image

Mapambano ya waislamu dhidi ya maadui wa kiyahudi madina

Mayahud Mwanzoni Mayahud walipoona kuwa Waislamu wanafunga siku ya Ashura pamoja nao na wanaelekea Qibla cha Baitul- Muqaddas pamoja nao hawakuonyesha chuki ya dhahiri dhidi ya Mtume(s.

Mapambano ya waislamu dhidi ya maadui wa kiyahudi madina

Mapambano ya waislamu dhidi ya maadui wa kiyahudi madina

Mayahud
Mwanzoni Mayahud walipoona kuwa Waislamu wanafunga siku ya Ashura pamoja nao na wanaelekea Qibla cha Baitul- Muqaddas pamoja nao hawakuonyesha chuki ya dhahiri dhidi ya Mtume(s.a.w) na Waislamu. Chuki yao dhidi ya Uislamu ilibainika pale Allah(s.w) alipowabadilishia Waislamu Qibla.



Kwa yakini tukiona unavyogeuzageuza uso wako mbinguni. Basi tutakugeuza kwenye Qibla ukipendacho. Basi geuza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu (Al-Kaaba); na po pote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu uliko (msikiti huo); na hakika wale waliopewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wao; na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda. (2:144)



Jambo hili la kubadilishwa Qibla liliwachoma sana Mayahud na lilijenga chuki na husuda dhidi ya Waislamu. Waliona kuwa kubadilishwa Qibla ni dalili ya Waislamu kufanywa umma bora na teule badala ya Mayahudi.Walihisi kuwa wamenyang’anywa cheo chao. Katika kudhihirisha chuki yao. Mayahud walifanya vitimbi vifuatavyo dhidi ya Mtume(s.a.w) na Waislamu:



Kwanza, Mayahudi walishirikiana na wanafiki kuwachochea Waislamu juu ya mabadiliko ya Qibla mpaka baadhi yao wakaanza kuwa na wasi wasi na kusema: “Inakuaje kwamba watu wakati mmoja wanaelekea huku (Baitul-Muqaddas) na wakati mwingine wanabadilisha tena wanaelekea huku (Baitul-Haraam)”. Allah(s.w) aliondosha wasi wasi huu kwa Waislamu kwa kushusha aya ifuatayo:




Karibuni wapumbavu miongoni mwa watu watasema:”Nini kilichowageuza kutoka kibla chao walichokuwa wakikielekea?” Sema: (uwambie) “Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; humwongoza amtakae katika njia iliyonyooka.” (2:142)



Pili, Mayahudi walitumia kifo cha Swahaba Amama, kutangaza kuwa Muhammad(s.a.w) si Mtume wa kweli, kwani angelikuwa Mtume wa kweli wa Allah(s.w) angelizuia kifo cha Amama.

Pia Mayahudi walipita wakitangaza kuwa Mtume(s.a.w) ni Mtume wa uongo pale Mtume(s.a.w) alipobadilisha Qibla.



Tatu, Mayahud waliifanyia Qur-an stihizai. Iliposhuka aya 245 ya Suratul-Baqarah:


Ni nani atakayemkatia Mwenyezi Mungu sehemu bora (ya mali yake kwa kuwapa masikini na kwa kutoa katika mambo mengine ya kheri) ili Mwenyezi Mungu amzidishie mzidisho mwingi, na Mwenyezi Mungu ndiye anayezuia na ndiye anayetoa, na Kwake (nyote) mtarejeshwa. (2:245)

Mayahudi walipita mitaani wakisema kuwa Allah(s.w) ni maskini anawaomba mali yao:




Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya wale (Mayahudi) waliosema:”Mwenyezi Mungu ni fakiri, na sisi ni matajiri.” Tumeyaandika haya waliyoyasema, na (tumeandika) kuua kwao Manabii bila ya haki, na tutawaambia (Siku ya Kiyama): “Onjeni adhabu ya kuungua.” (3:181)



Nne, walimjaribu Mtume(s.a.w) kwa kumuuliza maswali ya kubabaisha yasiyo na majibu ya dhahiri. Katika mkusanyiko wa Waislamu, Mayahudi walimuuliza Mtume:

“Kama Allah amewaumba binaadamu, yeye ameumbwa na nani? Mtume(s.a.w) alijibu swali hili kwa kuwasomea Suratul Ikhlas:





