Hija ya Kuaga

Mwaka mmoja baada ya msafara wa Tabuuk Bara Arab zima ilikuwa chini ya Dola ya Kiislamu. Kutokana na ujumbe wa Suratun- Nasr, sura ya mwisho kushuka, iliyoshuka baada ya Fat-h-Makka, na ukizingatia makundi ya watu kutoka makabila mbali mbali yalivyomininika Madinah kuja kusilimu na kujifunza Uislamu, baada ya msafara wa Tabuuk, ilikuwa wazi kwa Mtume(s.a.w) kuwa ujumbe wake umekamilika na kazi yake ya Utume imekaribia kwisha.Itakapofika nusura ya Mwenyezi Mungu na kushinda. Na ukawaona watu wakiingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi. Basi hapo mtakase Mola wako pamoja na kumsifu, umuombe maghufira (msamaha); hakika Yeye ndiye Apokeaye toba. (110:1-3)Mtume(s.a.w) hakuweza kushiriki kwenye Hija ya kwanza iliyofanyika 9 A.H. kutokana na shughuli nzito aliyokuwa nayo ya kupokea makundi kwa makundi ya makabila mbali mbali yaliyomiminika Madinah kuja kusilimu. Badala yake alimteua Abubakar kuongoza msafara wa Hija hiyo. Mwaka 10 A.H. Mtume(s.a.w) alinuia kufanya Hija kubwa na kuwajumuisha Waislamu wengi iwezekanavyo. Alituma wajumbe kwenda kwenye kona zote za Bara Arab kuwatangazia Waislamu kuwa waje kujiunga naye kwenye msafara wa Hija. Waislamu waliitikia wito na waliojiunga na msafara wa Hija ya Mtume kutoka Madinah ni 100,000 na jumla ya Waislamu waliosimama Arafa mwaka ule ni 120,000.

Hutuba ya Mtume(s.a.w) Katika Uwanja wa ‘Arafa, 9 Dhul-Hijjah 10 A.H.

Mchana wa 9 Dhul-Hijjah, Mtume(s.a.w.) akiwa juu ya ngamia wake alitoa hutuba ya kihistoria kwa mkusanyiko wa Waislamu laki moja na zaidi kama ifuatavyo:“Sifa zote anastahiki Allah, Tunamshukuru na tunamtaka msaada na msamaha na tunatubu kwake, Tunajikinga kwa Allah (s.w.) kutokana na uovu wetu na kutokana na ubaya unaotokana na matendo yetu (maovu). Hapana awezaye kumpoteza aliyeongozwa na Allah na hapana awezaye kumuongoza aliyepotezwa na Allah. Ninashuhudia kuwa hapana Mola ila Allah pekee asiye na mshirika. Ninashuhudia kuwa Muhammad ni mja na Mtume wake. Ninawausia enyi waja wa Mwenyezi Mungu, kumcha Mwenyezi Mungu na ninakusisitizeni kumtii Allah. Ninafungua khutuba yangu hii, na lile lililo zuri”.“Enyi watu, sikilizeni ujumbe ninaokupeni. Sijui kama nitapata fursa nyingine ya kukutana na nyinyi baada ya mwaka huu.“Enyi watu, hakika damu yenu (yaani uhai wenu), mali zenu na heshima yenu ni vitu vitukufu, katu visiharibiwe hadi mtakaposimamishwa mbele ya Mola wenu, kwani utukufu wa vitu hivyo ni kama ilivyo utukufu wa siku hii, wa mwezi huu na wa mji huu. Kwa hakika mtakutana na Mola wenu na atakuulizeni juu ya vitendo vyenu. Je, nimefikisha ujumbe? Ewe Mwenyezi Mungu shuhudia”.“Hivyo, kila aliye na amana yoyote, hana budi kumrejeshea mwenyewe”

