image

Kisa cha Israa na Miraji na kufaradhishwa swala tano

Safari ya Mi'rajKatika mwaka wa 12 B.

Kisa cha Israa na Miraji na kufaradhishwa swala tano

Kisa cha Israa na Miraji na kufaradhishwa swala tano

Safari ya Mi'raj
Katika mwaka wa 12 B.U(Baada ya Utume) sawa na Oktoba, 621, Mtume(s.a.w) alichukuliwa usiku na malaika Jibril na Mikailu



kwa safari ndefu sana lakini iliyochukua muda mfupi sana. Safari hii iligawanyika kaitka sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni safari ya hapa ardhini kutoka msikiti mtukufu wa Makka, Masjidil-Haraam mpaka msikiti mtukufu wa Jerusalemu, Baitul-Muqaddas, (Masjidul-Aq-Swaa). Safari hii ya hapa ardhini inajulikana kwa jina la Israa ambayo imetajwa katika Qur'an:




"Utukufu ni wake yeye ambaye alimpeleka mja wake usiku kutoka msikiti mtukufu (wa Makkah) mpaka msikiti wa mbali (wa Baytul Muqaddas - Jerusalem) ambao (tumeubariki na) tumevibariki vilivyomo pembezoni mwake. (tulimpeleka hivyo) ili tumuonyeshe baadhi ya alama zetu. Hakia yeye (Mwenyezi Mungu)ni Mwenye kusikia (na) Mwenye kuona". (17:1).



Sehemu ya pili ni safari ya mbinguni inayoanzia Baitul- Muqaddas mpaka mbingu ya Saba. Safari hii ya sehemu ya pili imeelezwa kwa urefu kaitka vitabu vya Hadithi. Kutokana na Bukhari na Muslim, Mtume(s.a.w) alielezea kisa hiki kama ifuatavyo:



Nililala Makka katika nyumba ya Umm Haani Binti Abu Talib dada wa Ally bin Abu Taalib, wakati Jibril aliponijia. Alinichukua mpaka kwenye kisima cha Zam-zam karibu na Ka'abah. Alinipasua kifua changu katika upande wa moyo, akautwaa moyo na kuuosha kwenye beseni la dhahabu, akaujaza hekima, huruma na imani na kisha akaurudishia mahali pake na kufunga kifua. Kisha akaleta mnyama kama farasi (Burak) mweroro na mweupe, mwenye umbo la kadiri, mdogo kuliko nyumbu na mrefu kuliko punda, mwepesi na mwenye mwendo wa kasi sana ambaye huweka kwato zake kila mwisho wa upeo wa macho. Nilimpanda mpaka Baytul-Muqaddas-Jerusalem na kumfunga mahali walipokuwa wakiwafunga wanyama wao Mitume.



Niliingia Msikitini na kuswali rakaa mbili pamoja na mitume wote, nilikuwa Imamu wao. Baada ya kutoka nje, Jibril aliniletea vyombo viwili, kimoja cha mvinyo na kingine cha maziwa. Nilichaguwa mazima na Jibril akasema umechagua kinywaji asilia. Kisha alinichukua mbinguni juu ya mnyama yule (Burak). Jibrili aliomba afunguliwe. Ikaulizwa: Wewe ni nani? Akajibu Jibril. Kisha aliulizwa: Nani uliyeongozana naye? Alijibu (Jibril): Muhammad. Ikaulizwa: Ameitwa? Jibril akajibu: Naam, hakika ameitwa.



Mbingu ya kwanza ilifunguliwa kwa ajili yetu na lo: Tunamuona Adam(a.s). Alinikaribisha na kuniombea kheri. Kisha tulipanda mpaka uwingu wa pili ambapo Jibril aliomba kufuguliwa na akaulizwa kuwa yeye ni nani? Akajibu Jibril; na aliulizwa tena: Ni nani mliye wote? Alijibu Muhammad. Ikaulizwa: Ameitwa? Akajibu: Naam, hakika ameitwa.



Mbingu ya pili ilifunguliwa, na nilipoingia nilikaribishwa na Issa bin Maryam na Yahya bin Zakariya mabinamu kwa upande wa mama walinikaribisha na kunitakia rehma. Kisha nilichukuliwa mpaka mbingu ya tatu na Jibril aliomba ifunguliwe. Aliulizwa: Nani wewe? Alijibu: Jibril. Aliulizwa tena: Nani anayeongozana na wewe? Alijibu Muhammad. Ikaulizwa je, ameitwa? Alijibu: Naam, hakika ameitwa. Tulifunguliwa na nilimuona Yusuf (a.s) aliyepewa nusu ya urembo na uzuri wa sura wa dunia nzima. Alinikaribisha na aliniombea kheri kisha tuliongozana mpaka uwingu wa nne. Jibril aliomba afunguliwe. Iliulizwa kuwa yeye ni nani. Alijibu: Muhammad. Ikaulizwa: Je, ameitwa? Alijibu: Naam, hakika ameitwa.



