Adam na Hawah Kushushwa Ardhini


(Wakumbeshe watu khabari hii) wakati Mola wako alipowaambia

Malaika: “Mimi niteleta Khalifa kukaa katika ardhi” (2:30).

Hivyo bustani aliyowekwa ilikuwa ni mapito tu. Awamu ya kwanza ya maisha ya mwanaadamu ilikuwa ni peponi, awamu ya pili ni maisha ya hapa ardhini awamu ya tatu maisha ya Barzakh (kaburini) na awamu ya nne baada ya hukumu (Siku ya Kiyama),

maisha ya milele, peponi au motoni. Mwanzo wa mwanaadamu kuishi katika ardhi unabainishwa na aya zifuatazo;


Akasema (Mwenyezi Mungu): “Shukeni (katika ardhi), nyinyi kwa nyinyi ni maadui. Na makao yenu yatakuwa katika ardhi, na starehe yenu (pia) mpaka muda (niutakao mimi mwenyewe)”.Akasema (Mwenyezi Mungu): “Mtaishi humo na mtafia humo, na mtatolewa humo (mtafufuliwa kwenda Akhera kulipwa)” (7:24-25).


Mwongozo wa Allah kwa Wanaadamu.
Allah(s.w) hakumuacha Khalifa wake aanze maisha gizani. Bali alimpa mwongozo wa namna ya kuutekeleza Ukhalifa wake. Tunasoma katika Qur’an:


Tukasema: “Shukeni humo nyote, na kama ukikufikieni mwongozo utokao kwangu basi watakaofuata uongozi wangu huo haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika, lakini wenye kukufuru na kuyakadhibisha maneno yetu, hao ndio watakaokuwa watu wa motoni, humo watakaa milele” (2:38-39).

Utaratibu wa Allah unaobainishwa na aya hizi wa kuleta mwongozo unafanya kazi toka binaadamu wa mwanzo, Adam, hadi wa mwisho wa maisha haya ya duniani. Ni ahadi aliyoichukua Allah(s.w) kuwaletea waja wake mwongozo. Mwongozo ambao unakusudiwa watu waufuate wasibuni mifumo ya maisha kinyume na ule aliouleta Allah(s.w). Na zipo njia mbili tu za kuujua mwongozo wa Allah(s.w).

Ama mtu kuletewa Wahyi (Mitume) au kusoma kutoka kwa walioletewa Wahyi. Ndio maana tunaona Allah(s.w) ameleta Mitume pamoja na vitabu kuubanisha mwongozo huo.

Mwongozo huo umeletwa hatua kwa hatua, hadi kufikia kwa Mtume wa mwisho. Ni mwongozo unaokigusa kila kipengele cha maisha kwa mtu binafsi, taifa, na kimataifa katika ngazi zote, hali zote, mahali popote na wakati wowote. Hapana anachokihitajia mwanaadamu ila kimebainishwa katika mwongozo wa Allah(s.w)