(i) Suratul- ‘Alaq (96:1-5)“Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba Aliyemuumba mwanaadamu kwa ‘alaq.
(i) Suratul- ‘Alaq (96:1-5)
“Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba Aliyemuumba mwanaadamu kwa ‘alaq. Soma na Mola wako ni karimu sana. Ambaye amefundisha kwa msaada wa kalamu. Amemfundisha mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui.” (96:1-5)
Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa Amri ya kwanza aliyopewa Mtume(s.a.w), na kwa hiyo waumini wote wa Ummah wake, ni kusoma au kutafuta elimu kwa ajili ya Allah(s.w). Kusoma kwa jina la Allah ni kusoma kwa lengo la kumuwezesha muumini kumjua na kumuabudu Mola wake vilivyo kisha kusimamisha Ukhalifa katika jamii.
Katika mazingira ya kupewa amri hii ya kwanza, pale pangoni Hira katika kilima cha Nuur (Jabal-Nuur), Mtume(s.a.w) alishinikizwa kusoma na Malaika Jibril kwa kumbana (kumkumbatia kwa nguvu) mara tatu pale alipojitetea kuwa hajui kusoma. Kubanwa huku kwa Mtume(s.a.w) na Malaika Jibril kunaashiria kuwa elimu kwa waumini ni amri ya kwanza inayotakiwa kutekelezwa kwa hima na kwa taklifu kubwa.
Hivyo Elimu ni amri ya kwanza inayotakiwa itekelezwe kwa juhudi na bidii zote. Ndiyo silaha kuu itakayowawezesha waumini kupata ushindi wa kusimamisha Uislamu katika jamii. Tukirejea nyuma katika historia, takrima ya kwanza aliyofanyiwa Adam(a.s) na Mola wake, ili kuandaliwa kuwa khalifa wa Allah(s.w) hapa duniani ni kufundishwa majina ya vitu vyote. Majina ya vitu vyote inaashiria fani zote za Elimu anazohitajia binaadamu ili aweze kuwa kiongozi wa dunia kwa niaba ya Allah(s.w). Pia tunajifunza kuwa chanzo cha fani zote za elimu ni Allah(s.w).
(ii) Suratul-Muzzammil (73:1-10)
“Ewe uliyejifunika maguo simama usiku kucha (kuswali) ila muda mdogo (tu hivi). Nusu yake au upunguze kidogo au uzidishe na soma Qur-an vilivyo. (73:1-4)
Hakika sisi tutakuteremshia kauli nzito. Hakika kuamka usiku kunawafikiana zaidi na moyo na maneno yake yanatuwa zaidi. Hakika mchana unashughuli nyingi. Na litaje jina la Mola wako na ujitupe kwake kwa kweli. (73:5-8)
(Yeye Ndiye)Mola wa mashariki na magharib, Hapana Mola ila yeye, basi mfanye kuwa mlinzi wako. Na subiri juu ya hayo wayasemayo na uwaepuke mwepuko mwema.” (73:9-10)
Aya ya kwanza ya sura hii inaashiria kuwa huu ni wahyi wa mwanzo mwanzo uliofuatia wahyi wa kwanza. Katika Hadith iliyosimuliwa na Bibi Aysha(r.a), tunafahamishwa kuwa Mtume(s.a.w) alistushwa sana na lile tukio la Pangoni Hira, la kulazimishwa kusoma na Malaika Jibril ambaye ilikuwa ni mara yake ya kwanza kukutana naye. Mtume(s.a.w) alirudi nyumbani akiwa anatetemeka kama mtu mwenye homa kali. Alimuomba mkewe Khadija amfunike nguo nzito(shuka). Baada ya muda hali ile ya khofu iliisha na kuweza kumhadithia mkewe yale yaliyomtokea. Alipomuona tena Jibril(a.s) anamjia kumletea wahay uliomo mwanzoni mwa sura hii (73:1-10) Mtume(s.a.w) alistuka tena na kujaribu kujihami asijefikwa na yale yaliyo mfika pangoni kwa kujifunika tena nguo. Lakini bado Jibril alimuendea Mtume(s.a.w) katika hali ile ile ya kujifunika na kumfikishia ujumbe huu wenye kumuamrisha kufanya yafuatayo:
1. Kusimama kwa swala ya usiku kwa kitambo kirefu kati ya saa 4 au theluthi (1/3) hadi saa 8 au theluthi mbili (2/3) za usiku.
