Maana ya Uchumi
Mfumo wa maisha wa Kiislamu humuelekeza binaadamu kujenga na kudumisha uhusiano wake na Al-lah (s.w), uhusiano wake na binaadamu wenziwe na uhusiano wake na vinavyomzunguka katika ulimwengu huu. Aidha mfumo wa Kiislamu una lengo la kuelekeza namna ya kukiendea kila kipengele muhimu cha maisha ya binaadamu uchumi ukiwa miongoni.
Uchumi hujumuisha uzalishaji, usambazaji na utumiaji wa mali na huduma. Uislamu umelipa suala la uchumi nafasi muhimu kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:
“Wala msiwape wapumbavu mali zenu ambazo Allah amezijaalia kuwa msingi wa maisha yenu…” (4:5)
Uislamu umeweka utaratibu wa kiuchumi unaohakikisha kuwa haki inatendeka kwa wote ili kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kweli katika jamii. Katika sura hii tutaangalia uchumi katika Uislamu kwa kuzingatia maeneo yafuatayo:
1.Nadharia ya uchumi wa Kiislamu.
2.Umuhimu wa uchumi katika Uislamu.
3.Mazingatio muhimu katika uchumi wa Kiislamu.
4.Sera ya uchumi katika Uislamu.
5.Haki na Uhuru wa kuchuma katika Uislamu.
6.Mgawanyo wa mali katika Uislamu.
7.Umuhimu wa Benki katika Uchumi.
8.Tatizo la Riba.