image

Vipengele vya mkataba wa Hudaibiya na faida zake katika Ukombozi (ufunguzi) wa mji wa Makkah

Vipengele vya mkataba wa Hudaibiya na faida zake katika Ukombozi (ufunguzi) wa mji wa Makkah

Vipengele vya mkataba wa Hudaibiya na faida zake katika Ukombozi (ufunguzi) wa mji wa Makkah

Mkataba wa Hudaybiyah

Mkataba wa Hudaybiyah ni mkataba uliofungwa baina ya Waislamu na Makafiri wa Kiquraish katika kitongoji cha Hudaybiyah kilicho karibu na Makka. Katika mwaka 6 A.H. Mtume(s.a.w) aliota kuwa anafanya ‘Umrah katika nyumba takatifu ya Al-Ka’abah. Kwa kuwa ndoto za Mitume ni agizo la moja kwa moja kutoka kwa Allah(s.w), Mtume(s.a.w) ilibidi atekeleze agizo hilo kwa kuwakusanya Waislamu wapatao 1,400 wa kuongozana naye kwenye msafara wa kuelekea Makka kwa ajili ya ‘Umarah. Makafiri wa Kiquraish waliwazuia Waislamu hao pamoja na Mtume(s.a.w)kuingia Makkah, katika kitongoji cha Hudaybiyah.Mtume(s.a.w) alituma wajumbe wawili, mmoja baada ya mwingine, kuwaomba wakuu wa Maquraish kuwa wawaruhusu waingie Makka na kuwahakikishia kuwa wanaingia kwa amani kwa ajili tu ya kufanya Umarah na hawakuwa na silaha yoyote. Baada ya wajumbe hawa kukataliwa na Maquraish, Mtume(s.a.w) alimtuma mjumbe wa tatu, ‘Uthman bin Affan, ambaye kulingana na heshima yake kwa Maquraish, ilitarajiwa kuwa ujumbe wake ungelikubaliwa. Kinyume chake, ‘Uthman alishikiliwa kwa kitambo kirefu na zikaja tetesi kuwa ameuliwa. Baada ya kupata tetesi hizi Mtume(s.a.w) aliwaita Waislamu chini ya mti na kuchukua ahadi (Bai’yah) kwao ya kulipiza kisasi cha kuuliwa ‘Uthman. Allah(s.w) aliitilia mkazo ahadi hii kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:
Bila shaka wale wanaofungamana nawe, kwa hakika wanafungamana na Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi (hizi) anavunja kwa kuidhuru nafsi yake; na atekelezaye aliyomuahidi Mwenyezi Mungu, (Mwenyezi Mungu) atamlipa ujira mkubwa. (48:10)Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waislamu walipofungamana nawe chini ya mti; na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawapa kushinda kwa zama za karibu. (48:18)Baada ya Waislamu kuchukua bai’yah kwa Mtume(s.a.w) iligundulika kuwa zile tetesi za kuuliwa ‘Uthman zilikuwa za uwongo na ‘Uthman alirudi kutoka kwa Maquraish akiwa salama. Hata hivyo, ilikuwa dhahiri kwa Maquraish kuwa kamwe hawanauwezo wa kuwazuia Waislamu kuingia Makka wakiyakumbuka vyema matukio ya Badr, Uhud na Handaq.Hivyo waliamua kumtuma Suhail bin ‘Amr, kwa niaba yao aje kuweka mkataba wa amani na Mtume(s.a.w) kwa niaba ya Waislamu. Baada ya mjadala mrefu pande zote mbili ziliafikiana kuweka mkataba wa amani wa miaka kumi (10) wenye masharti yafuatayo:

