Je Qur-an ilikusanywa na kuandikwa katika msahafu wakati wa uongozi wa Abu-Bakr(r.
Je Qur-an ilikusanywa na kuandikwa katika msahafu wakati wa uongozi wa Abu-Bakr(r.a)
Kwa muda mrefu imekuwepo nadharia kuwa Qur-an katika umbo lake la Msahafu au kitabu imeanza wakati wa Khalifa Abu Bakr baada ya kushauriwa na 'Umar ibn Khattab(r.a). Na inavyosemekana ni kwamba kwanza Abu Bakr (r.a) alikataa ushauri huo kwa kuwa jambo hilo Mtume(s.a.w)hakufanya. Baada ya kuona kuwa ni kweli Qur-an itaweza kupotea maadamu wale waliokuwa wamehifadhi wanakufa, Abubakar alikubali ushauri wa Umar.
Tunaambiwa kuwa Khalifa Abu Bakr(ra) alimchagua Zaid bin Thabit kuifanya kazi ya kuandika Msahafu. Kazi hii ilifanyika kwa kukusanya mifupa, mawe, makozi ya mitende pamoja na ngozi ambamo inasadikiwa kuwa ndimo Qur-an ilimokuwa imeandikwa wakati wote wa miaka 23 ya Utume. Hebu turejee Hadith iliyopokelewa na Imam Bukhari, na kusimuliwa na Zaid bin Thabit (ra) kuwa:
"Abu Bakr alinitumia mtu kuja kuniita wakati watu wa Yamama walipouliwa (masahaba walipopigana na Musailama). (Nilikwenda) na nilimkuta 'Umar bin Khattab amekaa pamoja naye, Abu Bakr akaniambia: "'Umar amenijia na akaniambia kuwa siku ya Yamama, mauaji mengi yametokea kwa mahafidhi wa Qur-an na nahofia kuwa huenda mauaji yakatokea tena kwa mahafidhi katika vita vingine jambo ambalo linaweza kupelekea sehemu kubwa ya Qur-an kupotea. Hivyo nakushauri (wewe Abu Bakr) kuwa uamrishe kuwa Qur-an ikusanywe." Nikamwambia 'Umar: "Vipi nitafanya jambo ambalo Mtume wa Allah hajalifanya?" 'Umar akaniambia kuwa: "Wallahi; kufanya hivyo ni jambo zuri", na hakuacha kunitaka kufanya hivyo mpaka Allah akaondosha uzito kifuani mwangu na nikaanza kuona uzuri wa mawazo aliyoyaona Umar. Kisha Abu Bakr akaniambia (mimi Zaid): "Wewe ni mtu mwenye akili na hatuna wasi wasi nawe, na wewe ulikuwa ukimuandikia wahyi Mtume (s.a.w).
Hivyo vitafute vipande vya Qur-an na uvikusanye'. Wallah! (anasema Zaidi kuwa) lau kama wangeniamrisha kuondoa mmojawapo wa milima, basi lisingelikuwa jambo gumu (zito) kuliko kuikusanya Qur-an. Kisha nikamuuliza Abu Bakr: "Vipi utafanya kitu ambacho Mtume wa Allah hakukifanya?" Abu Bakr alijibu: "Wallahi; kufanya hivyo ni jambo zuri", na akaendelea kunitaka nifanye hivyo mpaka Allah akanipa wepesi kifuani mwangu kama alivyofanya kwa Abu Bakr na 'Umar. Hivyo nikaanza kuitafuta Qur-an (iliyokuwa imetapanyika vipande vipande) katika makozi ya mitende, mawe na mahafidhi na kuikusanya mpaka nikaipata aya ya mwisho ya Suratul-Tawbah kwa Abi Khuza 'ymal Ansari; na sikuikuta aya hii kwa yoyote isipokuwa yeye 'Amekujieni Mtume aliye jinsi moja na nyinyi, yanamuhuzunisha yanayokutaabisheni…" mpaka mwisho wa aya (9:128-129). Kisha nakala ya Msahafu ikabakia kwa Abu Bakr mpaka alipofariki, kisha ikabaki kwa 'Umar mpaka mwisho wa maisha yake na hapo tena kwa binti yake Hafsa. (Bukhari).
Hadithi hii pamoja na kuwa imepokelewa na Imam Bukhari bado inatupa maswali mengi sana ya kujiuliza kwani kwanza inapingana na Qur-an yenyewe, pili inapingana na ushahidi wa kihistoria pamoja na hadithi nyingine na tatu haikubaliki hata kiakili (kimantiki).
