image

Chokochoko na Upinzani wakati wa khalifa uthman khalifa wa Tatu

KUPOROMOKA KWA DOLA YA KIISLAMU ALIYOICHA MTUME(S.

Chokochoko na Upinzani wakati wa khalifa uthman khalifa wa Tatu

KUPOROMOKA KWA DOLA YA KIISLAMU ALIYOICHA MTUME(S.A.W)


Dola ya Kiislamu ilianza kuporomoka katikati ya Uongozi wa Khalifa ‘Uthman palipotokea fitna iliyowapelekea Waislamu kugombana wenyewe kwa wenyewe kiasi cha kuwafikisha mama wa waumini, Aysha (r.a) mkewe Mtume(s.a.w)na Ali bin Abu Taalib kupambana kijeshi. Fitina hii ilipelekea kuuliwa kwa Uthman na Ali na kusambaratika kwa Dola ya Kiislamu na kuanza uongozi wa Kifalme. Mzizi wa Fitna hii ni Myahudi ‘Abdallah bin Sabaa’ wa Yemen aliyesilimu kinafiki. Ili kupata mafunzo ya kina Waislamu hatuna budi kuipitia kwa makini historia hii ya kusikitisha, iliyopelekea kusambaratika kwa dola ya Kiislamu, katika kipindi cha Khalifa ‘Uthman na Ali.


Upinzani Kutoka Miongoni mwa WaislamuUkhalifa wa Uthman ulichukua miaka 12. Katika miaka sita ya kwanza Dola ya Kiislamu iliimarika na mipaka yake kupanuka . Katika miaka sita aliyomalizia ukhalifa wake kulikuwa hakuna utulivu: Miongoni mwa Waislamu walizusha malalamiko ya uongo dhidi ya Khalifa na Serikali yake. Kiongozi wa kundi hili la wapinzani ni Abdullah Ibn Sanda alijulikana sana kwa jina la Ibn Sanda au Ibn Sabaa. Ibn Sanda alikuwa Myahudi anayetoka Yemen, alisilimu kinafiq kama alivyosilimu Abdallah bin Ubay wa Madinah, lakini ibn Sabaa tangu aliposilimu alikuwa tayari na mpango wake wa kuudhuru Uislamu hatua kwa hatua. Kundi la wanafiqi lililoongozwa na Ibn Sabaa lilitumia shutuma dhidi ya Khalifa na Serikali yake kuficha unafiki wao kwa sababu madai yao yalikuwa ni ya uongo na pale walipopewa maelezo ya kweli waliyafumbia macho na hawakuyakubali.Madai Dhidi ya Khalifa ‘UthmanUpinzani mkubwa ulitokea Misri ambapo Abdallah bin Sa’ad aliteuliwa badala ya Amri bin al As. Abdallah hapana shaka ni ndugu wa Uthman lakini mchango wake katika Uislamu ulikuwa mkubwa sana. Ndiye aliyeanzisha jeshi la majini la Dola ya Kiislamu na ushindi wake Afrika ya kaskazini. Ushindi huu ulionesha kuwa Abdallah bin Sa’ad alikuwa na uwezo wa kuongoza hivyo Khalifa alikuwa sahihi kumpa ugavana na hapana upendeleo hapa. Hata hivyo wanafiki hawa alipovamia Madinah na kudai kuwa hawamtaki Gavana Sa’ad; Khalifa alimbadilisha na kumuweka mtu wanayemtaka, Muhammad bin Abubakar.


Kutokana na maelezo haya ni dhahiri kuwa Khalifa Uthman hakuwa na upendeleo kwa ndugu zake kwa kuwapa nafasi za ugavana. Kama angekuwa nao ni dhahiri asinge waachisha kazi na pale walipokosea kuwachapa. Isitoshe magavana hawa waliteuliwa mwanzoni mwa ukhalifa wake wakati akipendwa kama Khalifa Umar. Ni kweli Uthman aliwavua madaraka baadhi ya magavana kama alivyofanya Umar kwa manufaa ya uislamu.


