DARSA ZA SWALA
SWALA
Umuhimu wa Kusimamisha
Swala Kwa mujibu wa Hadith ya Ibn Umar (r.a) tuliyoirejea mwanzoni, kusimamisha swala ni nguzo ya pili ya nguzo za Uislamu. Katika kuonyesha umuhimu wa kusimamisha nguzo hii Mtume (s.a.w) amesema: Swala ndio nguzo kubwa ya Dini (Uislamu) mwenye kusimamisha swala amesimamisha dini (Uislamu) na mwenye kuiacha swala amevunja Dini .(Uislamu)
Katika Hadithi nyingine, amesimulia Jabir (r.a) kuwa Mtume wa Allah amesema: Tofauti yetu sisi (Waislamu) na ukafiri ni kuacha swalah. (Muslim) Pia Mtume (s.a.w) amesema: Tofauti iliyopo kati yetu (Waislamu) na wengine (wasiokuwa Waislamu) ni swala (Ahmad, Abu Daud, An-Nasai, Tirmidh) Kutokana na hadithi hizi, tunajifunza kuwa mtu ambaye hasimamishi swala, hatakama anajiita Muislamu si Muislamu bali ni kafiri kama makafiri wengine. Anakuwa kafiri kwa sababu amekanusha amri ya Allah iliyowazi kama inavyobainika katika aya zifuatazo: Waambie waja wangu walioamini, wasimamishe swala.(14:31) Basi simamisheni swala, kwa hakika swala kwa waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati makhsusi.h (4:103) Na waamrishe watu wako kuswali (kusimamisha swala) na uendelee mwenyewe kwa hayo...h (20:132).
Tukumbuke kuwa hawi Muumini yule anayekuwa na hiari katika kutekeleza amri ya Allah na Mtume wake kama tunavyokumbushwa katika aya ifuatayo: Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotofu ulio wazih. (33:36)
Lengo la Kusimamisha Swala
Bila shaka swala imepewa umuhimu mkubwa kiasi cha kufanywa nguzo kubwa ya Uislamu kutokana na lengo lake. Lengo la swala limebainishwa katika Qur-an kama ifuatavyo ”Soma uliyoletewa wahyi katika kitabu (Qur-an) na usimamishe swala. Bila shaka swala (ikiswaliwa vilivyo) humzuilia (mwenye kuswali na) mambo machafu na maovu, na kwa yakini kumbuko la Mwenyezi Mungu (lililomo ndani ya swala ni jambo) kubwa kabisa (la kumzuilia mtu na mabaya). Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyatenda.” (29:45).
Kutokana na aya hii tunajifunza kuwa lengo la kusimamisha swala ni kumtakasa mja na mambo machafu na maovu. Kwa maana nyingine, tunajifunza kuwa swala ikisimamishwa vilivyo, humfanya msimamishaji awe mtu mwema mwenye kutakasika na mambo machafu na maovu na mwenye kuendea kila kipengele chake cha maisha kwa kumtii Allah (s.w).
Labda tujiulize swali: Ni nguvu gani au ni msukumo gani uliomo katika swala unaomfanya mwenye kuswali atakasike na maovu na awe na tabia njema anayoridhia Allah (s.w) Linaloleta mabadiliko haya makubwa katika tabia na utendaji wa Muumini, ni lile kumbuko la Allah (s.w) lililomo ndani ya swala. Kwa hiyo lengo hili la swala litapatikana tu pale mwenye kuswali atakapokuwa na mazingatio na kumkumbuka Allah (s.w) katika kila hatua ya swala.
Maana ya Swala
Maana ya Swala
(a)Kilugha Katika lugha ya Kiarabu neno Swalaat lina maana ya ombi au dua. Katika Qur-an tunaamrishwa kumswalia Mtume, yaani kumuombea dua Mtume (s.a.w) katika aya ifuatayo: Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamswalia Mtume (wanamtakia Rehema). Basi, enyi mlioamini mswalieni (muombeeni au mtakieni Mtume) Rehema na muombeeni amani (33:56)
Vile vile katika Hadith, Mtume (s.a.w) anatuambia: Yule atakayealikwa kwenye karamu ya harusi aitikie wito huo, kama hataweza kuitika amswalie (amuombee dua) aliyemkaribisha. (Muslimu).
