Uchaguzi wa Uthman bin Afan


Uchaguzi wa Uthman bin Affan Kuwa Khalifa wa Tatu Uislamu sio dini iliyofungwa katika mabano bali ina sifa ya kwenda na wakati kwa maana kuwa maamuzi yake ilimradi yamo katika mfumo wa Uislamu yanakubalika. Hali ilivyokuwa wakati alipotawafu Mtume(s.a.w) imetofautiana na ile ya wakati alipotawafu Abubakar. Wakati wa kifo cha Abubakar, Umar alikuwa amejitokeza kuwa ndiye Khalifa bila upinzani lakini wakati wa kifo cha Umar hali ilikuwa tofauti. Walikuwepo watu wengi wenye sifa zinazolingana hivyo alichokifanya Umar ni kuteua jopo la wagombea sita wa ukhalifa ambao walikuwa Uthman, Ali, Saad bin Waqqas, Talha, Zubair na Abdur-Rahman bin Auf.26 Agizo lingine alilotoa ni kuwa katika muda wa siku tatu baada ya kifo chake wawe wameshaamua wao wenyewe nani miongoni mwao awe
Khalifa.


Jopo hili lilikaa kwa muda mrefu bila kufikia uamuzi ndipo Abdur-Rahman bin Auf aliposhauri kuwa kati yao mmoja ajitoe ili aweze kutoa uamuzi. Alipokosa jibu alijitoa mwenyewe na akaanza kazi ya kutafuta maoni ili kukamilisha uteuzi. Talha hakuwepo hivyo wagombea walibaki wanne. Imetokea kuwa Ali alimpendekeza Uthman na Uthman alimpendekeza Ali. Zubair na Saad walimpendekeza Uthman. Baada ya kushauriana na Maswahaba wengine na kwa kuzingatia muda wa siku tatu Abdur-


Rahman bin Auf alitoa uamuzi asubuhi ya siku ya nne na kumtangaza Uthman kuwa ndiye Khalifa. Abdur-Rahman bin Auf (r.a.) alianza kumpa bai’at (mkono wa ahadi ya utii) na kutambua Ukhalifa wake ndipo Waislamu waliokuwa msikitini wakafuatia na kwa namna hii Uthman akawa Khalifa wa tatu. Talha aliporudi Madinah, Uthman alimshauri achague moja kati ya mawili, achukue nafasi ya Ukhalifa au ampe mkono wa ahadi ya utii. Talha alikubali kumpa mkono wa ahadi ya utii.


Utaratibu huu pia umo katika mkondo wa Uislamu na ni aina ya tatu ya utaratibu unaokubalika wa kupata viongozi katika Uislamu.