2. Kusoma Qur-an kwa mazingatio.
3. Kumdhukuru au kumkumbuka Allah(s.w) kila wakati.
4. Kujitupa kwa Allah kikweli (kumtii Allah kwa unyenyekevu)
5. Kumfanya Allah kuwa mlinzi (wakili) pekee.
6. Kufanya subira juu ya yale wayasemayo makafiri na kuwaepuka mwepuko mwema.
Imebainishwa wazi kuwa Mtume(s.a.w) amepewa amri hizi ili iwe maandalizi ya kupokea kauli nzito. Kauli nzito si nyingine ila lile lengo aliloletwa kwalo la kusimamisha Uislamu katika jamii.
Yeye ndiye aliyemleta Mtume wake kwa uongofu na Dini ya haki ili aijaalie kushinda (Dini hii) Dini zote, ijapokuwa watachukia hao washirikina. “(9:33)
Kuchukia kwa washirikina kunaashiria mapambano.
(iii) Suratul-Muddaththir (74:1-7)
Ewe uliyejifunika maguo. Simama uonye (viumbe). Na Mola wako umtukuze. Na nguo zako uzisafishe. Na Mabaya yapuuze, (endelea kuyapuuza). Wala usiwafanyie ihsani (viumbe) ili upate kujikithirishia (wewe hapa duniani). Na kwa ajili ya Mola wako fanya subira (kwa kila yatakayokufika). ( 74:1-7)
Muda mfupi baada ya kupewa amri sita zilizomo katika suratul-Muzzammil(73:1-10) na kuanza kuzitekeleza, Mtume (s.a.w)akiwa katika hali ile ile ya kujifunika funika aliamrishwa tena na Mola wake, ili kumalizia kazi ya maandalizi, kufanya yafuatayo:
1. Kusimama na kuonya – kulingania Uislamu.
2. Kumtukuza Allah.
3. Kutakasa nguo.
4. Kupuuza mabaya.
5. Kufanya ihsani kwa ajili tu ya kutafuta radhi za Allah(s.w).
6. Kufanya subira kwa ajili ya Allah.
Mafunzo Yatokanayo na Maandalizi ya Kimafunzo
Kutokana na maandalizi haya ya awali aliyopewa Mtume(s.a.w) mwanzoni mwanzoni mwa Utume wake tunajifunza kuwa ili tuweze kusimamisha Uislamu katika jamii kama alivyofanikiwa kuusimamisha Mtume(s.a.w) na maswahaba zake , tunajifunza yafuatavyo:
(i) Elimu katika Fani zote
Ukiacha ila ya uchawi iliyoharamishwa,ndio nyenzo ya msingi ya kutuwezesha kusimamisha Uislamu katika jamii. Hivyo Waislamu hawanabudi kutilia mkazo suala la elimu na kuandaa mitaala na mazingira yatakayowezesha kuielimisha jamii kwa lengo la kusimamisha Ukhalifa katika ardhi.
(ii) Kisimamo cha usiku
Ni nyenzo kuu ya pili inayofuatia katika maandalizi ya kusimamisha Uislamu katika jamii. Allah(s.w) anatubainishia kuwa hekima ya kupewa amri ya kisimamo cha usiku (Qiyamullayl) ni ili tupate maandalizi ya “Ukomandoo” (Ujasiri wa nafsi) yatakayotuwezesha kukabiliana na suluba (misuko suko) ya kusimamisha Uislamu katika jamii. Allah(s.w) anabainisha pia kuwa maandalizi haya hayafai mchana ila usiku kwa sababu kuna mazingira mazuri ya utulivu yatakayompelekea huyu askari wa Allah kuwa na khushui (unyenyekevu) ya hali ya juu inayohitajika kuomba hidaya na msaada kutoka kwa Allah(s.w). Pia kuamka usiku na kukatisha utamu wa usingizi katika theluthi ya mwisho ya usiku, humpa Muislamu zoezi la uvumilivu na subira. Hivyo, ni wazi kuwa, kisimamo cha usiku, kikitekelezwa vilivyo, kinauwezo mkubwa wa kumfanya Muislamu awe na ujasiri wa kusimamisha Uislamu katika jamii kwa hali yoyote iwayo. Hivyo kwa waumini wa kweli, wanaojua kuwa wanadhima ya kuusimamisha Uislamu katika jamii na kuuhami usiporomoke baada ya kusimama, kisimamo cha usiku, si jambo la khiari kwao kama Mola wao
anavyowatanabahisha:
Je, afanyae Ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama na kuogopa Akhera na kutarajia rehema ya Mola wake (ni sawa na asiyefanya hayo)? Sema: “Je, wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua?” Wanaoatanabahi ni wale wenye akili tu. “(39:9)
Pia tunafahamisha katika Qur’an kuwa miongoni mwa sifa za waja wa Allah(s.w) ni kusimama usiku.
