(g) Adabu ya kukaa na kula katika nyumba za watu.


"Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kiguru, wala si vibaya kwa mgonjwa, wala kwenu, kama mkila katika nyumba zenu, au nyumba za baba zenu, au nyumba za mama zenu, au nyumba za ndugu zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za ami zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za dada wa mama zenu, au za wale mliowashikia funguo zao, au rafiki zenu. Si vibaya juu yenu kama mkila pamoja au mbali mbali. Na mnapoingia katika majumba toleaneni salamu; (maamkio haya) ni zawadi itokayo kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka, na mema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu Anavyokubainishieni Aya (zake) ili mpate kufahamu." (24:61)"Enyi mlioamini! Msiingie nyumba za Mtume ila mpewe ruhusa kwenda kula, pasipo (kwenda kukaa) kungojea kiivie. Lakini mtakkapoitwa ingieni, na mnapokwisha kula tawanyikeni. Wala msiweke mazungumzo, maana jambo hili linamuudhi Mtume, naye anakuoneeni haya; lakini Mwenyezi Mungu Haoni haya kusema haki. Nanyi mnapowauliza (wakeze) waulizeni nyuma ya pazia. Kufanya haya kutasafisha nyoyo zenu na nyoyo zao. Wala haikupasieni (haitakikani) kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu. Wala kuwaoa wake zake baada yake; kabisa. Hakika jambo hilo ni (dhambi) kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. (33:53)
Tukizingatia aya hizi tunapata maelekezo ya kimaadili yafuatayo:(i) Pamoja na kwamba Uislamu unahimiza ukarimu, haumuhusu kwa pande mmoja, kuingia na kula katika nyumba za watu pasi na mwaliko rasmi. Kuvamia chakula katika nyumba za watu ni kuvuruga utaratibu wa familia na kuleta kero, jambo ambalo halikubaliki katika Uislamu. Kwa upande mwingine, katika mafundisho ya Uislamu, akija mgeni asiyerami (mgeni wa kupita) asitoke bila ya kumkirimu chochote, angalau maji ya kunywa; naye apokee lakini ahakikishe kuwa hawakalifishi wenyeji wake.(ii)Wanaoruhusika kula chakula watakacho kikuta ni wanafamilia wenyewe na jamaa wa karibu kama walivyotajwa katika aya (24:61). Marafiki walioainishwa katika aya hii ni wale marafiki wa ndani walioshibana na familia (rafiki ndugu).(iii)Wengine wanaoruhusika kula chakula katika nyumba za watu bila mwaliko rasmi ni wagonjwa, vilema, na wengine walioathirika kiuchumi wanaotambulika kisheria na wanaohitajia msaada wa Waislamu.(iv)Waislamu watakapopata mwaliko wa kwenda kula katika nyumba za watu, waje pale kwa wakati uliopangwa na baada ya kula waombe ruhusa ya kuondoka ili kuwapa wenyeji wao uhuru wa kufanya mambo yao mengine ya faragha (yanayohusu familia).