Sura za Makka na Madina
Kutokana na historia ya kushuka kwake sura za Qur-an zimegawanywa katika makundi mawili - sura za Makka na sura za Madina.Sura za Makka ni zile zilizomshukia Mtume (s.a.w) katika kipindi cha Utume cha Makka kilichodumu kwa miaka 13. Maudhui ya sura za Makka kwa kiwango kikubwa yamejikita katika kujenga imani za watu kwa kutoa hoja madhubuti zilizozingatia mazingira ya wakazi wa Makka wa kipindi hicho. Muundo wa sura za Makka ni ule wa kishairi. Nyingi ya sura za Makka zimeundwa na aya fupi zenye kufikisha ujumbe moja kwa moja kwa mtindo wa kishairi uliozingatia mazingira ya watu wa Makka wa wakati ule.Katika siku za mwanzo za kushuka kwa Qur-an, watu wa Makka walidhania kuwa Qur-an ni mashairi aliyotunga Muhammad (s.a.w), lakini baada ya kupitia aya zake kwa makini, kama alivyofanya bingwa wa washairi wa wakati huo, Labiid bin Rabiah, na baada ya kushindwa kutoa angalau sura moja mithili ya sura ya Qur-an, kimaudhui na kimuundo, ilidhihiri wazi kuwa Qur-an si mashairi bali ni Wahy kutoka kwa Allah (s.w).


Sura za Madina ni zile zilizomshukia Mtume (s.a.w) baada ya kuhamia Madina katika kipindi cha pili cha Utume wake kilichodumu kwa miaka 10.


Maudhui ya sura za Madinah yamejikita kwenye kuunda na kuendesha Dola ya Kiislamu. Nyingi ya sura za Madina zina aya ndefu zenye kufafanua mambo kwa uwazi ili kuwawezesha Waislamu kutekeleza wajibu wao katika kusimamisha na kuhami dola ya Kiislamu. Pia aya nyingi za Madina zimeshehenezwa na maamrisho na makatazo mbali mbali ili kuunda jamii imara itakayoweza kusimamisha Ukhalifa katika ardhi.