Mambo ya Msingi Aliyofanya Mtume(s.
Mambo ya Msingi Aliyofanya Mtume(s.a.w) Katika
Kuanzisha Dola ya Kiislamu Madinah.
Mtume(s.a.w) alipofika Madinah alitumia fursa ile ya mazingira ya amani na kuanzisha Dola ya kiislamu kwa kufanya yafuatayo:
(i) Kujenga msikiti wa Madina
(ii) Kujenga ummah wa kiislamu
(iii) Kuweka mkataba wa Madinah(Madina Cherter)
(iv) Kuweka mikataba ya amani na makabila ya Kiyahudi pembezoni mwa Madinah.
(v) Kuandaa Ummah kijeshi na kiusalama. (vi) Kuimarisha uchumi.
(vii) Kuunda(kuanzisha) sekretarieti. (viii) Kuteua shura.
(i) Kujenga Misikiti wa Madinah
Jambo la kwanza alilolifanya Mtume(s.a.w) alipoingia Madinah ni kujenga msikiti uliojulikana kwa jina la “Msikiti wa Mtume” au “msikiti wa Madinah”. Msikiti ulijengwa katika uwanja ulionunuliwa kutoka kwa yatima mawili, Sahl na Suhail. Mtume(s.a.w) alipowaeleza vijana hawa juu ya nia yake ya kutaka kununua uwanja wao, si tu kwamba walikubali kwa furaha, bali walimtaka Mtume(s.a.w) awakubalie wautoe bure. Mtume(s.a.w) hakukubali ombi lao, bali alimuamuru Abubakar anunue uwanja ule kwa niaba yake.
Msikiti wa Mtume(s.a.w) ulitumika kwa kazi nyingi. Ulitumika kama mahali pa kuswalia swala za jamaa, darasa, Ikulu ya Mtume, Mahakama, ukumbi wa bunge (shura), kituo cha jeshi, mapokezi ya wageni, makazi ya maskini, n.k. Kwa ufupi Msikiti wa Mtume ulikuwa kituo cha harakati za kuhuisha na kusimamisha Uislamu katika jamii.
(ii) Kujenga Ummah wa Kiislamu
Kabla ya Hijira, Yathrib ilikaliwa na Mayahud na Waarabu wa Kabila la Aus na Khazraj. Aus na Khazraj daima walikuwa katika uhasama na vita visivyokatika wakichochewa na Mayahud ili waweze kuwa juu yao na kuwanyonya kiuchumi. Baada ya Aus na Khazraj kuwa Waislamu, walisahau kabisa tofauti zao zote na wakashikamana pamoja na kuwa kundi moja la Answar (wenye kunusuru Uislamu) kama Mtume(s.a.w) alivyowaita. Hali kadhalika watu wa Makka nao waliposilimu walitupilia mbali ukabila na kushikamana na udugu wa Kiislamu. Waislamu wa Makka walipohamia Madinah, kama kundi waliitwa Muhajirina (waliohamia).
