Qur-an na majina yakeQur-an ni wahy (ufunuo) kwa Mtume Muhammad (s.a.w) kutoka kwa Allah (s.w) kupitia kwa Malaika Jibril (a.s). Qur-an kama vitabu vingine vya Allah (s.w), imeshushwa kwa lengo la kuwaongoza wanaadamu katika kila kipengele cha maisha ya kila siku ya kibinafsi na kijamii. Lengo la Qur-an linabainishwa katika aya ifuatayo:


“Ni mwezi wa Ramadhani ambamo imeshushwa Qur-an ili iwe mwongozo kwa watu na hoja zilizo wazi na upambanuzi (baina ya haki na batili) " (2:185)
Katika kuendea lengo lake hili, Qur-an humuongoza mwanaadamu kukiendea kila kipengele cha maisha yake ya kibinafsi na kijamii na hutoa hoja zenye mashiko dhidi ya wapinzani wake.Katika kuonesha uwezo wake katika kumuongoza mwanaadamu katika kila kipengele cha maisha yake, Qur-an imeitwa (imesifiwa) kwa majina yafuatayo:1. Al-Qur-an
Maana yake ni "Chenye kuunganishwa pamoja" au "chenye kusomwa. "Yaani Qur-an ni kitabu kilichofumwa na herufi, silabi, maneno, aya na sura, kinachosomwa mara kwa mara. Kitabu hiki kimeitwa kwa jina hili la "Al-Qur-an" kwa sababu ni mkusanyiko wa mafunzo ya msingi ya maisha ambayo mtu hanabudi kuyarejea mara kwa mara. Qur-an ndio Mwongozo sahihi pekee wa maisha ya mwanadamu hivi sasa.2.Kalamullah:
Maneno ya Allah (s.w). Qur-an yote ni maneno ya Allah (s.w) yenye kutoa mwongozo kwa walimwengu wote kupitia kwa Mtume Muhammad (s.a.w) kwa njia ya Wahy kupitia kwa Malaika Jibril (a.s).3.Al-Mus-haf:
Mkusanyiko wa kurasa. Hili ni jina mashuhuri lililotumiwa na maswahaba wa Mtume (s.a.w) baada ya Qur-an kukamilika kushuka na kuwekwa katika sura ya kitabu kikubwa.4.Al-Kitaab:
Kitabu pekee (Unique book). Qur-an ni kitabu kikamilifu kisicho na upogo wala dosari yoyote wala hakina mfano wa kitabu chochote kimuundo, maudhui na uwasilishaji wa maudhui hayo. Qur-an yenyewe imeliweka hili wazi katika aya ifuatayo:


"Hiki ni kitabu pekee (Al-Kitaab) kisicho na shaka ndani yake na ni mwongozo kwa wamchao Mwenyezi Mungu." (2:2)5.Al-Furqaan:
Kipambanuzi cha Haki na Batili au ukweli na uwongo. Yaani Qur-an ndio kipimo cha Haki na Batili au Zuri na Baya au Jema na Ovu, Tawhiid na Shiriki, Uislamu na Ukafiri6.Adh-Dhikru:
Mawaidha au ukumbusho. Qur-an ni mawaidha yenye kumkumbusha kila mwenye kusoma na kuzingatia.


7.At-Tanziil:
Mshuko au wahy kutoka kwa aliye juu. Jina hili linasisitiza kuwa Qur-an ni kitabu cha Allah (s.w) kilichoshushwa kwa njia ya wahy kwa Mtume Muhammad(s.a.w) kupitia kwa malaika Jibril(a.s) ili awaongoze walimwengu kwacho.8.Al-Hukmu:
Kitabu pekee kinachostahiki kumuhukumu mwanaadamu. Hukumu yoyote kinyume na Hukumu ya Qur-an ni upinzani na uasi dhidi ya Allah (s.w) na ni dhulma dhidi ya wanaadamu kama inavyosisitiza Qur-an yenyewe:


“…Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri." (5:44)


“….Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu." (5:45)