(i) Waislamu warudi Madinah bila ya kufanya ‘Umrah.(ii) Waislamu wanaweza kurudi mwakani (7 A.H) kufanya
‘Umrah lakini wakae Makka siku tatu tu.(iii) Wakija Makka kufanya ‘Umrah wasije na silaha yoyote ila panga ndani ya ala.(iv) Waislamu hawataenda nao Madinah Waislamu
wanaoishi Makka na wala hawatamzuia yeyote miongoni mw ao anayetaka kubakia Makka.(v) Kama yeyote wa Makka atatoroka kwenda Madinah
kusilimu Waislamu hawanabudi kumrudisha(wasimmpokee), lakini yeyote kutoka Madinah akitoroka kwenda Makka Maquraish hawatapaswa kumrudisha Madinah (watampokea).(vi) Makabila ya Kiarabu yatakuwa huru kufanya Itifaki (urafiki) na upande wowote ule (wa Maquraish au wa Waislamu) wanaoupendelea.(vii) Pasiwe na vita kwa kipindi cha miaka kumi baina ya Waislamu na Maquraish na baina ya Waitifaki (Allies) wa Waislamu na waitifaki wa Maquraish.(viii)Hapana ruhusa ya kutengua hata shuruti moja katika hizi kabla ya miaka kumi kupita.Mkataba huu ulitiwa sahihi na Muhammad bin ‘Abdullah (s.a.w) kwa niaba ya Waislamu na Suhail bin ‘Amr kwa nia ya Maquraish. Baadhi ya Waislamu walichukizwa sana na mkataba kutokana na mazingira ya ushabiki na unyanyasaji yaliyodhihirishwa na Maquraish. Suhail alikataa mkataba usianzwe kwa Bismillahir-Rahmaanir-Rahiim, kama ilivyo Sunnah kwa Waislamu katika kuanza kila jambo lao. Pia Suhail alikataa mkataba usiwe baina yake na “Muhammad Rasuulullah”, wao hawamtambui kuwa ni “Rasuulullah” (Mjumbe wa Allah), bali wanamtambua kuwa ni “Muhammad bin Abdullah bin Abd-al- Muttaalib”.Baadhi ya Waislamu pia waliona kuwa baadhi ya vipengele vya masharti ya makataba, hasa kipengele cha tano (5), vilikuwa vikiwanyanyasa na kuwakandamiza Waislamu, kiasi kwamba wengine walifikia hatua ya kumshawishi Mtume(s.a.w) kuwa waukatae mkataba ule. Kwa mfano kabla mkataba kutiwa sahihi na pande zote mbili, Abu Jandal bin Suhail, aliyekuwa akipata mateso kwa ajili ya kusilimu kwake, alimkimbilia Mtume(s.a.w) ili apate salama. Suhail alidai kuwa Abu Jandal arudishwe, kwa mujibu wa kipengele cha tano (5) cha mkataba. Aliporudishwa Suhail alimcharaza viboko vya miba pale pale kadamnas: Umar bin Khattab hakuweza kuvumilia hali ile na alimuuliza Mtume(s.a.w) kwa uchungu: “Wewe si Mtume wa kweli wa Allah(s.w)? Je, sisi hatuko katika njia ya haki?” Mtume(s.a.w) alijibu kuwa yeye ni Mtume wa Allah(s.w) na kuwa wao wako katika njia sahihi, pia alimfahamisha kuwa anafanya kila jambo kama alivyoamrishwa na Allah(s.w).Kwa upande mwingine, machoni mwa Allah(s.w) na Mtume wake na kwa baadhi ya waislamu wenye uoni wa mbali, mkataba ule ulikuwa ni ushindi kwa Waislamu. Mkataba kutoandikwa “Bismillahir-Rahmaanir-Rahiim” na “Muhammad Rasuulullah”, hakukuwapunguzia Waislamu chochote. Vile vile kuteswa kwa akina Abu Jandal ni jambo la muda mfupi. Hivyo, Mtume(s.a.w) alitia sahihi mkataba na akawaamuru Waislamu wachinje na kunyoa pale pale na kurejea zao Madinah. Njiani, kabla ya Waislamu hawajafika Madinah, Mtume(s.a.w) alishushiwa wahay wa kuwapongeza Waislamu kwa ushindi watakaoupata kutokana na mkataba wa Hudaybiyah.
Bila shaka tumekwishakupa kushinda kuliko dhahiri. Ili Mwenyezi Mungu akusamehe makosa yako yaliyotangulia na yanayokuja, na kukutimizia neema zake na kukuongoa katika njia iliyonyooka(48:1-2).


