Harun(a.s), Achaguliwa Kuwa Msaidizi Musa(a.s) na kumkabili (kumlingania) firauni

Nabii Musa(a.s)alimuomba Allah(s.w) amsaidie(amuwezeshe) kulimudu jukumu zito alilompa na pia alimuomba amfanye Harun(a.s) awe msaidizi wake. Harun alikuwa ndugu yake Musa(a.s)Akasema: Ewe Mola wangu! Nipanulie kifua changu(nipe subira). Na unifanyie wepesi katika kazi yangu. Na ufungue fundo lililo katika ulimi wangu. Wapate kufahamu maneno yangu. Na unifanyie waziri katika jamaa zangu. Ndugu yangu Harun. Nitie nguvu kwa huyu. Na umshirikishe katika kazi yangu hii. Ili tukutukuze sana. Na tukutaje kwa wingi. Hakika Wewe unatuona (20:25-35)Allah(s.w) alilikubali ombi la Nabii Musa (a.s), akamfanya Harun(a.s) kuwa Nabii pamoja naye. Allah(s.w) akasema kumwambia Musa: Hakika umekubaliwa maombi yako, Ewe Musa (20:36)


Musa na Harun(a.s) Kumkabili Firaun

Jukumu kubwa la kwanza walilokabidhiwa Musa(a.s) na Harun(a.s) lilikuwa kumwambia Firauni amwamini Allah(s.w) na awache kukiuka haki za binadamu kwa kuwapa Waisraili uhuru wao. Basi wakamkabili Firaun wakamwambia:
...................Kwa hakika sisi ni Mitume wa Mola wako. Basi waachie wana wa Israili watoke pamoja nasi, wala usiwaadhibu. Hakika tumekuletea ishara zitokazo kwa Mola wako. Na amani itakuwa kwa wale wanaofuata uongofu (20:47)Firauni kwa jinsi alivyokuwa amezama katika siasa za kidhalimu na unyonyaji hakupenda kabisa kuona Wana Israil wanarejeshewa haki zao za kibinadamu za kuwa huru. Akasema Firauni kwa kibri na jeuri kubwa kuwa: ............Enyi wakuu! Simjui kwa ajili yenu, mungu asiyekuwa mimi............(28:38)

Akasema: Mimi ndiye mola wenu mkuu. (79:24)Nabii Musa(a.s.) alijitahidi kumuelimisha Firauni na watu wake juu ya Mungu mmoja anayekataza dhulma, ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu. Lakini Firauni kwasababu ya kupenda sana dhulma, akazusha uongo akiwatangazia watu kwa kuwaambia:

Bila shaka Mtume wenu aliyetumwa kwenu ni mwendawazimu(26:27)Pamoja na kujibiwa kwa dharau na kukashifiwa, Musa aliendelea kufafanua zaidi juu ya Mwenyezi Mungu anayemiliki ulimwengu mzima.

.........(Allah ndiye) Mola wa Mashariki na Magharibi na vilivyomo baina yake ikiwa (mna akili) mfahamu (26:28)Aliposhindwa kujibu hoja hiyo, Firauni akapandwa na hasira na kuanza kumtishia Musa(a.s):

Firauni akasema: Kama ukishikilia (kuwa kuna) Mungu mwingine badala yangu, kwa hakika nitakufanya miongoni mwa wenye kufungwa gerezani(26:29)Lakini Musa(a.s) hakutishika kabisa kwa hizo kauli za Firauni. Badala yake akataka kumdhihirishia kuwa Allah(s.w) ana nguvu na uweza wa kufanya mambo makubwa ya kutisha zaidi kuliko hayo magereza yake.
Basi(Musa) akatupa fimbo yake, mara ikawa nyoka aliye dhahiri. Na akatoa mkono wake, na mara ukawa mweupe (kweli kweli) kwa watazamao(26:32-33)

Hapo Firaun akatishika na alidhani kuwa ile miujiza aliyokuja nayo Nabii Musa(a.s) ni sawa na mazingaombwe au viinimacho wanavyofanya wachawi.Akasema, kuwaambia wakuu waliomzunguka: Hakika huyu ni mchawi ajuae sana. Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake; basi mnasemaje? (26:34-35)