“Na wale wanaopitishas baadhi ya saa za usiku kwa ajili ya Mola wao kwa kusujudu na kusimama”(25:64)
Hakika wanao ziamini aya zetu ni wale tu ambao wanapokumbushwa kwazo huanguka kusujudu na kumtukuza Mola wao kwa sifa zake, nao hawatakabari.
Huinuka mbavu zao kutoka vitandani wakati wa usiku ili kumuambudu Mola wao kwa kuogopa moto na kutarajia pepo; na kutoa katika yale tuliyowapa.”(32:15-16)
Pia tunafahamishwa na Mola wetu kuwa kuamka usiku hupandishwa cheo.
Na katika usiku jiondoshee usingizi(kidogo) kwa kusoma hiyo Qurani ndani ya Sala). Hiyo ni (ibada) zaidi kwako. Huenda Mola wako akakuinua cheo kinichosifika. (17:79)
(iii) Kusoma Qur-an kwa mazingatio
Kusoma Qur’an kwa mazingatio kwa lengo la kuifanya kuwa dira pekee ya maisha yetu ya kila siku, ni nyenzo nyingine itakayotuwezesha kusimamisha Uislamu katika jamii. Uislamu ni mfumo wa maisha wa kutii na kufuata utaratibu wa kuendesha maisha ya kibinafsi na ya kijamii anaouridhia Allah(s.w).
Utaratibu huu wa maisha anaouridhia Allah(s.w) umeainishwa na Qur-an, kitabu chake cha mwisho. Hivyo, waumini wa kweli; ili waweze kusimamisha Uislamu katika jamii, hawanabudi kuisoma Qur-an kwa mazingatio kiasi cha kuweza kuielewa vilivyo na kuifanya mwongozo wa kukiendea kila kipengele cha maisha ya kibinafsi na ya kijamii. Vile vile jamii ya Waislamu hainabudi kuandaa mtaala wa kufundisha Qur-an kwa lengo la kuwaandaa wasomaji wa rika zote kuwa Makhalifa wa Allah(s.w).
(iv)Kumdhukuru na kumtukuza Allah(s.w)
Kumdhukuru Allah(s.w) na kumtukuza ni nyenzo nyingine muhimu itakayowawezesha waumini kusimamisha Uislamu katika jamii. Ili Waislamu wawe na msimamo thabiti, hawanabudi kuwa na yakini juu ya kuwepo Allah(s.w) na sifa zake tukufu. Imani ya kweli juu ya Allah(s.w) inathibitishwa na matendo ya Muumini ya kila siku pale atakapofuata maagizo na kuchunga mipaka ya Allah(s.w) katika kukiendea kila kipengele cha maisha yake.
(v) Kujitupa kwa Allah kwa kweli
Kujitupa kwa Allah kwa kweli au kumtii Allah(s.w) kwa unyenyekevu, ni nyenzo nyingine ya kumuwezesha Muumini kusimamisha Uislamu katika jamii. Pamoja na kuwa kusimamisha
Uislamu ni “kauli nzito” (jambo zito), Muumini mwenye kujitupa kwa Allah kwa kweli, hatamchelea yeyote awaye au lolote zito liwalo, katika kutekeleza amri ya Allah(s.w) iliyombele yake.
(vi)Kumfanya Allah kuwa Mlinzi Pekee
Kumfanya Allah(s.w) kuwa Mlinzi Pekee ni nyenzo nyingine inayompa Muumini ujasiri wa kusimamisha Uislamu katika jamii. Kuwa tegemezi kwa Allah(s.w) ambaye ni Al-qahhaaru (mwenye nguvu juu ya kila kitu) humfanya Muislamu asichelee kizuizi au nguvu yoyote inayozuia Uislamu kusimama.
(vii)Kusimama na kuonya
Kusimama na kuonya ni amri ya kuwalingania watu juu ya upweke wa Allah(s.w) kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na kisha kuwafahamisha namna ya kumuabudu Allah(s.w) pekee katika kila kipengele cha maisha. Baada ya kufikisha ujumbe huu wa Tawhiid, kwa hekima na mawaidha mazuri (rejea Qur-an 16:125), Mtume na Waumini kwa ujumla wanaamrishwa kuwaonya watu juu ya adhabu kali itakayowafika wale wote watakaoishi kinyume cha Tawhiid – katika maisha ya akhera.