(a)Kupingana na Qur-an:
Hadithi hii inayosimulia kuwa Qur-an ilikusanywa na Zaid bin Thabit(r.a) kutoka kwenye makozi ya mitende na mawe na kutoka kwa mahafidhi inapingana na Qur-an kwa sababu zifuatazo:
(i) Mwenyezi Mungu (s.w) ameikusudia Qur-an iwe kitabu hata kabla ya kuumbwa chochote katika maumbile yake aliyoyaumba.Kama inavyoashiriwa katika aya mbali mbali kwamba Qur-an ilikuwako kwenye Lawhil Mahfudh hata kabla ya kuteremshwa kwa Mtume (s.a.w) kulingana na matukio
“Bila shaka hiki (mnachosomewa) ni kitabu kilichokusanya kila yanayohitajiwa na chenye heshima. Kimetolewa katika hicho kitabu kilichohifadhiwa kweli kweli." (56:77-78).
"Bali hii ni Qur-an tukufu. (Iliyotolewa) katika huo ubao uliohifadhiwa (wa Allah)." (85:21-22).
Aidha Mwenyezi Mungu katika aya mbali mbali amekuwa akiiashiria Qur-an na akiita kitabu:
"Hiki ni kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uongozi kwa wamchao Mwenyezi Mungu." (2:2). Vile vile rejea 3:3, 7; 7:2; 10:1; 13:1; 14:1, n.k
Kutokana na marejeo hayo haiwezekani kuwa pawe hapana kitu cha aina hiyo lakini bado Mwenyezi Mungu arudie namna hiyo. Kweli, neno "kitab" linatumika kwa vitu mbali mbali vilivyoandikwa kama mikataba au hata barua lakini bado katika Qur-an neno hili limetumika kurudia kitabu katika maana halisi hasa ya kitabu. Chukua mfano, aya ya 7 ya Suratul Al-Im ran:
“Yeye ndiye aliyekuteremshia Kitabu. Ndani yake zimo aya Muhkam (nyepesi kufahamika) ambazo ndizo msingi (asili ya Kitabu). Na ziko nyingine Mutashabihat…" (3:7)
Hivyo Allah(s.w) alipotaja neno Al-Kitab kwa kuirudia Qur-an alikuwa na maana hiyo na ndiyo maana Mtume(s.a.w) alipokuwa katika Hija yake ya kuaga alisema nimekuachieni vitu viwili - Kitabu cha Allah na Mwendo wangu. Mtume(s.a.w) asingelisema hivyo kama kitabu hicho hakikuwepo.
(ii)Hadith hiyo pamoja na kuwa imepokelewa na Imam Bukhari bado inakataa aya zifuatazo za Qur-an:
Na (Naapa) kwa Kitabu kilichoandikwa katika karatasi ya ngozi (iliyo safi na) kikakunjuliwa (kisomwe)." (52:2-3).
Katika aya hii Allah (s.w) anatuambia wazi wazi kuwa Qur-an ni Kitabu kilichoandikwa katika karatasi za aina fulani ambazo zilikuwa zikitumika wakati wa zama hizo. Ni karatasi za aina hiyo h iyo, kama tutakavyoona baadaye, am bazo Mtu me(s.a.w) alizitumia kuandikia barua zake na kuwatumia wafalme mbali mbali na kutumiwa na baadhi ya Masahaba kuandikia vitabu vyao.
Kabla hatujaendelea kufafanua zaidi hoja hii ni vyema kunukuu maneno ya mwanazuoni - Qutubi alivyofafanua aya hizo:
"… Na ameapa (Mwenyezi Mungu) kwa "Kitabu manshurin" (kitabu kilichoandikwa) yaani kilichoandikwa nacho ni Qur-an wanayoisoma Waislamu katika Masahafu na wanayoisoma Malaika katika Lawhul Mahfudh. Na pia inasemwa kuwa (Allah) ameviapia vitabu vingine vyote vilivyoteremshwa kwa Mitume kwani kila kitabu kilikuwa katika karatasi (ya ngozi) wakikunjuliwa watu wake wakisome. Ama "Arraqqu" ni ile iliyotengenezwa kwa ngozi ili iandikiwe ".4
Lawhul Mahfudh ambao ni ubao uliohifadhiwa hautegemewi kuwa karatasi za ngozi kwani hii ni teknolojia ya mwanaadamu ambayo Mtume(s.a.w) alikutana nayo. Hivyo makusudio ya aya ni Qur-an au Msahafu.