Sema: Yeye ni Mwenyezi Mungu Mmoja (tu). Mwenyezi Mungu (tu) ndiye anayestahiki kukusudiwa (na viumbe vyake vyote kwa kumuabudu na kumuomba na kumtegemea). Hakuzaa wala Hakuzaliwa. Wala hana anayefanana Naye hata mmoja. (112:1-4)



Siku moja kundi la wanachuoni (Rabb) wa Kiyahudi walimwendea Mtume(s.a.w) na kumwambia kuwa endapo atajibu kiasi cha kuwatosheleza maswali yao watasilimu. Miongoni kwa maswali waliyoyauliza ni haya yafuatayo:



Usingizi wako ukoje? Ni vitu gani Israil (Nabii Yaquub) alivyojiharamishia mwenyewe na kwa nini? Ni Malaika yupi anayekuletea wahay. Maswali yote Mtume(s.a.w)aliyajibu vilivyo, bali kuhusu swali la nne walisema:



“Lakini, Ewe Muhammad! Jibril ni adui yetu. Kila anapokuja anakuja na makamio ya adhabu na maangamizi dhidi yetu. Hatuna maelewano mazuri na yeye. Kama si huu uadui kati yetu na yeye bila shaka tungalikuja kwako na kukutii”. Mtume(s.a.w) aliwajibu kwa kuwasomea aya ifuatayo:



“Sema: Anayemfanyia ushinde Jibril (kwa kuwa ndiye aliyemletea utume Nabii Muhammad na asiwapelekee Mayahudi bure, hana kosa Jibril) hakika yeye ameteremsha Qur-an moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ............” (2:97)



Anayemfanyia ushinde Mwenyezi Mungu na Malaika wake na mitume wake na Jibril na Mikail (anatafuta kuangamia) kwani Mwenyezi Mungu atakuwa mshinde wa makafiri hao”. (2:98)



Tano,kuwanyanyasa na kuwadhallisha waislamu kutokana na hali duni ya uchumi waliyokuwanayo. Kila mwanzo mgumu. Waislamu walipoanzisha Dola ya Kiislamu ya Madinah, hali yao haikuwa nzuri kutokana na sababu mbali mbali za msingi. Muhajirina walikwenda Madinah mikono mitupu na mali yao yote wakaibakisha mikononi mwa makafiri wa Makka.





Answar waliwapokea ndugu zao kwa mapenzi na udugu na kuwasitiri kwa mali zao kwa kadiri ya uwezo wao. Pamoja na hivyo makafiri wa Makkah waliwafuata Waislamu wa Madinah na kuhujumu uchumi wao kwa kuiba mifugo, kuchoma mashamba n.k. Mayahudi walitumia udhaifu huu wa uchumi wa Dola ya Kiislam katika kuwanyanyasa na kuwavunja moyo Waislamu. Walikuwa wakiwakopesha Waislamu na kuwadai hadharani popote pale watakapowakuta na wakati wowote hata kabla ya muda walioahidiana kufika. Kwa mfano Bilal alikopeshwa fedha na Mayahudi. Siku moja Bilal(r.a) alipokuwa anataka kutoa adhana kwa ajili ya swala, huyu myahudi alimuita kwa sauti na kumwambia kuwa kama hatalipa deni lile atachukuliwa tena utumwani. Bilal(r.a) alisononeshwa sana na tukio lile na alikwenda kumhadithia Mtume(s.a.w) ambaye alifanya mpango wa kulipwa kwa deni lile.



Kuna matukio mengi ya namna hii waliyofanyiwa Waislamu pamoja na Mtume mwenyewe. Mwishowe, Mayahudi wakishirikiana na wanafiki pamoja na matajiri wengine wa Madinah wasiokuwa Waislamu waliweka mikakati wa kutowakopesha Waislamu au kuwapa msaada wowote wa kifedha, ili wafilisike kabisa na waamuea kuacha Uislamu. Qur-an inabainisha njama hizi kama ifuatavyo:




“Wao ndio wanaosema: “Msitoe mali kwa ajili ya wale walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ili waondokelee mbali (hapa nchini kwetu, Madinah) . Na hazina za mbingu na ardhi ni za Mwenyezi Mungu; lakini wanafiki hawafahamu” (63:7).



