Sahihi Muslim
Sahihi Muslim ni kitabu cha Hadith sahihi kinachofuatia sahihi al-Bukhari kilichokusanywa na Abul Husain Muslim bin al-Hajjaj anayejulikana kwa jina la Imamu Muslim. Imamu Muslim alizaliwa katika mji wa Misabur, 202 A.H./817 A.D. na alifariki 261 A.H./875
A.D. katika mji huo huo. Kama alivyokuwa Imamu Bukhar, naye alisafiri sana huku na huko katika nchi za Uarabuni, Misr, Syria (Sham) na Iraq ambapo alipata fursa ya kusoma kwa wanazuoni wengi waliokuwa mashuhuri. Miongoni mwa wanazuoni mashuhuri ambao alisoma kwao ni Ahmad bin Hambal, mwanafunzi wa Imam Shafii.
Imam Muslim alikusanya Hadith 300,000 na katika hizo ni Hadith 9,200 tu alizoziandika katika kitabu chake kinachojulikana kwa jina mashuhuri "Sahihi Muslim". Alimpenda sana Imam Bukhari na kazi yake. Kama imam Bukhari, Muslim naye amekifuma kitabu chake kulingana na mada za fiq-h. Naye alichukua uangalifu mkubwa mno katika kuchagua Hadith zilizo sahihi kwa kiasi ambacho Hadith zake nyingi zimeku baliana na zile za Al-Bukhari. Alikuwa mwangalifu sana katika kuchambua sehemu ya upokezi (isnad) kwa kiasi ambacho Hadith moja ilikuwa na isnad nyingi (misururu mingi ya wapokeaji). Kwa msomaji, Sahihi Muslim imekuwa katika mpango mzuri zaidi kuliko ule wa Sahihi al-Bukhari.