Jina Al-Khidhri halikutajwa mahali popote katika Qur’an.
Jina Al-Khidhri halikutajwa mahali popote katika Qur’an. Ila Hadith sahihi za Mtume(s.a.w) na vitabu kadhaa ya historia vimemtaja mja wa Allah habari zake zilizobainishwa katika Qur’an (18:60-82) kuwa ndiye Al-Khidhri. Upo utata katika kubaini uhakika wa Al-Khidhri kwamba alikuwa binadamu au malaika. Sheikh Abdallah Saleh Farsy katika tafsiri yake ya Qur’an anasema Khidhri alikuwa binadamu na Mtume ila alikuwa amepewa neema ya elimu ya ghaibu. Yaani alipewa uwezo wa kujua mambo yasiyo wazi au yasiyofahamika kwa kutumia uwezo wa milango ya fahamu ya kawaida tuliyonayo.
Sheikh Abul Ala Mauduud, anasema ama Khidhri alikuwa malaika au kiumbe kingine ambacho utendaji wake hauongozwi na sheria hizi za kawaida zinazowaongoza wanaadamu. Hoja zake ni kuwa Khidhri alitoboa jahazi la mtu na akaua kijana. Japo maelezo yanatolewa kuwa alifanya hivyo kwa sababu ya elimu ya ghaibu aliyoletewa na Mwenyezi Mungu kwamba atoboe jahazi ili isije likaporwa kwa kuonekana zuri na pili amuue kijana kwa kuhofia atakuja kuwa mbaya baadae, lakini huo si ushahidi mbele ya sheria za Mwenyezi Mungu zinazowahukumu watu hapa duniani. Kwa hoja hiyo Mauduud anadhani Khidhri alikuwa malaika anayepokea amri na kufanya kama anavyoamrishwa na Allah au vinginevyo alikuwa kiumbe wa hali (nature) nyingine lakini si Mtume.
Kisa cha Al-Khidhri kinaanzia pale Mtume Musa (a.s) alipoweka azma ya kufanya safari hadi afikie makutano ya bahari mbili:
Na (kumbukeni) Musa alipomwambia kijana wake: “Nitaendelea tu kwenda mpaka nifike katika maungano ya bahari mbili; au niendelee karne na karne (mpaka nikutane na huyo ninayetaka kukutana naye)” (18:60).
“Basi walipofika wote wawili (mahali) zinapoungana (hizo bahari mbili) walimsahau samaki wao; naye akashika njia yake kwenda baharini; hali ya kuwa inafanya alama” (18:61).
Na walipofika mbele (Musa) alimwambia kijana wake: “Tutoe chakula chetu cha asubuhi, maana tumepata uchovu (mkubwa) katika safari yetu hii” (18:62).
Akasema: “Unaona! Pale tulipopumzika katika mlima basi hapo nimesahau (kukupa habari za) yule samaki. Na hakuna aliynisahaulisha isipokuwa shetani, nisikumbuke. Naye akashika njia yake baharini kwa namna ya ajabu” (18:63).
(Musa) akasema: “Hapo ndipo tulipokuwa tunapataka”. Basi wakarudi nyuma kwa kufuata njia yao (ile ile)” (18:64).
Basi wakamkuta mja katika waja wetu tuliyempa rehema kutoka kwetu na tuliyemuelimisha ilimu (nyingi) zinazotoka kwetu” (18:65).
Musa akamwambia: “Je! Nikufuate ili unifundishe katika ule uwongofu uliofundishwa?” (18:66).
Kwa mujibu wa mafundisho ya aya hizi, yaelekea Mtume Musa(a.s) alikuwa amepewa maelekezo na Allah(s.w) amtafute Khidhri akapate mwongozo na mafundisho kadhaa kupitia kwake. Makutano ya bahari mbili yaelekea ndipo Nabii Musa alipotakiwa akutane na Khidhri.
Mtume Musa(a.s) alikuwa na elimu ya kutosha kufanya kazi yake ya Utume kwa watu wake. Lakini hakuwa na elimu ya mambo yasiyo dhahiri. Kwa sababu hiyo Khidhri alikataa ombi la Mtume Musa la kutaka kuandamana naye. Hata hivyo baadaye alimkubalia ila kwa sharti kuwa asimuulize chochote katika yale atakayomuona anayafanya. Qur’an inabainisha hali hii katika aya zifuatazo:
Musa akamwambia: “Je! Nikufuate ili unifundishe katika ule uwongofu uliofundishwa?” akasema: “Hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami. (Utaona usiyoweza kustahimili kuyaona)”. “Na utawezaje kuvumilia yake usiyojua hakika yake?” Akasema: “Akipenda Mwenyezi Mungu, utaniona mvumilivu, wala sitaasi amri yako”. Akasema: “Basi kama
utanifuata, usiniulize kwa lolote (utakaloliona) mpaka mimi nianze kukwambia” (18:66-70).