Pia amri hii ya kuwaonya watu inakwenda sambamba na kuwabashiria malipo mema watakayopata wasimamishaji wa Tawhiid katika maisha ya akhera. Kuufundisha Uislamu na kuweka wazi faida itakayopatikana kwa wale watakaoufuata vilivyo na hasara itakayowafika wale watakaoukanusha, ni hatua muhimu na ya msingi mno katika harakati za kusimamisha Uislamu katika jamii.
(viii)Kutakasa nguo
Kutakasa nguo ni amri inayoashiria kuwa mwenye kulingania
Uislamu anatakiwa awe mfano wa kuigwa kwa tabia njema. Pamoja na mlinganiaji kutekeleza amri ya kutakasa nguo zake na mwili wake ili awe kivutio kwa watu atakaokutana nao katika harakati za kulingania Uislamu, anatakiwa awe na tabia njema itakayovuta usikivu wa watu. Katika kutekeleza amri hii Mtume(s.a.w) alikuwa akipendelea vazi jeupe na kujipaka manukato ili asiwe kero kwa watu kutokana na harufu mbaya inayotokana na nguo chafu na majasho.
Sambamba na usafi huu wa nguo na mwili, Mtume(s.a.w) alikuwa na tabia njema kabisa.
“Na bila shaka una tabia njema kabisa.” (68:4)
Mlinganiaji kuwa kiigizo kwa tabia inasisitizwa katika aya zifuatazo:
Enyi mlioamini! Mbona, (kwa nini) mnasema msiyoyatenda? Ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu kusema msiyoyatenda. (61:2-3)
(ix)Kupuuza Mabaya
Kupuuza Mabaya ni pamoja na kutojali au kutokatishwa tamaa na mabaya unayofanyiwa na maadui wa Uislamu. Pia amri hii ya kupuuza mabaya ni pamoja na kujiepusha kuyafanya, kutoyathamini maovu hatakama yanafanywa na watu maarufu na kuyachukia. Kupuuza mabaya ni nyenzo nyingine muhimu katika kusimamisha Uislamu. Kama muumini hatakuwa na tabia ya kupuuza mabaya anayofanyiwa na maadui wa harakati za kusimamisha Uislamu, atafikishwa mahali pakukatishwa tamaa na kususa harakati.
(x) Kufanya ihsani kwa ajili tu ya kutafuta radhi za Allah(s.w)
Kufanya ihsani kwa ajili tu ya kutafuta radhi za Allah(s.w) ni amri inayowataka wanaharakati wa kuhuisha na kusimamisha Uislamu katika jamii wasitegemee malipo ya kazi hii kutoka kwa watu bali wategemee malipo yao kutoka kwa Allah(s.w). Kazi ya kusimamisha Uislamu katika jamii, Allah(s.w) ameifananisha na biashara kati yake na waumini ambapo waumini wanamuuzia Allah(s.w) mali zao na nafsi zao, naye Allah awalipe malipo makubwa yanayobainishwa katika aya zifuatazo:
Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao (watoe nafsi zao na mali zao katika kupigania Dini) ili na yeye awape Pepo. Wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu; wanaua na wanauawa. Hii ndiyo ahadi aliyojilazimisha (Mwenyezi Mungu) katika Taurati na Injili na Qur-an. Na ni nani atekelezaye zaidi ahadi yake kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyofanya naye (Mwenyezi Mungu). Na huko ndiko kufuzu kukubwa. “(9:111)
Enyi mlioamini! Je! Nikujulisheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iumizayo? (Biashara yenyewe ni hii) Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganieni Dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu. Haya ni bora kwenu ikiwa mnajuwa (61:10-11)
(xi) Kufanya Subira kwa ajili ya Allah
Kufanya Subira kwa ajili ya Allah ni nyenzo nyingine ya msingi itakayowawezesha Waumini kusimamisha Uislamu katika jamii. Katika harakati za kusimamisha Uislamu katika jamii, kuna kero na bughudha nyingi zinazoandaliwa na kusimamiwa na wapinzani wa Uislamu. Ukirejea historia ya Mtume(s.a.w), kero hizi huanza na kujenga mazingira ya kukatisha tamaa. Katika mazingira hayo, Mtume(s.a.w) aliitwa mwongo, mwenda wazimu, mtunga mashairi, mchawi, aliyepagawa, mkatikiwa na kheri (Abtari), n.k.