(b)Kisheria Katika sheria ya Kiislamu, swalaa ni maombi maalumu kwa Allah (s.w) yanayofanywa kwa kufuata utaratibu maalumu uliowekwa na Allah (s.w) na kufundishwa kwa matendo na Mtume wake. Katika maombi haya maalumu mwili mzima huhusika katika maombi haya kwa kusimama, kurukuu, kuitidali, kusujudu, kukaa na kuzingatia yale yote anayosema katika kuleta maombi haya.
Kusimamisha Swala.
Maana ya Kusimamisha Swala Kusimamisha swala ni tofauti na kuswali. Kuswali ni kufanya vitendo vya swala kama vile kusimama, kurukuu, kuitidali, kusujudu, n.k.
Kusimamisha swala ni kuitekeleza swala kwa kuchunga na kutekeleza kwa ukamilifu yafuatayo:
(i) Sharti zote za swala.
(ii) Nguzo zote za swala.
(iii) Kuwa na khushui (unyenyekevu) wakati wote wa kutekeleza sharti na nguzo za swala.
Mtu akiswali bila ya kuzingatia na kutekeleza kwa ukamilifu mambo haya matatu, ataonekana kuwa kaswali, lakini atakuwa hajasimamisha swala na atastahiki kuadhibiwa vikali na Mola wake kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo: Basi adhabu kali itawathibitikia wanaoswali, ambao wanapuuza swala zao (kwa kutozisimamisha), ambao hufanya ria (107:4-6).
Kupuuza swala ni pamoja na kutotekeleza ipasavyo sharti za swala, nguzo za swala, na kutokuwa na unyenyekevu wakati wa kutekeleza sharti na nguzo za swala. Hivyo, swala inayokubalika mbele ya Allah (s.w) ni ile iliyosimamishwa kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo: Hakika wamefuzu waumini ambao katika swala zao ni wanyenyekevu. (23:1-2) Na ambao swala zao wanazihifadhi. (23:9) Kuhifadhi swala ni kutekeleza kwa ukamilifu sharti na nguzo zote za swala.
Sharti za Swala
Sharti za Swala Sharti za swala ni yale mambo ya lazima anayotakiwa Muislamu ayachunge na kuyatekeleza kabla hajaanza kuswali. Mambo haya ni:
1. Twahara.
2. Sitara.
3.Kuchunga wakati.
4.Kuelekea Qibla.
Zifuatazo ni nguzo za Swala:
1. Nia - dhamira moyoni.
2. Takbira ya kuhirimia (au Takbira ya kufungulia Swala).
3.Kusoma suratul-Fatiha.
4. Kurukuu.
5.Kujituliza katika rukuu.
6.Kuitidali (kusimama kutoka katika rukuu).
7.Kujituliza katika itidali.
8.Kusujudu.
9.Kujituliza katika sijda.
10.Kukaa kati ya sijda mbili.
11.Kujituliza katika kikao cha kati ya sijda mbili.
12. Kusujudu mara ya pili.
13. Kujituliza katika sijda ya pili.
14. Kukaa Tahiyyatu.
15.Kusoma Tahiyyatu.
16. Kumswalia na kumtakia rehema Mtume (s.a.w) na Waislamu.
17. Kutoa Salaam.
18. Kuswali kwa kufuata utaratibu huu (1 - 17).
Nguzo hizi za swala tunaweza kuzigawanya kwenye makundi manne: (a)Nia. (b)Nguzo za matamshi (visomo) (c)Nguzo za vitendo. (d) Kufuata utaratibu. Katika nguzo 18,
nguzo za matamshi ni hizi tano zifuatazo: (i)Takbira ya kuhirimia swala. (ii)Kusoma suratul-Fatiha (Al-hamdu). (iii)Kusoma Tahiyyatu. (iv)Kumswalia Mtume. (v) Kutoa Salaam. Nguzo zote zilizobakia, ukiacha nia na kufuata utaratibu ni nguzo za vitendo.
