Njama za Mayahudi Kutaka Kumuua Nabii Isa(a.s)


Njama za kutaka kumuua Nabii Isa(a.s) zilianza kwa kumuuliza maswali ya kumtega na kumfitinisha kwa Serikali ili imuone kuwa anachochea watu wasilipe kodi na kuhatarisha maslahi ya wakubwa Serikalini. Fitina hizi zilifanywa na Mafarisayo na Makuhani, wakamwendea Yesu wakisema:Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yeyote, kwa maana hutazami sura za watu. basi utuambie waonaje? Ni halali kumpa kaisari kodi, ama sivyo? (Mathayo 22:16-17)Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema:

Mbona mnanijaribu enyi wanafiki? Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu (Mathayo 22:18-21)Baada ya hila hizi kushindwa, zikapangwa njama za kutaka kumuua.

Basi wakuu wa Makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu anafanya ishara nyingi.Tunamwachia hivi, watu wamwamini. Yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie Taifa zima(Mathayo11:47-48,50)


Ahadi ya Allah(s.w) Kumuokoa Nabii Isa(a.s)


Nabii Isa(a.s) alimuomba Allah(s.w) amlinde na shari za watu wabaya waliopanga njama dhidi yake. Yesu alikwenda bustani ya Gestmane kuomba. Alipofika, akawaambia wanafunzi wake:Roho yangu ina huzuni kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.(Mathayo 26:38 39)

Mwenyezi Mungu alikubali dua ya Nabii Isa (a.s) kwa kumuhakikishia kuwa atamlinda dhidi ya njama za watu madhalimu.
“Mwenyezi Mungu aliposema: “Ewe Isa! Mimi nitakukamilishia muda wako wa kuishi na nitakuleta kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru, na nitawaweka wale waliokufuata, juu ya wale waliokufuru mpaka siku ya kiama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu,Nitakuhukumuni katika yale mliyokuwa mkihitilafiana”(3:55)

Katika mahubiri yake huko nyuma, Nabii Isa (a.s) aliwasisitiza sana watu kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa kumuomba msaada. Aliwaambia:Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona, naye abishaye hufunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, Je! si zaidi Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? (Mathayo 7:7-11)Kwa mujibu wa Yesu mwenyewe, Mwenyezi Mungu humsikiliza maombi yake na kumkubalia daima. Hebu na tuyarejee maneno yake aliyoyasema pale alipoomba jambo kubwa la kumfufua Lazaro:Yesu akainua macho yake juu, akasema: Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia siku zote; lakini ni kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kuwa ndiwe uliyenituma. Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake umefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.
(Yohana 11:41-44)Ndiyo kusema kuwa ikiwa Yesu ametangaza kuwa,”Ombeni, nanyi mtapewa”, Na kwakuwa Mungu, huwapa “mema wao wamwombao”, na Yesu mwenyewe anakiri kuwa Mungu anamsikia siku zote, haiwezekani kabisa asulubiwe hali ya kuwa Mungu yupo na alishamuomba!