Kusibu kwa Bishara ya Ushindi
“Kushinda kuliko dhahiri” kunakotokana na mkataba wa Hudaybiyah kunabainika katika matukio ya fuatayo:Kwanza, kuwapa fursa Waislamu wa Madinah kubakia Makka au kuja Makka mara kwa mara kufanya Da’awah. Kwa mujibu wa wanahistoria, katika kipindi cha miaka miwili tu ya mkataba wa Hudaybiyah, watu waliosilimu Makka ni wengi zaidi kuliko wale waliosilimu katika miaka yote ya nyuma. Ni katika kipindi hiki walisilimu majemadari wa Kiquraish, Khalid bin Walid na ‘Amr bin al-‘As pamoja na Suhail bin Amr mwenyewe.Pili, maquraish wenyewe waliomba lile sharti la kuwazuia watu wa Makka waliosilimu kwenda Madinah liondolewe kwa sababu wale wote waliokataliwa kujiunga na Waislamu wenzao Madinah, Ibn Abu Jandal na wenzake, waliweka kambi njiani na kuwa kikwazo kikubwa kwa misafara ya biashara ya Maquraish. Maquraish wakaomba waruhusiwe kuingia Madinah ili nao wawe ndani ya mkataba wa amani wa Hudaybiyah.Tatu,Mtume(s.a.w) na Waislamu kwa ujumla walipata fursa ya kulingania Uislamu kwa watu wa karibu na mbali. Ni katika kipindi cha mkataba, Mtume(s.a.w) alituma wajumbe na barua kwa falme mbali mbali za Bara Arab na nje ya Bara Arab. Alikumbusha Waislamu kuwa jukumu la kuufikisha Uislamu kwa watu si lake peke yake bali ni la kila Muislamu. Katika kuwakumbusha hili Mtume(s.a.w) aliwahutubia Waislamu:“Enyi watu! Allah(s.w) amenituma kuwa Rehema kwa wanaadamu (wote) na kuwa Mtume wa ulimwengu mzima. Kwa hiyo, linganieni Uislamu kwa niaba yangu na Allah atakurehemuni. Kwa hiyo nakuusieni msifarikiana kama (watu wa) Isa mwana wa Mariam”21

Baada ya khutuba hii, Mtume(s.a.w) aliteua wajumbe wenye akili (intelligent) na uwezo wa kujieleza, miongoni mwa maswahaba wake na kuwapa barua za kupeleka kwa tawala mbali mbali za nchi za Mashariki ya kati ikiwa ni pamoja na Misri na Uhabeshi. Takriban barua zote zilikuwa na maudhui moja zikizingatia mazingira ya mtawala anayepelekewa. Kwa mfano barua aliyopelekewa Heracleus, mfalme wa Warumi iliandikwa kama ifuatavyo:


Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu; Kutoka kwa Muhammad bin ‘Abdullah kwenda kwa Heracleus,
mfalme wa Warumi (Eastern Roman Empire). Amani iwe juu ya yule anayefuata mwongozo. Baada ya hayo ninakuitia kwenye Uislamu. Ukisilimu utakuwa katika amani na Allah(s.w) atakulipa mara dufu. Lakini ukikataa wito huu madhambi ya raia zako utayabeba. Akanukuu aya ya Qur-an ifuatayo:
“Sema: Enyi watu waliopewa kitabu (Mayahud na Manasara) njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu, ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu wala tusimshirikishe (Mwenyezi Mungu) na chochote; wala baadhi yetu tusiwafanye wengine kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu (au pamoja na Mwenyezi Mungu). Wakikengeuka semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.” (3:64)Nne, Waislamu walipata fursa ya kujiimarisha kiuchumi. Kwa kuondokewa na adui yao mkubwa, makafiri wa Kiquraish, Waislamu waliweza kufanya biashara zao za masafa marefu kwa amani.Tano, Waislamu walipata fursa ya kujizatiti kijeshi na kuwashughulikia maadui zao wengine waliokuwa wakiwakera mara kwa mara. Ni katika kipindi hiki waliwashinda Mayahudi kimoja katika vita vya Khaybar. Pia waliwaonyesha Warumi cha “Mtema kuni” katika vita vya Muttah vilivyopiganwa 7 A.H. Kumbukizi za vita hivi ziliwatia Warumi khofu na woga. Pamoja na ushujaa wao uliofahamika katika ulimwengu wa enzi hizo, waliwakimbia Waislamu katika vita vilivyokuwa vipiganwe Tabuuk.