Sunnah za Swala Sunnah za Swala Vipengele vya sunnah katika swala ni vile ambavyo mwenye kuswali akivitenda husaidia sana kukuza daraja ya swala yake na kuipa nguvu na msukumo mkubwa wa kuiwezesha kufikia lengo lililokusudiwa kwa urahisi zaidi.
Ama mwenye kuswali akiacha kipengele chochote katika vipengele vya sunnah, swala yake itakamilika iwapo atatekeleza vipengele vyote vya nguzo. Katika Hadith tumeona kuwa Mtume (s.a.w) katika swala yake pana vipengele vya ziada ya nguzo kama ifuatavyo: 1.Kuinua viganja vya mikono mkabala na mabega, usawa wa vigingi vya masikio wakati wa kuhirimia swala, kwenda kwenye rukuu, baada ya rukuu na baada ya kutoka kwenye Tahiyyatu ya kwanza. 2. Kusoma dua baada ya takbira ya kuhirimia. 3. Kuanza na afudhubillaah (kumlaani Shetani) kabla ya kuanza kusoma suratul-Fatiha. 4. Kuitikia Aaminhbaada ya kumaliza Suratul Fatiha. 5. Kusoma aya za Qur-an baada ya Suratul-Fatiha katika rakaa mbili za mwanzo. 6. Kuleta Tasbih, Tahmid na dua katika rukuu, itidali na sijda. 7. Kutoa takbira katika kubadilisha kitendo kimoja kuendea kingine isipokuwa tu kutoka kwenye rukuu kwenda kwenye itidali ndipo tunaposema: SamifAllahu liman hamidah - Rabbanaa lakal-hamdu. 8. Kukaa na kusoma Tahiyyatu kila baada ya rakaa mbili, kwa swala zenye rakaa zaidi ya mbili. 9. Kusoma dua baada ya kumswalia Mtume na kabla ya kutoa Salaam.
Namna ya kuswali kama alivyoswali Mtume (s.a.w)Mtume (s.a.w) ametuagiza katika Hadith maarufu kuwa tuswali kama alivyokuwa akiswali. Hivyo katika sehemu hii tutajitahidi kuonesha utekelezaji wa swala hatua kwa hatua kwa kurejea Hadith Sahihi za Mtume (s.a.w):
1.Nia na Takbira ya kuhirimia Nia ni kudhamiria moyoni kuwa unaswali, swala unayoikusudia kisha unaanza swala kwa kusema: “Allaahu Akbar” Allah ni Mkubwa kwa kila hali”. Wakati wa kuhirimia swala ni sunnah kuinua viganja vya mikono,mkabala na mabega. Kuhusu unyanyuaji wa mikono mkabala na mabega imeripotiwa kuwa Mtume (s.a.w) alikuwa akifanya hivyo katika sehemu nne tofauti: 1. Wakati wa kuhirimia swala (kuanza swala). 2.Wakati anaposema Allaahu Akbar kwa ajili ya rukui. 3.Wakati anaposimama kutoka kwenye rukuu. 4.Wakati anaposimama kutoka kwenye tahiyyatu ya kwanza ili kuendelea na rakaa ya tatu.
Hii tunaipata katika Hadith aliyosimulia Abdullah bin ‘Umar kuwa: “Mtume (s.a.w) aliposimama kwa ajili ya swala alinyanyua mikono yake mkabala na mabega yake na kisha kuhirimia (kusema Allahu Akbar). Alipotaka kurukuu alinyanyua mikono kama alivyofanya kwanza na aliposimama kwa ajili ya itidali alifanya hivyo hivyo na alisema Allah anamsikia yule anayemsifu. (Bukhari, Muslim na Bayhaqi). Nafa’a(r.a) ameeleza kwamba Ibn ‘Umar (Abdullah)(r.a) aliposimama kwa ajili ya rakaa ya tatu alikuwa akinyanyua mikono; jambo ambalo alilihusisha na Mtume (s.a.w). (Bukhari, Abu Dawud, Nasai).
