(v)Kukosolewa Mtume (s.a.w) katika Qur-an ni Ushahidi Mwingine kuwa Qur-an ni Kitabu cha Allah (s.w):Hoja nyingine inayotufanya tuamini pasi na tone la shaka kuwa Qur-an ni Kitabu cha Allah (s.w) ni kule kukosolewa Mtume (s.a.w) ndani ya Qur-an. Si jambo la kawaida kwa mwanaadamu yeyote mwenye akili timamu kutangaza aibu zake na kujikosoa kwa namna Mtume (s.a.w) alivyokosolewa katika Qur-an, katika Kitabu chake mwenyewe. Atakalolifanya mwandishi mkweli na muadilifu ni kuacha tabia mbaya au udhaifu aliokuwa nao na kuwapa wengine ujumbe kuwa waache udhaifu huo.


Lakini katika Qur-an tunaona kuwa pale Mtume Muhammad (s.a.w) alipoonesha kidogo udhaifu wa kibinaadamu na akaenda kidogo nje ya utendaji anaouridhia Allah (s.w) pale pale Allah (s.w) alimkosoa na kumrejesha katika njia iliyo sawa. Kwa mfano Mtume Muhammad (s.a.w) alipohisi ugumu katika kutekeleza amri ya Allah(sw) ya kumuoa Zainabu bint Jahsh baada ya kuachwa na Zaidi bin Harith, aliyekuwa mtoto wake wa kulea kwa kuchelea Uislamu kutukanwa na kupakwa matope na makafiri na wanafiki, Allah (s.w) ali mzi ndua katika aya zifuatazo:Na(wakumbushe)ulipomwambia yule ambaye Mwenyezi Mungu amemneemesha (kwa kumuafikia Uislamu) na wewe ukamneemesha kwa kumpa uungwana. naye ni Bwana Zaid bin Haritha ulipomwambia): “Shikamana na mkeo na umche Mwenyezi Mungu(usimuache)” na ukaficha katika nafsi yako aliyotaka Mwenyezi Mungu kuyatoa(Nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu amekuamrisha umuoe wewe huyo mkewe atakapomuacha ili iondoke ile itikadi iliyokuwa ikiitakidiwa ya kuwa mtoto wa kulea ni kama mtoto wa kumzaa), na ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye haki zaidi ya kumchelea. Basi alipokwisha Zaidi haja yake na mwanamke huyo, Tulikuoza wewe ili isiwe taabu kwa Waislamu kuwaoa wale wa watoto wao wa kupanga wanapokuwa hawana haja nao. na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa (33:37)
Mfano mwingine ni pale Mtume (s.a.w) aliposusa kula asali ili kuwaridhisha wake zake ambapo Allah (s.w) alimwonya kama aya ifuatayo inavyotufahamisha:


Ewe Mtume! Mbona (kwa nini) unaharamisha alichokuhalalishia Allah? Unatafuta radhi za wake zako ndiyo maana ukafanya hivi! Na Allah ni mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. (66:1)Mfano mwingine ni ule wa kukosolewa Mtume (s.a.w) katika Qur-an ni pale alipomkasirikia sahaba kipofu aliyetaka kupata mawaidha mapya na badala yake akawaelekea wakubwa wa makafiri kwa matumaini kuwa watasilimu na kuleta nafuu kubwa katika kazi ya kuusimamisha Uislamu. Kitendo hiki hakukiridhia Allah (s.w) na akamkosoa Mtume wake katika aya zifuatazo:


Alikunja (Mtume) paji akageuza uso, kwa sababu alimjia kipofu, na nini kilichokujulisha (kuwa huyo sahaba pofu hahitaji mawaidha mapya) labda atatakasika (akisikia mawaidha mapya), au atakumbuka (aliyoyasahau) ukumbusho huo upate kumfaa, ama ajionaye hana haja (ya dini), wewe ndiye unayemshughulikia! Na si juu yako kama hakutakasika, lakini anayekukimbilia - naye anaogopa, wewe unampuuza (usifanye hivyo). Sivyo! Hakika hii (Qur-an) ni nasaha (mawaidha), basi kila apendaye atawaidhika (asiyetaka basi muachilie mbali). (80:1-12).Ni dhahiri kuwa kama Mtume (s.a.w) asingelikuwa Mtume wa Allah(s.w) na kama ndiye yeye aliyeiandika Qur-an, kamwe asingelithubutu kudhihirisha aya hizo katika kitabu chake. Kwa aya hizi na nyingine kama hizi kubakia katika Qur-an na Mtume (s.a.w) kuzitangaza kwa watu kama zilivyo kwa muda wote wa maisha yake ya Utume, ni hoja nyingine kuwa Qur-an si maneno ya Mtume Muhammad (s.a.w) bali ni maneno matukufu ya Allah (s.w).