Katika mazingira ya sasa makafiri wanajitahidi kuwa katisha tamaa wanaharakati kwa kuwaita siasa kali (fundamentalist), mashabiki wa Kidini (fanatics), magaidi (terrorists), n.k. Allah(s.w) anatuamrisha tusubiri juu ya hayo wayasemayo dhidi yetu na tuwaepuke mwepuko mwema. Kuwaepuka mwepuko mwema ni kuyapuuza hayo wayasemayo dhidi yetu na tusilumbane nao ili wasije kututoa katika agenda yetu. Jibu la tusi kwa muungwana ni “hewala” na jibu la muumini kwa jahili ni “salama”.
“Na waja wa Rahmani, ni wale wanaokwenda ulimwenguni kwa unyenyekevu; na majahili wakisema nao (maneno mabaya) huwajibu (maneno ya) salama.” (25:63).
Tukirejea historia, baada ya makafiri kushindwa kuzuia harakati za kusimamisha Uislamu kwa maneno ya kukatisha tamaa, waliandaa nguvu za kuzuia Uislamu kwa matendo kama vile kutesa, kufunga gerezani, kufukuza nchini na kuua. Haya ndiyo mazingira halisi katika harakati za kusimamisha Uislamu na ndiyo sunnah ya harakati aliyoiweka Allah(s.w) kama anavyotukumbusha:
Na namna hii tumemfanyia kila Nabii maadui; (nao ni) mashetani katika watu na (mashetani katika) majini. Baadhi yao wanawafunulia wenziwao maneno ya kupambapamba ili kuwadanganya. Na kama Mola wako angalipenda wasingalifanya hayo, (angewalazimisha kwa nguvu kutii). Basi waache na uwongo wao. (6:112)
Je! umeipenda hii post?
Ndio Hapana Save post
Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Topic: Sira Main: Post File: Download PDF Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 553
Sponsored links
👉1 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)
👉2 Kitau cha Fiqh
👉3 Kitabu cha Afya
👉4 Simulizi za Hadithi Audio
👉5 kitabu cha Simulizi
👉6 Madrasa kiganjani
Mbinu walizotumia Makafiri wa Kiqureish katika kuupinga Uislamu Makkah.
Mbinu walizotumia Makafiri wa Kiqureish katika kuupinga Uislamu Makkah. Soma Zaidi...
Nabii Ibrahiim(a.s) Kumlingania Uislamu Baba Yake
Baada ya NabiiIbrahiim(a. Soma Zaidi...
Si Yesu Aliyesulubiwa (yesu hakufa msalabani wala hakusulubiwa
Katika Qur,an tukufu, Mwenyezi Mungu aliye muweza na mjuzi wa mambo anathibitisha kuwa aliyesulubiwa si Nabii Isa(a. Soma Zaidi...
Tukio la kupasuliwa kifua Mtume Muhammad S.A.W
Sura na historia ya Mtume Muhammad S.A.W, sehemu ya 7 Soma Zaidi...
Bara la Arabu Zama za Jahiliyyah
Wakati Mtume(s. Soma Zaidi...
Nini maana ya tabii tabiina
Soma Zaidi...
Mambo ya Msingi Aliyofanya Mtume(s.a.w) Katika Kuanzisha Dola ya Kiislamu Madinah.
Mambo ya Msingi Aliyofanya Mtume(s. Soma Zaidi...
Kisa cha Malkia wa Sabaa.
Sabaa ulikuwa mji katika nchi inayojulikana leo kama Yemen. Soma Zaidi...
Zakaria(a.s) Akabidhiwa Ulezi wa Maryam
Baada ya kupigwa kura juu ya nani awe mlezi wa Maryam, Nabii Zakaria akachaguliwa kuwa mlezi wa Maryam. Soma Zaidi...
Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Adam(a.s)
(i) Utukufu wa mtu katika Uislamu hautokani na nasaba, rangi,kabila,utajiri ila uwajibikaji kwa Allah(s. Soma Zaidi...
Mapambano ya waislamu dhidi ya Makabila ya kiarabu wakati wa Mtume
Soma Zaidi...
Uendeshaji na Kupanuka kwa Dola ya Kiislamu Kipindi cha Makhalifa Waongofu
Soma Zaidi...