Baada ya kuhirimia swala mwenye kuswali hushusha mikono yake na kuiweka kifuani, mkono wa kulia ukiwa juu ya mkono wa kushoto kwa mujibu wa Hadith zifuatazo: Hulab At-Tai(r.a) amesimulia: “Nilimuona Mtume (s.a.w) akiswali hali ameweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto juu ya kifua chake.” (Ahmad na At-Tirmidh)
Naye Wail bin Hijr (r.a) ameripoti: “Niliswali pamoja na Mtume (s.a.w) na aliweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto juu ya kifua chake”. (Ahmad na At-Tirmidh).
Imamu Abu Dawud na Nasai wamepokea kutoka kwa Ibn Khuzaimah kuwa Mtume (s.a.w) alipokuwa akiswali alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya kiwiko (wrist) cha mkono wa kushoto na sehemu ya mkono inayofuatia kiganja .
2.Kusoma Dua ya Kufungulia Swala Kusoma dua ya kufungulia swala ni sunnah. Katika Hadithi ya Bukhari na Muslim iliyosimuliwa na Abu Hurairah (r.a), baada ya kuhirimia swala Mtume (s.a.w) alikuwa akileta dua ifuatayo: “wajahtu wajhi lilladhi fatwaras-samaawat wal-ardha hanifam-muslima wamaa aana minal-mushrikina. Inna swalatiy wanusukii, wamah-haya, wamaamatiy, lillahi rabil-alamiina laa sharikalahu wabidhalika umirtu wa-ana minal-muslimiina.”“Nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeziumba mbingu na ardhi. Nimeacha dini za upotovu. Mimi si miongoni mwa washirikina. Hakika swala yangu (na ibada zangu zote) na uzima wangu na kufa kwangu (yote) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, bwana (Rabbi) wa walimwengu wote. Hana mshirika wake. Na haya ndio niliyoamrishwa na mimi ni wa kwanza walio jisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu. (6:79, 162-163)
3.Kupiga Audhu Billah Kabla ya kuanza kusoma Qur-an ni amri ya Allah (s.w) kujikinga na sheitwani kama inavyodhihirika katika aya ifuatayo: 109 “Na ukitaka kusoma Qur-an piga Audhu billah (jikinge) kwa Allah (akulinde) na Sheitwani aliyefukuzwa (kwenye Rehema). (16:98) Hivyo tuanze kusoma Qur-an kwa kusema “A’udhu-billahi minash-shaytwanir- Rajiim” Najikinga kwa Allah na sheitwan aliyefukuzwa-kwenye Rehma yako
4.Kusoma Suratul-Fatiha Kusoma Suratul-Fatihah ni nguzo ya tatu ya swala na ndio nguzo kubwa ya swala. Tunasoma suratul-Fatiha kama ifuatavyo:- Bismillahir Rahmaanir Rahiim (1) Alhamdu liLLahi rabbil-’Aalamiin (2). Rrahmaanir Rahiim (3) Maaliki yaumiddiin (4) Iyyaakana ‘abudu waiyyaaka nasta‘iin (5) Ih dinasw-swiraatwal mustaqiim (6) Swiraatwa lladhiina an ‘amta ‘alaihim; ghairil maghdhuubi ‘alaihim wala dhw-dhwaaliin (7) 110
Tafsri: (1) Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu: (2) Shukrani zote anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola wa Walimwengu wote: (3) Mwingi wa Rehema mwenye kurehemu (4) Mwenye kumiliki siku ya malipo: (5) Wewe tu ndiye tunayekuabudu, na wewe tu ndiye tunaye kuomba msaada: (6) Tuongoze njia iliyonyooka: (7) Njia ya wale uliowaneemesha; siyo (ya wale ) waliokasirikiwa, wala ya wale waliopotea
5.Kusoma Qur-an baada ya Suratul-Fatiha Katika rakaa ya kwanza na ya pili ni Sunnah baada ya kusoma Suratul-Fatiha kuleta Surah au aya nyingine za Qur-an:
6. Kurukuu Baada ya kusoma Suratul-Fatiha na Surah nyingine, au baadhi ya aya katika sura nyingine unasema Allahu-akbar kisha unarukuu (kuinama). Rukuu ni nguzo ya swala pamoja na kujituliza humo. Katika rukuu ni sunnah kumsabihi Allah (s.w) kwa kusema kimya kimya mara tatu au zaidi “Subhana Rabbiyal’Adhiim” “Utukufu ni wako Ee Bwana (Mlezi) wangu Uliye mkuu”
7.Kuitidal Kuitidali ni kusimama wima kutoka kwenye rukuu, ni sunnah kusema wakati wa kunyanyuka maneno haya:“sami’a llahu liman hamidahu” Mwenyezi Mungu anamsikia kila mwenye kumhimidi. Na baada ya kusimama sawa ni sunnah kusema “rabbanaa walakal-hamdu”ewe mola wetu sifa zote za ukamilifu ni zako. Pia ni sunnah kusema maneno haya “rabbanaa walakal-hamdu mil-as-samaawati wamil-al-ardhi wamil-amashi-ita minshai-in ba’adah” Ewe Mola wetu sifa zote za ukamilifu ni za kwako, kutoka mbinguni, kutoka ardhini na katika vitu vyote vilivyo baina yao (mbingu na ardhi) na kutoka katika vinginevyo unavyo viridhia
8.Kusujudi Ni nguzo pamoja na kujituliza katika sujudi. Mkusujudi ni kuvituliza chini viungo saba kwa utaratibu wa swala. Vingo hivyo ni , paji a uso, viganya viwili vya mikono, magoti mawili na matumbo ya nyayo za vidole vya miguuni.viungo vyote hivi vinatakiwa vielekee kibla. Paji la uso ni pamoja na pua iguse chini.utasema kwenye sijda “subhaana rabbiyal-a’alaa” utukufu ni wa kwako Mola uliye tukuka.
9.kukaa baina ya sijda mbili Hiki ni kitako kinachopatikana baada ya kutoka kusujudi. Sifa ya kikao hiki ni kukalia unyayo wa mguu wa kushoto na kuweka mikono miwili juu ya mapaja. Ni sunnah kusema maneno haya: “rabbigh-firliy warhamnii wa’afinii warzuqniy”Ewe Mola wangu nisamehe, na unirehemu, na unipe afya na uniruzuku
10.kikaa tahiyyatu Katika kukaa Thiyyatu mtume alikuwa akikalia futi la mguu wa kushoto na kusimamisha futi la mguu wa kulia na katika tahiyyatu ya mwisho alikaa chini na kuulaza mguu wa kushoto katika uvungu wa mguu wa kulia na alisimamisha futi la mguu wa kulia, katika vikao vyote hivyo viwili,
Mtume (s.a.w) alivilaza viganja vyake juu ya mapaja karibu na magoti kama tunavyoelezwa katika hadith ifuatayo: Abdullah bin Jubair(r.a) ameeleza kuwa wakati Mtume (s.a.w) alipokaa tahiyyatu, alikuwa akiweka kiganja chake cha mkono wa kulia juu ya paja lake la kulia na kiganja cha mkono wa kushoto juu ya paja la mguu wa kushoto na alikuwa akinyoosha kidole chake cha shahada (wakati wa k u s e m a , “ A s h - h a d u anllaaillaha illallah) na kukiegemeza juu ya kidole gumba na alikuwa akiweka kiganja chake cha mkono wa kushoto juu ya goti lake (la mguu wa kushoto). (Muslim).
11.Kusoma Tahiyyatu Kusoma tahiyyatu ni nguzo ya swala. “Tahiyyatu” ina maana ya “Maamkizi”, ukiwa umekaa kikao cha tahiyyatu unaleta maamkizi kama ifuatavyo: “Attahiyyaatu lillaah, wasw-swalawaatu, watwa-yyibaatu, assalaamu ‘alaika ayyuhannabiyyu, warahmatullaahi wabarakaatuhu, assalaamu ‘alay-naa wa-’alaa ‘ibaadillaahi swswaalihiina. Ash-hadu an-llaailaaha illallaahu wa-ash-hadu anna Muhammadan ‘abduhuu warasuuluhu”. “Maamkizi yote ni ya Allah, na swala zote na yote mazuri, Amani iwe juu yako, ewe Mtume na Rehma na Baraka za Allah. Na amani iwe juu yetu na juu ya waja wema wa Allah. Ninashuhudia kuwa hapana Mola ila Allah. Na ninashuhudia kuwa Muhammad ni Mja na, ni Mtume wake”. (Muslim).