“Kumbukeni, hakuna atakayebeba lawama kwa kosa lolote isipokuwa yule aliyelitenda kosa hilo. Mtoto hawezi kulaumiwa kwa kosa la baba wala baba kwa kosa la mwanawe”.“Enyi watu, yasikilizeni maneno yangu na yazingatieni. Fahamuni kuwa Muislamu ni ndugu wa Muislamu, na Waislamu wote ni ndugu wamoja. Si halali kwa Muislamu kuchukua chochote kutoka kwa nduguye Muislamu isipokuwa kile alichoruhusiwa. Hivyo msioneane. Yaa Allah, nimefikisha ujumbe?”“Fahamuni, mambo yote ya ujahili yamewekwa chini ya nyayo zangu. Visasi vya damu vya zama za jahiliya vimeondolewa. Hakika, kisasi cha damu cha kwanza ninachokifuta ni kile cha Ibn Rabi’ah ibn Harith aliyelelewa na kabila la Sa’d na ambaye Wa-Hudhail walimwua.Riba za kipindi cha jahiliya zimefutwa. Lakini mtapata mtaji wenu. Msidhulumu nanyi hamtadhulumiwa. Allah amekataza riba. Riba ya kwanza ninayoifuta ni ile ya Abbas ibn Abdul Muttalib. Imefutwa moja kwa moja.“Enyi watu, mcheni Allah kuhusiana na wanawake. Mmewaoa kwa amana ya Allah na mnawaingilia kwa amri ya Allah.Hakika mnazo haki kutoka kwao na wanawake wanazo haki kutoka kwenu. Haki zenu kwao ni kwamba wasimruhusu mtu yeyote kuvuruga vitanda vyenu na wasimruhusu mtu yeyote msiyemridhia kuingia katika nyumba zenu. Wakifanya hivyo Allah amewaruhusu nyinyi kuwakemea, kutengana nao vitanda na kuwapiga lakini siyo kwa nguvu, wakijirekebisha basi na wapewe kwa haki chakula chao na mavazi yao kutoka kwenu.Yapokeeni kwa wema mafundisho haya juu ya wanawake. Kwani wao ni wasaidizi wenu. Hawamiliki kwa ajili ya nafsi zao chochote, nanyi hamwezi kumiliki chochote kutoka kwao kisichokuwa hicho. Wakikutiini basi kaeni nao kwa wema. Je, sijafikisha ujumbe?“Enyi watu, msikilizeni na mtiini Amiri anayetekeleza kitabu cha Allah miongoni mwenu hata kama atakuwa ni mtuwa wa Kihabeshi”.“Enyi watu, hakika Allah amekadiria kila mtu riziki yake. Wasia haujuzu kwa mrithi na wasia si halali ukiwa zaidi ya theluthi ya mali”.
“Mtoto ni wa kitanda cha halali na mzinifu arujumiwe. Mtu anayejinasibisha (ukoo wake) kwa asiyekuwa baba yake humshukia laana ya Allah, Malaika na watu wote. Allah hatakubali kutoka kwa mtu kama huyo toba wala amali njema. Enyi watu, shetani amehuzunishwa sana kwa kutoabudiwa tena katika hii nchi yenu. Lakini anatosheka na kule kutiiwa katika mambo ambayo nyinyi mnadhani ni madogo. Hivyo kuweni waangalifu sana katika dini yenu.Kwa hakika nimekuachieni vitu viwili ambavyo iwapo mtavishika katu hamtapotea – Kitabu cha Allah na Sunnah za Mjumbe wake.

“Enyi watu, Jibril amenijia, amenisomea salaam kutoka kwa Mola wangu na amesema, Hakika Allah amewasamehe watu wa ‘Arafat na wa Ka’abah na amechukua dhamana ya kuwasamehe upungufu wao”.‘Umar-ibnul Khattab akasimama na kuuliza: “Ya Rasulullahi, msamaha huo ni kwa ajili yetu sisi tu?” Akajibu: “Ni kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale watakaokuja baada yenu hadi siku ya Kiyama”.“Na mtaulizwa juu yangu, mtajibu vipi?” Wakasema: “Tunashuhudia kwamba umefikisha ujumbe, umetimiza wajibu wako na umetunasihi.”

Halafu akasema hali ya kuwa amekiinua kidole chake cha pete na kukielekeza mbinguni: “Ya Allah shuhudia, Yaa Allah, Shuhudia, Yaa Allah, Shuhudia”.22Baada ya hutuba hii Mtume(s.a.w.) alimuamuru Bilal atoe adhana kisha wakaswali jamaa ya Adhuhuri pamoja na Asr kwa rakaa mbili mbili (Qasr). Baada ya swala Mtume(s.a.w.) alishushiwa Wahay unaokamilisha kazi yake na akasoma aya hiyo mbele ya watu wote waliohudhuria Hija mwaka ule:


“...........Leo waliokufuru wamekata tamaa katika dini yenu, basi msiwaogope bali niogopeni mimi. Leo nimekukamilishieni dini yenu na kukutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe Dini yenu............” (5:3)

Pamoja na nasaha nzito alizotuachia katika khutuba yake ya kuaga, Mtume(s.a.w) alimalizia kwa kuwatumainisha Waislamu wa zama zote:

“Kwa hakika nimekuachieni vitu viwili ambavyo iwapo mtavishika katu hamtapotea – Kitabu cha Allah na Sunnah za mjumbe wake.”