Mapambano ya waislamu dhidi ya Makabila ya kiarabu wakati wa Mtume

Makabila Mengine ya Kiarabu


Makabila mengi ya Kiarabu yaliyoleta chokochoko dhidi ya Dola ya Kiislamu ya Madinah, Mtume(s.a.w) aliyashughulikia mpaka yakasalimu amri na kulipa jizya. Ukiacha Maquraish makabila ya Kiarabu yaliyokuwa na nguvu sana na kujiamini ni makabila ya Khawaizin na Thaqif yaliyokuwa yakiishi katika maeneo ya mji wa Taif. Makabila haya yalipambana na jeshi la Mtume(s.a.w) katika vita vya Hunain vilivyopiganiwa mwaka wa 8 A.H. mwezi mmoja baada ya Fat-h-Makka. Waislamu walipata ushindi mkubwa sana katika vita hivi vilivyokuwa mwisho wa mapambano na makabila ya Kiarabu kwani yote yalikuja silimu na kuwa chini ya Dola ya Kiislamu. Vita vya Hunain vinaelezwa katika Qur-an:
Bila shaka Mwenyezi Mungu amekunusuruni katika mapigano mengi, na siku ya Hunayni (pia); ambapo wingi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni chochote, na ardhi ikawa dhiki juu yenu; ingawa ilikuwa yenye wasaa, kisha mkageuka mkarudi nyuma (mnakimbia). Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya walioamini. Na akateremsha majeshi (ya Malaika) ambayo hamkuyaona, na akawaadhibu wale waliokufuru; na hayo ndiyo malipo ya makafiri. (9:25-26)Aya hizi zinatupa picha halisi ya tukio la Hunain. Baadhi ya Waislamu mwanzo mwa vita walitelezeshwa na sheitani wakawa na fikra mbaya kuwa watashinda kutokana na ukubwa wa jeshi lao lililokuwa na askari 12,000 waliojizatiti vizuri, wakasahau kuwa ushindi wote unatoka kwa Allah(s.w). Mazingira ya vita yaliwadhihirishia kuwa wingi wao haukuwasaidia chochote. Mwanzoni wengi wa Waislamu walisambaratishwa na maadui na kumuacha Mtume(s.a.w) na waumini wachache kwenye uwanja wa mapambano wakiwa wamezungukwa na jeshi kubwa la maadui.Mtume(s.a.w) na waumini wachache aliokuwa nao walipigana kwa ujasiri wakiwa na yakini kuwa Allah(s.w) yuko pamoja nao. Waislamu waliokimbia walipokumbushwa kuwa wamemuacha Mtume wa Allah na waumini wachache kwenye uwanja wa vita, walitanabahi na kujitupa tena kwenye uwanja wa vita bila ya woga wowote kwa kutegemea radhi za Allah(s.w) peke yake. Walipofanya hivyo, Allah(s.w) aliwasaidia kwa kuwashushia jeshi la Malaika na wakapata ushindi mkubwa kwa namna ya ajabu kabisa.