Sita, Waislamu 2,000 walifanya ‘Umrah pamoja na Mtume (s.a.w), mwaka wa 7 A.H. na ndoto ya Mtume ikawa imesadifu:Kwa yakini Mwenyezi Mungu amemhakikishia Mtume wake ndoto yake ya haki; Bila shaka nyinyi mtaingia katika Msikiti Mtukufu Insha-Allah kwa salama; mkinyoa vichwa vyenu na mkipunguza nywele (kama ilivyo wajibu kufanya hivyo wakati wa Hija). Hamtakuwa na hofu (wakati huo). Na (Mwenyezi Mungu) anajua msiyoyajua. Basi kabla ya haya atakupeni kushinda (kwanza) kuliko karibu (kuwashinda Mayahudi). (48:27)Ni ushindi kwa sababu Mtume(s.a.w) katika ndoto yake hakufahamishwa ni lini atafanya ‘Umrah, japo alijiandaa kuitekeleza katika mwaka wa 6 A.H. Vile vile ni ushindi kwa sababu idadi ya Waislamu waliofanya ‘Umrah mwaka 7 A.H. ni kubwa zaidi kwa watu 600 kuliko wale waliokuwa kwenye msafara wa mwanzo ambao walikuwa 1,400 tu.Saba, baada ya muda mfupi Maquraish waling’amua kuwa mkataba wa Hudaybiyah haukuwa unawanufaisha wao bali kinyume chake. Hivyo waliamua kuuvunja baada ya miaka miwili tu. Mtume(s.a.w) alichukua fursa ile ya kuvunjika kwa mkataba kuikomboa Makka. Katika kuikomboa Makka hapakutakiwa kutokee mapigano, kwani ingelikuwa vigumu kuwatambua Waislamu walioko Makka ambao walisilimu katika miaka miwili ya mkataba na wale walioshindwa kuhamia Madinah kutokana na sababu za msingi. Hivyo Mtume(s.a.w) aliandaa jeshi kubwa la askari 10,000 kwa siri kisha likaja kuzingira Makka ghafla bila Maquraish kupata habari. Abu Sufyan, kiongozi wa Makka wakati huo, Ramadhani, 8 A.H, ilibidi asalimu amri na kuwaachia Waislamu kuikomboa na kuitwaharisha Ka’abah bila ya upinzani.Nane, ukombozi wa Makka,(Fat-h Makka) ulikuwa ndio kilele cha ushindi kwani, takriban viongozi wote wa Maquraish walisilimu, akiwemo Abu Sufyan na mkewe Hindu bint ‘Utbah aliyekuwa adui nambari “one” wa Mtume(s.a.w). Kusilimu kwa viongozi wa Makka kulichangiwa sana na ile tabia ya usamehevu na huruma aliyoonesha Mtume(s.a.w). Baada ya kuikomboa Makka alitangaza kuwa wamesamehewa wote kwa yale yote waliyowafanyia Waislamu kwa kipindi cha miaka 21 iliyopita kama Nabii Yusufu(a.s) alivyowasamehe ndugu zake.

Akasema (Yusufu): “Hakuna lawama juu yenu leo; Mwenyezi Mungu atakusameheni, naye ni Mwenye rehema zaidi kuliko wanaorehemu (wote).” (12:92) Kwa msamaha huu viongozi wa maquraish waliyakinisha kuwa Muhammad(s.a.w) ni Mtume wa Allah aliye rehema kwa walimwengu wote.

