Baada ya NabiiIbrahiim(a.s) kutoa shahada ya kweli alipomuahidi Mola wake: “Nimejisalimisha kwa Bwana Mlezi wa Walimwengu Wote” alianza kulingania Tawhiid kwa watu wa jamii yake. Kwa hekima aliona aanze kumlingania baba yake, aliyekuwa mchonga masanamu na kiongozi wa Ibada ya masanamu. Alianza kumlingania kwa kutumia hoja zenye mashiko katika akili ya mwanaadamu kama ifuatavyo:
(Wakumbushe) alipomwambia baba yake: “Ewe baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyosikia na visivyoona na visivyofaa chochote?” (19:42)
“Ewe baba yangu! Kwa yakini imenijia ilimu isiyokujia. Basi nifuate nitakuongoza njia iliyo sawa.(19:43)
Ewe baba yangu! Usimuabudu Shetani, hakika Shetani ni mwenye kumuasi (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa rehema.(19:44)
“Ewe baba yangu! Hakika naogopa kukupata adhabu inayotoka kwa Mwingi wa rehema (Mwenyezi Mungu), (ukifanya hivyo) utakuwa mwenziwe shetani.” (19:45)
Babu yake, badala ya kuyatia akilini aliyofikishiwa na mwanawe, alimkemea, kumtisha na badaye kumfukuzilia mbali nyumbani kwake.
“Akasema (yule baba yake) “Je! Unaichukia miungu yangu, ewe Ibrahim? Kama huachi (haya unayosema) lazima nitakupiga mawe. Na niondokelee mbali kwa muda mchache (huu).” (19:46)
Nabii Ibrahim(a.s)hakutetereka na kurudi nyuma alipofukuzwa nyumbani mwa baba yake. Alibakia na msimamo wake wa kulingania Dini ya Allah(s.w) kwa moyo mkunjufu huku akitarajia msaada kutoka kwake Allah(s.w) pekee.
“Na mimi nakuondokeeni (na kujiepusha) na mnayoyaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu. Hakika sitakuwa mwenye kukhibu (kukosa ninalotaka) kwa kumuomba Mola wangu.” (19:48).