Mbinu za Da’wah Alizotumia Nuhu(a.s)


Katika kufikisha ujumbe huu kwa watu wake Nuhu(a.s), alijitahidi kutumia mbinu mbali mbali ili wapate kumuelewa vizuri na kufuata ipasavyo ujumbe aliowaletea. Miongoni mwa mbinu alizozitumia ni hizi zifuatazo:Kwanza alitoa hoja kwa watu wake za kuonesha haja na umuhimu wa kumuamini Allah(s.w) na kumuabudu ipasavyo. Aliwatanabahisha:


Mumekuwaje hamuweki hishima ya Mwenyezi Mungu. Na hali yeye amekuumbeni namna baada ya namna? Je hamuoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyoziumba mbingu saba tabaka- tabaka(moja juu ya moja). Na Akakaufanya mwezi ndani yake uwe nuru na Akalifanya jua kuwa taa? Na Mwenyezi Mungu amekuotesheni katika ardhi, mimea. Kisha atakurudisheni humo na atakutoeni tena.Na Mwenyezi Mungu amekufanyieni ardhi kuwa busati (kitu kizuri mlichotandikiwa). Ili mtembee humo katika njia zilizo pana. (71:13-20)Pili aliwabashiria malipo au jaza watakayopata endapo watamwamini na kumtii Allah(s.w) ipasavyo. Kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:Akasema (Nuhu) Enyi watu wangu! Kwa hakika mimi ni mwonyaji niliyedhahiri kwenu. Ya kuwa mwabuduni Allah na mcheni na mnitii.(71:2-3)Atakusameheni madhambi yenu na atakuakhirisheni (bila ya balaa) mpaka muda uliowekwa...........(71:4)
Atakuleteeni mawingu yanyeshayo mvua nyingi. Na atakupeni mali na watoto, na atakupeni mabustani na atakufanyieni mito.” (71:11-12)Tatu aliwakhofisha watu wake na adhabu ya Allah(s.w) ya hapa duniani na huko akhera, endapo watakataa kumuamini Allah (s.w) na kumuabudu ipasavyo:Na sisi tulimpeleka (tulimtuma) Nuhu kwa watu wake, (akawaambia): “Mimi kwenu ni Muonyaji anayebainisha (kila kitu). Ya kwamba msimuabudu yoyote isipokuwa Mwenyezi Mungu tu; hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya siku (kubwa hiyo) inayoumiza.” (11:25-26)“Hakika sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake, ya kwamba waonye watu wako kabla ya kuwajia adhabu iumizayo.” (71:1)

Nne aliwalingania usiku na mchana:

“Akasema (Nuhu): Ee Mola wangu: Kwa hakika nimewalingalia watu wangu usiku na mchana, lakini wito wangu haukuwazidishia ila kukimbia” (71:5-6)Tano, aliwalingania kwa njia ya muhadhara kwa sauti: Tena niliwaita kwa jahari. (71:8)Sita, aliwalingania kwa siri kwa kumuendea mmoja mmoja:“Kisha nikawatangazia kwa kelele, tena nikasema nao kwa siri’. (71:9)Saba,aliwaweka watu wake wazi kuwa hakuwa anawalingania kwenye Dini ya Allah(s.w) kwa kutaraji malipo yoyote kutoka kwao bali alifanya hivyo kwa manufaa yao wenyewe.
“Na sikutakini juu yake ujira, ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.” (26:109)Nane,alisubiri na kudumu kuwalingania kwa mbinu zilizoainishwa kwa muda wa miaka elfu kasoro hamsini (950).“Na bila shaka tulimtuma Nuhu kwa watu wake na akakaa nao miyaka elfu kasoro hamsini, (wasikubali kumfuata), basi tufani liliwafika, (wakaghariki), na hali walikuwa madhalimu (29:14)