HISTORIA YA NABII IBRAHIIM(A.S) NA KUANDALIWA KWAKE:

Nabii Ibrahiim(a.s) ni Mtume wa Allah(s.w) aliyemfuatia Salih(a.s) katika wale waliotajwa katika Qur-an. Alizaliwa na kulelewa katika mji wa Ur huko Iraq. Baba yake,Azara,alikuwa akichonga masanamu na kuyauza kwa washirikina waliokuwa wakiyaabudu badala ya Allah(s.w). Hivyo ni wazi kuwa NabiiIbrahiim(a.s) aliletwa kwa jamii iliyozama katika giza la ushirikina.Kuandaliwa kwa Nabii Ibrahiim(a.s)
Tangu angali mdogo, NabiiIbrahiim(a.s) aliyakinisha kuwepo kwa Allah(s.w) kwa kuchunguza dalili zilizomzunguka katika maumbile ya mbingu na ardhi. Baada ya kuyakinisha kuwepo kwa Allah(s.w), alichukua azma ya kumtii kwa unyenyekevu katika maisha yake yote kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:“(Kumbukeni habari hii) Mola wake (Ibrahim) alipomwambia “Silimu” (Jisalimishe) akanena: Nimejisalimisha kwa Mola wa walimwengu wote”. (2:131)Imani yake ya kweli juu ya Allah(s.w), ilimpelekea kuwa na tabia njema isiyo na mfano wake katika jamii kama tunavyojifunza katika Qur-an:

Hakika Ibrahim alikuwa Imamu (mfano mzuri wa wema wa kuigwa), mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, mtii kamili, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.(16:120)(Alikuwa) mwenye kuzishukuru neema Zake (Mwenyezi Mungu zilizo juu yake), akamchagua na kumuongoza katika njia iliyonyooka. Na tukampa wema katika dunia; na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema (pia). (16:121-122)

“...........Kwa yakini Ibrahim alikuwa mwingi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu na mvumilivu”. (9:114)“Na mtaje Ibrahim katika kitabu (hiki) bila shaka yeye alikuwa mkweli sana, Nabii.” (19:41)Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa NabiiIbrahiim(a.s) alikuwa Hanifa, yaani aliyejiepusha na Dini za upotevu na hakuwa mshirikina. Alikuwa mnyenyekevu kwa Allah(s.w) na mtii kamili. Alikuwa mwenye kushukuru neema za Allah(s.w), alikuwa mkweli, mwingi wa kurejea kwa Allah(s.w) na alikuwa mvumilivu. Pia alikuwa mwepesi katika kukirimu wageni kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:“Na wajumbe wetu walimwendea Ibrahim kwa bishara, (njema) wakasema: “Salaam – amani”, akasema (Ibrahim). “Juu yenu pia iwe amani”. Na hakukaa (Ibrahim) ila mara alileta ndama (aliyechomwa vizuri).” (11:69)