HISTORIA YA MTUME ISA(A.S)


Nabii Isa(a.s) huitwa “Yesu”, na “Jesus” katika Biblia ya Kiswahili na Kiingereza. Majina yote hayo matatu yanamkusudia mwana wa Maryamu aliyezaliwa bila baba, ambaye ni Mtume wa mwisho kwa Bani Israil.


Nasaba na kuzaliwa Nabii Isa(a.s)


Nabii Isa(a.s) ni mtoto wa Maryamu aliyekuwa mwana wa Imraani. Kizazi cha Imraani kilichaguliwa na Allah(s.w) kupewa Utume kama tunavyofahamishwa:


Hakika Mwenyezi Mungu alimchagua Adamu na Nuhu na kizazi cha
Ibrahiimu na kizazi cha Imraani juu ya walimwengu wote(3:33)


Kuzaliwa Maryamu, Mama wa Nabii Isa(a.s)


Mke wa Imraani aliweka nadhiri kwa Allah(s.w) kuwa mtoto atakayemzaa atamuweka wakfu. Alitarajia kuwa atazaa mtoto wa kiume.Aliposema mke wa Imraani: “Mola wangu! Nimeweka nadhiri kwako aliye tumboni mwangu kuwa wakfu, basi nikubalie, bila shaka Wewe ndiye usikiaye na ujuaye.(3:35)Basi alipomzaa alisema: “Mola wangu! Nimezaa mwanamke”- Na Mwenyezi Mungu anajua sana aliyemzaa -”Na mwanaume si sawa na mwanamke. Na nimempa jina Maryam. nami namkinga kwako, yeye na kizazi chake, uwalinde na shetani aliyewekwa mbali na rehema zako (3:36)