Kuibuka kwa Khawarij


Baada ya makubaliano, Ali aliwatangazia makubaliano haya wapiganaji wake. Lakini ndugu wawili wa kabila la Azza walisimama kupinga suluhu kwa hoja kuwa wanazo hukumu za Mwenyezi Mungu katika Qur’an hivyo hawahitaji wasuluhishi. Watu wengi waliunga mkono rai hii na kufikia 12,000. Wao hawakurudi Kufa, walipiga kambi mahali paitwapo Harorah. Walimteua Sheikh bin Rabi kuwa kamanda wao na Abdullah bin Kawa kuwa Imam wa kuongoza Swala. Walitangaza imani yao ambayo ilikuwa:


“Ba’iyah iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu, yeye tu ndiye wa kutiiwa. Kuhubiri mema na kukataza mabaya. Hakuna Khalifa au Amir. wote Ali na Muawiya wana makosa, Muawiyah anamakosa kwa kutomtii Ali, na Ali anamakosa kwa kukubaliana na Muawiyah juu ya suluhu. tutaposhika mamlaka tutaanzisha mfumo wa maisha ya jamii uliojengwa juu ya Qur’an”.


Ali aliporudi Kufa alimtuma Abdullah bin Abbas, Harorah kuzungumza na Khawarij. Aliweza kuwavuta na wakakubaliana na Khalifa baada ya mazungumzo ya muda mrefu. Hata hivyo kukubali huku kulikuwa kwa muda tu.