7.Swalatudh-DhuhaaSwala ya Dhuhaa ni sunnah inayoswaliwa kati ya kipindi cha baada ya jua kupanda juu kiasi cha mita tatu hivi na kabla ya jua kufikia katikati. Lakini ni bora kuswali katikati ya kipindi hicho.Swala hii inaswaliwa kwa rakaa mbili mbili hadi zitimie nane, lakini kwa uchache unaweza kuswali rakaa mbili tu na pia unaweza kuswali zaidi ya rakaa nane.
Umuhimu wa swala ya Dhuhaa uko wazi. Kipindi kati ya swala ya Alfajir na Dhuhuri ni kirefu sana kiasi kwamba mja anaweza kusahau kumkumbuka na kumtaja Allah (s.w). Kama tunavyofahamu kumkumbuka Allah (s.w) kila wakati ndio ngao pekee ya kumzuia mja na mambo maovu na machafu. Hivyo Swalatudh-Dhuhaa kwa mtu mwenye wasaa katika kipindi hicho cha harakati nyingi za kutafuta riziki, itampa msukumo mpya wa kumkumbuka na kumuabudu Allah ipasavyo.Kutokana na hadith iliyopokelewa na Abu Daud na Ahmad, Buraidah (r.a) amesema kuwa Mtume (s.a.w) amesema: “Katika mwili wa binaadam kuna viungo (joints) 360 na binaadam ni lazima akitolee sadaka kila kiungo kimoja”. Watu wakauliza:“Nani awezaye kufanya hivyo ewe Mjumbe wa Allah?”Mtume akawajibu: “Mtu anaweza kufanya hivyo kwa kuondosha kitu chenye madhara njiani. Na iwapo hatoweza, kufanya hivyo basi rakaa mbili za Dhuhaa zitamtosheleza ”.