Zakatul-FitriZakatul-Fitri ni zakat inayomlazimu kila Muislamu mwanamume na mwanamke,mdogo na mkubwa, ambayo hutolewa baada ya funga ya Ramadhani kabla ya kuswali swala ya Iddil-Fitri. Watoto, wanawake, wazee, na wengine wasio na uwezo wa kulipa zakatul-fitr watalipiwa na mawalii wao. Kwa mfano mume atamtolea mkewe na watoto ambao hawajaweza kujitegemea; pia atawatolea wazazi wake kama hawana uwezo wa kujilipia; vile vile baba atalazimika kuwalipia Zakatul-fitr wale wote wengine ambao ni Waislamu walio chini ya uangalizi wake. Mtoto mchanga aliyezaliwa dakika chache kabla ya kuandama mwezi wa Shawwal atatolewa Zakatul-Fitri.Umuhimu wa Zakatul FitriZakatul Fitri ni faradhi iliyoambatanishwa na faradhi ya funga ya Ramadhani. Mtume (s.a.w) ameamrisha Zakatul-Fitri kutolewa na kila Muislamu mwanamume na kila Muislamu mwanamke na amebainisha wazi kuwa Swaumu ya mja haipokelewi endapo hajajitolea Zakatul Fitri na kuwatolea wote wale walio chini ya uangalizi wake. Msisitizo wa utoaji Zakatul-Fitr tunaupata katika Hadith ifuatayo:Ibn Umar (r.a) amesema kuwa Mtume wa Allah ameamrisha ulipaji wa Zakatul-fitr baada ya Ramadhan kwa kila Muislamu muungwana na mtumwa, mume na mke, (Mkubwa na mdogo) kwa (kila mtu) kutoa sai moja ya tende zilizokaushwa au sai moja ya shairi (Barley).(Bukhari na Muslim).Nisaab ya Zakatul-FitriZakatul Fitri inamlazimu yeyote yule mwenye kupata chakula cha kumtosha yeye mwenyewe na wale walio chini ya uangalizi wake kwa siku ya Idd na Usiku wake na akawa na ziada. Ziada hiyo ataitoa zakatul fitri kwa viwango vinavyostahiki.Kiwango cha Zakatul-Fitri
Kwa mujibu wa hadithi ya Ibn Umar (r.a) kiwango cha Zakatul-Fitri kwa kila kichwa ni Sa’i moja ya chakula kinacholiwa kwa wingi katika sehemu husika. Kwa mfano chakula kinachopendelewa sana na watu wa mikoa ya pwani ya Tanzania ni mchele na kile kinachopendelewa sana na mikoa ya bara ni mahindi, uwele na mtama.Sa’i iliyotumika wakati wa Mtume (s.a.w) imelinganishwa na pishi inayotumika katika mazingira ya Tanzania. Pishi moja ya vyakula hivyo vilivyotajwa ni sawa na kilo mbili na nusu (2.5kg). Pia inajuzu kuthaminisha pishi ya chakula husika na fedha taslimu. Kihalisia ni vizuri zaidi kutoa fedha taslimu ili kumuwezesha huyo anayepewa zakatul-fitri aweze kununua chakula husika pamoja na viungo mbali mbali vitakavyo kifanya chakula hicho kiwe kizuri na cha kuvutia kwa ajili ya kusherehekea Idd.Muda unaofaa kutolewa Zakatul-FitriMuda wa kutoa Zakatul fitri umebainishwa katika Hadith ifuatayo:
Ibn Umar (r.a) ameeleza kuwa Mtume (s.a.w) aliwaamuru watu kuwa walipe zakatul fitri kabla ya swala (ya Iddil-Fitri) (Muslim).Kulipa Zakatul Fitri mapema kabla ya kuswali Idd au mapema zaidi ya hapo, kutawawezesha maskini na mafakiri kufurahia Idd pamoja na Waislamu wengine. Ikitokea sababu ya msingi, kama vile kusahau, mtu akachelewa kutoa Zakatul-fitri mpaka Idd ikaswaliwa, hana budi kuitoa baada ya swala. Lakini jambo la kuzingatia ni kwamba, amri ya kutoa Zakatul-fitri kabla ya swala imetolewa na Mtume (s.a.w), hivyo, mtu akiivunja amri hii makusudi au kwa uzembe ajue kuwa kutoa kwake huko hakutamnufaisha chochote.Watu wanaostahiki kupewa Zakatul-FitriZakatul-Fitri si malipo ya maimamu wa Tarawehe kama wengi wanavyoichukulia bali ni chakula cha maskini na wale wote wasiojiweza kujipatia chakula pamoja na wale walio chini ya uangalizi wao kwa siku ya Idd na usiku wake ili nao wajisikie na wafurahie Idd pamoja na Waislamu wenzao wenye uwezo. Kama ilivyo katika Zakatul-Mal, akipewa Zakatul-Fitri asiyestahiki itakuwa ni kudhulumu haki ya wale wanaostahiki na mtoaji na mpokeaji wa zakatul-fitri hiyo watakuwa ni mad ha lim u.Ili kuhakikisha kuwa katika jamii au katika mtaa wa Waislamu kila anayestahiki kupewa zakatul fitri amepata na kuzuia uwezekano wa mtu mmoja kulundikiwa zakatul-fitri kiasi kikubwa sana, na mwingine kukosa au kupata kiasi kidogo sana kisichotosheleza mahitaji yake ya siku ya Iddi, ni vyema Waislamu wa mtaa mmoja au wa sehemu moja waikusanye Zakatul-Fitri kwa pamoja, na kisha waigawanye kwa wote wanaostahiki katika mtaa au sehemu hiyo wakizingatia mahitajio yao kulingana na majukumu ya kifamilia waliyo nayo.