Dai lingine lililopikwa na wanafiki wa kundi la Sabaa ni matumizi mabaya ya pesa za Serikali (Baitul-mal). Khalifa alisingiziwa kuwa anatumia vibaya pesa za Serikali na kuwapa ndugu zake. Dai hili halikuwa la kweli kabisa kwa Sababu zifuatazo:


Uthman alikuwa tajiri mkubwa Arabia hata akaitwa “Ghanir” (mtu tajiri). Lakini hakuwa tajiri tu lakini anajulikana kwa mchango wake katika njia ya Uislamu wakati wa Mtume(s.a.w.) na baada ya Mtume(s.a.w.) wema wake uliendelea. Katika Ukhalifa wake alitumia mali yake mwenyewe kusaidia maskini na ndugu zake. Katika ukhalifa wake kwa muda wote wa miaka 12 hakuchukua posho kwa ajili ya ukhalifa wake kutoka kwenye Baitul-Mal. Kulikuwa na zogo kubwa wakati Khalifa alipotamka kumpa zawadi Abi Sarh 1/5 ya ngawira ya Afrika ya kaskazini kwa kazi nzito aliyoifanya ya kuteka Afrika kaskazini kama motisha. Jambo hili lilipolalamikiwa na watu, Khalifa alimtaka Sarh arudishe ile ngawira na akafanya hivyo. Vile vile ikasemwa kuwa amemruhusu mpwae Marwan anunue kasma ya Serikali ya mateka. Jambo hili na mengine kuhusu tuhuma hii kama kweli au sikweli tusome hotuba ya Khalifa mwenyewe.


Watu wa Madina wanasema, nina pembe laini kwa ajili ya ndugu zangu na ninawafanyia wema (ninawapendelea ndugu zangu). Lakini kuwapenda kwangu hakuathiri haki ya mtu yeyote. Ninawapa wanachostahili kutokana na mali yangu. Sijafikiria kujihalalishia mali ya Serikali kwa ajili yangu au mtu mwingine yeyote. Wakati wa Mtume, Abubakr na Umar nilitoa mali nyingi ingawa nilikuwa naipenda na bakhili. Hivi sasa niko ukingoni mwa uhai wangu na nimewaachia watoto na ukoo wangu, makafiri wanaeneza madai ya uzushi dhidi yangu. Hakuna mji uliotozwa kodi kwa ajili ya kufuja mali, bali kwa manufaa ya wananchi, Nina hisa ya moja ya tano, lakini sichukui kitu chochote kwa ajili yangu, inatumiwa na Waislamu wanaostahili. Katika mali ya Mwenyezi Mungu hakuna kinachoibwa wala sichukui kitu. Ninaishi kwa kutegemea kipato changu.37


Shutuma nyingine aliyotupiwa Khalifa Uthman ni kuchoma moto Qur’an. Dai hili pia si la kweli. Ukweli ni kuwa Uthman alituma nakala za Qur’an inayotokana na ule msahafu asili na kuamuru nakala nyingine zote zichomwe moto. Alichukua hatua hii kwa sababu zilikuwepo naksi za Qur’an zisizokuwa na mpangilio wa Mtume kwa mujibu wa aya na sura kama Jibrili alivyomuelekeza Mtume. Baadhi ya nakala zilizokuwa nje ya Madina zilikuwa hazikukamilika. Hali kadhalika miandiko tofauti ilileta tofauti. Tofauti nyingine ilikuwa ile ya usomaji. Hivyo ni dhahiri misahafu haikuchomwa na dai hili kama mengine ni la uongo kwani kwa kazi hii Uthman amepewa jina la Jami-ul-Quran (mkusanyaji wa Qur’an).


