(b)Umbile la Mwanaadamu ni la kidini


Ukizingatia maana halisi ya dini, kuwa dini ni utaratibu wa maisha, utadhihirikiwa kuwa umbile la mwanaadamu ni la kidini.


Umbile la mwanaadamu kama maumbile mengine yaliyomzunguka hufuata mfumo maalum bila ya matashi au hiari ya mwanaadamu.


Kwa maana nyingine umbile la mwanaadamu limedhibitiwa na sheria za maumbile (natural Laws - biological, chemical, and physical laws).


Kwa mfano, ukichunguza hatua anazozipitia mwanaadamu katika tumbo la uzazi mpaka kuwa kiumbe kamili, ni utaratibu madhubuti ambao uko nje kabisa ya uwezo au matashi yake. Kuhusu kuumbwa kwa mwanaadamu Allah (s.w) anatukumbusha katika Qur-an:


Na kwa yakini tulimuumba mwanaadamu kwa udongo ulio safi, kisha tukamuumba kwa tone la manii lililow ekw a katika makao yaliyohifadhika.


Kisha tukalifanya tone hilo kuwa kitu chenye kuning’inia na tukakifanya hicho chenye kuning’inia kuwa pande la nyama, kisha tukalifanya pande hilo la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivisha nyama,kisha tukamfanya kiumbe kingine.


Basi Ametukuka Allah, Mbora w a w aumbaji… (23:12-1 4)
Si tu kuwa mwanaadamu hana mamlaka na kuzaliwa kwake bali pia hana mamlaka na kukua kwake, na kufa kwake kama tunavyokumbushwa tena katika Qur-an:


Enyi watu! Kama mumo katika shaka juu ya ufufuo, basi (tazameni namna tulivyokuumbeni)! Kwa hakika tulikuumbeni kwa udongo, kisha kwa manii, kisha kuwa kitu chenye kuning’inia, kisha kuwa kipande cha nyama kinachoumbika na kisichoumbika, ili tukubainishieni.


Nasi tunakikalisha tumboni tunachokitaka mpaka muda uliowekwa, kisha tunakutoeni kwa hali ya utoto, kisha tunakuleeni mpaka mfikie baleghe yenu. Na kuna wanaokufa (kabla ya kufikia umri huu).


Na katika nyinyi kuna wanaorudishwa katika umri dha lili, asijue chochote baada ya kule kujua kwake… (22:5).
Aya hizi zinatukumbusha na kututhibitishia kuwa kuumbwa kwa mwanaadam, kukua kwake na kufa kwake hufuata utaratibu madhubuti uliowekwa na Muumba wake bila ya hiari yake.
Vile vile ukizingatia ufanyaji kazi wa mwili wa mwanaadamu utagundua kuwa mwili wa mwanadamu ni mashine ya ajabu inayofanya kazi kwa kufuata utaratibu uliofungamana


na sheria madhubuti. Kwa mfano ukichunguza mwili wa mwanaadamu utakuta kuwa kuna mifumo mbali mbali kama vile mfumo wa usagaji chakula (digestion system), mfumo wa hewa (respiratory system), mfumo wa fahamu (nervous system), mfumo wa uzazi (reproduction system) na kadhalika.


Mifumo hii hufanya kazi yake kwa kufuata utaratibu na sheria madhubuti nje kabisa ya mkono wa mwanaadamu. Utaona kuwa mwili wa mwanaadamu hufanya kazi yake na kumwezesha mwanaadamu kuwa katika hali ya uzima alionao, kwa kufuata sheria madhubuti za maumbile zilizowekwa na Muumba wake kama tunavyofahamishwa katika Qur-an:


Basi uelekeze uso wako katika dini iliyo sawa sawa - ndilo umbile Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu (yaani dini hii ya Kiislamu inaafikiana bara bara na umbile la binaadamu). Hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe vya Mw enyezi Mungu. Hiyo ndiyo dini ya Haki, lakini watu wengi hawajui.


(30:30)
Katika aya hii tunajifunza kuwa mwili wa mwanaadamu hufuata dini ya Allah (s.w), yaani hufuata bara bara utaratibu au sharia madhubuti alizoweka Allah (s.w).


Lakini mwanaadamu mwenyewe katika kuendesha maisha yake ya kila siku ana uhuru kamili wa kufuata dini ya Allah (s.w) kwa kufuata kwa ukamilifu na kwa unyenyekevu sharia madhubuti alizoziweka Allah (s.w) katika kukiendea kila kipengele cha maisha (rejea juzuu ya 2 EKP uk. 33 au kufuata dini za watu kwa kufuata utaratibu wa maisha walioufuma watu katika kukiendea kila kipengele) kinyume na utaratibu wa Allah (s.w). Ni katika kuutumia uhuru huu, Allah (s.w) anamtanabahisha mwanaadamu.Je, wanataka dini isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu na hali kila kilichomo m binguni na ardhini kinam tii yeye, kipende kisipende? Na kwake watarejeshwa wote.


(3:83).
Aya hii inamtanabahisha mwanaadamu ili achukue uamuzi wa busara wa kufuata dini ya Allah (s.w), ambayo dini hiyo ndiyo inayofuatwa na mwili wake na maumbile mengine yote yaliyomzunguka.


Ni dhahiri kwamba atakapoamua kufuata dini nyingine yoyote isiyokuwa dini ya mwili wake, atakuwa ameamua kufuata utaratibu wa maisha unaopingana na umbile lake, na matokeo yake ni kukosa furaha na amani, katika maisha au kuishi maisha ya migongano, vurugu na huzuni.