12.Kumswalia Mtume (s.a.w) Kumswalia Mtume (s.a.w) ni nguzo ya swala inayofuatia baada ya kusoma Tahiyyatu. Kumswalia Mtume si faradhi katika swala tu bali pia ni faradhi kumswalia kila anapotajwa kwa jina lake. Msisitizo wa amri ya kumswalia Mtume unaonekana katika aya ifuatayo:
“Hakika Mwenyezi Mungu anamteremshia Rehema Mtume; na Malaika wake (wanamuombea dua). Basi; enyi Mlioamini msalieni (Mtume, muombeeni Rehema) na amani”. (33:56)
Pia hadithi zifuatazo zinasisitiza umuhimu wa kumswalia Mtume (s.a.w) kila atajwapo na kila mtu apatapo wasaa. Ali (r.a) amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Bakhili ni yule anayesikia nikitajwa, lakini haniswalii. (hanitakii rehma). (Tirmidh).
Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: “Anayenitakia Rehma (anayeniswalia) mara moja, Allah humrehemu mara kumi”. (Muslim).
“Ibn Mas’ud amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Atakayekuwa kipenzi changu katika watu, katika siku ya Kiama atakuwa ni yule aliye mbele kuliko wote katika kunitakia Rehma (kuniswalia). (Tirmidh).
Namna ya kumswalia Mtume (s.a.w) imeelezwa katika Hadithi nyingi lakini iliyomashuhuri katika hizo ni ile iliyosimuliwa na Abdur- Rahman bin Ubaidillah(r.a) na kupokelewa na Maimamu wote wa Hadithi kuwa Mtume (s,.a.w) ametufundisha tumswalie (tumtakie Rehma) kama ifuatavyo;
“Allahumma swalli ‘alaa muhammad wa’alaa aliy Muhammad kamaa swallaita ‘alaa ibraahima wa’alaa ali ibraahim innaka hamiidum-majid. Wabaaik ‘alaa muhammad wa’alaa ali muhammad kamaa barakta ‘alaa ibraahima wa’alaa ali ibraahima innaka hamiidum-majid”
Ewe Mola mrehemu Muhammad na wafuasi wake kama ulivyomrehemu Ibrahim na wafuasi wake hakika wewe ni mtukufu na msifiwa wa haki. Ewe Mola mbariki Muhammad na wafuasi wake kama ulivyombariki Ibraahim na wafuasi wake hakika wewe ni wewe ni mtukufu na msifiwa wa haki.
13.Dua kabla ya salamu Ni sunnah kuleta dua kabla ya salamu. Dua hizi ni nyingi ila miongoni mwanzo ni Dua aliyotufundisha Mtume (s.a.w) kwa msisitizo mkubwa kama tunavyofahamishwa katika Hadithi ya Muslim, iliyosimuliwa na Ibn Abbas, ni hii ifuatayo: Allahumma Inni-audhubika min-’adhaabi-lqabri,Wa-auudhubika min fitnatil masiihi-ddajjaal, Wa-auudhubika min fitnatil-mahyaa wal-mamaati, “Ee Allah najikinga kwako kutokana na adhabu ya kabr, na najikinga kwako kutokana na fitina za masiihi Ddajjaal na najikinga kwako kutokana na matatizo ya maisha na mauti.