Kutokana na ufafanuzi huo hatuwezi kusema Qur-an ilikuwa imeandikwa katika mifupa wala makozi ya mitende kwani itapingana na aya hii ambayo iko wazi. Haitakuwa na nafasi hata ikipokelewa na maimamu wote kwani kigezo kikuu cha Hadithi ni kutopingana na aya yeyote ya Qur-an. Na kwa nini Zaid(r.a) aone uzito wa kukusanya Qur-an ambayo imeashiriwa na Allah(s.w) kuwa ni kitu kilichopo? Na uzito wenyewe uwe ni zaidi ya kuusogeza mlima!
Kusema hivyo ni kukana aya nyingine za Qur-an pale Allah (s.w) aliposema kuwa kazi ya kuikusanya Qur-an ni yake. Turejee aya zifuatazo:
"Usiutikise ulimi wako kwa (kuufanyia haraka) wahyi (unapoteremka).Kwa hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha." (75:16-17)
Hapa aya inasema wazi kuwa kazi ya kuikusanya Qur-an siyo kifuani mwa Mtume(s.a.w) tu bali kuhakikisha kutoharibiwa kwake pamoja na kuteremka kwake kidogo kidogo ni ya Allah(s.w) kinyume chake Hadith inasema kazi hiyo aliifanya Zaid(r.a)!
(b)Kupingana na Ushahidi wa Kihistoria
Hadith hii pia inapingana na ushahidi wa kihistoria kwa sababu:
(i) Katika hadithi maarufu sana iliyopokelewa na Imam Muslim toka kwa Ibnu Mas-'ud, Mtume amesema katika Hijja yake ya kuaga kuwa:
"Na nimewaachieni vitu wili ambavyo mkishikamana navyo hamtapotea kamwe baada yangu - Kitabu cha Allah na Sunnah yangu." (Musilim)
Hadith hii kiakili haiashirii kitu ambacho hakijulikani kilipo na chenye ugumu kupatikana kama alivyoeleza Zaid (r.a) bali ni kitu ambacho kila mmoja anatarajiwa kukifikia pasipo na ugumu wowote. Wala Hadith hii haishirii kitu ambacho kimetawanyika katika mawe na mifupa ambayo pa kupatikana hapafahamiki bali ni kitu kilichokusanywa na kuhifadhiwa mahala maalumu.
(ii)Ukiacha hadithi hiyo, kuna hadithi nyingine ambayo ameipokea mwenyewe Imamu Bukhari ambayo inasema wazi kabisa kuwa Mtume ameacha Msahafu:
'Abdul'-Aziz bin Rufai(ra) ameeleza kuwa: "Mimi na Shaddad bin Ma 'aqil tuliingia kwa Ibnu "Abbas. Shaddad akamuuliza: Je Mtume (s.a.w) ameacha chochote?" akajibu (Ibn 'Abbas) "Hakuacha chochote isipokuwa (hiki) kilichopo baina ya magamba mawili (ya Qur-an)." Baadaye tulimtembelea Muhammad bin Al-Hanafiyya na akamuuliza suala (lile lile). Akajibu (Al-Hanafiyya), Mtume hakuacha kitu isipokuwa (hiki) kilichopo baina ya magamba mawili (ya Qur-an)." Hadithi hii, kwanza, inaisadikisha Qur-an kuwa ni kitabu (mas-hafu) ambacho kimeandikwa katika kurasa na kuwekewa magamba (bindings or covers) ili kihifadhike.
Pili, Hadithi hii inaisadikisha Hadith tuliyoirejea juu miongoni mwa vitu ambavyo Mtume ameviacha. Hapa tunaambiwa alichoacha ni kile kilicho baina ya magamba mawili - la mwanzo na mwisho - yaliyokuwa yamehifadhi Qur-an ambayo hapana shaka ilikuwa ndani ya karatasi za aina yake na siyo ndani ya mawe au m ifu pa.
Tatu,Hadith hii inathibitisha kuwa kweli Allah (s.w) aliikusanya Mwenyewe Qur-an na akaihifadhi katika muundo wa kitabu kupitia kwa Mtume wake.