Mlango ulifunguliwa kwa ajili yetu, na lo! Idris (a.s) alikuwa pale. Alinikaribisha na kuniombea kheri. Na Allah (s.a.w) amesema: "Na tulimuinua (Idris) daraja ya juu kabisa" (Qur'an: 19:57). Kisha tulipanda naye mpaka uwingu wa tano na Jibril aliomba (mlango) ufunguliwe. Iliulizwa tena: Ni nani mliyeongozana? Alijibu: Muhammad. Ikaulizwa: Je, ameitwa? Akajibu: Naam, hakika ameitwa. Tulifunguliwa na Lo! Nikawa na Haruun (a.s). Alinikaribisha na akaniombea kheri. Kisha nilichukuliwa mpaka uwingu wa sita. Jibril aliomba ifunguliwe. Ikaulizwa; nani wewe? Akajibu: Jibril. Ikaulizwa tena; nani uliye pamoja naye? Alijibu: Muhammad. Kisha ikaulizwa: Ameitwa? Akajibu: Naam, hakika ameitwa.



Tulifunguliwa na kumkuta Mussa(a.s). Alinikaribisha na kuniombea kheri. Kisha nikapelekwa mpaka uwingu wa saba. Jabir aliomba pafunguliwe. Ikaulizwa: Nani wewe ? Akajibu: Jibril. Ikaulizwa tena: Ninani uliyeongozana naye? Akajibu: Muhammad. Ikaulizwa: Ameitwa? Akajibu: Hakika ameitwa. Tulifunguliwa na nikamuona Ibrahim akiwa ameegemea Baitul'Ma'muur na kunaingiwa humo na malaika elfu sabini (70,000) kila siku ambao hawatazuru tena sehemu hiyo milele. Kisha nilipelekwa "Sidratul-'Muntahaa, (Mti wa Kivuli) ambao majani yake mapana kama masikio ya tembo na matunda yake kama vyombo vikubwa vya udongo. Na ulipofunikwa kwa amri ya Allah ulibadilika kwa kiasi ambacho hakuna yeyote katika viumbe anayeweza kuusifu uzuri wake; (Qur'an 53:16). Kisha Allah(s.w) aliniletea (alinishushia) wahyi na akanipa amri ya Swala hamsini kwa kila mchana na usiku.



Kisha nilishuka kwa Musa (a.s) (uwingu wa sita) akaniuliza: Ni kitu gani Mola wako alichokiamrisha kwa Umma wako? Nikajibu: Swala hamsini. Akasema (Musa): Rejea kwa Bwana wako umuombe akupunguzie (idadi ya swala hizo) Umma wako hautaweza kulibeba jukumu hilo. Nimewajaribu wana Israil (nikawakuta dhaifu mno kiasi cha kutoweza kubebe jukumu hilo). Nilirudi kwa Bwana wangu na kumuomba Ee Mola wangu, Nifanyie tahfifu kwa Umma wangu. Allah(s.w) akanipunguzia swala tano zikabakia arobaini na tano). Nikaenda chini kwa Musa(a.s) na kumueleza: Allah amenipunguzia swala tano. Akasema (Musa a.s): Hakika Umma wako hautaweza kubebe jukumu hili, rejea kwa Bwana wako umuombe akufanyie tahfifu.



Nilibakia kwenda na kurudi kati ya Allah(s.w) na Musa(a.s) mpaka Allah(s.w) akasema: "Kuna swala tano kwa kila mchana na usiku wake (kwa kila siku). Ee Muhammad, kila moja italipwa kama kumi, kwa hiyo inafanya idadi ya swala hamsini (5 x 10 = 50). Yule atakayenuia kufanya kitendo kizuri na asikifanye atalipwa au ataandikiwa jaza ya jema moja na akifanya atalipwa kama mtu aliyetenda kitendo hicho mara kumi; ambapo yule atakayenuia kufanya kitendo kiovu na asikifanye, hatalipwa chochote, na kama atakifanya, atalipwa jaza ya kitendo kibaya kimoja tu". Kisha nilishuka chini na nilipompitia Musa(a.s) na kumueleza, alisema: Rudi kwa Bwana wako umuombe tahfifu. Juu ya jambo hili nilisema: "Naona haya kurudi tena kwa Bwana wangu". (Bukhari na Muslim).