Baada ya ujenzi wa msikiti, jambo la pili alilolishughulikia Mtume(s.a.w), ni namna ya kutatua tatizo la kiuchumi lililokuwa likiwakabili Muhajirin. Takriban Waislamu wote waliohamia kutoka Makkah walikuwa na hali mbaya kiuchumi kwa vile nyumba zao na mali yao nyingi isiyochukulika ilibakia Makkah. Hivyo wengi wa Muhajirina walifika Madinah wakiwa masikini hohe-hahe. Hawakuwa na makazi, chakula, nguo na mahitaji mengine muhimu ya maisha. Mtume(s.a.w), akiwa kiongozi mweledi wa Dola ya
Kiislamu, aliona utatuzi pekee wa tatizo hili ni kuuingiza udugu wa Kiislamu katika matendo. Aliwakusanya Muhajirina wote na akachagua wanaojiweza kidogo kiuchumi miongoni mwa Answar kiasi cha ile idadi ya Muhajirina. Kisha akapiga kura na kila mmoja katika wale Answar likamuangukia jina la mmoja wa Muhajir ili awe ndugu yake wa Kidini. Udugu huu wa Kidini uliofungamana na mapenzi na huruma ulikuwa mzito kuliko udugu wa damu kiasi kwamba ndugu wa upande wa Answar alikuwa radhi kutoa nusu ya kila alichomiliki ampe ndugu yake wa upande wa Muhajirina kama tunavyojifunza katika Hadith ifuatayo:
“Amesimulia Anas (r.a), Abdur-Rahman bin ‘Auf alipokuja kwetu (Madinah) Mtume wa Allah aliunganisha udugu baina yake na Sa’d bin Ar-Rabi aliyekuwa tajiri: Sa’d akasema: Answar wananifahamu kuwa mimi ni tajiri mkubwa kuliko wao wote, hivyo nitagawanya mali yangu katika sehemu mbili, yako na yangu, na nina wake wawili, chagua umpendaye, Ili nimpe talaka na baada ya kipindi cha eda umuoe” Abdur-Rahman alisema: “Allah akubariki wewe na familia yako (wake zako). (Badala yake aliomba aonyeshwe sokoni akafanye biashara) alikwenda kufanya biashara sokoni na siku ile akarudi na faida ya mkate wa Yoghurt na siagi…” (Sahihi na Bukhari).
Hadithi hii ni kielelezo cha ukarimu wa Answar kwa ndugu zao Muhajirina na Allah(s.w) amewasifu kwa ukarimu wao huo katika aya zifuatazo:
(Basi) wapewe (mali ) mafakiri wa miongoni mwa Muhajirin ambao walifukuzwa katika nyumba zao na mali zao (wakakhiari kuacha hayo) kwa ajili ya (kutafuta) fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi (yake) na kuinusuru (Dini ya) Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi hao ndio Waislamu wa kweli.(59:8)
Na (pia wapewe) wale waliofanya maskani yao hapa (Madinah) na wakautakasa Uislamu (wao) kabla ya kuja (hao Muhajirin) na wakawapenda hao waliohamia kwao, wala hawaoni dhiki nyoyoni mwao kwa hayo waliyopewa (hao Muhajir), na wanawapendelea kuliko nafsi zao ingawa wenyewe wana hali ndogo. Na waepushwao na ubakhili wa nafsi zao hao ndio wenye kufaulu kweli kweli”. (59:9).
Kwa muunganisho wa udugu, Waislamu kutoka Makkah walijisikia kama wapo nyumbani na walipata fursa nzuri ya kujijenga upya kiuchumi. Hata hivyo kutokana na tabia nzuri ya Kiislam waliyokuwa nayo, Muhajirin hawakutaka kuwa mzingo kwa ndugu zao na walijitahidi kutokubali kupokea msaada mwingi kupita kiasi kutoka kwa ndugu zao na walijitahidi kujitegemea kwa kufanya kazi mbali mbali, hasa biashara, kwa kadiri walivyoweza kama tunavyojifunza katika Hadithi ifuatayo:
“Amesimulia Abu Hurairah (r.a): Answar walimwambia Mtume (s.a.w), “Tafadhali gawanya mashamba yetu ya mitende kati yetu na Muhajirin. Mtume(s.a.w) alikataa. Answar wakasema (katika pendekezo lingine): “Muhajirin wafanye kazi katika bustani (zetu za mitende) kisha tutagawana matunda yatakayopatikana.” Muhajirin wakasema, “Hili tunakubaliana nalo” (Sahihi Bukhari).
Udugu wa Kidini kati ya Muhajirin na Answar, unabainishwa pia katika aya ifuatayo:
Hakika wale walioamini na wakahama na wakapigania Dini ya Allah kwa mali zao na nafsi zao (Nao ni wale Muhajirin). Na waliowapa (Muhajirin) mahali pa kukaa (nao ni Answar) na wakainusuru Dini ya Allah; hao ndio marafiki wao kwa wao. Na wale walioamini lakini hawakuhama nyinyi hamna haki ya kurithiana nao (mpaka wahame)............” (8:72)
Udugu wa Kidini baina ya Answar na Muhajirin, ulikuwa mzito kiasi kwamba mwanzoni ndugu hawa wawili walirithiana. Baada ya Uislamu kuimarika na kuenea kote Bara Arab na watu wengi kusilimu ikiwa ni pamoja na watu wa Makka, sharia ya kurithiana kwa misingi ya udugu wa Kidini iliondolewa na Waislamu wakawa wanarithiana kwa sharia ya mirathi tunayoifuata hivi leo . Sharia ya kurithiana baina ya Answar na Muhajirin ilifutwa na aya ifuatayo:
“Na wale watakaoamini baadaye, wakahajiri nao, wakapigana pamoja nanyi (katika kupigania Dini) basi hao ni katika nyinyi. Na ndugu wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (katika kurithiana. Ndivyo vilivyo) katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu” (8:75).