(iii)Inapingana na Hadith iliyotolewa na Maimamu Tirmidhi na Darimi kuwa Mtume(s.a.w) amesema kwamba msafiri mzuri ni yule anayeianza Qur-an upya kila anapomaliza kuisoma na kwamba hili ndilo tendo analolipenda Allah. Wakati wa Mtume(s.a.w) tunaambiwa kuwa masahaba wengi walikuwa wamehifadhi Qur-an yote lakini bado walipatikana wengine ambao hawakufikia hatua hiyo. Na kwa namna tunavyowafahamu masahaba ambao walikuwa wakishindana katika kufanya mambo mazuri ni lazima wawe ambao huirudia tena na tena kama alivyoashiria Mtume (s.a.w). Sasa watu hawa walikuwa wakiipata wapi Qur-an ambayo ilikuwa imetawanyika kiasi cha aya nyingine kutojulikana zilipo na kugundulikana baadaye kama zilivyokuwa aya za Suratut-Tawbah?
Mitume wa Allah(s.w) siku zote waliwafundisha wafuasi wao vitu wanavyoweza kuvitekeleza na vipo katika mazingira yao, hivyo Mtume (s.a.w) naye alipoongea hivyo aliashiria kitu cha aina hiyo. Tunasoma katika historia kwamba hata baadhi ya masahaba ambao walikuwa mahafidhi wa Qur-an walikuwa wakisoma ile iliyoandikwa. Khalifa 'Uthman bin 'Affan aliuawa wakati akisoma Mas-hafu yake. Hii inawezekana kabisa kuwa ilikuwa ni desturi ya masahaba wengi na ndivyo Mtume (s.a.w) alivyoashiria.
(iv)Mpangilio wa sura zote zilizomo Msahafuni ukilinganishwa na kushuka kwake umeonekana ni tofauti. Mpangilio huu ni ule ambao Mtume (saw) mwenyewe aliuelekeza kama alivyoelekezwa na Allah (s.w). Fikiria aya 6666 ambazo zimeshuka kwa kipindi cha miaka 23 na hazifahamiki zilipowekwa (nani alikuwa mtunzaji) katika hayo mawe na mifupa ni vipi Mtume(s.a.w) angeweza kuashiria kwa waandishi wake kuwa aya hii iwekeni baada ya aya fulani na sura hii baada ya sura fulani?
Tukizingatia maneno ya Zaid(r.a) utakuta kuwa jambo hilo lisingeliwezekana kwani tangu kufariki Mtume(s.a.w) na alipoanza hiyo kazi haukuwa umepita hata mwaka mmoja na waandishi wa Mtume(s.a.w) wote walikuwepo bado. Lakini bado anasema aya moja hakuwa nayo yeyote yule zaidi ya Abu Khuzaymal Ansari ambaye hatuambiwi kuwa alikuwa ni mwandishi wa Mtume! Hadith hii inakataana na hali halisi kama tunavyoendelea kuiona.
(v)Tumeona kuwa Mtume (s.a.w) alikuwa na pupa ya kuhifadhi wahyi ili asije akasahau kiasi Allah(s.w) akamwambia asifanye hivyo:
"Usitikise ulimi wako kwa (kuufanyia haraka) wahyi (unapoteremka)." (75:16)
"Wala usiifanyie haraka (hii) Qur-an (kwa kusoma), kabla haujamalizika wahyi (ufunuo) wake." (20:114).
Sasa Mtume(s.a.w) ambaye alikuwa na pupa kiasi kama hicho cha kuhakikisha amehifadhi kila alicholetewa na Jibril(a.s) na kuhakikisha anaandikwa kila aya inayoteremka, iweje tena kuandika kwenyewe kuwe ndani ya mawe, makozi ya mitende na mifupa kiasi kwamba alipofariki haijulikani ameiweka wapi hiyo mifupa! Mtume(s.a.w) kulingana na khofu hiyo kabisa asigeliandika Qur-an mahala kama humo halafu asiweke mtu wa kuitunza bali iwe pata-potea. Hapana shaka huku ni kumsingizia Mtume(s.a.w) kuwa alikuwa haijali Qur-an:
(vi)Swali jingine la kujiuliza, kwa nini Mtume atumie mawe, mifupa na makozi ya mitende kuandikia maneno matukufu ya Allah(s.w) na wakati karatasi zilikuwepo na zikitumika? Qur-an yenyewe inathibitisha kuwa wakati ule karatasi zilikuwepo:
"Na lau tungelikuteremshia maandishi katika karatasi(kama wanavyotaka) na wakayagusa (wakakigusa hicho kitabu) kwa mikono yao, bila shaka wale waliokufuru wangelisema: "Haya si chochote ila ni uchawi dhahiri." (6:7)
Historia (tarekh) inatuambia kuwa Mtume (s.a.w) ametumia karatasi kuandikia:
- Katiba yake iliyoandikwa mara tu baada ya kuingia Madina.