Sita, Walifanya jitihada za kuwachochea na kuwafarakanisha Waislamu. Mayahudi daima hawakulala katika jitihada zao za kutaka kuuhilikisha Uislamu na kuuvuruga udugu wa Waislamu. Walijaribu kuyachonganisha makabila mawili ya Aus na Khazraj, ambayo yaliishi kwa uadui baina yao kabla ya Uislamu kuingia Madinah. Siku moja walipokuwa katika mkutano wao, Mayahudi waliingia mle na kupenyeza habari zenye lengo la kukumbushia kisa cha vita vya Bua’ath, vita vikubwa vya kihistoria vilivyopiganwa kati ya Aus na Khazraj. Mayahudi hao waliendelea kuwachochea na kuwakumbusha uadui baina yao wa miaka iliyopita. Kutokana na uchochezi huu Answar walianza kukasirikiana wao kwa wao na panga zikawa nje nje. Habari za tukio hili zilimfikia Mtume(s.a.w) na akaja kuamua. Kutokana na tukio hili Allah(s.w) aliwaonya Waislamu kwa aya ifuatayo:




“Enyi mlioamini mkiwatii baadhi ya wale waliopewa kitabu (Mayahudi) watakurudisheni kuwa makarifi baada ya Uislamu wenu” (3: 100).



Saba, Walishirikiana na wanafiki katika njama za kutaka kumuua Mtume na kuuhilikisha Uislamu. Wanafiki wa Madinah, chini ya kiongozi wao ‘Abdullah bin Ubayy, walikuwa wakila njama dhidi ya Mtume na dhidi ya Waislamu wakishirikiana bega kwa bega na Banu Qainuqa’, kabila la kwanza la Mayahudi kufukuzwa Madinah, katika kumnyanyasa na kumuudhi Mtume na Uislamu.



Nane, Walivunja au kusaliti mikataba ya amani waliyowekeana na Mtume (s.a.w).

Mtume(s.a.w) alichukua hatua kali dhidi ya kila kitimbi walichokifanya Mayahudi dhidi ya Uislamu. Mtume(s.a.w) alitoa hukumu ya vifo kwa wale waliosimama kidete binafsi kuupiga vita Uislamu. Aliyafukuza Madinah makabila ya Banu Nadhir, Banu Qainuqa na Banu Quraizah baada ya kuvunja mikataba ya amani na kumpiga vita Mtume na Waislamu.



Mayahudi baada ya kuhamishwa Madinah walijikusanya Khaibar, kilomita 320 Kaskazini ya Madinah, Mayahud wa Khaibar wakishirikiana na rafiki zao, wanafiki na washirikina, waliazimia kuivamia Dola ya Kiislamu Madinah mwaka 7 A.H. Mtume(s.a.w) alipopata taarifa juu ya azma hiyo, aliwaendea huko huko Khaibar kwenye ngome yao na kuwacharaza vibaya na huo ukawa ndio mwisho wa chokochoko za Mayahudi katika kipindi cha Mtume(s.a.w).



                   



           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Kama unahitaji kuuliza maswali Bofya hapa

Mwandhishi Tarehe 2018-08-01     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 281


Download our Apps
👉1 Madrasa kiganjani     👉2 Kitabu cha Afya     👉3 kitabu cha Simulizi     👉4 Kitau cha Fiqh    

Post zifazofanana:-

Historia ya maimam Wanne wa fiqh
Soma Zaidi...

Nasaba ya mtume
Bara arabu zama za jahiliyyah (EDK form 2 dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Yusufu(a.s.) Akutana na Ndugu Zake
Njaa ilitokea na ikawa hapana sehemu nyingine yoyote yenye chakula ila Misri. Soma Zaidi...

Mtume amezaliwa mwaka gani?
Na tumemuusia mwanaadamu afanye wema kwa wazazi wake. Soma Zaidi...

Mafunzo ya sura zilizochaguliwa
Quran (EDK form 2: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Kuporomoka kwa Dola ya Kiislamu
Soma Zaidi...

Historia ya Vijana wa Pangoni
Makafiri wa Kiquraish walikuwa na tabia ya kumghasi Mtume(s. Soma Zaidi...

Kuanzishwa kwa Polisi na magereza kati uislamu wakati wa Makhalifa
Kuanzishwa kwa Polisi. Soma Zaidi...

Historia ya Dhulqarnain
Dhulqarnain sio jina la mtu bali cheo, maana yake ikiwa: “Mwenye Pembe Mbili”. Soma Zaidi...

Historia ya vita vya Muta
hii ni historia ya vita vya Muta. Katika makala hii utajifunza sababu ya vita hivi na yaliyojiri katika uwanja wa vita. Soma Zaidi...

Imam Tirmidh na Jami'u At-Tirmidh
Soma Zaidi...

Mbinu na njia walizotumia maadui wa uislamu dhidi ya waislamu na dola ya kiislamu madinah
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...