Muhajirina walikuwa wakifanya biashara walipokuwa Makka, hivyo walijiingiza katika biashara na katika muda mfupi wengi wao waliinukia kuwa wafanya biashara wakubwa kama ‘Uthman bin Affan na Abdur-Rahman bin ‘Auf. Answari nao kulingana na mazingira ya Madinah walipendelea kilimo zaidi. Ni dhahiri kuwa kwa kuchangaya kilimo na biashara, uchumi wa Madinah uliinuka haraka haraka. Uchumi wa Madinah ulizidi kwenda juu kutokana na ngawira walizozipata Waislamu kutokana na ushindi walioupata katika vita mbali mbali vya jihad. Kwa mara ya kwanza ulianzishwa mfuko au hazina ya Serikali – Baitul Mal – kwa ajili ya kuendesha shughuli za Serikali ya Kiislamu na kwa ajili ya kuwasaidia wasiojiweza, hasa wale wakazi wa Suffah. Waislamu walichangia mfuko huu kwa kutoa zakat na Sadaqat.
(iii)Kuweka Mkataba wa Madinah
Mtume(s.a.w) aliona kuwa, ili kuhakikisha mji wa Madinah unakuwa na amani, hapanabudi kuandikiana mkataba wa amani na Mayahudi. Mtume(s.a.w)aliwaendea Mayahudi na kuwafahamisha kuwa yeye ni Mtume wa Allah(s.w) kama Mitume wengine waliomtangulia na kuwa anakuja kuthibitisha Dini ya Mitume hao na sio kuipinga. Aliwathibitishia kuwa yeye ni Mtume aliyeletwa kwa upande wa Waarabu kama Mussa(a.s) alivyoletwa kwa upande wa wana Israil (Mayahudi).
“Hakika sisi tumekuleteeni Mtume aliyeshahidi juu yenu, kama tulivyompeleka Mtume kwa Firaun”. (73:15).
Mayahudi walipoona kuwa Mtume(s.a.w) na Waislamu wanafunga pamoja siku ya Ashura na wanaelekea Qibla kimoja cha Yerusalem (Masjidul-Aqswaa) wakati wa kuswali, walihisi kuwa Waislamu wako pamoja nao. Ni katika kipindi hiki cha awali Mtume(s.a.w) alifunga nao mkataba wa amani na ukawekwa wazi katika katiba ya Dola ya Kiislamu. Mkataba wa Madinah uliainisha mahusiano mema baina ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu
katika mji wa Madinah. Katika mkataba huu kila kundi la watu, Waislamu, Mayahudi na Washirikina (Waarabu waliokuwa hawajasilimu), walikuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa mji wa Madinah unakuwa katika amani na wote waliwajibika kuuhami endapo utavamiwa na maadui zao. Kila watu walikuwa na uhuru wa kufuata Dini waipendayo.
(iv)Mikataba ya Amani na Makabila ya Kiyahudi pembezoni mwa Madinah
Pamoja na mkataba wa Madinah, Mtume(s.a.w) aliweka mikataba ya amani na makabila mbali mbali yaliyo pembezoni mwa mji wa Madinah. Miongoni mwa koo za Kiyahudi zilizokuwa zikiishi pembezoni mwa mji ni Banu Quraizah, Banu Qainuqa na Banu Nadhir. Hizi zilikuwa koo maarufu za Kiyahudi zenye nguvu. Mtume(s.a.w) alifunga nazo mikataba ya amani.
