri kwa kila mtu kuwa hakuna yeyote miongoni mwao, ila amezidiwa na Yusufu(a.s) kwa uadilifu na tabia njema kwa ujumla. Haiwi ni kitu cha ajabu basi tunapoona Yusufu anapewa dhamana ya kuangalia hazina yote ya nchi. Huu ni wadhifa unaohitajia mtu aliyepea kwa uadilifu na hakuwepo aliyemzidi Yusufu(a.s).