Katika Qur'an sehemu ya safari inagusiwa katika aya zifuatazo:


"Na (Mtume) akamuona (Jibril) mara nyingine (kwa sura yake ya kimalaika katika usiku wa Mi'raj). Penye mkunazi wa kumalizikia (mambo yote). Karibu yake ndio kuna hiyo Bustani (Pepo) itakayokaliwa (daima na hao watu wema). Kilipoufunika mkunazi huo kilichoufunika (katika mambo ya kiajabu ya huko mbinguni). Jicho halikuhangaika wala halikuruka mipaka. Kwa yakini aliona (Nabii Muhammad) mambo makubwa kabisa katika alama za Mola wake". (53:13-18).



Safari ya Mi'raj kama ilivyoelezwa katika Qur'an na Hadith yaonesha ilikuwa na malengo mawili makubwa.

Kwanza, yaonyesha ilikuwa na lengo la kumpa Mtume(s.a.w) mafunzo zaidi juu ya kazi yake kutokana na alama mbali mbali

alizokusudiwa kuonyeshwa na Mola wake. Qur'an inatufahamisha juu ya lengo hili na inatuhakikishia kufikiwa kwake kama ifuatavyo:


".............li tumuonyeshe baadhi ya alama zetu............." (17:1)



"Kwa yakini aliona mambo makubwa kabisa katika alama za Mola wake". (53:18).



Mtume(s.a.w) akiwa ni mwalimu wetu na kiigizo chetu, pamoja na kupewa miongozo na kufahamishwa juu ya mambo mbali mbali kwa njia ya wahay kupitia kwa malaika Jibril, bado Mola wake alimtaka aone alama mbali mbali katika mambo ya ghaibu ili ziwe msaada kwake katika kufikisha ujumbe wake kwa watu. Kuona na kutafakari juu ya alama za Allah(s.w) hukomaza zaidi imani ya mja na hivyo humfanya awe madhubuti zaidi katika kufikisha na kusimamisha ujumbe wa Allah(s.w) katika jamii. Izingatiwe kuwa Muhammad(s.a.w) ni Mtume wa mwisho na ujumbe wake unatakiwa udumu mpaka siku ya mwisho. Kwa hiyo Mtume(s.a.w) ilibidi awe madhubuti na mfanyaji kazi zaidi katika kufikisha ujumbe wake kuliko mitume wengine. Si hivyo tu bali alitakiwa ahakikishe kuwa watu wanaupokea na kuuelewa vilivyo ili na wao waufikishe vilivyo kwa watu wengine watakaoendelea na kazi hiyo mpaka siku ya mwisho.



Pili, yaonyesha pia safari hii ilikuwa na lengo la kuwatahini watu. Katika hali ya kawaida, ni jambo lisilowezekana kwa mtu kusafiri kutoka Makka hadi Jerusalem kwa masaa machache ya usiku katika enzi hizo ambapo hapakuwa na vyombo vya usafiri vya kileo. Hivyo Mtume(s.a.w) kusafiri hadi Jerusalem na kwenda mbinguni kisha akarejea Makka katika usiku mmoja ulikuwa ni mtihani mkubwa kwa watu, hasa kwa Waislamu, kama wataamini uwezo wa Allah, au la. Asubuhi iliyofuatia usiku wa safari yake,



Mtume(s.a.w) aliwafahamisha watu waliokusanyika katika eneo la Ka'abah kuwa usiku alikwenda Baitul-Muqaddas na kurudi na hakutaka kuwatajia kwanza safari ya mbinguni. Alipowapa habari hii Maquraish wakiwemo baadhi ya waislamu walimzomea na kumwita mwongo. Mara akaja Mut'im bin Adi yule aliyempa Mtume hifadhi ya kukaa Makka, pale alipokataliwa kuingia Makka baada ya safari ya Taif, akamwambia:



"Muhammad! Mambo yote kabla ya leo yalikuwa mepesi. Ama ya leo uwongo wako ni dhahiri. Mimi nashuhudia kuwa wewe ni mwongo. Baitul Muqaddas tunakwenda na kurudi kwa muda wa miezi miwili, iweje udai kuwa umekwenda huko na kurudi kwa usiku mmoja? Leo mwisho wangu na wewe, huna hifadhi yangu katika mji wa Makka”13



Wakatoka wale Waislamu waliorejea ukafirini (kutokana na safari hii, wakaenda kumhadithia Abubakar juu ya maelezo ya Mtume(s.a.w) juu ya safari yake ili naye apate kurejea ukafirini kama wao. Abubakar akawajibu, "Kama Muhammad anadai hayo, basi mimi nimemsadiki. Namsadiki kwa habari za mbinguni anazoshushiwa na Allah kila siku, seuze za hapo Baitul- Muqaddas"? Abubakar alikwenda pale alipokuwa Mtume(s.a.w), akamkuta anaelezea ulivyo msikiti wa baitul-Muqaddas, baada ya kutakiwa afanye hivyo na wapinzani wake waliokuwa wamemzonga pale. Baada ya kumaliza maelezo yake juu ya msikiti wa Baitul-Muqaddas, Abubakar alisema, "Sadakta, Sadakta" - umesema kweli, umesema kweli". Kuanzia siku hiyo Mtume(s.a.w) alimpa jina la Abubakr "al-Saddiq" - yaani Abubakar "Msadikishaji kuliko watu wote".