Kwa makubaliano hayo Nabii Musa(a.s) akafuatana na Khidhri. Lakini kama Khdhri alivyoonesha wasiwasi, Musa hakuweza kustahimili matendo ya Khidhri. Awali Khidhri alitoboa jahazi waliyopanda. Musa hakustahimili ikabidi aulize kulikoni:
Hata walipopanda jahazi (yule Khidhri) aliitoboa. (Musa) akasema, “Je! Umeitoboa ili uwazamishe waliomo? Hakika umefanya jambo baya”. (18:71).
Khidhri ilibidi amkumbushe sharti la kuandamana naye. Musa akaomba msamaha wakaendelea. Mbele ya safari wakamkuta kijana mdogo Khidhri akamuua. Hili nalo Musa hakuweza kuhimili. Ikabidi amuulize Khidhri kwanini amemuua kijana asiye na hatia. Qur’an inatuambia:
Basi wote wawili wakaendelea kwenda. Hata wakamkuta kijana mdogo, na (yule Khidhri) akamuua. (Musa) akasema: “Ala! Umemuua mtu asiye na kosa wala hakumuua mtu? Bila shaka umefanya jambo baya kabisa” (18:74).
Nabii Musa(a.s) akakumbushwa tena makubaliano yao na akaomba msamaha.
Hatimaye walifika katika mji ambapo waliomba chakula lakini wakanyimwa. Wakakuta ukuta wa moja ya nyumba za mjini hapo
unakaribia kuanguka. Khidhri akausimamisha. Hapa Musa aliuliza tena. Hii ikiwa ni mara ya tatu Musa kukhalifu makubaliano yao; Khidhri hakumsamehe tena. Khidhri akamsimulia hikma na tafsiri ya yote aliyoyafanya kisha wakafarikiana. Qur’an inatuambia:
(Khidhri) akasema: “Huku ndiko kufarikiana baina ya mimi na wewe. Hivi sasa nitakwambia hakika ya yale ambayo hukuweza kuyavumilia”.“Ama ile jahazi, ilikuwa ya masikini wafanyao kazi baharini, na nilitaka kuiharibu kwani mbele yao kulikuwa na mfalme anayekamata kila jahazi (zuri) kwa jeuri”. “Na ama yule kijana, wazazi wake walikuwa Waislamu kamili, tukahofia kwamba asije akawapelekea (wazee wake hao) katika uasi na ukafiri. Basi tulitaka Mola wao Awabadilishie mtoto aliye bora kuliko yeye kwa kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma”. Na ama ukuta ulikuwa wa watoto wawili mayatima mjni pale, na chini yake kulikuwa na khazina yao, na baba yao alikuwa mwema, kwa hivyo, Mola wako alitaka wafikie baleghe yao na wajitolee khazina yao. Hiyo ni rehema inayotoka kwa Mola wako. Nami sikufanya haya kwa amri yangu. Hiyo ndiyo hakika ya yale ambayo hukuweza kuyavumilia” (18:78-82).
Kwanza, Ni hali ya kawaida kwa binaadamu kupitisha maamuzi yake kutokana na taafira za wazi na matukio bayana. Undani na hikma ya matukio hufahamika kwa wale tu waliotunukiwa hikma na fikra zilizotulizana. Katika maisha ya kila siku wafalme na watawala jeuri hupita katika ardhi wakifuja neema za Allah(s.w) huku wakiwadhalilisha wengine kwa jeuri. Watu wema na watiifu kwa Mola wao wakati mwingine waweza kuonekana dhalili wasio na mali wala cheo katika jamii. Wasiomuamini Allah(s.w) wakiwa na mali na vyeo hutakabari na kumkana Mwenyezi Mungu. Wakaona maguvu yao ndio kila kitu kwa hiyo wakazidisha fisadi katika ardhi.
Pili, Kwa waumini uangalifu wahitajika vile vile kwa mtu anayetenda mema lakini hali yake kiuchumi kila siku inazidi kushuka ilhali makafiri wanazidi kujilimbikizia mali; aweza kuvunjika moyo na kukata tamaa.
