4. Sera ya uchumi katika UislamuKwanza, katika Uislamu utekelezaji wa mambo yote hutegemea zaidi ucha-Mungu wa mtu binafsi na kuogopa kwake kusimamishwa mbele ya Allah na kuhisabiwa, kuliko usimamizi wa vyombo vya dola kama sheria, mahakama, na askari polisi. Hii ni kwa sababu hisabu siku ya kiyama itakuwa kwa kila mtu binafsi. Hapana shaka vyombo vya dola vipo katika Uislamu na vinafanya kazi lakini msisitizo wa utekelezaji wa mambo yote upo katika uadilifu na taqwa kuliko katika kuogopa polisi na ma ha k ama.Pili, uhuru wa watu binafsi kufanya wanalolitaka ndio sera inayofuatwa katika Uislamu. Yaani katika masuala ya uchumi Uislamu umempa uhuru kila mtu afanye lile analoliona linafaa. Na serikali ya Kiislamu haitaingilia uhuru wake huo isipokuwa tu pale ambapo haki haitatendeka iwapo uhuru huo hautaingiliwa. Mtume (s.a.w) amelielezea kwa ufasaha sana suala hili pale alipoyapigia mfano maisha ya watu katika jam ii na wasafiri waliomo chomboni baharini:“Hebu tuchukue mfano wa meli inayosafiri baharini ikiwa imejaza abiria ambao wamekaa katika sehemu zote za chini na juu. Sasa iwapo abiria mmoja aliyekaa katika sakafu hiyo ataamua kujipatia maji kirahisi kwa kutoboa pale alipoketi na iwapo abiria wengine watamzuia kufanya hivyo (na ni wajibu wa abiria wote walio juu na chini kumzuia) watamnusuru yeye na wao wenyewe na kufa maji. Iwapo watamwacha atoboe basi watazama wote waliochini na juu ya meli.” (Bukhari).Mfano huu unatuonesha kuwa japo Uislamu unampa kila mtu uhuru wa kufanya alitakalo lakini uhuru huo una mipaka. Iwapo mtu atafanya jambo lisilo la haki basi serikali ya Kiislamu lazima iingilie kati kwa maslahi ya jamii nzima.Tatu, wajibu mkubwa wa serikali ya Kiislamu ni kusimamia haki na kuzuia dhulma katika maisha ya jamii.