- Sulhu ya Hudaybia.
- Barua alizowatumia wafalme mbali mbali.
Je kusema kuwa Mtume(s.a.w) ametumia mawe na mifupa kuandikia Qur-an haionekani kuwa Mtume(s.a.w) amethamini zaidi maandishi mengine kuliko maneno ya Mwenyezi Mungu? Haiwezekani iwe hivyo bali ni visa vilivyobuniwa kuudhoofisha ukweli na Hadhi ya Qur-an.
Huenda pia ikadhaniwa kuwa, kwa sababu ya ugumu wa kupatikana karatasi ndiyo Mtume akawa anatumia mawe na mifupa. Dhana hii vile vile haina msingi kwani tunaambiwa kuwa masahaba mbali mbali walikuwa na vitabu vyao wakiandika mafunzo ya Uislamu. Hebu turejee Hadith zifuatazo:
Abu Hurayrah(ra) amesema: "Hapana hata mmoja katika masahaba wa Mtume ambaye amesimulia Hadith nyingi zaidi kuliko mimi ukimtoa (isipokuwa) 'Abdullah bin 'Amr ambaye alikuwa anaandika wakati mimi sikufanya hivyo." (Bukhari).
"Abu Hudhaifa(ra) amesema: Nilimuuliza Ali je muna kitabu chochote kile (zaidi ya Qur-an)? Ali alisema hapana isipokuwa kitabu cha Mwenyezi Mungu au uwezo wa ufahamu ambao amepewa Muislamu au hiki kilichomo katika upande huu wa karatasi (sahifa)…" (Bukhari).
Hivyo suala la ugumu wa karatasi halipo kwani hapana hata sahaba mmoja ambaye angekataa kutoa karatasi ya kuandikia Qur-an kama angetakiwa kufanya hivyo.
(vii)Suala la karatasi kuwepo tena kwa wingi linaonekana hata kwa Mayahudi na Wakristo ambao walikuwa na vitabu vyao vinavyobebeka siyo vya mifupa wala mawe.Hebu turejee Hadith ifuatayo: 'Abdallah bin 'Umar amesema:
"Mayahudi walikwenda kwa Mtume na kueleza kwamba mwanamke na mwanamume mmoja wao amezini Mtume akawauliza: 'Je katika Tawrat hakuna sheria ya kupiga mawe mpaka kufa?" Wakajibu: 'Tunawafedhehesha kisha tunawapiga bakora! 'Abdullah bin Salaam akasema: "Waongo kwa hakika ndani ya Tawrat imo habari ya kupiga mawe hadi kifo. "Wakalete Tawrat isomwe na mmoja wao akaifunika ile aya ya kupiga mawe kwa mkono wake na badala yake akasoma aya ya juu na chini. 'Abdallah bin Salaam akamwambia: "Ondoa mkono wako." Akaondoa na mara ikaonekana aya ya kupiga mawe. Akasema "Muhammad amesema kweli kweli kwani imo aya ya kupiga mawe…" (Bukhari na Muslim).
Huo ni ushahidi wa vitabu vilivyokuwepo. Na hata katika Qur-an tunaambiwa kuwa imeandikwa katika karatasi (52:2-3) jambo ambalo limejitokeza wakati aliposilimu Umar bin Khatab. Tunaambiwa kuwa kilichomsilimisha ni suhufa - ukurasa wa karatasi ya wakati ule ambao ulikuwa umeandikwa Surat Taha.