“…. Na wasiohukumu kwa yale alioteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio waasi (mafasiki)." (5:47)
Neno “wasiohukumu” hapa limetumika kwa maana ya wanaoendesha maisha yao kinyume na yale aliyoteremsha Allah au wale wasioendesha maisha yao kwa mujibu wa Qur-an9.Al-Hikma:
Kitabu pekee chenye Hikima isiyo kikomo. Ni kitabu cha Allah (s.w) ambaye ndiye chimbuko (source) la Elimu na Hekima. Hekima ni jambo la sawa sawa lililofanywa kwa namna ya sawa sawa katika mazingira na wakati wasa wasa ili kufukia lengo tarajiwa. Qur’an ni Hikma na humuuongoza binaadamu aishi maisha ya Hikma.10.Ash-Shifau:
Ponyo au dawa pekee. Qur-an imeitwa kwa jina hili la "Ponyo pekee" kwa sababu Qur-an ndio dawa pekee ya kuponya maradhi ya "nafsi". Maradhi makubwa ya nafsi ni Ukafiri, Ushirikina, Unafiki na Uasi wa kila aina. Qur-an imejizatiti katika kuyaelezea magonjwa haya ili kila mtu mwenye akili timamu ayafahamu bayana na imeelekeza kwa ufasaha namna ya kuyatibu.11.Ar-Rahmat:
Rehema kwa watu. Vipawa vinavyomfanya binaadamu atofautiane na wanyama ni akili na elimu. Vipawa hivi vikitumika bila ya kufuata mwongozo kutoka kwa Allah (s.w) humpelekea binaadamu kufanya uharibifu katika ardhi kuliko mnyama yoyote yule. Binaadamu akitumia akili yake na elimu aliyotunukiwa kwa kufuata mwongozo wa Qur-an huwa juu na bora kuliko viumbe vyote.12.Al-Khayr:
Qur-an ni kheri pekee. Yaani Qur-an ndio chanzo cha kheri zote. Kheri hupatikana kwa kufuata Qur-an vilivyo.
13.Ar-Ruuhu:
Qur-an ni roho ya maisha. Yaani mtu asiyeishi kwa kufuata Qur-an ni kama maiti japo anaishi. Allah (s.w) anawaasa waumini wasiwakumbatie wapinzani wa Qur-an (makafiri) kwani wao ni kama maiti walio makaburini."Enyi mlioamini! Msifanye urafiki wa ndani na watu ambao Mwenyezi Mungu amewakasirikia na wamekata tamaa ya akhera kama walivyokwisha kata tamaa makafiri waliozikwa makaburini." (60:13)14. Al-Bayaana:
Qur-an ni kitabu pekee chenye maelezo ya wazi na kinachofafanua aya zake kwa uwazi kwa kutumia mifano iliyozoeleka katika mazingira ya watu kwa nyakati zote za historia. Hivyo, kila mwenye akili timamu anao uwezo wa kuielewa Qur-an na ikamuongoza.15.An-Nuur:
Qur-an ni nuru pekee. Qur-an ni mwanga unaomuonesha binaadamu njia sahihi ya maisha itakayomfikisha kwenye lengo la kuumbwa kwake. Kuishi bila ya kufuata Qur-an ni sawa na mtu anayetembea katika giza nene na matokeo ya kutembea kwenye giza nene yanafahamika kwa kila mwenye akili timamu. Qur-an inatukumbusha:


"Allah ni kiongozi wa walioamini. Huwatoa kwenye giza na kuwaingiza katika nuru (mwanga). Lakini waliokufuru viongozi wao ni Matwaghuti huwatoa katika nuru na kuwaingiza katika giza. Hao ndio watu wa motoni, humo watakaa milele." (2:257)16. Al-Burhan:
Hoja pekee iliyowazi. Qur-an ni kitabu kinachotoa hoja zilizo wazi kwa wasomaji wake. Kwa mfano Qur-an inatoa hoja zilizo wazi, kuwa lazima pawe na Muumba mmoja wa ulimwengu na vyote vilivyomo mwenye ujuzi na Hekima. Pia Qur-an pamoja na kutoa hoja maridhawa juu ya kumuamini Allah (s.w) na nguzo nyinginezo za imani , huonesha lengo la kumuabudu Allah (s.w) na umuhimu na hekima ya kufuata Qur-an na Sunnah kama mwongozo pekee wa njia sahihi ya maisha ya binaadamu.17. Al-Haqq:
Qur-an ni Haki. Qur-an ni haki kwa sababu ni maneno ya Allah (s.w) ambaye ni mjuzi wa kweli aliyeepukana na upungufu wa aina yeyote. Qur-an humuongoza binaadamu kwenye njia ya haki na huhukumu kwa waki.18 .Ahsan-ul-Hadith:
Maneno mazuri au maelezo mazuri kuliko yote kwa kuwa yanatoka kwa Allah (s.w), Mjuzi, mwenye hekima.
Kitabu hiki cha Allah (s.w), kilichosifiwa kwa majina haya, kina aya 6,236 zilizogawanywa katika sura 114 (Rejea jedwali 1). Pia kitabu cha Qur-an (Al-Mas-haf) kimegawanywa kwenye juzuu au mafungu (30) yaliyo sawa sawa.