Sijidat-Sah-wi (Sijda ya kusahau) Sijdat Sah-wi ni sijidah anayoileta mtu kabla ya kutoa salaam ili kufidia kitendo cha sunnah alicho kisahau kwa mfano kusahau kukaa tahiyaatu ya kwanza.Vile vile mtu akisahau au akikosea jambo lolote ambalo halibatilishi swala kwa mfano akaswali rakaa tano badala ya rakaa nne kwa swala ya Adhuhuri. Kabla hajamaliza swala alete sijidat Sahau. Hivi ndivyo tunavyojifunza kutokana na Hadithi zifuatazo: Abdullah bin Mas’ud (r.a) amesimulia: Mtume wa Allah alituswalisha Adhuhuri rakaa tano.Tukamuuliza kama pameamrishwa na Mwenyezi Mungu kurefushwa swala akajibu, La! Tukamuambia: “Umetuswalisha rakaa tano. Akasema (Mtume): Mimi ni binaadamu kama nyinyi, nakumbuka kama mnavyokumbuka na nasahau kama mnavyosahau. Kisha akasujudu sijdah mbili zikawa ni fidia kwa kusahau. (Bukhari na Muslim).
Muhimu: Kumbuka kuwa sijda hii Mtume (s.a.w) aliileta baada ya kutoa salaamu na baada ya kukumbushwa. Abdullah bin Buhaymah (r.a) amesimulia kuwa Mtume (s.a.w) aliswalisha swala ya adhuhuri, akasimama baada ya rakaa mbili, alipomaliza swala akasujudu mara mbili huku akisema: “Allah Akbar” katika kusujudu na katika kuinuka, wakati amekaa kabla ya kutoa salaam, na watu wakasujudu pamoja naye. Hii ilikuwa ni kufidia ile tahiyyatu ya mwanzo aliyoisahau”. (Muslim)
14.kutoa salamu. Kutoa salamu ni nguzo katika nguzo za swala. Ukamilifu wa kutoa salamu ni kusema “as-salaamu alykum warahmatullahi wabarakaatuh” salamu zipo mbili yakwanza utatoa upande wa kulia na ya pili utatoa upande wakushoto. Sifa ya kugeuka kwa kutoa salamu ni kuwa utageuka mpaka mashavu yawze kuonekana kwa mtu aliye nyuma.
Lugha ya Swala Lugha ya swala, kuanzia kwenye Takbira ya kuhirimia Swala mpaka kumalizia swala kwa Salaam, ni Kiarabu. Hekima yake iko wazi. Kiarabu ndio lugha ya Qur-an tukufu na kwa hiyo ndio lugha rasmi ya Kiislamu inayowaunganisha Waislamu wote ulimwenguni. Waislamu ni umma mmoja tu na Waislamu wote ni ndugu moja wasio baguana kwa lugha, rangi, taifa wala ubaguzi mwingine wa aina yoyote ile.Muislamu yeyote anaweza kuwa Imamu mahali popote ilimradi tu awe anatekeleza masharti ya Uimamu. Muislamu hana msikiti maalum. Misikiti yote ni yake na anaweza kuswali kwenye msikiti wowote ulimwenguni bila ya kupata tatizo lolote la lugha. Kwa sababu hii kila Muislamu inabidi ajifunze kiasi cha uwezo wake kutamka, kwa Kiarabu yale yote tuyasemayo katika swala.