Baada ya kuuelezea msikiti wa Baitul-Muqaddas ulivyo, Maquraish walimtaka aeleze juu ya misafara yao, Muhammad(s.a.w)alitoa habari zote za misafara yao na alama alizowaachia wasafiri mahali alipowakuta. Maquraish wakasema



"Ngojea ikija misafara hiyo na yakathibitika haya unayotueleza, papo hapo tutakuamini sote". Hata siku ilipokuja misafara hiyo na yakathibitishwa yale aliyoyaeleza Mtume(s.a.w) aliruka Walid bin Mughira akasema, "Wallah" huyu ni mchawi mkubwa, wala hatumuamini mchawi sisi". Wote waliokuwa hapo walisema, "kasema kweli Walid, sisi hatumwamini mchawi".



Safari hii ya Mi'raj, ilikuwa ni kichujio cha kuwatenganisha waumini wa kweli na waumini waliokuwa na ati-ati (wasiwasi) na kuamini uwezo wa Allah(s.w) na sifa zake zote. Kweli hapana linaloshindikana kwa Allah(s.w). Akitaka jambo liwe hauliamrisha "kuwa" na likawa ple pale. Mtihani huu haukuishia kwa Waislamu wa wakati ule tu bali mpaka leo hii kuna baadhi ya watu wajiitao waumini wa Allah(s.w), lakini bado hawaamini kuwa safari ya Mi'raj ilikuwa ya kimwili kama ilivyoelezwa katika Qur'an na Hadithi Sahihi. Wao wanadai kama walivyodai Maquraish, kuwa haiwezekani ikawa safari ya kimwili, bali ya kiroho. Maquraysh baada ya ushahidi wa kutosha walidai kuwa safari ile ilikuwa ya kichawi. Je, wale wanaodai kuwa safari ya Mtume(s.a.w) ya Mi'raj ilikwa ya kichawi au ya kiroho, wanaamini kuwa pia hizi television,internet,umeme, safari katika anga na vitu vingine vya kiteknolojia ya hivi leo, navyo ni vitu vya kichawi au vya kiroho?



                   





           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 1938


Sponsored links
👉1 Kitabu cha Afya     👉2 Kitau cha Fiqh     👉3 kitabu cha Simulizi     👉4 Madrasa kiganjani    

Post zifazofanana:-

Upinzani Dhidi ya Dola ya Kiislamu Wakati wa Makhalifa
Soma Zaidi...

Imam Abu Hanifa: Nuuman Ibn Thabit
Soma Zaidi...

Kuangamizwa kwa Watu wa Lut(a.s) watu wa Sodoma na Gomora
Watu wa Lut(a. Soma Zaidi...

HISTORIA YA MAISHA YA MTUME S.A.W KABLA YA UTUME
MAISHA YA MTUME (S. Soma Zaidi...

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Ismail(a.s)
Kutokana na Historia ya Nabii Ismail(a. Soma Zaidi...

Kuandaliwa kwa Muhammad wakati na baada ya kupewa utume
Bara arabu zama za jahiliyyah (EDK form 2: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Kuporomoka kwa Dola ya Kiislamu
Soma Zaidi...

Maana ya Funga ya ramadhani kisheria na Aina za funga
Amesema mtume (s.a.w) kuwa Allah (s.w) amesema: kila amali ya mwanaadamu ni kwa ajili yake isipokuwa funga. Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ismail katika quran
KKatika somohili utakwenda kujifunzahistoriaya Mtume Ismail Mtoto wa Nabii Ibrahim Soma Zaidi...

Hija ya kuaga kwa mtume, na hutuba ya mwisho aliyotowa mtume katika hija
Mwaka mmoja baada ya msafara wa Tabuuk Bara Arab zima ilikuwa chini ya Dola ya Kiislamu. Soma Zaidi...

Imam Tirmidh na Jami'u At-Tirmidh
Soma Zaidi...

Kukomeshwa kwa Riddah na Chokochoko Nyingine katika dola ya kiislamu
Soma Zaidi...