Tatu, Kisa hiki cha Musa(a.s) na Khidhri kinatubainishia kuwa zaidi ya elimu hii tunayoidhibiti kwa milango yetu ya fahamu ipo hikma ya mambo mengi ambayo hatuijui mpaka tufunuliwe na Allah(s.w) Mtu aweza kuwa na neema fulani kumbe neema hiyo ni yenye shari na yeye. Na kinyume chake.
Nne, Ili Mtume Musa(a.s) apate kufahamu japo sehemu ndogo ya elimu aliyonayo Khidhri ilibidi afunge safari ndefu. Elimu yote ni milki ya Allah na humkunjulia amtakaye kiasi atakacho. Lakini pia juhudi kubwa sana inahitajika katika kutafuta elimu.
Tano, Kisa hiki ni kiashiria cha upana wa elimu ya Allah(s.w). Mtume Musa(a.s) alikuwa Mtume na aliletewa Wahay akafahamu mambo mengi sana. Hata hivyo anakutana na Khidhri mwenye elimu ambayo kwa Musa(a.s) inaonekana kama miujiza.
Sita, Mambo matatu aliyoyafanya Khidhri akiwa na Mtume Musa(a.s) yanatupa mafundisho yafuatayo: Mosi; hasara au uharibifu wa jambo fulani yaweza kuwa ndio kheri yenyewe. Kutobolewa kwa jahazi kulilifanya lionekane si zuri. Hii ilifanya kinga kumzuia mfalme asilipore. Pili; ukatili wakati mwingine waweza kuwa ndio amani na msaada kwa watu. Maisha hutolewa muhanga kwa faida ya Ummah. Tatu; matendo ya wema si lazima yazae matunda hapo hapo. Wema unahimizwa hata pale ambapo hakuna dalili ya kulipwa wema.
Je! umeipenda hii post?
Ndio Hapana Save post
Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Topic: Sira Main: Post File: Download PDF Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 1622
Sponsored links
👉1 Simulizi za Hadithi Audio
👉2 kitabu cha Simulizi
👉3 Madrasa kiganjani
👉4 Kitau cha Fiqh
👉5 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)
👉6 Kitabu cha Afya
KAZI ALIZOFANYA MTUME MUHAMMAD (S.A.W) KABLA YA UTUME
KAZI ALIZOKUWA AKIFANYA MUHAMMAD (S. Soma Zaidi...
Musa(a.s) Kuwaongoza Bani Israil Hadi Palestina
Baada ya matukio haya ndipo Musa(a. Soma Zaidi...
Historia ya maimam Wanne wa fiqh
Soma Zaidi...
Kuporomoka kwa Dola ya Kiislamu
Soma Zaidi...
Si Yesu Aliyesulubiwa (yesu hakufa msalabani wala hakusulubiwa
Katika Qur,an tukufu, Mwenyezi Mungu aliye muweza na mjuzi wa mambo anathibitisha kuwa aliyesulubiwa si Nabii Isa(a. Soma Zaidi...
Muhutasari wa sifa za wanafiki
Kwa kuzingatia aya zote tulizozipitia juu ya wanafikitunaweza kutoa majumuisho ya sifa za wanafiki kama ifuatavyo:- (1)Hutenda kinyume cha imani wanaodai kuwa nayo. Soma Zaidi...
Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Lut (a.s)
(i) Tujitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu kuondoa maovu katika jamii kwa mikono yetu na ikiwa hatuwezi tuyakemee kama alivyofanya Nabii Lut(a. Soma Zaidi...
Hawa ndio waaasi wakwanza wa Dola ya kiislamu wakati wa makhalifa
Soma Zaidi...
Historia ya Dhana ya Kudhibiti Uzazi
Soma Zaidi...
Darsa za Sira historia ya Mtume (s.a.w) Jaribio la 05
Soma Zaidi...
Mapambano ya waislamu dhidi ya maadui wa kiyahudi madina
Mayahud Mwanzoni Mayahud walipoona kuwa Waislamu wanafunga siku ya Ashura pamoja nao na wanaelekea Qibla cha Baitul- Muqaddas pamoja nao hawakuonyesha chuki ya dhahiri dhidi ya Mtume(s. Soma Zaidi...
NAMNA MTUME(S.A.W) ALIVYOSIMAMISHA DOLA YA KIISLAMU MADINAH
Safari ya Mtume(s. Soma Zaidi...