Mambo yanayobatilisha Swala Mtu akiwa katika swala yuko katika hali maalum na haruhusiwi kufanya kitu kingine nje ya swala hata vile vitendo vya kawaida alivyovizoea. Hivyo ukiwa ndani ya swala ukifanya au kukitokea moja ya mambo yafuatayo, swala yako itakuwa imebatilika na itabidi uanze upya. (a)Kutoelekea Qibla kwa kifua pasi na dharura yoyote ya kisheria. (b) Kupatikana na hadathi kubwa, ndogo au ya kati na kati. (c) Kufikwa na najisi mwilini, nguoni au mahali pa kuswalia. (d) Kuvukwa na nguo ukawa uchi. Wanaume wanaovaa shati fupi wajihadhari sana hapa kwani,hasa wakati wa kurukuu na kusujudu, migongo yao (viuno vyao) chini ya usawa wa kitovu (panda za makalio) huwa wazi na hivi huhesabiwa kuwa wako uchi. (e) Kusema au kutamka makusudi lau herufi moja yenye kuleta maana nje ya maneno ya swala.Mtume (s.a.w) amesema: gHakika ya hii swala, haifai ndani yake maneno ya watu kwani swala yenyewe ni Tasbih, Takbir na kusoma Qur-an. (Muslim) (f) Kula au kunywa japo kwa kusahau. (g) Kufanya jambo lisilowiana na swala mfululizo mara tatu. (h) Kuiacha nguzo yoyote ya swala (i) Ukizidisha nguzo yoyote ya swala makusudi. (j) Kumtangulia Imam au kuchelewa kwa nguzo mbili za kimatendo kwa makusudi. (k) Kutia nia ya kuikata swala au kujishauri moyoni kuwa uikate au usiikate swala. (l) Kuwa na shaka kuwa umetimiza au hujatimiza sharti au nguzo yoyote ya swala. (m) Kupotewa na akili au kulala ndani ya swala. (n) Kutoa Salaam kwa makusudi kabla ya kwisha swala. (o) Kuswalishwa na asiyekuwa Muislamu. (p) Kukhalifu utaratibu wa nguzo za swala, yaani kutangulia kutekeleza nguzo ya swala kabla ya kutekeleza nguzo inayostahiki kutangulia katika utaratibu wa swala. (q) Kuleta dua ya kuomba kitu haramu au muhali. (r) Kumshirikisha Allah (s.w) katika kuleta dua yaani kuleta dua ya kuomba kitu cha halali lakini humuombi Allah (s.w) peke yake.
Dua na Dhikri Baada ya Swala Ni vizuri mara Muislamu anapomaliza kuswali kama hana dharura yoyote asiondoke bila ya kuleta Dhikri na dua kama alivyofundisha Mtume (s.a.w), kwani zina umuhimu mno katika kumsaidia mja kufikia lengo la swala na lengo la kuumbwa kwake kwa ujumla iwapo atayafahamu na kuyazingatia yale anayoyatamka. Kutokana na Hadithi iliyosimuliwa na Samura bin Jandab(r.a) na kupokelewa na Bukhari(r.a), baada ya swala Mtume (s.a.w) aliwageukia Waislamu aliokuwa akiwaswalisha. Kisha aliomba maghfira (msamaha) mara tatu na kuongezea maneno yaliyoelezwa katika Hadithi zifuatazo: Thawban (r.a) amesimulia kuwa Mtume (s.a.w) alipomaliza swala aliomba maghfira (msamaha) mara tatu kwa kusema: Astagh-firullah (Mara tatu) Ninaomba msamaha kwa Allahh na kusema “Allahumma Antassalam waminkas-salaam Tabaarakta YaaDhal jallaali Wal-ikraam.” Ewe Allah, wewe ni Amani, na kwako ndiko iliko Amani. Wewe ndiye Mbariki Ewe Mwenye Utukufu na Heshima (Muslim)
Baada ya nyiradi hizi, ni vizuri pia kuomba dua yoyote kulingana na haja zako kwa lugha yoyote. Jambo hili la kuomba dua baada ya swala, umuhimu wake unadhihirika katika hadithi ifuatayo: Abu Umamah amesimulia kuwa: Iliulizwa: Ee Mtume wa Allah. ni dua gani ambayo hukubaliwa zaidi?h (Mtume) alijibu: (moja) ni ile ya katikati ya nusu ya pili ya usiku na (pili) kila baada ya swala ya faradhi. (Tirmidh)
Hivyo ni jambo la msingi mno kuomba dua yoyote kila baada ya swala na dua zilizo nzito zaidi ni zile zilizomo kwenye Qur-an na hadithi za Mtume (s.a.w). Kwa mfano ni vizuri kila baada ya swala, au baada ya dhikri zilizotajwa tuombe dua ifuatayo: Rabii ij’alnii muqiimas-swalaati wamindhurriyyatii Rabbana Wataqabbal du’aaai. Mola wangu! Nijaalie niwe msimamishaji swala, na kizazi changu! (Pia kiwe hivi). Mola wetu! Na upokee maombi yangu mengine... (14:40-41).
Pata kitabu Chetu Bofya hapa