Maryam Apewa Habari ya Kumzaa Isa(a.s)


Baada ya maandalizi hayo ya kimalezi pamoja na hifadhi ya Allah(s.w) aliyopewa Maryam, Allah(s.w) akamtuma Malaika kumueleza Bi Maryam habari za kumzaa masihi, Isa(a.s) bila ya baba ila kwa amri ya Allah(s.w) ya “Kuwa ikawa”. Malaika akamwambia:


Ewe Maryam! Mwenyezi Mungu anakupa habari njema (za kumzaa mtoto kwa) neno litokalo kwake. Jina lake Masihi Isa bin Maryam, mwenye heshima katika dunia na akhera, na ni miongoni mwa waliotukuzwa.(3:45) Naye atazungumza na watu katika utoto na katika utu uzima wake, na ni katika watu wema (3:46)



Maryam Akasema:Mola wangu! Nitapataje Mtoto hali mtu yoyote hakunigusa? Akajibu: Ndivyo, vivyo hivyo; Mwenyezi Mungu huumba anavyopenda: anapohukumu jambo, huliambia ‘Kuwa’, likawa(3:47) Na Mwenyezi Mungu atamfunza kitabu na hekima, na kujua Taurati na
Injili. Na ni Mtume kwa wana wa Israili...................(3:48-49)



Kuzaliwa Nabii Isa(a.s)


Allah(s.w) anatueleza kuwa Nabii Isa(a.s) alizaliwa chini ya mtende, na wala hakuzaliwa kwenye zizi la ng’ombe lenye najisi kama wanavyodai katika Biblia.




Basi (Maryam)akachukua mimba yake, na akaondoka nayo mahali pa mbali. Kisha uchungu ukampeleka katika shina la mtende, akasema: “Laiti ningekufa kabla ya haya, na ningekuwa niliyesahaulika kabisa. (19:22-23)

Mara ikamfika sauti kutoka chini yake inamwambia: “Usihuzunike”. Hakika Mola wako amejaalia kijito cha maji chini yako”. Na litikise kwako shina la mtende, litakuangushia tende nzuri, zilizo mbivu. (19:24-25) Basi ule na unywe litue jicho lako.(19:26)