Watu wa Lut(a.s) walipokataa kabisa kuonyeka kwa nasaha na maonyo ya Nabii Lut(a.s) na badala yake wakazidi kushabikia machafu na kupania kuwafanyia ubaya waumini, Allah(s.w) alipitisha hukumu yake ya kuwanusuru waumini na kuwaangamiza makafiri.
(Wale wajumbe) wakasema: “Ewe Lut! Sisi ni wajumbe wa Mola wako (Malaika). Hawatakufikia (kwa baya lolote). Na ondoka pamoja na watu wako katika sehemu ya pingapinga la usiku.Wala yoyote miongoni mwenu asitazame nyuma. Isipokuwa mke wako (mwanamke mbaya huyo hatakufuata). Naye utampata msiba utakaowapata hao. Hakika miadi yao ni asubuhi. Jee, asubuhi si karibu tu? (Basi tuliza moyo wako. Umekwishafika wakatiwao wa kuangamizwa).(11:81)
Basi ilipofika amri yetu, tulifanya (ardhi hiyo iwe juu chini); juu yake kuwa chini yake, na tukawateremshia mvua ya changarawe za udongo mgumu (wa motoni uliyokamatana). (11:82) (Changarawe) zilizotiwa alama kwa Mola wako (kila moja kuwa ya mtu fulani). Na (adhabu) hii haiko mbali na madhalimu (wengine kama hawa watu wa umma huu wanaofanya machafu haya). (11:83)
Jeshi la Allah lililotumika kuwaangamiza watu wa Lut(a.s) ni mvua ya changarawe kutokea motoni na kisha ardhi ikapinduliwa juu – chini.
Na majeshi ya mbingu na ardhi ni ya Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. (48:7)