Hata kazi ya kupanua eneo la Kaaba, na msikiti wa Madina ililaumiwa. Kazi ya upanuzi wa eneo la Kaaba ilianzwa na Umar na Uthman aliiendeleza. Wenye nyumba za karibu zilizovunjwa walikataa kuchukua fidiya, na kuanza kulalamika. Baadhi ya maswahaba walipinga kutumia fedha za Serikali kupanulia msikiti wa Madina na uwanja wa Kaaba. Hata hivyo mnamo mwaka 29 A.H. Uthman aliamua kupanua msikiti wa Madina kwa pesa zake. Magogo ya miti yaliondolewa na kuta zikajengwa kwa matofali. Hebu ona kama sio unafiki na ukafiri kazi ya kurekebisha msikiti na upanuzi wa uwanja wa Kaaba ni vya kulalamikiwa, tena kwa gharama ya Khalifa mwenyewe ?


Lawama nyingine ambayo ni kuhusu mjomba wa Uthman Hakam Ibn Al-Aas ambae alikuwa akiwatendea vibaya jirani zake na kumcheza shere Mtume. Alihamishwa Madina. Baada ya miaka michache Uthman alimuombea kwa Mtume na baada ya kuombwa mara nyingi Mtume aliahidi kulitazama upya suala hilo. Mtume alipokufa jambo hili lilikuwa halijapatiwa ufumbuzi. Uthman aliwaomba Abubakr na Umar wamrejeshe kutoka uhamishoni katika ukhalifa wao, lakini hawakuruhusu. Katika ukhalifa wa Uthman alimrudisha mjomba wake baada ya miaka 17 ya kuishi uhamishoni. Hili nalo limemfanya Khalifa kulaumiwa.


Hadithi zikavumishwa kuwa Khalifa amewanyanyasa baadhi ya maswahaba mfano unaotolewa ni wa Abu Dharr Ghifari. Swahaba huyu alikuwa mchamungu kama maswahaba wengine ila yeye alichukua muelekeo wa kisufi. Kwa imani yake hii alilaumu waliokuwa wanaishi maisha ya kujiweza hasa baada ya watu kupata utajiri kutokana na ngawira. Hali kadhalika alitaka Baitul Mal, pasiwe na salio. Fedha au mali igawiwe na itumike kadiri inavyokuja. alianza kueneza imani yake hii Syria. Gavana wa jimbo la Syria, Amir Muawiya alimuandikia Khalifa kumfahamisha juu ya shughuli za Abu Dharr Ghifari. Khalifa Uthman alimwita Abu Dharr Madinah. Abdallah bin Sabaa alijaribu kumuombea alipokuwa Syria lakini Gavana Muawiya alimwambia imani anayofundisha ni mpya katika Uislamu na nia yake nikuleta mtafaruku miongoni mwa Waislamu.


Abu Dhar alipofika Madinah alijadiliana na Khalifa. Khalifa alimuuliza Abu Dhar: “Watu wakishatekeleza wajibu wao mimi nina mamlaka gani ya kuwataka watoe zaidi?” Abu Dhar alipoona hakuweza kumbadili Khalifa alikwenda kuishi kijiji cha Rabdhah karibu na Madinah na alifia hapo. Wanafiki waligeuza maneno na kusema kuwa Abu Dhar alitakiwa aishi kijijini hapo kwa amri ya Serikali hivyo alinyanyaswa. Ni dhahiri Khalifa hata kama alifanya hivyo alikuwa sahihi kwa vile ni kweli imani ya Abu Dharr haikuwa ya Kiislamu. Inasemekana pia kuwa maswahaba aliowanyanyasa ni pamoja na Ammar bin Yasir na Abdullah bin Masud. Dai hili ni la uongo kama tulivyoonesha. Lakini linathibitika zaidi wakati Abu Ammar alipoteuliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa kwenda mikoani kuchunguza matatizo ya magavana.


Khalifa Uthman anatoka ukoo wa Banu Umayyah wa makureish. Kabla ya kuzaliwa Mtume kulikuwa na kutoelewana baina ya ukoo wa Banu Ummayah na ukoo wa Banu Hashim anaotoka Mtume ambao nao ni wa Kikureish. Wasabaai waliwashawishi ukoo wa Banu Hashim kuwa Khalifa anapendelea ukoo wa Banu Ummaya kwa kuwapa nafasi za juu na kuwaondoa madarakani ukoo wa Banu Hashim.


