Historia ya Firaun, Qarun na Hamana


Karun na Hamana waliishi zama za Mtume Musa(a.s) na walikuwa viongozi waandamizi wa Firaun. Walikuwa ni watu maarufu katika jamii yao na walikuwa mstari wa mbele katika kumpinga Mtume Musa(a.s).“Na kwa yakini tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu na hoja (dalili) zilizo dhahiri. (Tulimpeleka) kwa Firauni na Hamana na Karun, wakasema: “(Huyu ni) Mchawi, muongo mkubwa” (40:23-24).

Katika aya nyingine Mwenyezi Mungu anatufahamisha kuwa aliwaangamiza Firaun, Hamana na Qarun kwa sababu waliyakanusha mafundisho ya Mtume Musa na wakatakabari:Na (vile vile) Qarun na Firauni na Hamana (waliangamizwa); na hakika aliwajia Musa kwa miujiza waziwazi, lakini walijivuna katika ardhi, lakini hawakuweza kumshinda Mwenyezi Mungu. Basi kila mmoja tulimtesa kwa sababu ya dhambi zake. Miongoni mwao wako tuliowapelekea kimbunga cha changarawe; na miongoni mwao wako waliotolewa roho kwa ukulele mkubwa, na miongoni mwao wako tuliowadidimiza ardhini na miongoni mwao wako tuliowagharikisha na hakuwa Mwenyezi Mungu Mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu (wenyewe) nafsi zao” (29:39-40).Qarun alijaaliwa kuwa na mali nyingi sana. Lakini alilisahau lengo la maisha akatakabari. Watu walio karibu naye walimnasihi lakini hakuzinduka. Alijivuna na kuona kuwa utajiri aliokuwa nao kaupata kwa juhudi na elimu yake. Alisahau kuwa hiyo ni neema kutoka kwa Allah(s.w).
Hakika Qarun alikuwa katika watu wa Musa, lakini aliwafanyia dhulma. Na tulimpa hazina ambazo funguo zake zinawatopeza watu wenye nguvu (kuzichukua). Walimwambia watu wake: “Usijione (usijigambe), hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanaojigamba” (28:76).
Akasema: “Hakika nimepewa haya kwa sababu ya ilimu niliyo nayo”. Je, hakujua ya kwamba Mwenyezi Mungu amewaangamiza kabla yake watu waliokuwa wenye nguvu zaidi kuliko yeye na wenye mkusanyo mwingi zaidi (kuliko wake yeye)?” (28:78).

Kwa kutakabari kwake huko, Qarun aliangamizwa kwa kudidimizwa ardhini yeye na nyumba yake.
“Basi tukamdidimiza yeye (Qarun) na nyumba yake ardhini, wala hapakuwa na kundi lolote la kumsaidia kinyume na Mwenyezi Mungu, wala hakuwa miongoni mwa walioweza kujisaidia” (28:81).Mafunzo:


Yapo mafunzo mengi kutokana na maisha ya Qarun. Funzo la kwanza ni kuwa kama utajiri hautatumiwa vyema, waweza kuzaa maovu yafuatayo:


(i) Humfanya mwenye mali kujisahau na kutakabari.

(ii) Humfanya mwenye mali kuwasahau wenye shida na wahitaji. Hali hii huzaa jamii ya wenye mali ambao hula na kusaza wakati wengine hubaki ombaomba wasio na msaada wowote.


Funzo la pili linalolandana na maisha ya Qaruni ni kuwa mali, cheo na mamlaka ya mtu hayawezi kumsaidia chochote Mwenyezi Mungu anapopitisha hukumu yake. Qaruni alitamba kwa mali yake, lakini hukumu ya Allah(s.w) ilipofika alididimizwa yeye na mali yake ardhini.