Kulipia RamadhaniMtu anapodaiwa siku alizo kula katika mchana wa mwezi wa Ramadhani,au siku ambazo swaumu yake ilibatilika, si lazima azilipe mara tu baada ya Ramadhani, japo ni bora mtu kumaliza deni lake haraka. Tunafahamishwa katika Hadith kuwa Bibi ‘Aysha (r.a) alikuwa akilipia Ramadhani katika mwezi wa Shaaban:Aysha (r.a) ameeleza: “Nilikuwa na madeni ya swaumu ya Ramadhani. Sikuweza kulipa kadha ila katika mwezi wa Shaaban. (Bukhari na Muslim).Hali kadhalika si lazima mtu kulipa mfululizo siku zote anazodaiwa, bali anaweza kuzilipa kidogo kidogo kutokana na Hadith ifuatayo:Ibn Umar (r.a) ameeleza kwamba Mtume (s.a.w) amesema juu ya kulipa Ramadhani: (Mtu) akitaka na afarikishe; na akitaka na afululize. (Daru Qu tni).Kama mtu amechelewa kulipa siku anazodaiwa mpaka Ramadhani nyingine ikaingia, basi kwanza ataifunga hiyo Ramadhani iliyomuingilia. Baadaye ndipo alipe hiyo deni yake wala halipi fidia; iwe kuchelewa huko ni kwa udhuru ama si kwa udhuru. Lakini ni vizuri zaidi kulipa siku anazodaiwa kabla ya kuingia Ramadhani nyingine.