Dai lingine ambalo halina msingi kama mengine linahusu mashamba ya Serikali ya kuchungia wanyama. Mtume(s.a.w.) alianzisha mashamba ya Serikali ya kuchungia wanyama. Umar aliongeza mawili. Wakati wa Uthman Farasi na ngamia wa Serikali waliongezeka. Kwa sababu hii Khalifa aliongezea mashamba ya kuchungia wanyama ya Serikali. Uzushi ukawa Khalifa ameruhusu ukoo wake wa Banu Ummaya uchungie wanyama wao katika shamba la Serikali.


Wingi wa vita ulilazimisha matumizi makubwa ya fedha kwa kuimarisha jeshi kwa kununua zana na vifaa vya jeshi la majini. Pamoja na ngawira iliyokuwa inatumika kwa kuimarisha jeshi. Uthman alitumia Zaka na Sadaka kuimarisha ulinzi. Wapinzani wake wakashutumu kuwa, Zaka na Sadaqa zina matumizi yaliyotajwa kwenye Qur’an hivyo haikuwa sahihi kutumia kwa kuimarisha jeshi. Hiki ni kichekesho kwani moja ya matumizi ya Zaka na Sadaqa ni kuimarisha dini ya Allah(s.w). Ulinzi nao huimarisha dini ya Allah(s.w). Hata hivyo Khalifa alieleza kuwa alitumia fungu kwa kuliazima na atalirudisha.


Malalamiko mengine yaliyotolewa na wanafiki wale ni kuswali swala kamili bila kupunguza katika Hija, kupiga mahema Minna na kutoza Zaka farasi - mambo ambayo wakati wa Mtume(s.a.w.) wala wa Abubakar na wa Umar hayakufanywa. Kuhusu kutopunguza swala Khalifa alipoulizwa alisema nimefanya hivyo ili wakazi wa maeneo hayo wasidhanie kuwa kupunguza swala ndio utaratibu. Ama kuhusu mahema ni suala la maendeleo na kwa watu wa leo ni jambo halina msingi kabisa. Kwa vile mahema na nyumba za kitalii zinatumika sio Minna tu bali hata Makka. Ama kuhusu farasi kutozwa au kutotozwa Zaka wakati wa Mtume na makhalifa wawili wa mwanzo yaweza kuwa uchache wao na kushiriki kwao kwenye vita. Wakati wa Khalifa Uthman na baada ya mfululizo wa vita hali ya uchumi ya Waarabu ilibadilika na Khalifa aliona ni Busara Zaka pia itolewe kwa farasi kama ilivyo kwa ngamia.


Sababu hasa ya chanzo cha ghasia hatimaye kumuua Khalifa Uthman hazikuanza wakati wa Uthman bali zilianza wakati wa Mtume(s.a.w.). Maadui wa Uislamu wakati wa Mtume walikuwa Maqureysh, Waarabu, Wayahudi, Wapersia na Wakristu wa Kirumi. Baada ya kutekwa Makka koo na makabila mengi yalisilimu, lakini walisilimu kwa nia mbali mbali ambapo hapa hatutazitaja. Linalothibitisha hili ni kule kuukana Uislamu kulikotokea mara tu baada yakutawafu Mtume(s.a.w), uasi ambao uliikumba karibu Arabia yote. Wapinzani hawa walishindwa nguvu wakati wa Abubakar halikadhalika wakati wa Umar. Lakini haiyumkini kuwa walikuwa wameridhika na ustawi wa uislamu. Kwa hiyo hili ni kundi moja ambalo miongoni mwao walitokea wapinzani.


Kundi la pili la wapinzani linatoka kwa wanafiki ambao njama yao ya kumuua Mtume ilitajwa kwenye Qur’an na hila zao kubainishwa mwaka wa 9 Hijria na hiki kilikuwa kipigo kikubwa kwao. Kubadilika kwa sera ya kuwataja wanafiki bayana na Mtume kukatazwa kuwaombea na kuwazika na kutotambulika katika jamii ya Waislamu kulistawisha chuki dhidi ya viongozi wa Waislamu.