(v) Kuandaa Ummah Kijeshi na Kiusalama
Mtume(s.a.w) aliwahimiza Waislamu kuwa wakakamavu, kujifunza shahaba na mieleka na kuwa na silaha. Kila Muislamu mwanamume alikuwa mpiganaji na mpelelezi dhidi ya maadui wa Uislamu na njama zao.
(vi) Kuimarisha Uchumi
Pamoja na Mtume(s.a.w) kuweka mazingira ya kusaidiana kiuchumi kwa kuunganisha udugu baina ya Answar na Muhajirina aliwahimiza Waislamu kufanya kazi kwa bidii na kujiimarisha kiuchumi. Utoaji wa Zakat na Sadaqat ulihimizwa ili kuondoa umaskini na kuimarisha huduma za jamii. Ilianzishwa Baitul- mal(Hazina ya Dola).
(vii) Kuteua Sekretarieti
Mtume(s.a.w) aliteua waandishi maalumu ambao walikuwa wakiandika na kuweka kumbukumbu ya mambo mbali mbali. Pamoja na waandishi wa Qur-an waliokuwepo tangu Makka,
alikuwa na waandishi wa mikataba, idadi ya watu, idadi ya mitende na mifugo, n.k. Palikuwa na taarifa na rikodi ya kila kitu.
(viii) Kuteua Shura
Pia Mtume(s.a.w) aliteua Waislamu weledi na wazoefu kuwa washauri wake katika mambo mbali mbali. Waliokuwa safa ya mbele katika washauri wake ni Abu bakar(r.a), ‘Umar bin Khattab(r.a), ‘Uthman bin Affan(r.a), ‘Ali bin Abu-Talib(r.a), Hamza bin Abdul-Muttalib na wengineo. Wengi wao walikuwa Muhajiriina. Hata hivyo Mtume(s.a.w) alipohitaji rai kutoka kwa watu wote, alipendelea sana kuanza kupata rai kutoka kwa Answar.
Je! umeipenda hii post?
Ndio Hapana Save post
Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Topic: Sira Main: Post File: Download PDF Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 1641
Sponsored links
👉1 Kitau cha Fiqh
👉2 Kitabu cha Afya
👉3 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)
👉4 kitabu cha Simulizi
👉5 Madrasa kiganjani
👉6 Simulizi za Hadithi Audio
Mfumo wa ulinzi na usalama katika fola ya uislamu madinah
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...
Mafunzo yatokanayo na kuanzishwa kwa dola ya uislamu madinah
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...
Maadui wakubwa wa dola ya uislamu madinah
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...
HISTORIA NA VISA VYA MITUME, MANABII NA WATU WEMA WALIOTAJWA KWENYE QURAN
Soma Zaidi...
Mafunzo yatokanayo na hijrah ya mtume na maswahaba wake
Bara arabu zama za jahiliyyah (EDK form 2 dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...
Historia ya Firaun, Qarun na Hamana
Karun na Hamana waliishi zama za Mtume Musa(a. Soma Zaidi...
Mbinu Alizozitumia Nabii Shu’ayb(a.s) Katika Kufikisha Ujumbe Wake
Soma Zaidi...
Jifunze historia ya uislamu toka mitume na manabii, kuja kwa makhalifa na maimamu hadi leo
Soma Zaidi...
Mjadala juu ya ndoa ya Mtume Muhammad s.a.w na bi Khadija.
Sara na historia ya Mtume Muhammad s.a.w sehemu ya 16. Hapa utajifunza maandalizi wa mjadala wa ndoa hizi. Soma Zaidi...
MJADALA JUU YA NDOA YA MTUME S.A.W NA BI KHADIJA (HADIJA)
LAKINI UMRI WANGU MKUBWABaada ya kuwaza na kufikiri muda mrefu, bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akafikia uamuzi wa kutaka kuolewa na Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam). Soma Zaidi...
Mambo ya Msingi Aliyofanya Mtume(s.a.w) Katika Kuanzisha Dola ya Kiislamu Madinah.
Mambo ya Msingi Aliyofanya Mtume(s. Soma Zaidi...
Kuanzishwa kwa dola ya kiislamu madinah
Dola ya kiislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...