(a)Dai la Kufundishwa na Padri Bahira:



Baadhi ya makafiri wanadai kuwa Mtume Muhammad (s.a.w) alijifunza Uyahudi na Ukristo katika safari zake mbili za biashara alizofanya Sham (Syria), hasa katika safari yake ya kwanza alipokutana na Padri Bahirah, alipokuwa na umri wa miaka 12. Tunavyojifunza katika historia ni kuwa Bahirah alikutana na Mtume (s.a.w) njiani na kuashiria kwa Ami yake Abutwalib, kuwa anamkisia kijana wake (Muhammad) ana sifa za yule mtume aliyetabiriwa katika Injili (Rejea Qur-an 61:6).


Je, inamkinika kuwa mazungumzo haya ya njiani ya muda mfupi yawe ndiyo yaliyompelekea Mtume (s.a.w) kuandika Qur-an miaka 28 baada ya makutano hayo? Ikumbukwe kuwa Mtume (s.a.w) alianza kushushiwa wahy wa Quran alipokuwa na umri wa miaka arobaini ambapo alikutana na Bahirah akiwa na umri wa miaka kumi na mbili.



Safari ya pili ya Mtume (s.a.w) kwenda Syria kwa biashara ni pale alipokodiwa na Bibi Khadijah alipokuwa na umri miaka ishirini na tano. Katika kumbukumbu za historia, Mtume (s.a.w) hakufanya mkutano wowote na Wakristo wala Mayahudi kabla ya Utume.