Kujitwaharisha Kutokana na NajisiKutokana na uzito wa kujitwaharisha tutazigawanya najisi katika makundi matatu
(a)Najisi ndogo.
(b)Najisi kubwa na
(c)Najisi hafifu
(a)Najisi Ndogo.Najisi Ndogo
Inahusu najisi zote isipokuwa najisi ya mbwa na nguruwe. Namna ya kujitwaharisha kutokana na najisi ndogo ni kuosha paliponajisika kwa maji safi mpaka iondoke rangi na harufu ya najisi.Kama tunatumia maji machache ambayo huharibika mara tu yatakapoingiwa na japo najisi ndogo, hatuna budi kutumia kata au chombo kingine cha kuchotea maji na kujitwaharisha pembeni kwa kujimiminia maji kupitia sehemu ile yenye najisi mpaka najisi hiyo iondoke.Katika hali ya kawaida, maji safi hutumika kwa kustanjia. Tunazitwaharisha sehemu zetu za siri kwa mkono wa kushoto mpaka tuhakikishe kuwa najisi imeondoka. Katika hali ya dharura ya kukosa maji au ugonjwa usioruhusu kutumia maji, tunaruhusiwa kustanji kwa kutumia vitu vikavu kama vile karatasi laini (toilet paper), mawe, n.k. Tukistanji kwa vitu vikavu, kama vile mawe makavu tutapangusa sehemu zetu za siri kwa mawe matatu. Kama najisi ingalipo, tutaongeza mawe mawili mawili mpaka turidhike kuwa najisi imeondoka.