Ujumbe wa Qur-an Utawafikiaje Wale wasio Waarabu au wale Wasiojua Kiarabu?Si jambo zuri na si hekima mtu kufikisha ujumbe kwa Kiarabu wakati wasikilizaji wake hawafahamu lugha hiyo. Ni kweli kuwa Kiarabu ni lugha ya Qur-an na lugha aliyoitumia Mtume (s.a.w) kufundishia yale aliyoteremshiwa kutoka kwa Allah (s.w). Hivyo ni lugha ambayo inampasa kila Muislamu ajitahidi kujifunza. Pamoja na umuhimu wa kuifahamu lugha ya Kiarabu, haina maana kuwa anayekijua Kiarabu ndiye Muislamu na yule asiyekijua ni Muislamu mwenye kasoro.La muhimu ni kuujua ujumbe wa Qur-an na kuendesha maisha ya kila siku kwa mujibu wa ujumbe huo. Ujumbe wa Qur-an unaweza kumfikia kila Muislamu pasina shaka yoyote kwa lugha yake kwa kusoma tafsiri na sherehe ya Qur-an ambayo kwa Rehema ya Allah (s.w) imetolewa katika lugha mbali mbali na wanachuoni wacha Mungu ambao ni mashuhuri katika uliwengu wa Waislamu.


Tukumbuke kuwa Qur-an imeshushwa kwa ajili ya walimwengu wote ambao Allah (s.w) amewajaalia kuzungumza lugha zinazotofautiana (rejea Qur-an (39:22). Naye Mtume (s.a.w) pia ameletwa kwa ajili ya walimwengu wote. Hivyo ili ujumbe wa Qur-an na Sunnah uwafikie walengwa wote, hauna budi kufasiriwa kwa lugha za walengwa wote. Kazi ambayo kwa Rehema ya Allah (s.w) imeshafanyika. Leo hii hapana udhuru kwa mtu yeyote ulimwenguni wa kutoufahamu ujumbe wa Qur-an kwa sababu si Mwarabu au hajui Kiarabu.Haja ya Kujifunza Lugha ya Kiarabu kwa Waislamu:
Ipo haja kubwa kwa Waislamu kujifunza lugha ya Kiarabu kuliko ile haja tunayoitambua ya kujifunza lugha za kigeni na za Kimataifa kama vile Kiingereza, Kifaransa, n.k. Kwa mfano hapa Tanzania tunajifunza lugha ya Kiingereza (English) ili tuweze kufaidika kitaaluma, kiuchumi, na kisiasa n.k. Tukijifunza lugha ya Kiarabu tunafaidika na hayo yote pamoja na ziada ifuatayo:(i) Tutaufahamu ujumbe wa Qur-an na mafundisho ya Mtume (s.a.w) kwa lugha yake ya asili. Daima tafsiri haikosi upungufu japo kidogo.(ii)Tutaweza kufahamu maana ya undani ya dua na dhikiri mbali mbali tunazoleta katika ibada maalum kama vile swala ambapo haturuhusiwi kutumia lugha nyingine isiyokuwa Kiarabu. Kufahamu maana ya yote tuyasemayo katika swala hutupelekea kuwa na khushui inayotakikana.(iii)Lugha ya Kiarabu ni chombo cha kuwaunganisha waislamu wote ulimwenguni ili wadumishe udugu na umoja wao kama wanavyotakiwa wawe. Kama Waislamu wanavyoshikamana katika swala kwa kutumia lugha moja ndivyo wanavyotakiwa waelewane na kushikamana katika ibada zote zinazofanywa kimataifa kama vile Ibada ya Hijja.