Kifo cha Mtume kiliwagawa Waislamu katika makundi matatu. Ukoo wa Mtume(Ahlul Bayt), Muhajirin na Ansaar. Pamoja na kuwekwa sawa hali hii wapo walioendeleza vikundi vyao nyoyoni na hasa pale upinzani ulipochukua umbo la kuonesha makosa Serikalini. Bado lilikuwepo tatizo la watu binafsi. Wapo Waislamu waliojiingiza katika upinzani kwa maslahi yao binafsi. Mfano mzuri ni Muhammad bin Abubakar na Muhammad bin Hudhaifa.


Wayahudi nao hawakusahau kutolewa kwao Madinah na hata huko Khaibar walikohamia bado walitezwa nguvu na kulazimika kulipa Jizya. Makundi yote haya yaliungana kwa kujuana na kutokujuana kwa kusimamisha upinzani dhidi ya Khalifa Uthman na Serikali yake na hatimaye kumuua.
                   
           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Kama unahitaji kuuliza maswali Bofya hapa

Mwandhishi Tarehe 2018-08-01     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 327


Download our Apps
👉1 Madrasa kiganjani     👉2 Kitau cha Fiqh     👉3 Kitabu cha Afya     👉4 kitabu cha Simulizi    

Post zifazofanana:-

NI UPI MKATABA WA AL-FUDHUL NA ASILI YAKE, ATHARI ZAKE NA WALOHUSIKA
MKATABA WA AL-FUDHULBaada ya vita hivi viongozi wa pande mbili hizi waliamuwa wakae chini na wakubaliane kuweka kanun i na utaratibu utakaozuia kutotokea uonevu kama huuu tena. Soma Zaidi...

Kuhifadhiwa kwa Quran
Quran (EDK form 2: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Kuangamia kwa Mtoto na Mke wa Nuhu(a.s)
Tukirejea Qur’an (11:36-48) na (23:26 -29) tunapata maelezo juu ya mchakato wa kuangamizwa makafiri na kuokolewa waumini katika kaumu ya Nabii Nuhu(a. Soma Zaidi...

Mkataba wa 'Aqabah na vipiengele vyake na mafunzo tunayoyapata katika mkataba wa aqaba
Mtume (s. Soma Zaidi...

NI IPI FAMILIA YA MTUME MUHAMMAD (S.A.W) NA NI IPI NASABA YAKE, UKOO WAKE NA KABILA LAKE
FAMILIA YA MTUME (S. Soma Zaidi...

HISTORIA YA NABII MUSA(A.S) NA HARUN(A.S)
Nabii Musa(a. Soma Zaidi...

Yunus(a.s) Kulingania Uislamu kwa Watu Wake
Nabii Yunus(a. Soma Zaidi...

Mambo ya Msingi Aliyofanya Mtume(s.a.w) Katika Kuanzisha Dola ya Kiislamu Madinah.
Mambo ya Msingi Aliyofanya Mtume(s. Soma Zaidi...

MTUME MUHAMMAD (S.A.W) KULELEWA NA BABA YAKE MDOGO MTUME (ABU TALIB)
KULELEWA NA BABA YAKE MDOGOBaada ya kufariki kwa mzee huyu, kiongozi mkubwa wa maquraysh na makkah, kiongozi ambaye jeshi la Abrah liliangamizwa ndani ya utawala wake. Soma Zaidi...

tarekh
MAPIGANO YA AL-FIJAR (MAPIGANO YA UOVU). Soma Zaidi...

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Yusufu(a.s)
“Kwa yakini katika (kisa cha) Yusufu na ndugu zake yako mazingatio mengi kwa wanaouliza (mambo wapate kujua)”. Soma Zaidi...

Mafunzo kutokana na vita vya badri
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...