(c)Hoja za Kiakili (mantiki - logic)
Kimantiki vile vile Hadith ya Zaid haina nguvu kwa sababu:
(i)Katika masahaba ambao Mtume (s.a.w) aliwachagua kama waandishi wake wa wahyi hatumkuti mtu anayeitwa Abu Khuzaymal Ansari. Ukiwatoa makhalifa wanne na baadhi ya Muhajiriin tunawapata Ansari wachache sana ambao walishughulikia uandishi wa wahyi wakati wa Mtume(s.a.w). Jambo la kushangaza na kutia wasi wasi katika simulizi hii ni kuwa wale waandishi wote wa Mtume (s.a.w) walioteuliwa maalum kuandika wahyi hawakuwa na aya hizo isipokuwa sahaba huyu ambaye hakuwemo! Hivyo ni kweli, Mtume(s.a.w) ambaye kila unapoteremka wahyi hata usiku huwafuata waandishi wake ili wauandike leo hii waandishi hao ambao walikuwa majirani zake wa pua na mdomo wasiwe na aya hizo mbili bali awe nazo mtu wa mbali ambaye ni mmoja tu? Haiwezekani kabisa.
Tatizo jingine la simulizi hii ni kupingana na Hadithi nyingine au tukio lingine ambalo vile vile ni lenye kutia wasi wasi. Katika simulizi nyingine aliyoitoa Anas bin Malik na kupokelewa na Imam Bukhari tunaambiwa kuwa Khalifa 'Uthman baada ya kupata habari kuwa Qur-an inatamkwa kinyume kabisa alivyoitamka Mtume(s.a.w) aliamrisha kuandikwa nakala sanifu kwa ajili ya marudio ya watu wote. Kazi hii ya kuinakili Qur-an kutoka Msahafu unaodaiwa wa Hafsa ambao uliandikwa wakati wa Abu Bakr walikabid hiwa:
- Zaid bin Thabit. (r.a)
- Abdallah bin Zubery.(r.a)
- Sa'id bin Al'As.(r.a)
- Abdulrahman bin Harith bin Hisham.(r.a)
Katika kunakili huku Msahafu wa Hafsa kulionekana kuwa aya moja ilikosekana na mara hii ilikuwa ni: "Wapo watu miongoni mwa walioamini waliotimiza ahadi walioahidiana na Mwenyezi Mungu …" (33:23)
Aidha aya hii ilipatikana kwa Khuzayma bin Thabit al-Ansari! Hivyo ni kweli kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi na mbili kitabu cha Allah(s.w) kiwe kimepungua aya na watu wote wasijue pamoja na kuwepo mahafidhi chungu nzima? Msahafu huo unaoambiwa kuwa umeandikwa wakati wa Abu Bakr(r.a) ulikuwa ndio rejea ya watu wote, je kama mtu atasema kuwa Qur-an haikuwa imetimia kwa kipindi kile atakuwa na makosa? Watu wote walirejea msahafu huo pungufu, je ahadi ya Allah(s.w) ya kuihifadhi Qur-an iko wapi wakati Msahafu pekee uliokuwapo ulikuwa na kasoro ya aya moja? Hivyo, ni visa vya kubuni tu.
(ii)Inavyofahamika ni kuwa Zaid bin Thabit (r.a)ni mtu wa Madina (Ansar) sasa vipi ilikuwa hali ya Makka ambapo yeye alikuwa hayupo? Bila shaka palikuwa pana waandishi wengine ambao walimtangulia kwenye kazi hiyo na akashirikiana nao walipokuwa Madina. Mtume(s.a.w) alikuwa na kikundi chake cha waandishi wa wahyi na maandishi mengine kama vile mikataba. Je, ni jambo lenye kuingia akilini kuwa watu wote hao ambao inasadikiwa kufika 42 waikose aya hiyo na badala yake awe nayo mtu wa mbali? Je waandishi hao walikuwa na kazi gani ikiwa kuna aya ambazo hawakuziandika? Desturi ya masahaba ilikuwa ni ya kusubiri wahyi mpya kama vile watu wanavyosubiri taarifa ya habari siyo wajue tu bali watekeleze. Masahaba walikuwa wanapangiana zamu za kwenda kukaa kwa Mtume ili kujua jambo lolote jipya linalowahusu wao binafsi au jamii. Simulizi hii inatuambia pamoja na kusikilizwa mahafidhi bado aya hii ilipatikana kwa mtu mmoja! Je tuseme kwa kipindi chote hicho tangu alipofariki Mtume hadi kuanza kuandikwa wakati wa 'Uthman watu walihifadhi msahafu wenye upungufu? Haiwezekani bali simulizi ni ya uzushi.
