Hitimisho


Maimamu wote wanne walikuwa wanachuoni wacha Mungu na waadilifu katika zama zao. Walifanya juhudi kubwa kusoma na kufanya ijtihada ya kutafsiri na kutoa maoni yao juu ya sheria na masuala mbalimbali ya Fiqh. Ni vizuri tunufaike na matunda ya juhudi zao, lakini tusigawike wala kubaguana kutokana na maoni tofauti ya Maimamu hao juu ya masuala mbalimbali. Wao wenyewe walisoma pamoja au kusomesha na wakaheshimiana na wakaafikiana kutofautiana katika mambo ya msingi bila ya kugombana.


Jambo jingine la msingi la kuzingatia ni kuwa Maimamu hawa walipata mateso makubwa kutokana na misimamo na juhudi zao katika kuuhuisha na kuusimamisha Uislamu katika


jamii. Walichapwa viboko, walifungwa gerezani na kufungwa minyororo na watawala madhalimu. Zaidi ya hivyo hawakukubali kununuliwa na Serikali. Walikataa kabisa kuwa vibaraka wa Serikali. Je, wakati tunafuata Fiqh na Fat’wa zao tunao pia uadilifu kama wao? Misimamo yetu juu ya Serikali za kidhalimu ni kama wao? Je, hatununuliwi na Serikali na kuifanyia kazi kinyume na maslahi ya Uislamu? Je, tupo tayari kufungwa na kuchapwa viboko kwa ajili ya kusimamisha haki kama Imam Abu Hanifa, Malik, Shafii na Hambal?