Nasi hatukukutuma, (hatukukuleta) ila uwe rehema kwa walimwengu (wote). (21:107)

Kusilimu kwa wakuu wa kabila tukufu la Quraish, kulipelekea makabila mengi ya Kiarabu kuja kusilimu kwa Mtume(s.a.w) makundi kwa makundi.Tisa, Baada ya Fat-h Makka dola ya Kiislamu ilitanuka. Katika kuimarisha Dola, Mtume(s.a.w) aliigawanya katika majimbo matano na kwa kila jimbo aliteua viongozi watatu wafuatao:

(1) Mkuu wa Jimbo - Walii (Gavana) (2) Kadhi – Hakimu.
(3) Amil – Mkusanyaji na mgawaji Zakat

Mtume(s.a.w) alikuwa mkuu wa Jimbo la Madinah.Mafunzo Yatokanayo na Mkataba wa Hudaybiyah.
Kutokana na mkataba wa amani wa Hudaybiyah tunajifunza kuwa:

(i) Mazingira ya amani ni jambo muhimu mno katika kuleta maendeleo ya aina yoyote. Hivyo, ni vyema kukimbilia mapatano kuliko mapambano.(ii) Katika kutafuta suluhu, lazima tuwetayari kupoteza
maslahi madogo madogo kama vile kuacha “Bismillah” na “Rasuulullah” kwenye mkataba wa Hudaybiyah, ili kujenga mazingira yatakayotuwezesha kufikia lengo kuu la Uislamu kuwa juu ya tawala zote:
Yeye ndiye aliyemtuma, (aliyemleta) Mtume wake kwa uwongofu na dini iliyo ya haki, ili aishindishe juu ya dini zote. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi. (48:28)(iii)Waislamu tuwe wepesi katika kutumia fursa zinazopatikana.
Mtume(s.a.w) alikuwa mwepesi mno katika kutumia fursa. Kwa mfano Mtume(s.a.;w) alitumia fursa ya kuvunjika mkataba wa Hudaybiyah kuikomboa Makka kabla Maquraish hawajajiweka sawa.                   

           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 947


Sponsored links
👉1 kitabu cha Simulizi     👉2 Kitau cha Fiqh     👉3 Kitabu cha Afya     👉4 Madrasa kiganjani    

Post zifazofanana:-

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Bani Israil
Soma Zaidi...

HISTORIA YA NABII SULEIMAN
Soma Zaidi...

Vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kif cha khalifa Uthman
Soma Zaidi...

Maana ya Funga ya ramadhani kisheria na Aina za funga
Amesema mtume (s.a.w) kuwa Allah (s.w) amesema: kila amali ya mwanaadamu ni kwa ajili yake isipokuwa funga. Soma Zaidi...

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Ismail(a.s)
Kutokana na Historia ya Nabii Ismail(a. Soma Zaidi...

Kujengwa upya al Kabah baada ya kuwa na mipasuko.
Sira na historia ya Mtume Muhammad s.a.w sehemu ya 18. Hapa utajifunza kuhusu tukio la kujengwa upya kwa al kaaba 🕋 Soma Zaidi...

Hadhi na haki za Mwanamke katika jamii za Mashariki ya Kati bara la arabu hapo zamani
Soma Zaidi...

HISTORIA YA KUUMBWA KWA NABII ADAMU (A.S)NA HADHI YAKE NA HADHI YA WANAADAMU DUNIANI
Adam(a. Soma Zaidi...

Darsa za Sira historia ya Mtume (s.a.w) Jaribio la 03
Soma Zaidi...

Kukomeshwa kwa Riddah na Chokochoko Nyingine katika dola ya kiislamu
Soma Zaidi...

TAREKH, HISTORIA NA SIRA YA UISLAMU NA MTUME MUHAMMAD KUTOKA KUZALIWA MPAKA KUFARIKI NA HARAKATI ZAKE
1. Soma Zaidi...

Mateso waliyoyapata waislamu wa mwanzo Maka, na orodha ya waislamu walioteswa vikali
Pili, Maquraish walimuendea Mtume(s. Soma Zaidi...