(iii)Simulizi hii vile vile inatupa wasi wasi zaidi kwani haiwezi kujibu maswali ya fuatayo: Kwa nini Zaid(r.a) aisake mifupa na mawe ambayo yametumika kuandikia Qur-an na siyo kwenda kuyachukua mahali fulani tu? Je ni sahaba gani aliyekuwa dhamana ya kulinda mifupa na mawe hayo? Wakati Mtume alipohama Makka, mawe yale na mifupa ilichukuliwa? makozi ya mitende katika kipindi cha miaka 13 hayaozi tu?!, Usafiri gani walitumia kubebea mawe,mifupa na makozi yaliyokuwa na aya za Qur-an? Kwa kusaidia kujibu maswali hayo ni kwamba lazima mawe au mifupa hiyo ingelikuwa imekusanywa katika mojawapo ya nyumba za Waislamu hivyo pasingekuwa na haja ya kusakwa. Ilivyokuwa hizo ni aya za Allah (sw), Mtume(s.a.w) asingethubutu kuwaachia makafiri wazichezee, hivyo lazima ingesimuliwa ni vipi alizihamisha, lakini hatuna habari kama hiyo. Ukizingatia idadi ya aya za Qur-an kuwa ni 6,236 ni lazima mawe na mifupa hiyo mikubwa ingekuwa imeshindiliwa katika magunia jambo ambalo siyo kweli. Hivyo maswali hayo na majibu yanatuthibitishia kuwa hiki ni kisa cha kubuni ambacho hakiingii akilini.
(iv)Al-Bukhariy ni binaadam, pamoja na udhibitifu mkubwa aliokuwa nao Al-Bukhary katika ukusanyaji, uchambuzi na uandishi wa Hadith bado yeye ni binaadam na anayomadhaifu, hakuwa akipokea wahy wowote hivyo ubinaadamu wake yatosha yeye kukosea kunakili jambo kama hili katika sahihi yake, kwani pia zipo Hadith nyingi tu dhaifu zinazopatikana katika sahihi yake. Pia inamkinika maadui wa Uislamu wakapachika Hadith hii katika kitabu chake. Tukikumbuka kuwa vitabu vya Hadith havina hivadhi ya Allah kama ilivyo Qur’an(15:9)
Je! umeipenda hii post?
Ndio Hapana Save post
Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Topic: Quran Main: Post File: Download PDF Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 1107
Sponsored links
👉1 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)
👉2 Simulizi za Hadithi Audio
👉3 Kitabu cha Afya
👉4 Madrasa kiganjani
👉5 Kitau cha Fiqh
👉6 kitabu cha Simulizi
Jinsi Mtume Muhammad (s.a.w) alivyoipokea Qur-an:
(iii)Jinsi Mtume Muhammad (s. Soma Zaidi...
Sababu za kushuka surat al Quraysh
Qurayh ni jina la kabila la Mtume Muhammad S.A.W. Sura hii itakwenda kukujulisha neema ambazo Maquraysh wamepewa na hawataoewa wao wowote baada ya wao. Soma Zaidi...
HUKUMU ZA TAFKHIIM NA TARQIQ
Jifunze namna ya kusoma quran, pata mafunzo ya tajwid hapa Soma Zaidi...
quran na sayansi
YALIYOMONENO LA AWALI1. Soma Zaidi...
Sababu za kushuka surat at Takaathur
Kuwa na tamaa huhitaji vitu vya watu si jambo jema. Ila kama tamaa hii itakuhamasisha na wewe kutafuta kitu hicho, kwa uwezo ambao Allah amekupa bila ha kuvuka mipaka yake, hili sio tatizo. Sura hii itakufundisha mengi Soma Zaidi...
Muhammad hakufundishwa quran na padri Bahira
Soma Zaidi...
IDGHAAM KATIKA LAAM
Jifunze namna ya kusoma quran, pata mafunzo ya tajwid hapa Soma Zaidi...
Lugha ya kiarabu Lugha ya quran: kwa nini quran katika lugha ya kiarabu
Soma Zaidi...
Madai ya makafiri dhidi ya quran na hoja zao
Soma Zaidi...
quran na tajwid
TAJWID Utangulizi wa elimu ya Tajwid YALIYOMO SURA YA 01 . Soma Zaidi...
Kushuka na kuhifadhiwa kwa quran, hatua kwa hatua: mafunzo ya baadhi ya sura za quran
QUR’AN 5. Soma Zaidi...
Maana ya qalqala na aina zake katika usomaji wa Quran tajwid
Qalqala imegawanyika katika makundi mawili ambayo ni Qalqalatul qubra yaani qalqala kubwa na qalqalat as shughura yaani qalqala ndogo. Soma Zaidi...